Ndugu
msikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, tulianza maandalizi
ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu
kwa kukufanualia maeneo muhimu katika historia na maisha ya Yesu.
Tumekwishatembelea Bethlehemu mahali alipozaliwa Yesu, tukavuka ng'ambo
ya pili ya Mto Yordan, mahali alipobatizwa na leo tuko chumba cha juu,
mahali alipoweka Ekaristi Takatifu na kuwataka wanafunzi wake wawe ni
watu wa huduma! 
Karibu
Wainjili wote wanatupatia maelezo ya karamu ya mwisho. Katika chumba
kilicho juu. Wainjili wanasema kwamba karamu hiyo ilikuwa ya Agano Jipya
na la milele.
Katika mazingira hayohayo ya kula Yesu akawaosha
miguu wafuasi wake. Kila mwenjili anajitahidi kutoa fundisho la pekee
kadiri anavyoona yeye. Hapa sisi tufuate maelezo ya mwinjili Luka. Sote
tunafahamu kilichotokea siku ile ya karamu ya mwisho. Maneno ambayo Luka
anayoyatumia na ambayo yabidi kuyafanyia tafakuri ni yake tunayoyasikia
katika kila misa: “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” Ni mwinjili Luka
peke yake anayesema maneno hayo.
Lengo la Yesu lilikuwa ni
kuwaalika wafuasi wake wote kumkumbuka Yeye, yaani daima kurudia kufanya
kitendo hicho. Lakini zaidi pia aliwataka wamege mkate na kula ikiwa
kama alama ya msingi katika imani yetu. Tendo la kumega mkate ni
ufupisho wa maisha yake yote toka kuzaliwa hadi kufa kwake. “Mimi
nimejifanya chakula ili kuyalisha maisha.” Ni kama vile angekuwa
Bethlehemu inayotembea (mobile bakery).
Luka anataka kutuambia
kuwa mnapokuwa katika karamu hii, au mnapokula chakula hiki, mnafanya
uchaguzi kama wangu wa kujitoa na kujitolea. Huo ni mwaliko wa kuwa kama
Kristu, wa kuwa mkate na kujigawa kwa wengine. Kwa hiyo haitaeleweka
kabisa kumwona mkristu baada ya kuadhimisha ekaristi, anashindwa
kusaidia wengine.
Hali halisi nyingine inayoonekana humo
chumbani, wakati wa sherehe hiyo kuliibuka mabishano mazito hasahasa
tungeweza kuyaita mahojiano makali kati ya mitume. Kisa walikuwa
wanabishana juu ya ukuu, juu ya kuwa na heshima na cheo kati yao “ni
nani anayehesabiwa kuwa mkuubwa.” Yesu akawaambia: “Wakuu wa mataifa
huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu
ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye
kuongoza kama yule atumikaye. Mimi niko kati yenu kama atumikaye.” Haya
tena ni maneno yanayoletwa na Luka peke yake wakati huu wa mlo. Ni
maneno kwa ajili ya kila mtu hasahasa yule anayejiita mkristu. Hayo
ndiyo mambo yanayoharibu jumuia za kiristu siku za leo. Kazi ya mtu
aliyeshiba ni kutafuta cheo.
Mahojiano hayo ya mitume hayakuishia
kwao tu. Mabishano hayo yameletwa hapa kuonesha kuwa yanaweza kumpata
kila mmoja katika maisha yake. Hasa kuhusu kujihoji wewe mwenyewe kuhusu
kuchagua mambo. Hali kadhalika Yesu Kristu katika maisha yake hapa
duniani alikabiliwa na changamoto hii ya kujihoji nafsini mwake.
Mahojiano
hayo ya Yesu tutayaona baada ya karamu ya mwisho akiwa kwenye mlima wa
Mizeituni. Tunaambiwa kuwa alipatwa na uchungu sana ambao katika Injili
ya Kiswahili wanafasiri kuwa ni dhiki. “Yesu akatoka akaenda mpaka mlima
wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; ...akajitenga na mitume
wake… huko akasali... kwa vile alikuwa katika dhiki... hari yake ikawa
kama matone ya damu yakidondoka nchi.”
Alikuwa katika katika
dhidi au tuseme alikuwa na hali mbaya sana. Yaani ni kama hali ile
anayokuwa nayo mtu kabla ya kufa. Neno hili uchungu pia limetokea katika
injili ya Luka peke yake, kwa kiingereza ni "Agony". Maana halisi ya
neno hilo agoni lamaanisha mapambano, mashindano au mahojiano makali.
Hasa mashindano kama yale ya wanariadha. Yesu aliingia katika mashindano
kama hayo.
Toka mwanzo wa maisha yake, Yesu ilimbidi aingie
katika mapambano na mashindano na nguvu za shetani. Mapambano hayo
hayakwisha katika vishawishi, yaani pale shetani alipomjia Yesu jangwani
mara tu baada ya kubatizwa. La hasha, baada ya vishawishi vile
tunasikia kuwa shetani alimwacha Yesu kwa muda. “Basi alipomaliza kila
jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.” (Lk. 4:13). Shetani
anakuja tena akijua kwamba hapa sasa ni lala salama!
Hapa kuna
mapambano makali ya roho yanayomdai Yesu kuwa mwaminifu na inabidi
kuyashinda. Yesu anashinda! Kuonesha kwamba hayo yalikuwa ni mashindano
makali, Yesu anatoka jasho, hilo kama vile jasho linalomtoka mwanariadha
wakati wa mashindano. Kwa hiyo "agony" siyo uchungu bali ni mapambano,
kuvutana, ukinzani, ugomvi ndani ya mtu. Mapigano yaliyoko ndani ya mtu.
Katika mapambano hayo Yesu anajiandaa kwa kujitenga na kusali.
“Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti
akaomba.” Anajiweka katika mahusiano na Mungu ili kuweza kuiona mipango
ya Mungu. Anajiweka katika mahusiano na Mungu, ili kujua Mungu anao
mpango gani kwa ajili yake. Yesu alisali sana na akawahimiza mitume wake
kukesha na kusali. “Alipofika mahali pake aliwaambia: ‘ombeni kwamba
msiingie majaribuni. Ondokeni, mkaombe msije mkaingia majaribuni.” Sala
inamsaidia Yesu. Kisha wanafika malaika kumliwaza. Hiyo ni alama ya kuwa
na mawazo ya ndani ya Mungu. Endapo alifikiria kutoroka maisha,
kutoroka mateso sasa anaimarika, na kuhiari kuurekebisha ulimwengu. Kwa
hiyo ili kushinda mapambano ya ndani ya mtu, yabidi kusali sana.
Kuunganisha mipango yako na mipango ya Mwenyewe Mungu.
Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican inakutakia hija njema na Baba Mtakatifu
Francisko huko Nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014
kwa kuongozwa na kauli mbiu " Wote wawe wamoja".
Imetaraishwa na
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
Jina
hili Bethlehemu linatokana na maneno mawili ya Kiebrania, Bet ni nyumba
na Lehem (lexem) ni mkate, kwa hiyo Beth-Lehem au bet-lexem maana yake
nyumba ya mkate. 
Kwa
lugha ya kigiriki cha zamani walitamka Bethleem. Ziko sehemu nyingi
zenye nyumba ya mkate mathalani Beth-lehem-ephratah, Bethlehemjudah,
lakini Bethlehemu iliyokuwa kusini karibu na Yerusalemu ndiyo iliyokuwa
inaitwa Bethlehemu katika mji wa Daudi. Hapo ndipo alipozaliwa Yesu. Ni
mji ambao toka zamani wameishi wakristu wengi, lakini sasa wanaishi pia
watu wa dini mchanganyiko. Sehemu hii wanafurika wahaji na watalii wengi
sana hususani wakati wa Kipindi cha Noeli.
Kisa cha kujulikana
Betlehemu kilianza na safari ya Yosefu na Maria aliyekuwa na baraka
tumboni. Walienda huko kwa ajili ya senza. Katika pilikapilika za
kutafuta mahali pa kulala mama akajifungua mtoto wake hapo Betlehemu mji
wa Daudi (Lk. 2:4). Baada ya kuzaliwa, mtoto huyo akaviringishwa nguo
za mtoto mchanga na kulazwa kwenye hori la kulishilia wanyama.
Hii
ndiyo alama ambayo malaika waliwapa maelezo wachungaji na kuwaagiza
waende huko kumwona mtoto. Malaika wakawaambia wachungaji: “Leo katika
mji wa Daudi amezaliwa kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristu Bwana. Na
hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto,
amelala katika hoi ya kulia ng’ombe.”
Kumbe yawezekana malaika
walikuwa wa kwanza kufika hapo Betlehemu na kushuhudia mambo yalivyo
kabla ya kwenda kuwahabarisha wachungaji. Tunaambiwa pia kwamba mara tu
baada ya malaika kuondoka, wachungaji nao wakaambizana wenyewe, Jamani
tusiilazie damu taarifa hii ya malaika: “Twendeni mpaka Betlehemu,
tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.” (Lk. 2:15). Baada ya
kumwona mtoto wakaanza nao wakaanza kutawanya habari: “Walipomwona
(mtoto Yesu) wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Halafu wote
waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.” (Lk 2:27).
Malaika walipoona utukufu umetua Bethlehemu, hawakuuacha utulie
tu pale pangoni, bali wakaondoka kwenda kuutangaza kwa wachungaji. Kwa
hiyo utukufu haukuhusu pango ila unawahusu wachungaji wanaowakilisha
wanyonge wote. Wachungaji ndiyo wanaodhihirisha utukufu wa Mungu. Mungu
anajidhihirisha na kutukuzwa pale tu ambapo wanyonge, fukara
wanapofurahi. Huo ni utukufu wa Mungu.
Wachungaji wanafurahi kwa
sababu kutokana na hali halisi ya unyonge wao, walijisikia kama watu
waliolaaniwa, kwa hiyo hawakutegemea kabisa kupata mawasiliano na Mungu.
Kumbe amezaliwa mchungaji mwenzao, anayejua unyonge wao. Hawakujiamini
wenyewe, na mara moja wakaanza kushauriana wenyewe na kuchukua maamuzi
ya kwenda kushuhudia na baadaye kutoa ushuhuda.
“Twendeni mpaka
Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.” Wanaenda
haraka, kushuhudia utukufu wa Mungu, ambao ni kutaka watu wapate furaha
haraka. Kwetu sisi tungetegemea kusikia mambo ya ajabu zaidi au hata
kusikia muujiza. Hakuna maelekezo zaidi, ni kama vile amezaliwa mtoto wa
kawaida. Maisha ya kawaida yanaendelea. Yesu kuwa Mungu hakutegemei
muujiza wa pekee, bali yeye mwenyewe jinsi alivyo. Yeye ni kama sisi,
Mungu amekuwa mwenzetu. Anayemtegemea Mungu wa kufanya miujiza, ujue
mungu aina hiyo ni mungu wa kipagani.
Wachungaji wanaenda
Betlehemu na wanamwona mtoto aliyeviringishwa nguo. Hiyo ndiyo picha
mpya ya Mungu anayejidhihirisha kwa binadamu. Watoto waliviringishwa
nguo ili kuwakinga na baridi lakini pia inayo maana ya kidini. Mtoto ni
safi, hivi huwezi kumshika tu kwa mikono, lakini kuna maana pia muhimu
ya kiroho, hasa mwinjili anaposisitiza jinsi mtoto alivyoviringishwa
nguo, hoja kubwa ni kusudi mtoto huyo aweze kuguswa, kushikwashikwa na
kubebwa na watu wote.
Aidha imeandikwa mara tatu kuwa aliwekwa
katika hori la kulishia chakula wanyama (ng’ombe). Kwa hiyo msisitizo
huo unahusu chakula. Mtoto aliviringishwa nguo, kama vile mkate
unavyoviringishwa karatasi au majani na kuwekwa kwenye nyumba ya mkate
(Bethlehemu). Kwamba Yesu anadhihirishwa hapa kama mkate yaani chakula.
Malaika wanawaelekeza wachungaji kwenda kwenye nyumba ya mkate
(bethlehemu) huko watauona mkate umeviringishwa.
“Na hii ndiyo
ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala
katika hoi ya kulia ng’ombe.”Yesu aliishi na kuhitimisha historia ya
maisha yake hapa duniani akijionesha mwenyewe daima kuwa ni mkate utokao
mbinguni. Maisha yake yote akayatolea hadi chembe ya mwisho ya mkate.
“Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha
Bwana.”
Wachungaji wanapofika pangoni wakamwona Maria, Yosefu na
mtoto mchanga amelala horini. Hawaoni cha pekee zaidi. Kisha wakatoa
taarifa juu ya kile walichoambiwa juu ya huyo mtoto. “Walipomwona (mtoto
Yesu) wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Halafu wote
waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.” Nadhani
watu wote walishangazwa na taarifa hizo kwani ni Mungu aina gani
anayeweza kuwatokea watu wanyonge kama wachungaji. Kama ndivyo basi hayo
ni maajabu.
Tunaambiwa jambo jingine lililotokea pale Bethlehemu
ni kuwa Maria akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.
Neno kufikiri, siyo tafsiri sahihi, kwa kigiriki “sinmbalus” inamanisha
kuweka mambo pamoja na kutafakari, hasa kule ambako mmoja unapoona mambo
lakini unashindwa kuyaelewa. Maria anatulia, anaangalia, anaunganisha
mambo anaweka pamoja mambo yanayomtukia. Atakuja kufahamu atakapokuwa
amesimama chini ya Msalaba.
Wachungaji wanaondoka wakimshukuru na
kumsifu Mungu – wameyaona maisha mapya. Wamemwona Mungu aliyejifanya
binadamu na kulingana na watu. Wamemwona Mungu anayejiacha
kushikwashikwa na watu wenye mikono michafu, watu wanaonuka, yaani
wanyonge, maskini, wazee, wenye dhambi, walalahoi. Watu hawa wanyonge
wameona na wanafurahi, wanamshukuru na kumsifu Mungu, kisha
wanamshuhudia.
Kumbe, watu hawa wanyonge tu ndiyo wanaoweza
kutambua na kushabikia sera hii kubwa ya Mungu kujifanya mtu. Ni watu
kama hawa ndiyo wanaoweza kuwa na furaha, na kusifu na kumshukuru Mungu.
Kwa wataalamu, wakuu, matajiri sera hii haiingii akili na mioyoni mwao.
Ni muhimu hata kwetu kwamba badala ya kujihoji na kufikri nini
tufanye nini katika maisha, baada ya kumwona Kristu tubaki tu kufurahi.
Tumeona tendo kuu la upendo alilotufanyia Mungu. Huo ndiyo mwanzo wa
uchumba kati ya Mungu na binadamu, kati ya Yesu na Kanisa lake. Sisi
tunafunganishwa na Yesu katika upendo. Ndiyo mwanzo wa maisha ya upendo
na ya furaha. Wanaopendana daima wanashika simu mkononi wakisubiri
”message au kupib”, au kuitwa na mpendwa wao ili kuongeana.
Sisi
tukitaka kugundua utukufu na upendo huo wa Mungu tuanza Bethlehemu, na
kuendelea mbele hadi kwenye majitoleo kamili ya Yesu kule Kalvari. Kwa
hiyo ndugu zangu “twendeni na Papa mpaka Betlehemu” tukirudi toka huko
tuwapagawaze watu kwa tutakayoyaona. Hebu sasa tutoke Bethlehemu
kuongozane na Papa hadi mto Yordani.
Imeandaliwa na
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
Katika
dini nyingi iko desturi nzuri ya kiroho ya kufanya hija pahala
patakatifu au sehemu za kihistoria za dini hiyo. Hija hiyo mara nyingi
hufanyika kama moja ya kuadhimisha tukio fulani muhimu linalomhusu mtu
binafsi ili kujichumia neema anayohitaji mhiji au alhaji. 
Papa
pia hufanya hija sehemu mbalimbali kama vile Lourdes, Fatima, Loreto,
Namugongo, Nchi Takatifu, nakadhalika. Hija ya Papa haiwi kwa ajili yake
binafsi tu, bali hasa ni kuchuma neema kwa ajili ya kanisa zima, pia
inakuwa kwa ajili ya kuimarisha mahusiano ya kuletesha haki, amani na
upendo kati ya nchi na nchi.
Mwaka huu kuna jubilei za dhahabu
kadhaa za kikanisa zitokanazo na Mtaguso wa pili wa Vatican. Zaidi pia
ni mwaka wa 50 tangu Papa Paulo VI alipohiji nchi ya ahadi na kuzungumza
na Patriaki Anathagora wa Yerusalemu. Papa Fransis atahiji nchi ya
ahadi ikiwa ni kuadhimisha jubilei ya dhahabu ya hija hiyo ya Papa Paulo
VI. Katika hija hiyo, Papa atakutana na viongozi muhimu wa serikali na
dini, atakutana pia na waumini wenzetu walioko huko.
Papa
atazuru sehemu chache muhimu. Mosi, ataenda Bethlehemu kuzuru na kusali
pahala alipozaliwa Yesu. Ataenda kuzuru na kusali kando ya mto Yordani
alikobatizwa Yesu. Mwisho ataenda kuangalia chumba ambacho Yesu alikula
Karamu ya Mwisho na mitume wake. Chumba hicho ni mandhali ya mwisho
aliyokuwa Yesu kabla ya kuteswa na kufa kwake.
Kwa hiyo, Wakristu
wote na watu wote wenye mapenzi mema tunaalikwa mosi, kuiombea hija hii
ya Papa, kusudi asafiri salama, aende akatuombee na kufanikisha
makusudio aliyojipangia kwa faida yake, na kwa manufaa ya kanisa zima na
ulimwengu kijumla, na hatimaye arudi salama, kusudi Mungu atukuzwe
katika yote.
Pili tunaalikwa sisi sote kutanguzana na Papa kwenda
katika hija hiyo, usikose kuwepo katika msafara huo wa Baba Mtakatifu.
Kutokana na msongamano wa watu na hasa kupanda gharama ya maisha, siyo
wote watafanikiwa kwenda hiyo hija. Tunaalikwa kukata tiketi ya kiroho
ambayo gharama yake ni bure sanasana inategemea uhuru wako mwenyewe, na
mkatishaji tiketi ni Roho Mtakatifu mwenyewe ambaye hata Yeye mwenyewe
ataenda kwenye hija hiyo ya awali tangu atoke huko alipokufa Yesu
Msalabani. “Akainama kichwa akaitoa Roho yake”.
Kwa watakaoenda
huko kwa tiketi ya Roho Mtakatifu, mnaalikwa kusoma ramani hii au
mwongozo ufuatao, utakaowasaidia kujua sehemu mbalimbali mtakazotembelea
na kuzihiji pindi mnaongozana na Papa. Hizo ni sehemu muhimu ambazo
kulifanyika mambo makuu na mazito yahusuyo ukombozi wetu. Katika
mwongozo huu tutajaribu kuzieleza kwa kifupi sana sehemu hizo
kijiografia na kiteolojia. Tutaona pia matukio yaliyotokea sehemu hizo,
yahusuhuyo Yesu au mitume wake na sisi tunaweza kupata fundisho gani
toka sehemu hiyo.
Hebu twendeni kwanza Betlehemu alikozaliwa
Yesu tuhimizane kwenda huko kwa maneno ya Wachungaji waliokuwa
wanahimizana kwenda huko baada ya kupata taarifa toka kwa malaika:
“Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha
Bwana.” (Lk 2:15).
Imeandaliwa na
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
Kuna
msemo ulioshamiri sana kwa Waswahili, hasa ikiwa mtu anayo matumaini ya
kupata kitu katika biashara na anakikosa anaambiwa: “Imekula kwako”.
Usemi huu ungeweza pia kutumika kwa mitume baada ya kifo na kuzikwa kwa
Yesu. Mitume na wafuasi waliweka matumaini yao yote kwa Yesu, lakini
sasa baada ya kufa kwake na kupita siku mbili tatu, wanakata tamaa na
kujisikia “imekula kwao.”
Wengi wao waliingiwa na woga na
kujifungia kwenye vyumbani, ili mradi tu kwamba walikuwa wameishiana na
mradi wa kumfuata Yesu. Wengine baada ya kwisha tu sikukuu ya Pasaka ya
kiyahudi siku iliyofuata kila mmoja akaanza kuchukua njia zake. Wafuasi
wawili walitanguzana mmoja hatajwi jina na mwingine anaitwa Kleopa
wakachukua zao kurudi kijijini Emmaus. Wamepoteza muda mrefu wa
kutumaini, wa kujitoa, myaka mitatu ya ushindi mkuu, miaka ya imani, ya
kusubiri, ya uzuri, miaka utamu ya mwanga. Lakini kifo kile cha Yesu
ndicho kilichochafua kila kitu. Ama kweli imekula kwao!
Wafuasi
hawa wawili walijisikia kuwa kama miali ya moto inayokaribia kuzimika.
Hebu tuone jinsi Bwana mfufuka anavyoihuisha tena: Wafuasi hao
wanatembea kwenye barabara kuu wanayopita watu wote, wakiwa katika
huzuni kubwa, katika upweke, wakijadiliana. Yesu hawaiti toka mbali na
kuwasimamisha, bali anawasogelea kama mtu mwenye haraka lakini anayetaka
kutanguzana nao. Wao wanageuka na kugundua kwamba kuna mtu anawafuata.
Hapa Yesu amejionesha kama msafiri wa kawaida tu ila mwenye haraka. Yeye
mfufuka angeweza kusafiri kwa mwendo wa kasi sana, kumbe anatanguzana
nao, anapima hatua zao zilingane na mwendo wao wa kuchoka, mwendo wa
waliojeruhiwa.
Wanaelekea Emmaus, yaani anatanguzana nao katika
kuchanganyikiwa kwao na katika matatizo na uchungu wao. Ndivyo Yesu
anavyokutana na watu mbalimbali hapa duniani na kutanguzana nao katika
safari yao ya maisha. Kila mmoja anamkuta akiwa na hali fulani ya pekee.
Tunasikia kwamba Magdalena alimkuta akiwa analia, kwa wale kumi
na mmoja kule kwenye ziwa jumapili ijayo, anawakuta wana uchungu na
wamechanganyikiwa baada ya kukesha usiku mzima wakivua bila kupata kitu,
wakati Tomaso jumapili iliyopita alimkuta katika hali ya kutoamini.
Wafuasi hawa anawakuta katika lindi la uchungu na la upweke. Wako wawili
tu, lakini sasa wanakuwa wasafiri watatu.
Katika uchungu wao huo
wanajadiliana na kuhubiriana juu ya suala zito na muhimu la maisha.
Wanaongeana juu ya jambo linalowakereketa kabisa ndani ya mioyo yao.
Wafuasi hawa wanazungumza juu ya Upendo. Yaonekana amewakimbilia, na
kuwakuta ili kuwapa moyo, kuwahimiza na kuwangaza. Hawakatishi
mazungumzo yao: Anatafuta mwanya wa kujiingiza katika mazungumzo yao kwa
utulivu, kwa utamu kwa kuuliza swali jepesi na rahisi tu.
Tena
anauliza kama vile mtu mjinga asiyefahamu kilichotokea. “Ni maneno gani
haya mnayosemezana hivi mnapotembea?” Kwa swali hili Yesu anaonesha
kuujali sana uchungu wao.
Swali hilo linamfanya Kleopa na
mwenzake waanze kumshangaa. Yaani msafiri mwenzao aliyetokea upande
wanakotokea wao kuwa hajavisikia vituko vilivyotokea huko Yerusalemu.
Habari
hizo zimevuma mji mzima na watu wote wanavizungumzia sana.
“Inawezekanaje, wewe unayetoka sasa hivi huko mjini usisikie habari hii
ya kusikitisha?”
Angekuwa mtu mwingine yeyote angeweza
kuwasimamisha na kuwaambia: “Kaeni chini hapa niwaeleze kinaganaga cha
mambo yalivyotokea.” Kumbe Yesu ameanza kwa kuwaamshia hamu ya kujieleza
zaidi hadi wanamgeuzia kibao: “Hivi wewe peke yako ni mgeni asiyejua…”.
Huwezi kujua ni jinsi gani Yesu alilipokea swali hilo la wafuasi. Swali
hilo la wafuasi linaonesha waziwazi vionjo vilivyokuwa vimejaa ndani ya
mioyo yao. Hadi hapo ilimtosha kabisa Yesu kujisikia kuaminiwa na watu
hawa. Kleopa aliyekuwa katika hali mbaya ya kukata tamaa, na aliyejaa
jazba, amefanikiwa kujimwaga mbele ya mgeni huyu.
Yesu anawaacha
waendelee kujimwaga. Bila kujitambua wakaendelea kujieleza hadi kufikia
kuzungumza mambo ya kiroho waliposema: “Mambo ya Yesu wa Nazareti,
aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za
Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu
walivyomtia katika hukumu yak ufa, wakamshulibisha… Tena wanawake kadha
wa kadha wa kwetu walitushitusha waliokwenda kaburini asubuhi na mapema,
wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika
waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda
kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye
hawakumwona.” (Lk 24:19-20, 22-24).
Hapa unaona kama vile
wamechanganyikiwa. Yaani, wanaonekana kwa upande mmoja kama vile
wanasadiki lakini halafu kwa upande mwingine hawasadiki. Watu hawa
wanateseka sana kisaikolojia lakini walikuwa bado na imani mioyoni
mwao. Kwa hiyo Yesu anawaambia: “Enyi wenye mioyo mizito ya kuamini yote
waliyoyasema manabii!” (Lk.24:25).
Yaani, hawa walikuwa watu wa
kutibiwa, siyo wa kuwalaani, watu wa kuwasahihisha na siyo kuwaachilia
tu, watu wa kuwapoza siyo kuwagombeza! Baada ya kuwatulia kidogo, Yesu
anaanza kuwapa dawa ya tiba. Anaanza kuwaelezea historia ya mambo
yaliyokuwa kadiri ya Maandiko matakatifu hadi wanakaribia kijiji cha
Emmaus.
Baadaa ya kumaliza kuwaeleza, Yesu angeweza kusema:
“Sasa jamani baada ya kuwaeleza haya yote, tafadhali rudini Yerusalemu
na mkawahabarishe wenzenu haya niliyowaambia ili msikose tena imani.
Yesu hafanyi hivi badala yake anajifanya kama vile anapitiliza na
kuendelea na safari zake. Hahitaji chochote, wala haulizi chochote, na
wala hategemei chochote toka kwao. Ndiyo maana hawa wasafiri wawili
wanaamua kumshawishi: “Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana
unakwisha.” (Lk 24:29). “Mgeni afike mwenyeji apone”. Je, sisi tumwambie
nani “Kaa pamoja nasi”?
Tunaweza kumwambia mtu aliyetutendea
jema fulani “kaa nasi”, au mgeni yule ambaye hatutii hasara, mtu
asiyekuwa mzigo. Wageni namna hiyo wako wachache sana na pengine hawako
kabisa. Kumbe Yesu aliye Mungu hahitaji chochote. Yesu aliyesukumwa na
upendo mtupu hataki kumtuliza tu mtu. Hatukani mtu, hasemi maneno yasiyo
na maana, huyu mgeni alitoa maneno ya kuhuisha. Aligusa hata mioyo yao,
aliwatia moyo, hadi wanamkaribisha kwao.
“Wakakikaribia kile
kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea
mbele.” (Lk 24: 28). Katika nafasi nyingine Yesu aliwapita wanafunzi
wake: Mathalani kwenye mto Yordani, au mbele ya Yohane Mbatizaji kule
Genesareti, au usiku ule wa dhoruba. Anapita pembeni ya Kanani bila
kusimama. Anampita kipofu bila kumponya. Yesu anafanya hivi ili mmoja
uweze kumtafuta, au uweze kumwita. Yesu anapenda kuitwa. Wakati mwingine
anaweka hata mazingira ya kuja kwake na matendo yake ili aweze kuitwa
na binadamu. Anavuvia, anadokeza, anashawishi, anahimiza lakini
anasubiri. Wanafunzi wanamwomba atulie, abaki akae nao.
Wao
wanahoja zao kinyume na ukweli ule wa ndani kabisa. Hoja wanayotoa ya
kumshawishi abaki ni kwamba: “kumekuchwa, na mchana unakwisha.” Badala
ya kumwambia kwamba tunapenda kuwa na wewe. Tumeshakupenda, licha ya
kutukosoa na kutusahihisha, na hasa kutokana na hilo tunataka ubaki
nasi. Yesu alilazimisha kwa wema. Alikuwa yeye wa kwanza kuwajongelea.
Sasa wamekuwa wao kutaka kumshikilia asiondoke. Anaingia na katika tendo
la kumega mkate, wanamtambua. Mioyo yao inafunguka: “Ni Yeye” wakasema.
Lakini kabla hawajafanikia kuwasiliana naye, akawa ameshatoweka machoni
pao.
Kumbe, ili aweze kutambulika, haoneshi vyeti vyake vya
utambuilisho, na vyeti vya shule. Anajitambualisha kwa kumega mkate.
Tendo ambalo wanafunzi wake wanamtambua mara moja. Yawezekana walimzoea
akifanya hivyo kila walipokuwa wanakula pamoja. Aidha tendo hilo
alilirudia karibuni tu kwenye karamu ya mwisho alipowaambia: “Fanyeni
hivi kwa kunikumbuka mimi.” (Lk. 22:19).
Hapo hapo wale
wanafunzi wawili wakaanza safari ya kurudi Yerusalemu, wale ambao
walipokuwa wanakuja Emaus walikuwa wamechoka, na kuchanganyikiwa. Sasa
wanarudi kwa mbio wakiwa na kiherehere cha kwenda kuwasimulia wenzao
kwamba Yesu amefufuka, anaishi, na kwamba wao wameonana naye. Waliochoka
kutembea sasa wanakimbia.
Kumbe umoja aina hii na Kristu unaleta nguvu mpya na ari mpya. Tunaalikwa kutanguzana na Kristu katika maisha yetu.
P. Alcuin Nyirenda
Mpendwa
mwana wa Mungu ninakuleteeni tena furaha ya Pasaka kwa njia ya tafakari
ya Neno la Mungu tukiwa tayari Dominika ya tatu ya Pasaka. Ujumbe wa
Neno la Mungu Dominika hii ni ule usemao, "Wakamtambua katika kuumega
Mkate". Katika somo la kwanza toka Kitabu cha Matendo ya Mitume tunapata
kukutana na sehemu ya mahubiri ya Mtakatifu Petro. 
Katika
mahubiri haya Mtakatifu Petro akiwa amejawa na Roho wa Mungu na nguvu
ya Pasaka anatangaza kuwa Kristu aliyedhihirishwa kwetu na Mungu na
kuteswa na kisha kutundikwa msalabani, amefufuliwa na Mungu. Jambo hili
ni la kweli na hakika, kwa maana sisi tu mashahidi. Mtakatifu Petro
anashuhudia hilo akisema tulikula, na tukanywa pamoja naye na si hilo tu
bali tumeshuhudia na kufuata mafundisho yake hadi anapofufuka.
Mpendwa
msikilizaji, Mt Petro analenga kufundisha na kusimika imani katika
Bwana mfufuka na tokea pale kuweza kusonga mbele katika utume kadiri
Bwana alivyoagiza.
Mpendwa mwana wa Mungu, Mtakatifu Petro
anasonga mbele akijaribu kuweka wazi mpango wa Mungu uliojificha katika
kifo cha Bwana. Anakazia na anasema ni kweli kifo chake kilikuwa ni
sehemu ya mpango wa Mungu. Katika hoja hii anajaribu kujibu maswali ya
wale walioona kifo cha Kristu kama kikwazo na hasa wanapofikiri na
kutambua kuwa yeye alikuwa Masiha! Anasema kile kinachoonekana kwetu
kama makwazo na madhulumu kwa Mungu ni ishara ya ushindi! Kwa njia ya
kifo kuna maisha mapya, yaani maisha ya ufufuko.
Katika somo II
toka barua ya Mt Petro, (1Pet. 1:17-21) tunakutana na mwendelezo wa
mafundisho juu ya ubatizo. Anawaambia wabatizwa wapya kwamba sasa wanao
uwezo na nguvu za kumwita Mungu “Baba” kwa sababu wamepokea maisha mapya
toka yeye. Ni zawadi kubwa na nono lakini pia inayo sehemu ya wajibu
mkubwa nao ni kuwa mpya na daima kukaa katika hali ya utu upya!
Mtakatifu Petro anasonga mbele akisema kwa kupata zawadi ya ubatizo na
yote yaambatanayo na zawadi hiyo, mfano kumwita Mungu “Abba” kunatupasa
kutambua kuwa kuna mmoja ambaye amelipia fidia.
Ndiyo kusema si
kwa fedha wala dhahabu bali kwa DAMU YA MWANA WA MUNGU!, Damu ya Kristu
mpakwa mafuta wa Bwana! Damu isiyo na doa la dhambi. Kumbe tumekombolewa
kwa Damu ya thamani kuu mno! Yule kondoo ambaye Waisraeli walikuwa
wakimchinja wakati wa sherehe za Pasaka ilikuwa ni kiashilio cha Kristu
kondoo wa AJ ambaye anajitoa kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu.
Katika
somo III toka Mwinjili Luk 24:13-35, tunapata simulizi la wanafunzi 2
wa Emmaus. Mmoja wa wanafunzi hawa anaitwa Kleopa na mwingine jina lake
halijulikani. Habari njema imewekwa katika mtindo wa katekesi, Ni Kristu
mfufuka anafundisha watu wake na ndio sisi wenyewe na mafundisho ni juu
ya ufufuko wake. Mwinjili Luka anamtaja mwanafunzi mmojawapo kuwa
Kleopa ambaye kadiri ya tafiti za kibiblia alikuwa ni kaka yake na
Yosefu, baba yake mlishi wa Yesu Kristu yaani Bwana.
Mwingine
hatajwi jina, Luka akitaka kuacha nafasi kwa ajili yetu sisi ambao
tunaalikwa kufuata nyayo zake tukimwelekea Bwana Mfufuka. Hawa wanafunzi
wanakimbia toka Yerusalemu kwa maana matarajio yao hayakutimia.
Walitarajia Masiha mshindi, mwenye nguvu, na mwenye kuishi maisha marefu
na badala yake wanamwona akishindwa na kufa akiwa na miaka 33!.
Mpendwa
msikilizaji, ndugu hawa wakiwa katika majadiliano ghafla Bwana
ataingilia majadiliano yao na kuwauliza mnajadiliana nini? Hawa
wanafunzi wawili wanasimama na kukasilika wakishangaa mtu huyu ni nani
asiyejua kilichotokea Yerusalemu? Atawauliza tena kwani kumetokea nini?
Basi
wanafunzi hawa watahadithia habari za Yesu Mnazareti jinsi alivyokuwa
na uwezo mkuu lakini wakuu wa walimtia nguvuni na kumsulubisha!
Wanafunzi hawa wanasema kwa kweli hatuoni tumaini tena na ndiyo maana
tunakimbia! Mara kadhaa hata sisi tunalo tumaini fulani katika maisha,
lakini inapojitokeza hatufaulu basi ni kuanza kulalamika na kukata tamaa
kama ndugu hawa na hata wengine kuliacha Kanisa.
Angalia hali
ya kisiasa kunakuwa na tumaini fulani kwa watu fulani na
wanaponyamazishwa basi matumaini yetu huanguka pia! Hata hivyo mpendwa
unayenisikiliza, mkristu anayeamini katika ufufuko hawezi kukatishwa
tamaa na mikasa inayojitokeza katika maisha bali anasonga mbele kama
Kristu mpaka Kalvari ambapo ndipo kuna ufufuko!
Mpendwa katika
Bwana, wanafunzi wa Emmaus walikuwa na ujuzi juu ya Bwana lakini ujuzi
wao uliishia katika kifo cha Bwana tu, hawakuweza kuendelea mbele!
Hawakutambua kuwa Bwana alikuwa amefufuka na hiki ndicho kisa cha kukata
tamaa, maana kama ni kifo tu, kwa hakika kinatisha na kukatisha tamaa.
Ndiyo kusema nasi wakati fulani tunapoanza safari ya kumtafuta Bwana
tunaishia kwenye kifo pasipo kwenda mpaka ufufuko na hapa ndo kuna taabu
na mikato ya tamaa isiyohesabika! Tunaalikwa kwenda mbele mpaka
ufufuko.
Hatupaswi kuishia katika kumwona Bwana kama mwana
mapinduzi bali kama mwokozi wetu. Tunaalikwa kwenda mpaka ufufuko ambao
huwezi kuufafanua kwa mahesabu bali kwa imani na hapa ndipo kuna hekima
ya Kimungu. Wanafunzi wa Emmaus wana huzuni kwanza kuacha jumuiya yao
ambamo wangeweza kupata majibu ya wasiwasi wao.
Shida nyingine
hawakutaka kufanya utafiti juu Ya kile kilichosemwa na akina mama
waliokwenda makaburini siku ya ufufuko. Pengine waliona kwa kuwa
kimahesabu haiwezekani kukifafanua na hivi wanazama katika dharau na
hili ni ukosefu wa imani! Leo hii katika Jumuiya yetu ya Kanisa kuna
watu ambao kukitokea shida kidogo ni kuanza kukimbia wakifikiria
wataweza kupata majibu na badala yake ni kukumbana na mkato wa tamaa na
udhaifu wa kiroho kukua na kuongezeka. Fundisho katika hili ni kwamba
yafaa siku zote kukaa na jumuiya na kutafuta suluhisho la matatizo yetu
na ya Kanisa ndani ya Jumuiya yetu.
Mpendwa katika Bwana pamoja
na kwamba ndugu hawa wawili wamekata tamaa na wanaujuzi nusunusu juu ya
Bwana, Bwana hawaachi anaambatana nao na kuwasaidia polepole ili waweze
kuelewa nini kilitokea na kwa nini ilikuwa vile. Hata kwetu hivi leo
Bwana anatupa company tunapokuwa katika hali ya kukimbia matatizo na
kukata tamaa. Ndiyo kusema nasi tuwape company kaka na dada zetu wakiwa
katika taabu.
Mpendwa msikilizaji, ndugu hawa pamoja na kwamba
Bwana amewasaidia katika shida yao ya kutoelewa vema maandiko matakatifu
bado wanamwona kama msafiri mwenzao, mwenye shida kama wao. Mpendwa
yatupasa kukazia lengo letu katika maisha, maana yake tukilipoteza hata
mmoja anapojaribu kutueleza akili haipokei haraka.
Katika shida
kama hii Bwana atafanyaje? Kwa hakika anaanza kuwafafanulia maandiko
matakatifu kuanzia AK mpaka AJ linalomhusu yeye mwenyewe na hasa juu ya
mateso hadi ufufuko wake. Ndiyo kusema Kwa njia ya Neno la Mungu mtu
huweza kutambua mafumbo ya Mungu. Hata hivyo pamoja na hilo hawakuweza
kuelewa kitu na Bwana atawakemea kwa mioyo migumu hiyo. Kwa hakika hata
hivi leo shida ya kutoelewa na hasa kutoguswa na Neno la Mungu ipo,
yafaa kuomba sana nguvu ya Roho Mtakatifu kwa ajili hiyo.
Mpendwa
Bwana akiendelea na katekesi yake inafika jioni na anataka kuendelea
mbele wakati wanafunzi wamefika. Basi wanamkaribisha nyumbani walipokuwa
wanaenda na kisha ataketi chakulani pamoja nao na KUUMEGA MKATE na
kuwapatia. Kwa tendo la kuumega mkate macho yalifunguka na wakamtambua
kuwa ni BWANA MFUFUKA na mara atatoweka! Swali linawajia kwa nini
hatukumtambua alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu? Basi mara
moja ndugu hawa walirudi Yerusalemu kwa furaha bila wasiwasi tena na
kutangaza habari njema wakisema tumemwona Bwana mfufuka na kweli
amefufuka.
Mpendwa katika Bwana simulizi la wanafunzi wa Emmaus
kadiri ya Mt. Yustini ni chimbuko la mpango wa Misa Takatifu. Waamini
kuingia mapema katika ibada, hii ni sawa na wanafunzi wa Emmaus kuwa
njiani tokea Yerusalemu, kuingia kwa Padre kwa maandamano ni ishara ya
kuingia kwa Kristu masiha katika majadiliano ya wanafunzi hawa. Mahubiri
ni ishara ya ufafanuzi wa Neno la Mungu uliofanywa na Bwana mfufuka na
Litrujia ya Ekaristi Takatifu yaturudisha katika ishara ya Kristu
kuumega mkate na kuwapa wanafunzi wa Emmaus.
Mwishoni mwa Misa
Padre huondoka kwa maandamano toka kwenye Misa kabla ya waamini wengine,
hii yaturudisha katika lile tendo la Bwana kutoweka mara baada ya
kumega mkate na kuwapatia. Wanafunzi wa Emmaus walipoelewa haya,
walirudi Yerusalemu wa furaha kutangaza furaha ya ufufuko. Mpendwa, wewe
je baada ya kuumega mkate waondoka katika Misa kwa furaha kwa ajili ya
kutangaza kwa wengine au warudi nyumbani kwa huzuni? Tafakari hili!
Nakutakieni
furaha tele katika kipindi chote cha Pasaka na Mungu azidi kuwa nawe,
nawe ukitekeleza mapenzi yake katika Jumuiya ukienda kutangaza habari ya
ufufuko wa Bwana kwa furaha kuu. Tukutane tena Dominika ijayo. Tumsifu
Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya
C.PP.S.
JANA ilikuwa Siku
kuu ya Wafanyakazi Duniani, maarufu kama Mei Mosi ni fursa inayotolewa
na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka kwa wafanyakazi kufanya tathimini ya
kina kuhusu kazi walizotenda, ufanisi na tija katika shughuli za
uzalishaji na utoaji wa huduma pamoja na kujiwekea malengo kwa siku za
usoni kwa kukazia umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau mbali mbali katika
kazi.
Katika mazingira ya utandawazi usiojali mateso na
mahangaiko ya watu, kuna haja ya kuanzisha na kuimarisha mshikamano wa
kidugu unaojengeka katika vyama vya ushirika miongoni mwa wafanyakazi,
kwa kutambua na kuendelea kudumisha sheria, kanuni na usalama kazini.
Mishahara mizuri, mazingira safi na bora ya kazi pamoja na vitendea kazi
vizuri ni mambo ambayo yanaweza kuchangia katika maboresho na ufanisi
kazini sanjari na ukuzaji wa pato la wafanyakazi.
Ubadhirifu wa
mali ya umma, ufisadi, wizi na hujuma kazini ni mambo ambayo daima
yamekwamisha ufanisi kazini na matokeo yake ni watu kuendelea kukomaa
katika ubinafsi na utandawazi wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya
jirani. Siku kuu ya Wafanyakazi Duniani, iwe ni fursa ya kukuza na
kuimarisha sheria za kazi, utawala bora na usalama kazini.
Siku
kuu ya Wafanyakazi imewekwa chini ya ulinzi wa Mtakatifu Yosefu
Mfanyakazi. Siku kuu hii ndani ya Kanisa ilianzishwa kunako mwak 1955 na
Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili. Lengo ni kutambua heshima ya
kufanya kazi kama sehemu ya utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Huu
ni mwendelezo wa kuutiisha ulimwengu, ili uweze kuwa ni mahali pazuri
zaidi pa kuishi. Watu wanapaswa kutambua kwamba, kazi ni sehemu muhimu
sana katika maisha ya mwanadamu kwani ni sehemu ya ubinadamu na matokeo
ya kazi.
Utu na heshima ya mwanadamu ndicho kipimo sahihi cha
heshima ya kazi. Kazi ni wajibu na utambulisho mwa wanadamu na kwamba,
nguvu kazi ina kipaumbele cha kiasili zaidi ya mtaji, kumbe, kuna haja
ya kuwa na uhusiano unaokamilishana kati ya kazi na mtaji, lakini utu na
heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza.
Baada
ya Baba Mtakatifu Francisko kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na
Yohane Paulo II kuwa watakatifu, Jumapili tarehe 27 Aprili 2014 katika
Ibada iliyohudhuriwa na maelfu ya watu waliokuwa wamefurika kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na viunga
vyake, watakatifu hawa wapya watakumbukwa kila mwaka mwezi Oktoba kadiri
ya Kalenda ya Liturujia ya Kanisa.
Kadiri ya Kalenda ya
Liturujia ya Kanisa kwa ajili ya kumbu kumbu ya Watakatifu, Yohane XXIII
atakumbukwa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba. Hii ni siku maalum
ambayo, kwa takribani miaka hamsini iliyopita, Yohane XXIII alikuwa
anafungua rasmi maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, tukio
ambalo limeleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa
katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Hili ni tukio la
kishujaa lililomstahilisha Papa Yohane XXIII kuitwa Mtakatifu.
Mtakatifu
Yohane Paulo II atakumbukwa kila mwaka ifikapo tarehe 22 Oktoba. Hii ni
siku ambayo Papa Yohane Paulo II alipoanza utume wake kama Khalifa wa
Mtakatifu Petro, akaendeleza maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa
Vatican pamoja na kukazia umuhimu wa Mama Kanisa kujikita katika
mchakato wa Umissionari na Uinjilishaji Mpya. Mwezi Oktoba ni mwezi wa
shughuli na mikakati ya kimissionari ndani ya Kanisa.
Tangu sasa
waamini na watu wenye mapenzi mema wanaweza kuwaenzi watakatifu hawa
wapya kwa maadhimisho ya: Ibada, Liturujia pamoja na kuwaweka kuwa
walinzi na wasimamizi wa shughuli mbali mbali katika maisha na utume wa
Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II atakuwa ni
msimamizi wa Siku za Vijana Duniani.
Vijana
wanaalikwa kumwangalia kwa namna ya pekee kabisa yule kijana tajiri
anayesimuliwa kwenye Maandiko Matakatifu aliyemwendea Yesu akiomba
ushauri ili aweze kuurithi uzima wa milele. Mitume wengi walikuwa ni
vijana na walifurahia sana walipokutana na kuzungumza na Yesu, kiasi
hata cha kuwabadilishia mwelekeo wa maisha, kwani waliweza kusikiliza
ufafanuzi wa Neno la Mungu kwa kina na mapana!
Baba Mtakatifu
Francisko katika ujumbe wake wa video kwenye maadhimisho ya Siku ya
Vijana Kikanda nchini Argentina, iliyoadhimishwa, Jumamosi tarehe 26
Aprili 2014 nchini Argentina, katika mkesha wa kuwatangaza Wenyeheri
Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, anawauliza vijana,
jinsi walivyojisikia kwa mara ya kwanza walipokutana na Yesu katika hija
ya maisha yao ya kiroho, Anawaalika kuwaangalia Mitume waliokutana na
Yesu kwa mara ya kwanza katika maisha yao.
Yesu alionesha upendo
wa pekee kwa yule kijana tajiri aliyejitahidi katika maisha yake kushika
Amri za Mungu, lakini akisoka ndani mwake ufukara wa maisha ya kiroho,
ndiyo maana anapoambiwa kwenda kuuza vyote alivyonavyo na kuwapatia
maskini, kisha amfuate Yesu, anashikwa na huzuni kubwa katika moyo wake.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, Maandiko Mataktifu yamesheheni mifano ya
vijana wa kina aina. Anawakumbusha yule kijana aliyeomba urithi kutoka
kwa Baba mwenye huruma, kisha akatokomea mjini kwenda kuponda mali na
baadaye akakiona cha mtema kuni kwa kukumbana na uso kwa uso na baa la
njaa! Hapa akajifunza kutubu na kuongoka, ili kukimbilia tena huruma ya
Mungu. Daima Baba yake alikuwa anamsubiri kwa hamu kubwa, kuona kijana
wake akirudi tena nyumbani. Siku ile aliporejea nyumbani, akamkumbatia
na kumwonjesha tena huruma na upendo usiokuwa na kifani.
Baba
Mtakatifu amewakumbusha vijana wa Argentina kuhusu yule kijana wa Naini
aliyekuwa amefariki dunia baadaye akafufuliwa na Yesu, kwa kumwonea yule
mama mjane huruma? Baba Mtakatifu anawauliza vijana wao wanajisikia
kuwa sehemu gani kati ya vijana wanaosimuliwa kwenye Injili? Je,
wanaonesha ari na shauku ya kuwashirikisha wengine ushuhuda wa kukutana
na Yesu? Au wamekata tamaa na kujikunyata? Au pengine tayari wamekwisha
kupoteza maisha ya kiroho ndani mwao?
Baba Mtakatifu Francisko
anawahamasisha vijana kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa
lake, kwa kutolea ushuhuda wa imani katika matendo, ili kujenga na
kuimarisha amani na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa
lake sanjari na kukumbatia Injili ya maisha pamoja na kuguswa na
mahangaiko ya wengine kama alivyofanya Bikira Maria kwenye arusi ya Kana
na mwishoni akasimama chini ya Msalaba wa Kristo.
Baba Mtakatifu
Francisko anawataka wasichana kuiga mfano wa Bikira Maria na wanawake
watakatifu wanaosimuliwa katika Injili kwa kutolea ushuhuda wa imani yao
kwa Kristo na Kanisa lake, wakimwachia Yesu nafasi ya kuwaongoza, ili
waweze kukua na kukomaa, tayari kuwahudimia Watu wa Mungu katika medani
mbali mbali za maisha.
Baba Mtakatifu amewatakia kheri na baraka
vijana hao katika maadhimisho ya Siku ya Vijana wa Argentina Kikanda,
ili wapate nafasi ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao, bila
kuwa na woga wala makunyanzi, bali wangalie Yesu na Bikira Maria, ili
waweze kusonga mbele, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa
watu wake.
Katika
dominika hii ya pili ya Pasaka, Injili inatuletea aina mbili za
mazingira yaliyo tofauti:Mazingira ya kwanza, Yesu anawatokea wafuasi
jioni ya siku ileile ya Pasaka, wakiwa chumbani pindi mtume mmoja
aitwaye Thomas hakuwepo. Mazingira ya pili, ni siku nane baadaye Yesu
anawatokea tena wafuasi chumbani sasa akiwepo hata Thomas. Mazingira ya
kutokea-tokea kwa Yesu baada ya ufufuko wake ni tofauti hasa ukikumbuka
alivyomtokea mara ya kwanza Maria Magdalena asubuhi ileile ya Pasaka.
Mazingira
aliyomtokea nayo yalikuwa ni ya nje kwenye bustani karibu na kaburi.
Lakini kwa mitume ilikuwa ni jioni tena chumbani milango ikiwa imefungwa
kutokana na woga wa wanafunzi. Mwinjili anataka kutuonesha kwamba Yesu
anafika katika ulimwengu kwa namna ambayo si ya kiyakinifu, ni yeye
lakini siyo yuleyule. Kitu cha muhimu zaidi kukiepa hapa ni matumizi ya
neno hili “kutokea”, kwa sababu neno hili halijatumika kabisa na
mwinjili. Fasuli inasema, Yesu alikuja na kusimama katikati. “Ikawa
jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwa wanafunzi, milango
imefungwa kwa hofu ya Wayahudi: akaja Yesu akasimama katikati,
akawaambia, “Amani iwe kwenu.” (Yoh. 20:19).
Siku ya Pasaka na
siku nane baadaye Bwana anakuja na kukaa katika jumuia yake
iliyokusanyika pamoja, na kama ilivyokuwa kwa wafuasi wale wa mwanzo
siku ya Pasaka kadhalika waumini siku ya Pasaka. Waumini hao hawana budi
kufungua sana macho yao, lakini siyo macho ya kiyakinifu, yanayoangalia
kwa udadisi na kuanisha mambo, bali kwa macho safi, macho ya imani
yanayoweza kuona mambo yasiyoweza kuonekana kwa macho ya kawaida.
Ndivyo
inavyotufundisha Injili ya leo jinsi ya kufungua macho ya imani na
kuangalia Yesu mfufuka anayefika na kukaa kati ya jumuia iliyokusanyika
pamoja. Wafuasi wanashangaa kwa kutokewa na Bwana kwani walikuwa na woga
sana. Wamekusanyika pamoja siyo kutokana na upendo waliokuwa nao kati
yao, la hasha, bali kutokana na woga, kwa vile wanaye adui mmoja
wanayemwogopa yaani wayahudi.
Angalia watu wengine wanaotembea
nje, wanawaacha tu hawa wafuasi wajifungie humo chumbani, wao hawana
wasiwasi wowote kwani ni kesi binafsi ya mitume walioingiwa na wasiwasi
kutokana na yaliyotokea. Hawa wanao woga kwa vile hawajamwona Bwana
mfufuka na kuhuishwa na roho ya mfufuka, hivi wanao woga. Woga huo
unawapata pia wakristu wowote katika jumuia kama endapo wanakuwa hawana
mang’amuzi ya Kristu mfufuka. Hali hiyohiyo inaweza kumkumba kila
mkristu mkereketwa na Kristu kama anakosa mang’amuzi ya Kristu mfufuka
katikati ya ndugu zake.
Woga huo wa Mkristu unatokana na mambo
mawili: Mosi, kuogopa kifo. Mkristu aliyemwona Kristu anayeingia katika
utukufu wa Baba hawezi kuwa na woga wowote ule wa kifo. Anaweza kuwa na
woga wa homa, ugonjwa, mateso, lakini siyo wa kifo. Mtu huyo atasubiri
kama “mlinzi akeshavyo akisubiri kuchomoza kwa jua la asubuhi”.
Kuingia
kwake makaoni kwa Baba yake ambako ni lengo la wote, hakuwezi kumpatia
woga wa kifo. Hata kama woga huo unabaki kutokana na kuachana na wapenzi
wake na vitu mbalimbali ambavyo Mungu ametupatia. Kwa hiyo hapa unauona
woga wa wanafunzi, ambao walikuwa bado hawajamwona Kristu mfufuka.
Woga
wa pili, unakuwa dhidi ya wengine ambao hawakuyapokea mapendekezo haya
ya Yesu hadi wakataka kumfifisha kabisa. Wenye woga aina hiyo hawawezi
kuwa wanafunzi wa kweli, kwani Yesu anawatuma wafuasi wake kama vile
kondoo kati ya mbwa mwitu. Kama unao woga kwa mbwa mwitu, basi ni bora
kutoroka na kwenda mbali kujificha.
Kadhalika woga ni ni kitu
kibaya kupita kila kitu kingine katika imani, kwa sababu unawafanya
wafuasi wa dini kuwa wenye msimamo mkali, hawaambiliki, hawataki
majadiliano, ni wagomvi, ni wachokozi, wanapiga makelele, wanapenda zogo
katika kuitangaza imani yao.
Kwa sababu kama imani yao na
wanachokisadiki kingekuwa cha ukweli na wanakiamini kwa dhati, basi
wasingekipigia makelele, badala yake wangekitangaza kwa furaha na kwa
utulivu. Pengine ingekuwa pia njia ya kujisaidia wao wenyewe ya kuuona
mwanga wa Pasaka. Kwa hiyo yatubidi tujiangalie sana, kwani woga
unatuingiza katika hatari ya kujifungia katika ukweli wetu usio na
msingi wa kuchochewa tu na mapokeo wa mambo yale tuliyozoea kuyatenda,
tunakuwa viziwi mbele ya hali halisi na hivi kujikuta unajihami mbele ya
kosoo ya imani yako, na unakuwa mwoga wa mambo mapya.
Katika
kipindi fulani cha historia ya Wakristu, Kanisa lilikuwa na hofu kubwa
sana wakati Biblia ilipokuwa inamilikiwa na Waprotestanti. Kulikuwa pia
woga wa demokrasia, na ule woga wa kukutana na utamaduni au mila
nyingine ngeni. Woga aina hiyo ni sawa na ule wa mitume wa kujifungia
ndani ya chumba. Yaani unakuwa na woga na mambo ya nje.
Huku
kujitenga na kujifungia ndani ya chumba katika nyumba moja, kuna maana
pia ya kiteolojia: Yohane anataka kuonesha kwamba mbele ya ulimwengu,
wanafunzi wanajisikia katika mazingira mageni, wanayo thamani ambayo si
sawa na zile za ulimwengu. Yesu anasema, ninyi mpo katika ulimwengu
lakini si wa ulimwengu huu. Ndiyo maana wanakuwa na woga.
Aidha,
endapo mmoja anajitangazia kwamba amemwona Kristu mfufuka, anatangaza
imani yake, hivi anaogopa kueleweka kuwa ni kichaa, yaani ni mtu
anayeishi nje ya ulimwengu, kwa sababu watu wamefungwa na mtindo wa
maisha ya ulimwengu huu hawaoni namna nyingine ya maisha. Kwa mfano
Mtakatifu Paulo anapozungumza juu ya ufufuko, watu wanamcheka na
kumwambia waziwazi kwamba “juu ya suala hilo tutakusikiliza tena wakati
mwingine”.
Ni ngumu sana kushuhudia imani yako hadharani. Hata
mapadre, usiku wa Pasaka, hatuwi hata na uso wa furaha wa kuona mwanga
wa ufufuko. Kwamba Yesu yuko na alifika kusimama mbele ya wafuasi. Yaani
mwanzo mpya wa kudumu wa uwepo wa Yesu. Amefufuka na kuonesha mikono
yake na kuwa katikati yao. Anaonesha mikono iliyofanya kazi na ubavu
wake, hiyo ndiyo kadi yake ya utambulisho. Mikono iliyotenda mema na
kupigiliwa misumari na moyo wake uliochomwa mkuki ilipotokea damu
kuonesha maisha na maji kuonesha Roho mtakatifu, maisha yaliyomwagwa
duniani maisha ya Roho yaliyotolewa ulimwengu. Hii ndiyo ID ya Yesu.
Mazingira
ya pili, aliyotokea Yesu ni ya siku nane baada ya ufufuko. Tomasi
hakuwepo pale alipotokea Yesu mara ya kwanza. Huyu Tomasi anaitwa Didimo
maana yake Pacha, “Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomas, aitwaye
Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. .. Basi, baada ya siku nane
wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomas pamoja. Akaja Yesu na
milango imefungwa akasimama katikati , akasema, “Amani iwe kwenu.”(Yoh.
20: 24, 26). Mwinjili anasisitiza sana jina hili Pacha (Didimo).
Yaonekana kuwa huyu ndiye pacha wa kila mmoja wetu. Kwa sababu hata sisi
tutapita safari hiyohiyo ya jinsi ya kumfuata Kristu mfufuka.
Katika
Injili, Thomasi anajitokeza mara tatu: Mara ya kwanza ni pale Yesu
anapotaka kwenda Yudea, alikokufa Larazo, Thomas anasema twende tukafe
sote huko: “Basi Tomas, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe,
“Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.” (Yoh. 11:16). Kwa hiyo ni
kweli Tomasi anayo mang’amuzi ya kifo tu, bali mang’amuzi ya ufufuko
hana kwa sababu hajayashuhudia. Amebakiwa na wazo lake lilelile,
“Twendeni tukafe naye”. Nafasi nyingine ni kwenye karamu ya mwisho, pale
Yesu anapowaambia wanafunzi kwamba kule ninakoenda ninyi mnafahamu
njia. Tomasi anasema, sisi hatujui unakoenda, tutawezaje kuijua njia?
“Nami niendako mwaijua njia.” Tomas akamwambia, “Bwana, sisi hatujui
uendako, nasi twaijuaje njia?” (Yoh. 14:4-5) Huyu ndiye ndugu yetu
Tomas, pacha wetu (Kurwa), kwa sababu anataka kujua. Kuna wakristu wengi
wanaopata taabu ya kuelewa mambo yote katika imani. Anaye pacha wa
Tomasi atauliza, “utuoneshe njia.” Kwani baada ya kuuliza Yesu anaweza
kujieleza: “Mimi ni njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa
njia ya mimi.” (Yoh. 14:6).
Hebu tuangalie ni katika vipengee vipi Tomas anaweza kuwa ni pacha wako.
Hoja
ya mojawapo yaweza kuwa Tomas alikuwa haelewi ni kwa nini wenzake
wamejifungia chumbani. Yeye ameondoka na kwenda kuzubaa sijui wapi kwa
sababu hajisikii kuwa na woga wowote ule. Katika kipengee hiki, Tomas ni
pacha au kurwa wa mtu yule ambaye hajisikii kuwa wa maana au bora zaidi
kuliko wengine, yaani, haelewi ni kwa nini wengine wamejifungia ndani.
Ni
dhahiri kwamba Tomas siyo pacha wa wale wanaojitenga na jumuia ya
kikristu kwa sababu labda wanachekwa na kudharauliwa na wengine;
wanaojisikia bora zaidi na kuwahukumu wengine wasio katika jumuia au
hata wanaowahukumu wale walio katika jumuia kwamba ni waovu kuliko
wengine, au kama wale wanaoacha dini yao na kuingia nyingine.
Tomas
hahukumu, wala kudharau wengine bali yawezekana anajiona kama
amedanganyika kidogo au amekwazika na jumuia ile. Yaani ni kama wakristu
wale wanaoona ndani ya kanisa kuna makwazo au mambo ya aibu, hivi
wanajisikia kukwazika na kuteseka mioyoni mwao. Hivi wanaona ni bora
kujiweka kidogo pembeni.
Aina ya nyingine ya kuwa pacha wa Tomas
ni pale wale ambao wamedanganyika na muundo wa kanisa, na uendeshaji wa
mambo ya kanisa, kukosa mpango mzuri. Hakuna uinjilishaji wa kutosha,
au kuna utawala wa kibabe, kuna kujionesha ukuu unaotegemea mali, na
hivi wanaona afadhali kujiepusha kidogo. Waumini wasioamini kama mambo
yanaweza kubadilika katika kanisa. Hawa ni pacha wa Tomas.
Anapofika
Tomas wenzake wanamhabarisha: “Tumemwona Bwana.” Kwa tamko hili
walikuwa wanataka kummweleza kwamba mambo yamebadilika, si kama
alivyodhani au kama alivyoyaacha. Tomas anataka kuhakikisha yeye
mwenyewe kama kweli mazingira aliyoyaacha yamebadilika.
Hapa sasa
tunakutana na pacha mwingine, yaani wale wanaotaka kuhakikisha kwa
kuona na kugusa. Pacha wa Tomas ni wale wasiomwona Yesu wa Nazareti
lakini wameitwa kumwamini ili kumshuhudia kwa ndugu zao. Pacha ni wale
wasioelewa. Yaani hao pia wameitwa ili kuelewa lakini wanayo namna mbili
ya kuelewa. Kimwili, kuamini kwao ni kama kule Tomas, lakini ndani yao
kuna haja na hamu ya kuamini ambayo wanataka kuihakikisha.
Aliye
na mang’amuzi haya ya ndani, ajue kwamba Tomas ni pacha wake. Na kwamba
tusiwe na woga wa kuungama mashaka yetu ambayo ni kama ya Tomas, kama
tunaweza kugusa kama Tomas hatuwezi kuwa na mashaka. Lakini kugusa huko
kwetu hakuwezekani.
Kwa hiyo ni vyema kabisa kuwa ndani yetu
tunaye huyo pacha wetu Tomas wa kuona mashaka kwamba huyo aliyetoa
maisha kwa kufa kwake kama mtumwa ameingia katika utukufu wa Baba. Kwa
hiyo fundisho kuu tunalopata hapa kwa huyu pacha wetu ni hili: Yesu
anapofika siku ya nane anaonesha majeraha yake na anamwita Tomas kuja
kuhakikisha.
Huo ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kuweka mikono
yetu ubavuni pake. Kualikwa na Yesu Mfufuka kuweka mikono yako ubavuni
mwake maana yake pale unapoweka mikono yako, shughuli zako zote, na hasa
ukijiweka wewe mwenyewe, kujiaminisha na kujitoka kabisa maisha yako
kwa upendo kama ya Yesu hapo umeingia katika ulimwengu wa Mungu na wa
utukufu wa ufufuo.
Upacha mwingine na Tomas ulio mzuri sana, ni
pale Yesu anapomwalika Tomas kuyatupa maisha yake kwenye mapendekezo ya
mwalimu: “Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono
wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.” (Yoh.
20: 27), naye Tomas anapojibu: “Bwana wangu na Mungu wangu!” (Yoh.
20:28). Hilo ni ungamo la imani katika Mungu wa kweli imani
inayojidhihirisha katika ufufuko wa Kristu. Imani kwa Mungu anayetoa
maisha yake kwa ajili ya upendo.
Tomas aliyekuwa na mashaka,
ndiye wa kwanza kushuhudia imani iliyo safi ya wakristu wa kwanza. Ni
yeye aliyeona uthibiti wa msulibiwa katika ufufuko. Haamini juu ya Mungu
anayeadhibu, anayezawadia, anayewapenda wema tu, amemwamini katika
Kristu aliyetoa maisha Mungu wa kweli ambaye hawezi kuwa mwingine
isipokuwa yule aliyesulibiwa kwa ajili ya upendo.
Uhakika kwamba
ameona na kugusa mikono na ubavu wa Mungu, uhakika ule anaweza kuwa nao
tu kwa mtazamo wa imani. Mtazamo unaotakiwa kuufungua daima pamoja na
jumuia. Sisi tunasikia sauti ya Bwana na katika mkate wa Ekaristi sisi
tunagusa mapendekezo yake ya maisha ya kujifanya mkate kwa ajili ya
kutupenda.
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
Utakatifu
ni hija ya maisha inayotekelezwa hatua kwa hatua kama walivyofanya
Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II watakaotangazwa kuwa
watakatifu, Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican. Huu ndio utakatifu ambao watu wanaendelea
kuushuhudia katika maisha na utume wa Wenyeheri hawa.
Padre
Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican akiwa ameambatana na wahusika
wakuu katika mchakato wa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane
Paulo II kuwa watakatifu: Padre Giovangiuseppe Califano pamoja na
Monsinyo Slawomir Oder, Jumanne, tarehe 22 Aprili 2014, wamepembua maana
ya utakatifu mintarafu maisha ya wenyeheri hawa wawili.
Yohane
XXIII katika maisha yake kama Padre, Askofu na Khalifa wa Mtakatifu
Petro alijiwekea nadhiri ya kuwa karibu na Yesu, kujificha katika Moyo
wake Mtakatifu, Kusali Rozari na kumpatia nafasi ya pekee katika maisha
yake. Haya ni mambo yaliyojionesha kwa namna ya pekee katika maisha na
utume wake kama Mchungaji na Baba.
Ni kiongozi aliyeyasimika
maisha yake katika furaha na ukarimu kiasi cha watu wengi kumwita kuwa
ni Papa mwema! Alikazia umuhimu wa mshikamano katika maisha na utume wa
Kanisa kwa kuitisha Sinodi ya Jimbo kuu la Roma na Mtaguso mkuu wa Pili
wa Vatican. Ni kiongozi aliyeonesha upendo na uelewa katika shughuli za
kichungaji; akawa kweli ni mtu wa msamaha na faraja kwa wote
waliomkimbilia. Alikazia utii na amani ya kweli duniani.
Monsinyo
Slawomir Oder anasema, utakatifu wa Mwenyeheri Yohane Paulo II ulianza
kuonekana tangu alipokuwa bado Chuo Kikuu, kiasi kwamba, baadhi ya
wanadarasa wake waliandika chumbani kwake, "Mtakatifu mtarajiwa",
kutokana na na moyo na bidii ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na
maisha adili. Yote haya yalimwilishwa kwa njia ya matendo ya huruma.
Alikuwa
na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, akawa na
ujasiri wa kukabiliana na changamnoto za maisha kwa imani na matumaini
pasi na kukata tamaa, kwani daima aliuona mkono wa Mungu ukiyaongoza
maisha yake! Watu wengi walitambua kuwa kweli Yohane Paulo II alikuwa ni
mtu wa Mungu aliyekuwa ni chemchemi ya maisha yake yote, kiasi cha
kujikita katika Uinjilishaji Mpya, ili wote waweze kuwa ni watakatifu
kwa kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Tunaendelea
tena katika tafakari yetu masomo Dominika ya II ya Pasaka mwaka A. Ni
kipindi cha furaha kwa sababu ya ushindi dhidi ya kifo kwa njia ya
ufufuko. Neno la Mungu, linakazia na kuahidi furaha ya kweli kwa wale
ambao hata kama hawakumwona Bwana wanayo imani na tumaini la kweli
katika yeye. 
Katika
Somo la kwanza, kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume latuonesha
furaha na tabia ya jumuiya ya kwanza ya Yerusalemu. Kwa nini tunaoneshwa
jambo hilo? Ni kwa sababu tunaalikwa kuishi mtindo uleule wa jumuiya ya
mwanzo katika mazingira yetu. Mambo msingi ya Jumuiya ya I yalikuwa
utii na usikivu wa watu kwa Neno la Mungu lililohubiriwa na Mitume.
Aidha waliweka mali yao na moyo wao pamoja kwa faida yao na kasi ya
Injili.
Ili kuimarisha mambo haya waliadhimisha pamoja Ekaristi
Takatifu na kusali pamoja kwa upendo. Mambo haya msingi yalifungamana na
furaha, uchangamfu, ushirikiano ambavyo vilikuwa vivutio kwa jumuiya
nyingine nje ya Yerusalemu. Ndiyo kusema waliishi na kukishuhudia kile
walichohubiri katika maisha yao, yaani waliuishi ufufuko ambao ndilo
chimbuko la haya yote.
Mpendwa msikilizaji, wito kwetu hivi leo
katika jumuiya zetu ni kuanza polepole kupalilia nguvu ya ufufuko, ndiyo
kusema tunaalikwa kushuhudia daima kwa maisha yetu yakuwa Kristu ni
mfufuka. Mpendwa, katika mantiki hiyo katika jumuiya zetu lazima tabia
za jumuiya ya kwanza zijitokeze na kukua na hivi kuwa kielelezo cha
mapendo kwa watu wa mataifa. Yafaa kukomaza ile tabia ya kushirikishana
tulichonacho hata kama ni kidogo. Tujifunze kuwa na kile kinachotufaa na
kinachobaki kiwe kwa ajili ya wale waliowahitaji katika jumuiya zetu.
Kumbuka
usemi wa Mtakatifu Basil akisema “kama mmoja wetu angechukua kwa ajili
yake kinachohitajika na kingine kikawa kwa ajili ya ndugu yake maskini,
basi kusingekuwa na tajiri wala maskini katika jumuiya”. Hii ni falsafa
ya mgawanyo sawa ambayo tungepaswa kuifikia kama kweli tunataka kumfuasa
Bwana kwa ukamilifu! Mpendwa msikilizaji inaonekana kuna ugumu katika
kushirikishana mali tulizonazo, na hasa kuwapeni maskini, je toka
tukiamini na kuendelea katika ugumu huu twaweza kusema tunaishi na
tunashuhudia ufufuko? Tafakari sana jambo hili!
Katika somo la
Pili toka barua ya kwanza ya Mtakatifu Petro tunakumbushwa siku ya
ubatizo wetu. Kwa njia ya ubatizo tulipata kuingia katika furaha isiyo
na mwisho. Ndiyo kusema Mt Petro anataka hata kama kuna madhulumu na
taabu mbalimbali tusisahau furaha ya milele. Anasema mateso ni ya
kitambo kidogo tu na baadaye yanapita cha msingi ni kutazama mbele
tukiendelea kukua katika neema ya ubatizo.
Mtakatifu Petro
anatukumbusha kuwa mkristu katika ulimwengu huu ni mgeni na hivi yuko
safarini kwenda nchi ya ahadi yaani mbinguni. Tunakumbushwa kuwa hakuna
mateso yanayoweza kuzima moto wa furaha na mapendo uliowashwa wakati wa
ubatizo. Wakristo ni kama dhahabu ambayo ili itengeneze kitu cha thamani
lazima ipitie moto ili ichomwe na kusafishwa tayari kwa kito cha
thamani.
Katika somo la Injili, hali ya maisha ya jumuiya inajionesha
wazi. Wanafunzi wako pamoja ingawa wanahofu! Bwana anawakuta wakiwa
pamoja na kuwatakieni amani. Anawaonesha alama za madonda na wanafurahi
na kusema tumemwona Bwana! Ni katika jumuiya hiyo Bwana anawavuvia Roho
Mtakatifu ili wapate kuondolea dhambi. Ni siku hii anaweka sakramenti ya
kitubio katika Kanisa na kisha anawatuma wakaende kutangaza habari
njema. Kumbe Toba ni mlango wa kazi ya kimisionari, ni mlango wa imani,
ni mlango wa wokovu. Analikabidhi kanisa ufunguo wa kufunga na kufungua
katika mambo yamhusuyo Mungu katika uhusiano wake na mwanadamu.
Jumuiya
wakati fulani zinakuwa na watu walio na mashaka katika imani. Hali hii
inajionesha leo pia. Ndiyo kusema, kumbe Mtume Tomaso ambaye hakuwapo
pamoja na wenzake siku ya kwanza haamini, bado ana mashaka kuhusu
ufufuko! “Siamini mpaka nitie vidole vyangu katika makovu ya Bwana!
Baada ya siku nane tukio hilo la kitaalimungu, Bwana anawatokea tena
Mitume na wakati huo Tomaso yupo.
Bwana anamwambia lete mikono yako
na uweke kidole chako katika ubavu wangu na usiwe asiyeamini! Tomaso
anajibu, Bwana wangu na Mungu wangu! Mpendwa, Mtume Tomaso anapokiri
udhaifu wake anatufundisha kuwa watu wa Imani na unyenyekevu mkubwa na
hivi baada ya ufufuko hakuna mashaka tena kinachobaki ni kwenda
kutangaza habari ya furaha kwa mataifa.
Mpendwa leo hii wapo watu wa
namna hii katika jumuiya zetu, kumbe wanaalikwa na Bwana kusadiki
pasipo kuona, na kwa namna hiyo Bwana anatangaza heri kwa wasioona
wakasadiki na si kwa wanaosadiki kwa sababu ya kuona. Mwishoni mwa
sehemu ya Injili ya Dominika hii, Mwinjili anatuambia pia zipo ishara
nyingi ambazo hazikuandikwa na hivi mtu asishangae ishara nyingine
ambazo hazimo katika Biblia lakini ni muhimu kwa imani yetu na maisha ya
Kanisa.
Nakutakieni furaha tele katika kipindi chote cha Pasaka na
Mungu azidi kuwa nawe, nawe ukitekeleza mapenzi yake katika Jumuiya kama
Jumuiya ya kwanza ya Waamini. Tukutane tena Dominika ijayo. Tumsifu
Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya
C.PP.S.
Daima
ni mchakamchaka. Tabia ya watu wa ulimwengu wa leo ni ile ya
mchakamchaka. Kila kitu kinaenda kwa kasi. Taarifa zinaenda kwa kasi kwa
njia ya pembejeo za mawasiliano ya haraka, barabara nzuri na za mikato,
na wenzetu walioendelea ndiyo wana magarimoshi yanayoenda kwa umeme kwa
mwendo wa kasi.
Tuna kila kitu tunachokitaka kwa haraka, daima
tuko katika mchakamchaka na kiherehere cha kufanya mambo kama vile tuna
wasiwasi wa kutofika tunakotaka kufika au kutofanikiwa kufanya kwa
wakati wake kile tunachotaka kukifanya. Ama kweli ni mchakamchaka wa
maisha. Mtu yupo katika kupiga mbio za maendeleo katika maisha. Mtu
anapiga mbio kwa vile hana uhakika wa kuwasili au kufikia juu kijamii au
kiuchumi au hata kuwazidi wengine. “Tukimbie wakati wengine
wanatembea!”
Hali hii ya mchakamchaka na ya mbiombio ndiyo
unayoikuta katika Injili ya leo. Mtakatifu Yohani anaposimulia kuhusu
kaburi wazi lililokutwa asubuhi ile ya ufufuko, anawaonesha wahusika
wote wa tukio lile wakiwa katika mbiombio na mchakamchaka: Maria
Magdalena ndiye mwanakiherehere aliyefungia. Alikurupuka asubuhi sana
kungali bado giza kwenda kaburini. Alipolikuta jiwe lililofunika kaburi
limeondolewa hapo ndipo ilipoanza patashika ya mchakamchaka. Akaenda
mbio kwa wanafunzi. Nao wale wanafunzi Simon Petro na Yohane wakaanza
mchakamchaka.
Tunaambiwa wakaondoka mbio wote wawili kwenda
kaburini. Yohane akamzidi mbio Petro akafika wa kwanza kaburini.
Kulikoni? Yaonekana mbio hizo zilipigwa kutokana na wasiwasi, na
kiherehere cha kujua kumetokea kitu gani. Budi ieleweke kwamba katika
mazingira kama haya, binadamu anakuwa amepagawa na kitu anachokuwa na
uhakika nacho kwamba kinaweza kikatokea. Yaani, kinakuwa ni kituko kipya
kabisa anachotegemea kukiona au kukipata, kitu kitakachotokea au
kilichoishatokea kabla. Katika mantiki hiyo mtu huwa haweza kutulia au
kujidanganya kutulia. Wasiwasi na kiherehere chake ni kutaka kukiona au
kukijua ni kitu gani ambacho ni budi kitokee lakini hakijui.
Endapo
kwa hawa wanafunzi wawili wangemwona Yesu kuwa si kitu cha maana au si
kitu cha kukijali, hapo tungewaona wametulia na kufanya mambo kitulivu.
Wangeenda kaburini kitulivu tena kwa ajili ya udadisi tu, siyo zaidi.
Injili ya Yohani inatafuta kutuingizia vionjo vya wanafunzi hawa wawili,
Petro na Yohani wanaokimbia kwenda kaburini. Nafikiri pengine, kwa
wote wawili kuna woga labda kuna kitu siyo kwamba hakikwenda sawa, bali
wanaonja kwamba imani yao inalazimika kukua ili kutobaki katika woga wa
kumtamani tu Bwana wao aliyekufa na sasa hayuko tena. Mbio yao
inadhihirisha imani yao. Siyo imani kama ya yule aliye na uhakika bila
wasiwasi, la hasha, vinginevyo wangekuwa wamepoozwa, na kukosa mwelekeo
na hivi kuchanganyikiwa na miguu kutetemea. Wangekosa nguvu kabisa ya
kukimbia, hivi daima wangekuwa wanajikwakwaa na kuanguka. La hasha, kuna
kitu!
Mbio na kiherehere cha Mkristu
Mkristu ni yule
anayekimbia, anayepiga mbio katika maisha. Mbio za mkristu siyo zile
zitokanazo na kutokuwa na uhakika wa kuwasili au kufikia juu kijamii au
kiuchumi au kupiga mbio za kuwazidi wengine, bali anakimbia kwa vile
anajisikia kuwa ni muhimu kuonja uwepo wa Mungu katika maisha yake
binafsi.
Tunajitambua katika mbio hizi? Tuna wasiwasi hata sisi
katika kumwelewa Kristu angalao kidogo Kristu ambaye wakati mwigine
tunaamini amekufa na kuzikwa katika maisha na katika maisha ya jamii?
Tunakubaliana
na kupokea hatari ya kuanguka na kujikwaa katika mwendo wetu wa imani?
Tunasadiki kwamba kuwa na imani kunamaanisha kwenda mbele katika
kutafiti na kuhitaji kupanua uelewa wetu wa imani. Au tunatafuta kwa
mbinu na gharama zozote zile kutafuta au kubaki mahali pamoja penye
kutupatia uhakika na usalama? Kanisa (tuko wote humo ndani) wakati
mwingine hupunguza kasi, au mwendo na kutamani au kutulia katika uhakika
na usalama wa hali tuliyofikia.
Petro na Yohane, wakiwa wameambukizwa na kasi ya Magdalena wanaanza kukimbia pamoja.
Tuanze
hata sisi mchakamchaka wa kumtafuta Yesu, tuwahusishe katika
mchakamchaka huo hata wale walio karibu nasi, labda wamezuiwa na
matatizo fulani au na harakati za maisha ya leo.
Heri sana kwa Pasaka yenye mbio… ili maisha yasikwame.
Ijumaa
Kuu Baba Mtakatifu Francisko majira ya saa tatu na nusu za usiku,
ataongoza Ibada ya njia ya Msalaba katika eneo la magofu ya Koloseo ya
mjini Roma. Tafakari katika za Ibada hii zimeandaliwa na Askofu Mkuu
Giancarlo Bregantini wa JImbo Kuu la Campobasso Boiano.
Askofu
mkuu Giancarlo Maria Bregantini wa Jimbo kuu la Campobasso- Boiano
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya matatizo ya kijamii, kazi, haki na
amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ndiye aliyepewa dhamana ya
kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka magofu ya Colosseo,
Ijumaa kuu tarehe 18 Aprili 2014 Ibada hii inatarajiwa kuongozwa na Baba
Mtakatifu Francisko kuanzia saa 3:15 Usiku kwa majira ya Ulaya, baadaye
atatoa baraka zake za kitume. 
Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha kwa ufupi,
tafakari ya Njia ya Msalaba iliyoandaliwa na Askofu mkuu Bregantini.
Naye
aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua kuwa
anasema ukweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana haya yalitukia
ili andiko litimie: hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko
lingine lanena: watamtazama yeye waliyemchoma. Hivi ndivyo Askofu mkuu
Bregantini anavyoanza tafakari ya Njia ya Msalaba, kwa kuonesha kwamba,
Yesu alipanda kwenda Mlimani Golgota bila kusita, kama kielelezo cha
upendo wa hali ya juu kabisa na akawaruhusu watesi wake kumtendea jeuri
bila kulalama!
Yesu, Mwana wa Maria alipenda kubeba mabegani
mwake, matendo ya giza yanayomwandama mwanadamu katika hija yake ya
maisha, ili kuweza kumkirimia mwanga, unaoleta nuru katika moyo wake.
Mateso na mahangaiko ya Kristo ni chemchemi ya wokovu wa mwanadamu;
machozi yake yanaonesha upendo wa Mungu. Yesu amesamehe dhambi za
binadamu ili kwa njia ya maisha yake, aweze kuwaonesha njia ya wokovu
kutokana na mateso pamoja na mahangaiko wanayokabiliana nayo katika
maisha, pasi na kukata tamaa.
Neno wa Mungu aliyefanyika mwili,
anajisadaka bila ya kujibakiza, kwa ajili ya wadhambi ambao kwa haki
kabisa walistahili kutundikwa pale juu Msalabani. Kiu inayooneshwa na
Yesu pale Msalabani ni chemchemi ya matumaini yaliyo wazi na mikono
iliyo tayari kumpokea mdhambi anayetubu na kumwongokea Mungu. Askofu
mkuu Bregantini anamwomba Yesu Msulubiwa kuwakirimia watu huruma yake
isiyokuwa na kifani, kwa kuwaonjesha harufu nzuri iliyoujaza mji wa
Bethania, mwanzo wa maisha mapya. Kwa kifo cha Kristo Msalabani, Yesu
awajalie waamini maisha ya uzima wa milele.
Katika tafakari yake,
Askofu mkuu Bregantini anagusia mashitaka yanayoendelea kujitokeza
ulimwenguni kwa kujikita katika ubaguzi wa rangi, hali ya kutojali wala
kuguswa na mahangaiko ya watu, kielelezo cha dhamiri mfu, inayoonesha
jinsi watu wanavyoshindwa kuwajibika na ukweli kutawala, changamoto ya
kusimama kidete kutetea wanyonge na kulinda ukweli.
Msalaba wa
athari za myumbo wa uchumi kimataifa unazidi kuwaelemea watu wengi kwa
kukosa fursa za ajira, mshikamano wa upendo na udugu; matumaini na imani
thabiti. Msalaba unaweza kuwa rahisi, ikiwa kama watu watajifunza
kuubeba pamoja na Yes una kwamba, kwa njia ya udhaifu wa kibinadamu,
watu wajifunze kujenga na kudumisha moyo wa ukarimu, kwani sura ya wote
wanaoteseka, inaonesha pia ile sura ya Mungu aliyetwaa mwili na kukaa
kati ya watu wake.
Kuna akina Mama na wanawake wanaoendelea
kuwalilia watoto wao wanaofariki dunia kutokana na sababu mbali mbali;
watoto kupelekwa mstari wa mbele vitani; watoto wanaofariki kwa saratani
kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira; watoto wanaotumbukizwa kwenye
utumwa mamboleo na matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa
kupindukia. Kwa kushikamana na Bikira Maria, hakuna hata chozi moja
linaweza kupotea, kwani Bikira Maria ni Mama wa wote.
Kuna haja
ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu, kwa kuguswa na
mateso na mahangaiko ya jirani, daima lengo likiwa ni kutafuta mafao na
ustawi wa wengi, ili kushinda vikwazo vya chuki, uhasama na kuonea wivu.
Tafakari ya Njia ya Msalaba inamwonesha Veronika, mwanamke mwenye
huruma anayethubutu kupangusa uso wa Yesu na hivyo kushiriki katika
mateso yake. Yesu anatambua upendo na ukarimu wa Veronika, changamoto ya
kuguswa na wale wanaoishi katika upweke hasi unaoweza kuwasababishia
kifo!
Wafungwa ni kundi la watu wanaoendelea kuteseka kutokana na
ukosefu wa haki jamii na mifumo duni ya maisha kwa kuishi hata kinyume
kabisa cha ubinadamu, hawa wanaendelea kuvikwa taji la miiba viwachani
wao. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza watu wanaojitolea kutoa huduma
mbali mbali za kiroho na kimwili kwa wafungwa gerezani.
Katika
tafakari hii, wanawake wakweli na waaminifu wanaoneshwa wakimsindikiza
Yesu katika Njia ya Msalaba, wanataka kumsalimia na kumfariji,
changamoto ya kuendelea kuwa imara katika imani na matumaini; kwa kutubu
na kumwongokea Mungu, ili kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na
kifani. Yesu anapoanguka mara kadhaa kwa kuelemewa na uzito wa Msalaba,
anawalika waamini kujibidisha kushinda tabia chafu zinazowaangusha daima
dhambini. Waamini wajenge umoja na mshikamano, kwa kusimama kidete
kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kwa kujikita katika
upatanisho, kwa kuwamngalia Yesu anayetundikwa Msalabani.
Watu
wajenge utamadni wa kuwaheshimu, kuwajali na kuwahudumia wagonjwa badala
ya kuwatelekeza na kuwatafutia njia ya mkato ya kumaliza mahangaiko yao
kwa kifo laini. Yesu hakushuka Msalabani, aliendelea kupenda na
kusamehe. Ugonjwa unaweza kuwa ni shule ya hekima ya kimungu, mahali pa
kukutana na Mungu mpole na mvumilivu, mwaliko wa kupambana na magonjwa
katika mwanga wa Pasaka na mafao ya familia na Jamii kwa ujumla.
Maneno
saba ya Yesu Msalabani ni chemchemi ya upendo na kwamba, kifo cha
Kristo kinafungua ukurasa mpya kwa kuonesha kwamba, kifo hakina tena
nguvu! Msamaha unaponya na kupyaisha; unawaunda watu katika maisha
mapya, mwaliko wa kuondokana na falsafa ya vita, kwani upendo na
mshikamano ni mambo yenye nguvu zaidi kuliko hata kifo! Huu ni mwaliko
wa kuchuchumilia huduma ya upendo kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa
Jamii. Fundisho kuu ambalo Yesu amewaachia wafuasi wake ni kupenda bila
ya kujibakiza, ndiyo maana Bikira Maria anathubutu kupokea maiti ya
mwanaye kwa imani na matumaini makubwa! Mwanadamu anakumbushwa kwamba,
hapa duniani ni mpita njia, iko siku ataungana na Muumba wake. Katika
kimya kikuu pale bustanini kulikokuwa na kaburi la Yesu, waamini
wajitaabishe kusikiliza sauti ya Yesu ikisema, mimi niko pamoja nanyi
hadi ukamilifu wa dahali.
Kwa ufupi, haya ndiyo mawazo makuu
yanayochambuliwa na Askofu mkuu Giancarlo Maria Bregantini katika
tafakari yake ya Njia ya Msalaba, Ijumaa Kuu kuzunguka magofu ya
Colosseo, mjini Roma.
Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Baba
Mtakatifu Francisko, Alhamis Kuu majira ya jioni, saa 11:30,
ataadhimisha Karamu ya Mwisho ya Bwana, na liturujia ya kuosha miguu
watu kadhaa kama ishara ya unyenyekevu na huduma, akiwa katika Kituo
walemavu cha Shirika la Mtakatifu Maria wa Kudra ya Mungu, cha
Shirika la la Don Gnocchi, cha mjini Roma. Shirika hili hufadhili watu
wapatao elfu tatu wenye ulemavu na tegemezi nchini kote Italia, Rome
kukiwa na vituo vyake 12 ambavyo hufadhili wageni wahitaji wanaoingia
jiji la Roma, kati ya vituo vya 29 vinavyofanya kazi katika mikoa tisa
ya Italia.
Baba Mtakatifu Francisko anasubiriwa kwa hamu na
wagonjwa na familia zao katika cha kituo cha Mtakatifu Maria wa Kudra
ya Mungu , mtaa wa Via Casal Marmo 401, Roma , ambako watu wa
kujitolea huhudumia wagonjwa na familia zao. Alhamis Kuu ya mwaka jana
Papa Francisko aliadhimisha pia Ibada ya Alhamis Kuu akiwa katika gereza
la watoto la mjini Roma.
Kwa Alhamis Kuu hii, taarifa zinaeleza
kwamba, tukio hili la Baba Mtakatifu, kukitembelea Kituo cha Waelmavu
cha Don Gnocchi, linafanyika baada ya kupita wiki chache kwa shirika
hili kuadhimisha sherehe kubwa ya kupita kwa miaka mitano tangu
mwanzilishi wa shirika Don Gnocchi kutajwa Mwenye Heri Februari ,
sherehe iliyohudhuriwa na waelfu ya waamini, kama sehemu ya mipango kwa
ajili ya maadhimisho ya miaka tano ya Don Carlo Gnocchi , kutajwa Mwenye
Heri. Sherehe zilizo hamasisha mwamko mpya wa utamaduni wake wa muda
mrefu na huduma maalum, isiyoweza kusahaulika, inayoonyesha kupandwa
kwa Mbegu ya mshikamano na umoja kwa jirani katika utendaji wa Papa, "
baba wa vilema ".
Kituo cha Mtakatifu Maria wa Kudra ya Mungu ,
ambacho zamani kilifanya kazi kwa jina la Mama Nasi, nyumba ndogo ya
Maongozi ya Mungu ya Cottolengo, ilifanywa kuwa Shirika la Don
Gnocchi Foundation Septemba 2003 na kwa sasa lina jumla ya 150 vitanda,
ambamo kuna makazi kwa ajili ya huduma ya Afya kwa Watu wenye ulemavu
60 vitanda, ambao hawahitaji kuunganisha na vifaa vya aina hospitali au
vituo vya ukarabati ); na pia kuna idara ya kisasa ya ukarabati wa
mwili “ neuromotor” wa ngazi ya juu, wanaotumia vitanda 60 , ambao pia
hupokea huduma ya mazoezi ya mwili, , huduma ya tiba , tathmini saidizi
teknolojia na ushauri nasaha, nasaha za kisaikolojia na elimu kwa
shughuli zinazo husiana na hali ya wagonjwa hao. Na vitanda 30 vilivyo
baki , ni kwa ajili ya wanaotoa huduma kwa wagonjwa.
Mbali na
huduma hiyo ya ndani pia huhudumia wagonjwa walemavu kama wagonjwa wa
nje kila siku, ambao hupewa tiba na ushauri wa ukarabati na huduma za
nyumbani .
Rais wa Shirika la Don Gnocchi, Mosinyori Angelo
Bazzari , akizungumzia Papa Francisiko kuendesha Ibada ya Karamu ya
Bwana katika kituo hicho cha Mtaa wa Via Casal Marmo , amesema ni furaha
kubwa kwao na wanamkaribisha Baba Mtakatifu kwa furaha kubwa ndani
mwao. Na kwamba, ishara ya kuosha miguu ni wazi inayoonyesha kwamba
Kanisa tangu kuanzishwa kwake, daima limeitwa kuhudumia kwa unyenyekevu
hasa watu masikini na dhaifu. Ni huduma ya upendo wa Papa katika
ulimwengu wa mateso na ishara ya huruma ya Kiiinjili, ambayo husaidia
kukumbuka kwamba , kiwango cha ustaarabu wa jamii kinapaswa kuwa kipimo
katika uwezo wake wa kutembea pamoja na watu dhaifu.
Upendo huu
wa kuhudumia dhaifu na wanyonge katika jamii, ni karama ya Don
Gnocchi , aliyowaachia kama urithi wafanyakazi zaidi ya elfu tano wa
Shirika lake, ambayo hufanya kazi kila siku kwa majitoleo ya bila
kujibakiza , kwa uaminifu na kama msimamo kila siku , katika dhamira
yao ya uwezo, nia, huduma na uendelezaji wa maisha ya maelfu ya watu
wanaotafuta huduma katika vituo vya shirik, kwa ajili ya Utafiti wa
Afya , mshikamano na huduma.
Papa
Francisko atatoa vItabu vya Injili vidogo vinavyoweza kuwekwa mfukoni,
vipatavyo elfu moja mia mbili, kama zawadi ya Pasaka kwa wafungwa
katika Gereza Kuu la Malkia wa Mbingu la Roma. Zawadi ya Papa
itawasilishwa Jumatano hii, na Askofu Mkuu Konrad Krajewski wakati
atakapo tembelea jengo la Gereza katika mtaa wa Lugara Roma.
Kitabu
hicho kidogo cha Injili chenye kuwa pia waraka wa Matendo ya Mitume,
Jumapili iliyopita pia kiligawiwa kwa waamini waliofika kumsikiliza Papa
wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana katika uwanja wa Kanisa Kuu la
Mtakatifu Petro, na pia kwa waliohudhuria Ibada ya Misa katika Kanisa
Kuu la Mtakatifu George Mkuu la Magliana Roma.
Na Jumapili ya
tarehe 4 Mei, Papa ana mpango wa kufanya ziara ya Kichungaji katika
Kanisa la Mtakatifu Stanslao la Botteghe la Roma.
Kisha 18 Mei 2014
, majira ya saa kumi za jioni , Papa Francesko atafanya hija katika
Madhabahu ya Bikira Maria wa Upendo wa Mungu, ambayo yako katika Mtaa wa
Via Ardeatina nell’Angola Romano , nje kidogo ya jiji la Roma. Hija
inayopendwa na watu wa Roma.
Madhabau ya Bikira Maria wa upendo wa
Mungu, ya Mtaa wa Via Ardeatina , yako kiasi cha umbali wa kilomita 12
Roma, katika kanda ya Agro Romano katika jengo la Castel di Leva.
ambalo kwa mara ya kwanza liliteuliwa na Papa Gregoria V11 kwa barua
yake ya kitume ya mwaka 1081, kama mali ya Abassia ya Mtume Paulo . Na
mwaka 1268, mali hiyo ililithishwa kwa Kanisa la Mtakatifu Sabina na
baadaye kupewa Wana shirika wa Orsinina mwaka 1295na tena kuhamishiwa
kwa Wasaveli.
Na baada ya kupitia katiak mbadiliko mbalimbali,
Desemba 1938, Madhabahu hayo yalifanywa kuwa Parokia ikiongozwa na
Paroko wa kwanza Don Umberto Terenzi ambaye mwaka 1942 alianzisha
Shirika la Mabinti wa Maria wa Upendo wa Mungu na mwaka 1962, madhabahu
hayo yakawekwa chini ya usimamizi wa Shirika la Oblates hadi leo.
Simulizi juu ya madhabahu hayo, huelezea tukio la mwaka 1740, juu ya
muujiza uliotokea kwa muhujaji mmoja aliyekuwa akisafiri kwenda Roma
kuhiji ambaye alipofika katika eneo hilo, kulitokea kundi la mbwa mwitu
wakali walotaka kushambulia, lakini mara aliomba msaada wa Mama Bikira
Maria na ghafla mbwa wao walizuiwa na kitu kisichoonekana na kutoweka
zao. Aidha watu wa Roma wanasadiki, Sanamu ya Bikira Maria wa Upendo wa
Mungu iliyo katika eneo hili iliweza kuuokoa mji wa Roma dhidi ya
kuanguka katika mikono ya maadui wakati wa vita kuu ya pili ya dunia.
Ushuhuda
wa kuokelewa na Bikira Maria wa Upendo wa Mungu, ndiyo asili ya hija
katika eneo hili ambako waamini wanapenda kwenda kuomba msaada wa kwa
Bikira Maria kutatua shida zao mbalimbali na pia kwa ajili ya kutoa
shukurani zao kwa mambo mbalimbali waliyofanikisha.
Maadhimisho
ya Jumapili ya Matawi, Kanisa linamshangilia Kristo alipoingia
Yerusalemu kwa shangwe na watoto wa Wayahudi wakatandaza nguo zao
njiani. Hii ni siku ya vijana kijimbo, inayoongozwa na kauli mbiu, "Heri
maskini wa roho maana ufalme wa mbingu ni wao".
Baba Mtakatifu
Francisko mara baada ya kubariki matawi, umati wa vijana ulianza
maandamano kuelekea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican, huku wakiimba kwa shangwe. Baba Mtakatifu katika Ibada hii
ametumia Fimbo ya Kiaskofu aliyozawadiwa na wafungwa kutoka gereza la
Sanremo, Italia. Huu ni mwanzo wa maadhimisho ya juma kuu, Kanisa
linapokumbuka mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.
Baba Mtakatifu
katika mahubiri yake anatawaka waamini kujitafakari kwa kuangalia hali
yao mbele ya Yesu, kama wako kweli na hamasa ya kuonesha furaha na
kumshangilia, au wamejikunyata na kumwangalia tu kama "nyanya mbichi".
Katika shida na mahangaiko ya Yesu, waamini wanajisikia namna gani na
wako upande gani? Je, ni kati ya kundi la wakuu wa Makuhani na Waandishi
waliokuwa wanasubiri fursa ya kumkamata na kumsulubisha Yesu?
Je,
wao pia ni sehemu ya akina Yuda Iskarioti waliomuuza Yesu kwa vipande
thelathini vya fedha? Au ni kati ya Mitume waliokuwa wanauchapa usingizi
wakati Yesu anakabiliana na mateso makali? Baba Mtakatifu anawauliza
waamini ikiwa kama wanataka njia ya mkato kwa kutumia upanga kama
ambavyo alitaka kufanya Mtakatifu Petro? au Yuda aliyemsaliti Yesu kwa
busu la unafiki? Au Wazee wa Baraza wanaofanya kila mbinu kwa kutafuta
mashahidi wa uwongo ili kumtia Yesu hatiani kwa kudhani kwamba ni kwa
ajili ya mafao ya wengi?
Baba Mtakatifu anaendelea kuwauliza
waamini ikiwa kama wanafanana na Pilato anapoona kwamba, "maji yamezidi
unga" ana nawa mikono ili kukwepa wajibu wake kwa kuwashirikisha
wengine. Katika hali ya kuchanganyikiwa na vurugu, Je, hata waamini nao
wanaendelea kupiga kelele wakitaka Barabara afunguliwe na Yesu ahukumiwe
kifo ili kuwafurisha watu na kumdhalilisha Yesu au kama wale Askari
waliomdhihaki, wakampiga mijeledi na kumtemea mate usoni?
Baba
Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake ambayo yalikuwa ni tafakari
inayomshirikisha mwamini binafsi anawauliza ikiwa kama kweli wamekuwa na
ujasiri wa Simoni wa Kirene aliyeshurutishwa kumsaidia Yesu kubeba
Msalaba wake naye kwa upendo mkubwa akatekeleza dhamana hii! Kuna watu
waliokuwa wanapita mbele ya Msalaba wakimdhihaki Yesu kwa vile
alijiaminisha kuwa ni Mwana wa Mungu. Baba Mtakatifu anawauliza waamini,
Je, hata wao wanajisikia kuwa na jeuri hata kumdhihaki na kumkejeri
Mwana wa Mungu?
Bikira Maria na baadhi ya wanawake wajasiri,
walisimama chini ya Msalaba kwa ujasiri mkubwa, wakateseka pamoja na
Yesu katika hali ya ukimya!, Je, waamini nao wanaendelea kuteseka na
Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku, tayari kama Yusufu wa
Arimatayo kwenda kuchukua Mwili wa Yesu ili kuuzika au wanawake
waliokuwa wanalia mbele ya kaburi la Yesu au wale Askari walioomba
ulinzi mkali kwenye Kaburi la Yesu aliyekuwa ametangaza kwamba, baada ya
Siku tatu angefufuka kutoka katika wafu? Hawa ni watu waliokuwa
wanataka kuzuia maisha mapya kwa njia ya ufufuko wa Yesu.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, haya ni maswali msingi ambayo yanaweza
kuwasaidia waamini katika tafakari ya maadhimisho ya Juma kuu, Kanisa
linapotafakari Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Yesu
Kristo.
Katika
ulimwengu wa leo suala la maandamano limeshamiri karibu katika kila
nchi. Maandamano hayo yanakuwa ya jamii fulani inayodai haki yake,
mathalani yanaweza kuwa maandamano ya wanawake wanaodai haki zao za
kijinsia, wafanyakazi, wanafunzi, waganga nk.
Maandamano mengine
yanakuwa ya kufanya kampeni ya uongozi, na mengine ni ya shamrashamra
za sikukuu fulani za kidini au arusi nk. Maandamano yoyote yanakuwa na
sehemu mbili maalumu yaani pahala pa kuanzia na pa kumalizikia, sehemu
hizo zaweza kuwa hospitalini, shuleni, uwanjani, ikulu au hata kanisani
nk.
Leo tutayaona maandamano ya namna yake yanayoendeshwa na
Yesu. Maandamano hayo siyo ya kufanya mgomo wa madai ya masilahi toka
serikalini, la hasha, bali tungeweza kuuingiza kwenye aina kama vile ya
kampeni ya kupigania sera zake za uongozi. Maandamano hayo yalikusanya
watu wengi sana, wakiwepo wanafunzi wake, mashabiki wengi na wapambe
kibao mpaka mji ukatikisika. Yerusalemu hapakutosha! Mapato yake hata
viongozi wa dini na wa serikali walipoyaona maandamano hayo wakataharuki
na kuulizana: “Ni nani huyu?”
Maandamano ya leo yalianza pahala
palipoitwa Bethfage na yakaishia mjini Yerusalemu tena ndani ya
Hekaluni. Humo hekaluni, Yesu anahitimisha maandamano siyo kwa kutoa
hotuba refu ya ahadi hewa, hapana, bali kwa kuwashughulikia watu
waliokuwa wanachenji hela na kufanya biashara ndogondogo hekaluni,
halafu siku ya pili yake anapokuwa na njaa anaulaani mtini usiozaa
matunda.
Sasa hebu tupaone kwanza pahala palipoanzia na
palipoishia maandamano hayo, yaani Bethfage na Yerusalemu. “Hata
walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa
Mizeituni.” Bethfage, ipo upande wa Mashariki ya mlima wa Mizeituni,
baada tu ya Bethfage kuna mlima wa Mizeituni ambako ukisimama juu yake
unaweza kuangalia vizuri sana mji wa Yerusalemu ulio chini yake. Neno
hili Bethfage ni muunganiko wa maneno mawili, Beth (Bayet) ni nyumba; na
Fage ni matunda ya tini yasiyokomaa. Kwa hiyo Bethfage ni nyumba ya
matunda ya tini yasiyokomaa.
Jambo la kushangaza ni kwamba baada
ya kuingia Yerusalemu na kuwasambaratisha wafanyabiashara hekaluni,
linafuata simulizi la mfano ule ambao unonesha kitu gani Mungu
anakitegemea toka kwa Taifa lake, yaani kitendo cha Yesu kwenda kutafuta
matunda kwenye mti wa mtini na bila kukuta kitu isipokuwa majani
matupu, anaulaani. “Mtini ukanyauka mara.” Tendo lile la Yesu ni mfano
hai unaolingana na kile anachokitegemea Mungu toka kwa watu wake
kifanyike ndani ya hekalu au katika ibada zao, lakini anakikosa.
Mungu
anategemea kupata matunda ya upendo, ya haki, ya kuwajali maskini,
wajane, yatima na watoto, wageni, badala yake ndani ya hekalu anakuta
majani, yaani, liturjia, nyimbo za kupendeza, madhehebu marefu, chetezo,
ubani na mishumaa kwa wingi. Vitu hivi havisemi chochote kile mbele ya
Mungu kama havizai matunda. Hivyo siyo sadaka ambazo Mungu anategemea
kuziona toka kwa watu, kwake Mungu vitu hivyo ni kama majani tu, au ni
kama Bethfage tu (matunda yasiyokomaa).
Baada ya kuona maana ya
mandhali ya maandamano, sasa tuwaone wahusika wakuu wa maandamano hayo.
Anapofika Bethfage anawaagiza wanafunzi wake wamletee usafiri: “Enendeni
mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na
mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia
neno, semeni, ‘Bwana ana haja nao,’” Maagizo haya ni ya muhimu sana na
umuhimu wake unaonekana jinsi masimulizi yanavyorudi mara mbili. Mosi,
pale anapowaagiza mitume wake: “mtaona Punda amefungwa, na mwanapunda
pamoja naye. Wafungueni mniletee.” halafu inarudiwa tena inaposemwa.
“Wale wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaamuru (kuwafungua),
wakamleta yule punda na mwanapunda”. Msisitizo upo katika kuwafungua hao
punda na kuwaleta ili waweze kutumika kwa kazi atakayoitaka Yesu
waifanye. Endapo maandamano haya ni ya kampeni za uongozi, basi
yaonekana siri na sera za uongozi huo zimelala katika Punda hao. Kwa
hiyo Punda ndiyo wasanii wakuu wa maandamano ya leo.
Kazi ya
wanafunzi waliotumwa ni kuwafungua punda. Wanyama hawa punda wana maana
gani katika Biblia? Mfalme wa enzi za Wayahudi aliwastaajabia sana
Farasi na wapanda Farasi waliojulikana kuwa hodari kwa kupigana vita.
Kwa mfano, tunasikia kuwa askari wa Farao Farasi na wapanda Farasi wao
wote waliangamizwa baharini. Hivi hata Wafalme wa kiyahudi walikuwa
wanatamani sana kuwa na farasi na wapanda farasi. Katika kitabu cha
Kumbukumbu la Torati, mfalme Salomoni anaonywa asiongeze idadi ya
Farasi, na asiuze ndugu zake kwa Wamisri kwa ajili ya kuwa na Farasi na
wapanda Farasi (askari). Kutembea juu ya farasi ni alama ya ukuu,
uongozi, utawala, ufalme, utajiri na ufahari. Namna ya usafiri unaonesha
hadhi ya mtu.
Siku za leo, tunaweza kupata picha ya magari ya
gharama na ya fahari wanayotembelea marais, mawaziri, wabunge,
makardinali, maaskofu, matajiri, maofisa, nk Itakuwa ni kichekesho na
haiwezekani kabisa kumwona kiongozi wa hadhi kama hizo kusafiri kwa lori
la mkaa, kwa Bajaji au kwa bodaboda, au baiskeli nk. Katika kampeni za
uongozi wa kisiasa, wagombea wanasafiri kwa magari ya gharama za
kutisha, kama vile gari aina ya Prado, VX, Helikopta. Hii ndiyo hadhi
yao.
Kumbe, katika maandamano ya kampeni za Yesu, anamchagua
Punda jike na mwanapunda kuwa prado ya kuingia nayo rasmi mjini
Yerusalemu. Hii ndiyo sera mpya ya utawala na uongozi anaotaka Yesu
kuuingiza ulimwenguni. Ni kiongozi pekee anayefanya hivyo. Marko anasema
kwamba hakukuwahi kutokea mtu mwingine yeyote yule aliyewahi kumpanda
yule Punda kabla: “Mtamwona mwanapunda amefungwa, asiyepandwa na mtu
bado” (Mk. 11:2). Tamko hilo la Marko ni muhimu sana, likimaanisha
kwamba, hakujawahi tokea mfalme au rais yeyote yule hapa duniani,
aliyewahi kujionesha, katika hali kama hii ya utumishi. Yesu ni mfalme
wa kwanza na wa mwisho anayependekeza aina hii mpya ya utawala.
Ili
kuelewa vizuri ujumbe tunaoletewa hapa hatuna budi kuangalia mwishoni
mwa kitabu cha Mwanzo ambako Yakobo anatoa baraka yake kwa watoto wake
kumi na wawili, anapotoa baraka kwa Yuda, ambaye ni mtoto wake wa kwanza
na atakayekuwa kiongozi wa kabila la Israeli, anasema: “Fimbo ya enzi
haitaondoka katika Yuda, wala mfanya sheria kati ya miguu yake, hata
atakapokuja Yeye, mwenye milki, ambaye mataifa watamtii. Atafunga punda
wake katika mzabibu, na mwanapunda wake katika mzabibu mzuri.” (Mwanzo
49:10-11). Sisi hapa tuko mbele ya kituko hicho cha Yesu anayemfungua
punda na mwanapunda kama rejea ya Yuda, yaani yule ambaye ataingiza sera
za uongozi, utawala mpya ambao hautakuwa na mwisho. Sasa amefika yule
ambaye ni kiongozi mpya wa taifa.
Yesu anasema: ‘Wafungueni
mniletee’ Wasanii wakuu tunaoletewa hapa leo, wanayo tabia ya pekee
sana. Mnyama huyu anafugwa na kuthaminiwa na binadamu hasa kutokana na
tabia yake ya kufanya kazi. Kutokana na tabia hiyo, mnyama huyu anayo
majina mengine mengi sana yanayowakilisha udundaji wake wa kazi, wengine
wanamwita, Nsikiri, Kihongo, Daqwai, Mbunda au Punda nk. Ukitaka
kumsifia mtu anayefanya kazi sana wanasema: “Anafanya kazi kama
kihongo.”
Hivi Punda ni alama ya kazi, utumishi, na uvumilivu,
hachoki kamwe, daima yuko tayari kubeba mizigo. Tabia hii ya Punda ndiyo
ilimvutia Yesu hadi akamchagua kuwa mfano wa kuigwa na kipeo cha
utumishi ambao unawakilishwa katika nafsi ya kila mtu. Sisi tunashangaa
tunapomwona Yesu anajilinganisha na Punda. Kumbe, yeye alitaka daima
ajioneshe kama mtu wa kutumikia. Kwa hiyo anapoagiza “wafungueni Punda”
anamaanisha kuwa, Punda hao walikuwa wamefungwa, na katika hali hiyo ya
kufungwa hawawezi kufanya kazi. Ilibidi kwanza wafunguliwe ili waweze
kufanya kazi.
Kila mmoja wetu anao uwezo wa kufanya kazi na
uwezo wa kutumikia. Tunayo hali hiyo kutokana na kufanana kwetu na Mungu
katika upendo. Upendo ni zawadi kwa maisha yetu maana yake ni kuwajali
wengine, yaani kutumikia. Ndani yetu sisi tunaye huyu Punda, Kihongo,
Nsikiri nk. Kwa hiyo, endapo punda hao ni sisi, basi yabidi tufunguliwe
tuwe huru kufanya kazi yaani, kutumikia, kuvumilia, kunyenyekea, kuwa
tayari daima... Yaani tunao uwezo wa kutumikia, lakini daima tumejifunga
hatutaki kujifungua ili tuwe huru kutumikia, badala yake tunataka daima
kutumikiwa.
Yesu anawapa wanafunzi wake kazi: “Enendeni mpaka
kijiji kile kinachowakabili, mtaona Punda amefungwa, na mwanapunda
pamoja naye. Wafungueni mniletee”. Kazi ya wanafunzi ni kuamsha nguvu ya
kutumikia iliyo ndani yetu, kuifungua na kumpelekea Yesu.
Yesu
anaongeza kusema: “na kama mtu akiwaambia neno, semeni, ‘Bwana ana haja
nao’”. Maana yake akitokea mtu fulani anakataza au anaonesha kupinga.
Mtu huyo si mwingine bali ni mimi ninayesema: Tafadhali uniache huru,
Usimfungue punda aliye ndani mwangu. Lakini Yesu anakuhitaji anasema:
“Nina haja nawe,” kwa sababu kwa njia ya ushirikiano wetu, Yesu anaweza
kuanzisha utawala wake duniani kwa kishindo, lakini siyo utawala wa
kukandamiza, bali wa utumishi, wa upendo, na wa haki. Yesu anahitaji
mchango wa kura ya moyo wako kwa kadiri ya uwezo wako yaani ujifungue,
uwe huru, ujiruhusu, kuwa na haki na upendo wa kutumikia, kuwa tayari
kusaidia wengine kusudi kuunda uongozi mpya.
Nabii Zakaria
anasema: “Tazama, (Yerusalemu) mfalme wako anakuja kwako, mpole, naye
amepanda Punda, na mwana Punda, mtoto wa Punda.” Nabii anasema, mfalme
huyo haendi vitani kama mpanda-farasi, bali amepanda punda ambaye ni kwa
ajili ya kazi ya kutumikia. Kwa hiyo mfalme (kiongozi) huyo anakuja
kutumikia. Wanyofu ndiyo watakorithi ulimwengu huu mpya.
Baada ya
kuipata sera ya Yesu kutokana na aina ya usafiri aliotumia katika
kampeni yake, sasa tuwaone waandamaji katika msafara huu wa Yesu. Punda
walipowasili, “wanafunzi wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu
yake. Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani: wengine
wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.” Vifaa hivi na matendo
ya waandamaji ni muhimu sana katika maandamano haya. Hebu tuyafuatilie.
Tafsiri
halisi ya nguo hapa ingekuwa mgolole au shuka, yaani ni nguo ya binafsi
inayomsitiri mtu anapoivaa au hata kujifunika anapolala. Kadhalika kwa
Myahudi, hiyo ilikuwa ni nguo yake binafsi. Ni sawa na vazi binafsi
ambalo mtu huwezi ukalitoa kwa yeyote. Unaweza ukagawa kitu kingine
lakini siyo shuka ya kujifunika au mgolole wa kujitanda. Kwa hiyo nguo
hizo ni alama ya utu wa mtu, nafsi yake, uwepo wake na kila kitu chake.
Wanafunzi
wanaweka au kutandika shuka na migolole yao juu ya Kihongo na mtoto
wake, inamaanisha kwamba wao wanayatoa maisha yao na kila kitu ikiwemo
utajiri wao, kwa utumishi unaopendekezwa na Yesu kutokana na tabia ya
huyo Kihongo. Yesu anaikalia hiyo migololi ya wanafunzi hao kuonesha
kuwa wako chini ya utawala ambao Yesu ndiye mfalme wake. Wanakubaliana
na uongozi huu pamoja na sera zake. Yesu mwenyewe akiwa mnyofu,
mnyenyekevu, mpole na mtii anasafiri juu ya Punda aliye mvumilivu,
mfanya kazi, mtumishi tu na anakaa juu ya migololi hii ya wanafunzi.
Wamepokea, na kuukubali uupya wa masiha huyu, mtumishi na mleta amani.
Ndiyo maana ya kuweka migololi yao juu ya Punda.
Watu wengine
wengi pia wanajitokeza kushangilia: Watu wengi katika ule mkutano
wakatandaza nguo zao njiani: wengine wakakata matawi ya miti,
wakayatandaza njiani.”
Watu hao wanafanya mambo tofauti na
wanavyofanya wanafunzi. Wanafunzi wanatandika migololi yao juu ya punda
kuonesha kwamba wao ndio wanaoendeleza sera za mtindo huo wa uongozi.
Watu wengine kumbe wanatandaza nguo zao njiani au barabarani.
Kiutamaduni ilikuwa kwamba, wakati wa kumtawaza kiongozi, watu walikuwa
wanatandaza nguo ardhini na kushangilia ikiwa na maana kwamba walikuwa
wanakubali kujitoa na kujiweka chini ya uongozi wa huyo mfalme.
Katika
nafasi hiyo watu walikuwa wanashabikia na kupiga vigelegele lakini mara
nyingi hawakuelewa sera za uongozi huo. Katika kundi la maandamaji wa
leo yaonekana kulikuwa na wapambe wengi sana: “Watu wengi katika ule
mkutano wakatandaza nguo zao njiani, na wengine wakakata matawi ya miti,
wakayatandaza njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata,
wakapaza wauti wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarakiwa, yeye
ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.” Watu hawa wote walikuwa
wanamshabikia mfalme huyu lakini pengine kadiri ya sera walizokuwa
wanazifikiria wao.
Wanampokea lakini kadiri wanavyoelewa wao aina
ya Mfalme wanayemtegemea. Ni tofauti na mitume wanaoweka nguo zao juu
ya punda. Hata katika mazingira yetu ya sehemu mbalimbali yaweza kutokea
wachache wanaoelewa maana ya utumishi ya kumfuata Yesu na watu wengine
wakabaki ni wapambe na mashabiki tu. Watu hao wanakata na matawi ya miti
kushangilia.
Kuhusu matawi ya miti, kunakumbushia Sikukuu ya
Vibanda. Siku hiyo waliyakata matawi ili kusherekea kumbukumbu ya
kukombolewa toka utumwani Misri. Hapa sasa wanakata matawi kuonesha kuwa
sasa wanao uhuru kwa sababu Masiha amefika. Lakini Masiha huyo
wanayemdhani ni wa aina gani? Hapo tunaona ukweli wa usemi kwamba
“katika msafara wa mamba kenge nao hawakosekani.” Watu waliendelea
kuimba “Mwana wa Daudi” lakini ni mwana wa Daudi wanayemtegemea wao.
Katika
sikukuu hii ya Matawi tunaalikwa kujihoji upya ushirika wetu na Kristu.
Endapo tunataka kidhati kuwa washiriki wa ufalme mpya anaotupendekezea
Yesu yabidi tumfungue punda aliye ndani mwetu ili kuwa na uwezo wa
kupenda ambao Mungu ametupatia. Tuwe Punda, Kihongo au Nsikiri
aliyefunguliwa na kukubali kumbeba Kristu, yaani kutumikia kwa upendo.
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.