Maadhimisho
ya Jumapili ya Matawi, Kanisa linamshangilia Kristo alipoingia
Yerusalemu kwa shangwe na watoto wa Wayahudi wakatandaza nguo zao
njiani. Hii ni siku ya vijana kijimbo, inayoongozwa na kauli mbiu, "Heri
maskini wa roho maana ufalme wa mbingu ni wao".
Baba Mtakatifu
Francisko mara baada ya kubariki matawi, umati wa vijana ulianza
maandamano kuelekea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican, huku wakiimba kwa shangwe. Baba Mtakatifu katika Ibada hii
ametumia Fimbo ya Kiaskofu aliyozawadiwa na wafungwa kutoka gereza la
Sanremo, Italia. Huu ni mwanzo wa maadhimisho ya juma kuu, Kanisa
linapokumbuka mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.
Baba Mtakatifu
katika mahubiri yake anatawaka waamini kujitafakari kwa kuangalia hali
yao mbele ya Yesu, kama wako kweli na hamasa ya kuonesha furaha na
kumshangilia, au wamejikunyata na kumwangalia tu kama "nyanya mbichi".
Katika shida na mahangaiko ya Yesu, waamini wanajisikia namna gani na
wako upande gani? Je, ni kati ya kundi la wakuu wa Makuhani na Waandishi
waliokuwa wanasubiri fursa ya kumkamata na kumsulubisha Yesu?
Je,
wao pia ni sehemu ya akina Yuda Iskarioti waliomuuza Yesu kwa vipande
thelathini vya fedha? Au ni kati ya Mitume waliokuwa wanauchapa usingizi
wakati Yesu anakabiliana na mateso makali? Baba Mtakatifu anawauliza
waamini ikiwa kama wanataka njia ya mkato kwa kutumia upanga kama
ambavyo alitaka kufanya Mtakatifu Petro? au Yuda aliyemsaliti Yesu kwa
busu la unafiki? Au Wazee wa Baraza wanaofanya kila mbinu kwa kutafuta
mashahidi wa uwongo ili kumtia Yesu hatiani kwa kudhani kwamba ni kwa
ajili ya mafao ya wengi?
Baba Mtakatifu anaendelea kuwauliza
waamini ikiwa kama wanafanana na Pilato anapoona kwamba, "maji yamezidi
unga" ana nawa mikono ili kukwepa wajibu wake kwa kuwashirikisha
wengine. Katika hali ya kuchanganyikiwa na vurugu, Je, hata waamini nao
wanaendelea kupiga kelele wakitaka Barabara afunguliwe na Yesu ahukumiwe
kifo ili kuwafurisha watu na kumdhalilisha Yesu au kama wale Askari
waliomdhihaki, wakampiga mijeledi na kumtemea mate usoni?
Baba
Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake ambayo yalikuwa ni tafakari
inayomshirikisha mwamini binafsi anawauliza ikiwa kama kweli wamekuwa na
ujasiri wa Simoni wa Kirene aliyeshurutishwa kumsaidia Yesu kubeba
Msalaba wake naye kwa upendo mkubwa akatekeleza dhamana hii! Kuna watu
waliokuwa wanapita mbele ya Msalaba wakimdhihaki Yesu kwa vile
alijiaminisha kuwa ni Mwana wa Mungu. Baba Mtakatifu anawauliza waamini,
Je, hata wao wanajisikia kuwa na jeuri hata kumdhihaki na kumkejeri
Mwana wa Mungu?
Bikira Maria na baadhi ya wanawake wajasiri,
walisimama chini ya Msalaba kwa ujasiri mkubwa, wakateseka pamoja na
Yesu katika hali ya ukimya!, Je, waamini nao wanaendelea kuteseka na
Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku, tayari kama Yusufu wa
Arimatayo kwenda kuchukua Mwili wa Yesu ili kuuzika au wanawake
waliokuwa wanalia mbele ya kaburi la Yesu au wale Askari walioomba
ulinzi mkali kwenye Kaburi la Yesu aliyekuwa ametangaza kwamba, baada ya
Siku tatu angefufuka kutoka katika wafu? Hawa ni watu waliokuwa
wanataka kuzuia maisha mapya kwa njia ya ufufuko wa Yesu.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, haya ni maswali msingi ambayo yanaweza
kuwasaidia waamini katika tafakari ya maadhimisho ya Juma kuu, Kanisa
linapotafakari Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Yesu
Kristo.
Katika
ulimwengu wa leo suala la maandamano limeshamiri karibu katika kila
nchi. Maandamano hayo yanakuwa ya jamii fulani inayodai haki yake,
mathalani yanaweza kuwa maandamano ya wanawake wanaodai haki zao za
kijinsia, wafanyakazi, wanafunzi, waganga nk.
Maandamano mengine
yanakuwa ya kufanya kampeni ya uongozi, na mengine ni ya shamrashamra
za sikukuu fulani za kidini au arusi nk. Maandamano yoyote yanakuwa na
sehemu mbili maalumu yaani pahala pa kuanzia na pa kumalizikia, sehemu
hizo zaweza kuwa hospitalini, shuleni, uwanjani, ikulu au hata kanisani
nk.
Leo tutayaona maandamano ya namna yake yanayoendeshwa na
Yesu. Maandamano hayo siyo ya kufanya mgomo wa madai ya masilahi toka
serikalini, la hasha, bali tungeweza kuuingiza kwenye aina kama vile ya
kampeni ya kupigania sera zake za uongozi. Maandamano hayo yalikusanya
watu wengi sana, wakiwepo wanafunzi wake, mashabiki wengi na wapambe
kibao mpaka mji ukatikisika. Yerusalemu hapakutosha! Mapato yake hata
viongozi wa dini na wa serikali walipoyaona maandamano hayo wakataharuki
na kuulizana: “Ni nani huyu?”
Maandamano ya leo yalianza pahala
palipoitwa Bethfage na yakaishia mjini Yerusalemu tena ndani ya
Hekaluni. Humo hekaluni, Yesu anahitimisha maandamano siyo kwa kutoa
hotuba refu ya ahadi hewa, hapana, bali kwa kuwashughulikia watu
waliokuwa wanachenji hela na kufanya biashara ndogondogo hekaluni,
halafu siku ya pili yake anapokuwa na njaa anaulaani mtini usiozaa
matunda.
Sasa hebu tupaone kwanza pahala palipoanzia na
palipoishia maandamano hayo, yaani Bethfage na Yerusalemu. “Hata
walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa
Mizeituni.” Bethfage, ipo upande wa Mashariki ya mlima wa Mizeituni,
baada tu ya Bethfage kuna mlima wa Mizeituni ambako ukisimama juu yake
unaweza kuangalia vizuri sana mji wa Yerusalemu ulio chini yake. Neno
hili Bethfage ni muunganiko wa maneno mawili, Beth (Bayet) ni nyumba; na
Fage ni matunda ya tini yasiyokomaa. Kwa hiyo Bethfage ni nyumba ya
matunda ya tini yasiyokomaa.
Jambo la kushangaza ni kwamba baada
ya kuingia Yerusalemu na kuwasambaratisha wafanyabiashara hekaluni,
linafuata simulizi la mfano ule ambao unonesha kitu gani Mungu
anakitegemea toka kwa Taifa lake, yaani kitendo cha Yesu kwenda kutafuta
matunda kwenye mti wa mtini na bila kukuta kitu isipokuwa majani
matupu, anaulaani. “Mtini ukanyauka mara.” Tendo lile la Yesu ni mfano
hai unaolingana na kile anachokitegemea Mungu toka kwa watu wake
kifanyike ndani ya hekalu au katika ibada zao, lakini anakikosa.
Mungu
anategemea kupata matunda ya upendo, ya haki, ya kuwajali maskini,
wajane, yatima na watoto, wageni, badala yake ndani ya hekalu anakuta
majani, yaani, liturjia, nyimbo za kupendeza, madhehebu marefu, chetezo,
ubani na mishumaa kwa wingi. Vitu hivi havisemi chochote kile mbele ya
Mungu kama havizai matunda. Hivyo siyo sadaka ambazo Mungu anategemea
kuziona toka kwa watu, kwake Mungu vitu hivyo ni kama majani tu, au ni
kama Bethfage tu (matunda yasiyokomaa).
Baada ya kuona maana ya
mandhali ya maandamano, sasa tuwaone wahusika wakuu wa maandamano hayo.
Anapofika Bethfage anawaagiza wanafunzi wake wamletee usafiri: “Enendeni
mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na
mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia
neno, semeni, ‘Bwana ana haja nao,’” Maagizo haya ni ya muhimu sana na
umuhimu wake unaonekana jinsi masimulizi yanavyorudi mara mbili. Mosi,
pale anapowaagiza mitume wake: “mtaona Punda amefungwa, na mwanapunda
pamoja naye. Wafungueni mniletee.” halafu inarudiwa tena inaposemwa.
“Wale wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaamuru (kuwafungua),
wakamleta yule punda na mwanapunda”. Msisitizo upo katika kuwafungua hao
punda na kuwaleta ili waweze kutumika kwa kazi atakayoitaka Yesu
waifanye. Endapo maandamano haya ni ya kampeni za uongozi, basi
yaonekana siri na sera za uongozi huo zimelala katika Punda hao. Kwa
hiyo Punda ndiyo wasanii wakuu wa maandamano ya leo.
Kazi ya
wanafunzi waliotumwa ni kuwafungua punda. Wanyama hawa punda wana maana
gani katika Biblia? Mfalme wa enzi za Wayahudi aliwastaajabia sana
Farasi na wapanda Farasi waliojulikana kuwa hodari kwa kupigana vita.
Kwa mfano, tunasikia kuwa askari wa Farao Farasi na wapanda Farasi wao
wote waliangamizwa baharini. Hivi hata Wafalme wa kiyahudi walikuwa
wanatamani sana kuwa na farasi na wapanda farasi. Katika kitabu cha
Kumbukumbu la Torati, mfalme Salomoni anaonywa asiongeze idadi ya
Farasi, na asiuze ndugu zake kwa Wamisri kwa ajili ya kuwa na Farasi na
wapanda Farasi (askari). Kutembea juu ya farasi ni alama ya ukuu,
uongozi, utawala, ufalme, utajiri na ufahari. Namna ya usafiri unaonesha
hadhi ya mtu.
Siku za leo, tunaweza kupata picha ya magari ya
gharama na ya fahari wanayotembelea marais, mawaziri, wabunge,
makardinali, maaskofu, matajiri, maofisa, nk Itakuwa ni kichekesho na
haiwezekani kabisa kumwona kiongozi wa hadhi kama hizo kusafiri kwa lori
la mkaa, kwa Bajaji au kwa bodaboda, au baiskeli nk. Katika kampeni za
uongozi wa kisiasa, wagombea wanasafiri kwa magari ya gharama za
kutisha, kama vile gari aina ya Prado, VX, Helikopta. Hii ndiyo hadhi
yao.
Kumbe, katika maandamano ya kampeni za Yesu, anamchagua
Punda jike na mwanapunda kuwa prado ya kuingia nayo rasmi mjini
Yerusalemu. Hii ndiyo sera mpya ya utawala na uongozi anaotaka Yesu
kuuingiza ulimwenguni. Ni kiongozi pekee anayefanya hivyo. Marko anasema
kwamba hakukuwahi kutokea mtu mwingine yeyote yule aliyewahi kumpanda
yule Punda kabla: “Mtamwona mwanapunda amefungwa, asiyepandwa na mtu
bado” (Mk. 11:2). Tamko hilo la Marko ni muhimu sana, likimaanisha
kwamba, hakujawahi tokea mfalme au rais yeyote yule hapa duniani,
aliyewahi kujionesha, katika hali kama hii ya utumishi. Yesu ni mfalme
wa kwanza na wa mwisho anayependekeza aina hii mpya ya utawala.
Ili
kuelewa vizuri ujumbe tunaoletewa hapa hatuna budi kuangalia mwishoni
mwa kitabu cha Mwanzo ambako Yakobo anatoa baraka yake kwa watoto wake
kumi na wawili, anapotoa baraka kwa Yuda, ambaye ni mtoto wake wa kwanza
na atakayekuwa kiongozi wa kabila la Israeli, anasema: “Fimbo ya enzi
haitaondoka katika Yuda, wala mfanya sheria kati ya miguu yake, hata
atakapokuja Yeye, mwenye milki, ambaye mataifa watamtii. Atafunga punda
wake katika mzabibu, na mwanapunda wake katika mzabibu mzuri.” (Mwanzo
49:10-11). Sisi hapa tuko mbele ya kituko hicho cha Yesu anayemfungua
punda na mwanapunda kama rejea ya Yuda, yaani yule ambaye ataingiza sera
za uongozi, utawala mpya ambao hautakuwa na mwisho. Sasa amefika yule
ambaye ni kiongozi mpya wa taifa.
Yesu anasema: ‘Wafungueni
mniletee’ Wasanii wakuu tunaoletewa hapa leo, wanayo tabia ya pekee
sana. Mnyama huyu anafugwa na kuthaminiwa na binadamu hasa kutokana na
tabia yake ya kufanya kazi. Kutokana na tabia hiyo, mnyama huyu anayo
majina mengine mengi sana yanayowakilisha udundaji wake wa kazi, wengine
wanamwita, Nsikiri, Kihongo, Daqwai, Mbunda au Punda nk. Ukitaka
kumsifia mtu anayefanya kazi sana wanasema: “Anafanya kazi kama
kihongo.”
Hivi Punda ni alama ya kazi, utumishi, na uvumilivu,
hachoki kamwe, daima yuko tayari kubeba mizigo. Tabia hii ya Punda ndiyo
ilimvutia Yesu hadi akamchagua kuwa mfano wa kuigwa na kipeo cha
utumishi ambao unawakilishwa katika nafsi ya kila mtu. Sisi tunashangaa
tunapomwona Yesu anajilinganisha na Punda. Kumbe, yeye alitaka daima
ajioneshe kama mtu wa kutumikia. Kwa hiyo anapoagiza “wafungueni Punda”
anamaanisha kuwa, Punda hao walikuwa wamefungwa, na katika hali hiyo ya
kufungwa hawawezi kufanya kazi. Ilibidi kwanza wafunguliwe ili waweze
kufanya kazi.
Kila mmoja wetu anao uwezo wa kufanya kazi na
uwezo wa kutumikia. Tunayo hali hiyo kutokana na kufanana kwetu na Mungu
katika upendo. Upendo ni zawadi kwa maisha yetu maana yake ni kuwajali
wengine, yaani kutumikia. Ndani yetu sisi tunaye huyu Punda, Kihongo,
Nsikiri nk. Kwa hiyo, endapo punda hao ni sisi, basi yabidi tufunguliwe
tuwe huru kufanya kazi yaani, kutumikia, kuvumilia, kunyenyekea, kuwa
tayari daima... Yaani tunao uwezo wa kutumikia, lakini daima tumejifunga
hatutaki kujifungua ili tuwe huru kutumikia, badala yake tunataka daima
kutumikiwa.
Yesu anawapa wanafunzi wake kazi: “Enendeni mpaka
kijiji kile kinachowakabili, mtaona Punda amefungwa, na mwanapunda
pamoja naye. Wafungueni mniletee”. Kazi ya wanafunzi ni kuamsha nguvu ya
kutumikia iliyo ndani yetu, kuifungua na kumpelekea Yesu.
Yesu
anaongeza kusema: “na kama mtu akiwaambia neno, semeni, ‘Bwana ana haja
nao’”. Maana yake akitokea mtu fulani anakataza au anaonesha kupinga.
Mtu huyo si mwingine bali ni mimi ninayesema: Tafadhali uniache huru,
Usimfungue punda aliye ndani mwangu. Lakini Yesu anakuhitaji anasema:
“Nina haja nawe,” kwa sababu kwa njia ya ushirikiano wetu, Yesu anaweza
kuanzisha utawala wake duniani kwa kishindo, lakini siyo utawala wa
kukandamiza, bali wa utumishi, wa upendo, na wa haki. Yesu anahitaji
mchango wa kura ya moyo wako kwa kadiri ya uwezo wako yaani ujifungue,
uwe huru, ujiruhusu, kuwa na haki na upendo wa kutumikia, kuwa tayari
kusaidia wengine kusudi kuunda uongozi mpya.
Nabii Zakaria
anasema: “Tazama, (Yerusalemu) mfalme wako anakuja kwako, mpole, naye
amepanda Punda, na mwana Punda, mtoto wa Punda.” Nabii anasema, mfalme
huyo haendi vitani kama mpanda-farasi, bali amepanda punda ambaye ni kwa
ajili ya kazi ya kutumikia. Kwa hiyo mfalme (kiongozi) huyo anakuja
kutumikia. Wanyofu ndiyo watakorithi ulimwengu huu mpya.
Baada ya
kuipata sera ya Yesu kutokana na aina ya usafiri aliotumia katika
kampeni yake, sasa tuwaone waandamaji katika msafara huu wa Yesu. Punda
walipowasili, “wanafunzi wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu
yake. Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani: wengine
wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.” Vifaa hivi na matendo
ya waandamaji ni muhimu sana katika maandamano haya. Hebu tuyafuatilie.
Tafsiri
halisi ya nguo hapa ingekuwa mgolole au shuka, yaani ni nguo ya binafsi
inayomsitiri mtu anapoivaa au hata kujifunika anapolala. Kadhalika kwa
Myahudi, hiyo ilikuwa ni nguo yake binafsi. Ni sawa na vazi binafsi
ambalo mtu huwezi ukalitoa kwa yeyote. Unaweza ukagawa kitu kingine
lakini siyo shuka ya kujifunika au mgolole wa kujitanda. Kwa hiyo nguo
hizo ni alama ya utu wa mtu, nafsi yake, uwepo wake na kila kitu chake.
Wanafunzi
wanaweka au kutandika shuka na migolole yao juu ya Kihongo na mtoto
wake, inamaanisha kwamba wao wanayatoa maisha yao na kila kitu ikiwemo
utajiri wao, kwa utumishi unaopendekezwa na Yesu kutokana na tabia ya
huyo Kihongo. Yesu anaikalia hiyo migololi ya wanafunzi hao kuonesha
kuwa wako chini ya utawala ambao Yesu ndiye mfalme wake. Wanakubaliana
na uongozi huu pamoja na sera zake. Yesu mwenyewe akiwa mnyofu,
mnyenyekevu, mpole na mtii anasafiri juu ya Punda aliye mvumilivu,
mfanya kazi, mtumishi tu na anakaa juu ya migololi hii ya wanafunzi.
Wamepokea, na kuukubali uupya wa masiha huyu, mtumishi na mleta amani.
Ndiyo maana ya kuweka migololi yao juu ya Punda.
Watu wengine
wengi pia wanajitokeza kushangilia: Watu wengi katika ule mkutano
wakatandaza nguo zao njiani: wengine wakakata matawi ya miti,
wakayatandaza njiani.”
Watu hao wanafanya mambo tofauti na
wanavyofanya wanafunzi. Wanafunzi wanatandika migololi yao juu ya punda
kuonesha kwamba wao ndio wanaoendeleza sera za mtindo huo wa uongozi.
Watu wengine kumbe wanatandaza nguo zao njiani au barabarani.
Kiutamaduni ilikuwa kwamba, wakati wa kumtawaza kiongozi, watu walikuwa
wanatandaza nguo ardhini na kushangilia ikiwa na maana kwamba walikuwa
wanakubali kujitoa na kujiweka chini ya uongozi wa huyo mfalme.
Katika
nafasi hiyo watu walikuwa wanashabikia na kupiga vigelegele lakini mara
nyingi hawakuelewa sera za uongozi huo. Katika kundi la maandamaji wa
leo yaonekana kulikuwa na wapambe wengi sana: “Watu wengi katika ule
mkutano wakatandaza nguo zao njiani, na wengine wakakata matawi ya miti,
wakayatandaza njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata,
wakapaza wauti wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarakiwa, yeye
ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.” Watu hawa wote walikuwa
wanamshabikia mfalme huyu lakini pengine kadiri ya sera walizokuwa
wanazifikiria wao.
Wanampokea lakini kadiri wanavyoelewa wao aina
ya Mfalme wanayemtegemea. Ni tofauti na mitume wanaoweka nguo zao juu
ya punda. Hata katika mazingira yetu ya sehemu mbalimbali yaweza kutokea
wachache wanaoelewa maana ya utumishi ya kumfuata Yesu na watu wengine
wakabaki ni wapambe na mashabiki tu. Watu hao wanakata na matawi ya miti
kushangilia.
Kuhusu matawi ya miti, kunakumbushia Sikukuu ya
Vibanda. Siku hiyo waliyakata matawi ili kusherekea kumbukumbu ya
kukombolewa toka utumwani Misri. Hapa sasa wanakata matawi kuonesha kuwa
sasa wanao uhuru kwa sababu Masiha amefika. Lakini Masiha huyo
wanayemdhani ni wa aina gani? Hapo tunaona ukweli wa usemi kwamba
“katika msafara wa mamba kenge nao hawakosekani.” Watu waliendelea
kuimba “Mwana wa Daudi” lakini ni mwana wa Daudi wanayemtegemea wao.
Katika
sikukuu hii ya Matawi tunaalikwa kujihoji upya ushirika wetu na Kristu.
Endapo tunataka kidhati kuwa washiriki wa ufalme mpya anaotupendekezea
Yesu yabidi tumfungue punda aliye ndani mwetu ili kuwa na uwezo wa
kupenda ambao Mungu ametupatia. Tuwe Punda, Kihongo au Nsikiri
aliyefunguliwa na kukubali kumbeba Kristu, yaani kutumikia kwa upendo.