“Kuzaliwa
kwa Yesu Kristo kulikuwa hivi. Maria mama yake, alipokuwa mchumba wa
Yosefu, kabla hawajakaa pamoja alionekana na mimba kwa uwezo wa Roho
Mtakatifu. Mumewe Yosefu akiwa mtu mwadilifu, hakupenda kumwaibisha
hadharani. Basi akanuia kumwacha kwa siri.” (Mt 1:18-19)
Baba
Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 16 Januari 2014 amekutana na
kuzungumza na wafanyakazi wanaotekeleza dhamana na utume wao kwenye
Makazi ya Papa mjini Vatican. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa huduma na
ukarimu wanaowashirikisha wageni mbali mbali wanaofika mjini Vatican kwa
ajili ya kukutana na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba
Mtakatifu anasema kwamba, Nyumba ya Papa ni mali ya Waamini wote wa
Kanisa Katoliki; mahali ambapo wanaonja tone la upendo na moyo wa
ukarimu wa kifamilia pamoja na msaada wa kulinda na kudumisha imani
ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mmiliki mkuu wa Nyumba
ya Kipapa ni Yesu mwenyewe na wengine wote ni wafuasi na wahudumu wa
Injili.
Baba Mtakatifu anasema kutokana uelewa huu, kuna haja kwa
wafanyakazi hao kukuza na kudumisha majadiliano ya kina kwa njia ya
sala, ili kuimarisha urafiki na uhusiano wa ndani kabisa, tayari kutolea
ushuhuda wa upendo na huruma ya Mungu kwa watu wake. Wafanyakazi hawa
anasema Baba Mtakatifu wanapotekeleza utume wao, kazi inaweza kuwa ni
fursa ya kuwashirikisha wengine furaha ya kuwa ni sehemu ya Fumbo la
Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Baba Mtakatifu anawaalika kuwa
makini katika kuisikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu inayowaita kila siku,
kumtumikia kwa ukomavu na moyo wa ukarimu. Baba Mtakatifu amewatakia
wafanyakazi hawa pamoja na familia zao, kheri na baraka kwa Mwaka Mpya
2014.