Week Hot newz

Tujiepushe kula ovyo kujilinda dhidi ya kisukari

DUNIA leo inaadhimisha Siku ya Kisukari. Ni ukweli usiokuwa na chembe ya shaka kuwa katika miaka ya karibuni ugonjwa wa kisukari umekuwa tishio miongoni mwa mataifa mengi kwani wakati zamani ulionekana kuwaathiri zaidi watu walioishi miaka mingi, sasa hata vijana wadogo na watoto wanaathiriwa na ugonjwa huo.

Takwimu za ugonjwa huo zinaeleza kuwa kwa sasa unashika nafasi ya tatu duniani kwa kusababisha vifo, huku watu milioni moja kila mwaka wakijikuta wakiishi katika madhila makubwa yanayotokana na ugonjwa huo kwa kuwa hulazimika kukatwa viungo vya miili yao, hasa miguu ndiyo viungo vinavyoathirika zaidi kwa kukatwa kutokana na usugu wa ugonjwa huo.


Pamoja na madhara makubwa ya kisukari kwa maisha ya watu, elimu juu ya ugonjwa huo bado ni ndogo sana ndani ya jamii, na hata wale ambao wamekwisha kuathirika ama hawazingatii vilivyo masharti yake au wanayapuuza huku wale ambao hawajafikwa na ugonjwa huo wakishindwa kujua hatua za kuchukua ili kubaki salama.
Kisukari ni ugonjwa unaosababishwa na uwapo wa kiasi kikubwa cha sukari kwenye damu.

Hali hiyo husababisha mtu kusumbuliwa na maradhi.  Maelezo ya kitabibu yanasema kuwa ingawa kuna mambo mengi yanayotajwa kuwa vyanzo vya ugonjwa huo, baadhi ya sababu zinazotajwa sana ni matokeo ya kutokuwa makini kuhusu lishe ambayo husababisha mabadiliko makubwa mwilini kwa maana ya kuongezeka sana uzito kupita kiasi.

Hali hii kwa vyovyote itakavyoangaliwa inaelezwa kuwa kushindwa kwa mtu kuwa na mpangilio mzuri wa chakula, kutokufanya mazoezi na kula kupita kiasi, matokeo yake mwili hujikuta ukinyemelewa na ugonjwa  wa kisukari.

Ipo imani potofu kwamba ulaji wa sukari ndiyo tu chanzo cha kupatwa na kisukari, taarifa za kitabibu zinasema kuwa vyakula vinavyoliwa na binadamu vya jamii ya wanga vina tabia ya kutengeza sukari. Wanga huu ni muhimu sana kwa ajili ya kuupa mwili nguvu.

Katika mfumo wa uyeyushaji wa chakula aina ya wanga, huyeyushwa na kuwa sukari ili iweze kutumika ndani ya mwili kwenye seli hai, kitendo chochote cha kushindwa kufyonzwa kwa sukari hii kutoa nishati kwa mwili, husababisha kubakia kwenye damu na hivyo madhara ya kisukari huanza kujitokeza.

Watalaam wa tiba wanauelezea mwili wa binadamu kama mashine yenye vifaa vingi, kila kimoja kikifanya kazi yake mahususi, kushindwa kwa kifaa kimoja kutekeleza kazi fulani, mashine nzima hupata hitilafu na kama ni injini ya gari huwa na matatizo.

Kwa mwili wa binadamu wataalamu wanasema kuwa kila kinachoingizwa mwilini kwa maana ya chakula ni lazima kiwe na uhusiano wa kiasi halisi kinachotakiwa, vinginevyo muhusika ni lazima afanye mazoezi ya kutosha ili kitumike.

Ulaji wa ovyo, kama vyakula vyenye mafuta mengi, nyama nyingi, kukwepa kufanya mazoezi kiasi cha mwili kutoka jasho la kutosha, husababisha seli hai kuzungukwa na mafuta na hivyo kushindwa kufyonza sukari ili ifanye kazi yake.

Pamoja na ukweli kwamba ugonjwa wa sukari una changamoto zake, hasa kutokana na kuwako kwa aina tofauti, kama vile aina ya `diabetes type 1 ambayo inaweza kumpata mtu yeyote katika umri wowote wakiwamo watoto kwa sababu ina uhusiano wa kinasaba kwa maana kwamba mara nyingi waathirika wengi huwa wamerithi katika ukoo au huzaliwa nayo, bado kuna njia nyingi za kisayansi za kupunguza madhara yake.

Ugonjwa wa kisukari una madhara mengi, ya kimwili, kijamii na kiuchumi. Wagonjwa wengi wamepoteza viungo vyao vya mwili, kama kutolewa figo, kukatwa kwa miguu au vidole vya miguu kwa sababu ya vidonda kushindikana kupona; kupoteza uwezo wa kuona na kusikia, kupoteza nguvu za kiume na mara nyingi husababisha kifo.

Mbali na madhara ya moja kwa moja kwenye mwili, uchumi wa mgonjwa na familia yake huyumba sana kutokana na kisukari kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa, kukosa nguvu ya kutafuta kipato na mara nyingine madhara ya kisaikolojia kwa mgonjwa na hata wale wanaomuhudumia huleta matatizo ya mahusiano ndani ya familia.

Pamoja na sababu zote za kisayansi zinazoweza kutolewa, hakuna ubishi kwamba binadamu alivyo ni matokeo ya kile anachokula, kwa maana hiyo ni mwito wa kitabibu kwa kila mwenye kujitakia afya njema kuzingatia mpangilio wa chakula, kufanya mazoezi ya viungo kila siku na kupima kiwango cha sukari mara kwa mara mwilini.

Kwa wale ambao hawajapata madhara ya kisukari ni rai ya kitabibu kuwa wadhibiti uzito na vile vile, kubadilisha mpangilio wa maisha; kufanya mazoezi mara kwa mara, kuzingatia mpangilio bora wa chakula na kupunguza au kuacha kabisa unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara.

Ni jambo la bahati mbaya kuwa kisukari kinaandama zaidi watu wenye uwezo mkubwa wa kumudu kile watakacho, lakini kwa bahati mbaya wengi hawazingatii kabisa kanuni za ulaji wa kulinda afya zao na matokeo yake hushia kununua ugonjwa huu kwa fedha zao wenyewe.

Kwa msingi huu wakati leo Watanzania wakiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya kisukari, ni vema kila mmoja akawa mlinzi wa afya yake ili kujiepusha na kisukari.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni