URAFIKI na Mahusiano ndio jina la safu hii mpenzi msomaji. Ni matumaini yangu umzima na unaendelea vema kukabiliana na shughuli mbambali za ujenzi wa taifa hili.
Nami bila hajizi nakukaribisha katika safu hii ili twende sambamba katika kuzungumzia suala la Siku ya Wapendanao (Valentine’s day), ambayo sherehe yake ni Ijumaa ya wiki ijayo – Februari 14.
Kwa kawaida huwa kuna sherehe nyingi na wengine kuwatumia zawadi wahusika kama familia na marafiki, na mojawapo ni hii Siku ya Wapendanao.
Hakuna binadamu yeyote duniani anayeishi duniani bila kukwaruzana na mtu yeyote, iwe rafiki au ndugu.
Hivyo hakuna kitu cha kukufanya uwe na wasiwasi juu ya siku hiyo kwamba utafanya nini kwa uwapendao au umpendae.
Unaweza kuifanya Siku ya Wapendanao iwe nzuri kwako. Kabla ya kufanya chochote; kwa maana kwamba ikiwa bado siku kadhaa hadi ifikie siku hiyo, tembelea maduka ya kadi na utazame aina mbalimbali za kadi.
Njia hii haitokufanya usahau kupata kadi nzuri na pia itakuepusha kukurupuka na kununua kadi ambayo haina mvuto wa kipekee.
Bila shaka wazo kubwa zaidi la zawadi ambalo huwepo miongoni mwa watu wengi ni maua.
Zawadi hizi pia huweza kutumiwa hata kwa walioajiriwa, yaani kwa wafanyakazi wa taasisi au kampuni fulani.
Hata hivyo, watu pia huwa wanasherehekea Siku ya Wapendanao kwa kuja na mitazamo tofauti na kutafakari ni zawadi gani inafaa kumtumia mtu.
Unaweza kuonyesha ukaribu na urafiki kwa wafanyakazi wenzako kwa kununua maua na kuwapa zawadi lengo likiwa ni kuonyesha upendo.
Lakini kwa wapenzi mbali na kupeana zawadi za maua yanayoonyesha upendo, pia wanaweza kutoka ‘out’ kwa ajili ya kwenda sehemu kubadilisha mawazo na kufanya siku hiyo iwe nzuri kwao.
Kama umepanga Siku ya Wapendanao ibaki kuwa kumbukumbu kwa ninyi wapendanao (wapenzi), usisahau kuhusisha zawadi zitokazo kwa sonara, kwani hakika ni chaguo zuri.
Kwa mfano unaweza kununua kimojawapo kati ya vitu vinavyopatikana sonara kwa lengo la kuboresha upendo wenu.
Epuka kuwa na kisirani pamoja na kumkera umpendae au uwapendao kwani kwa hakika utakuwa umeifanya siku hiyo kuwa mbaya kwako.