
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Dk. Agness Kijazi .
Akizungumza kwenye mkutano wa 41 wa masuala ya hali ya hewa na
utabiri unaofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali
ya Hewa nchini (TMA), Dk. Agness Kijazi (pichani), alisema kitaalam kuna
uwezekano wa kutokea kwa mvua kubwa katika nchi za Afrika Mashariki
katika kipindi cha Septemba mpaka Desemba, mwaka huu.
Alisema mkutano huo unawahusisha wataalam mbalimbali kutoka katika
nchi 11 na unaangalia mifumo ya hali ya hewa kwa Afrika Mashariki na
tayari wameona viashiria vya kutokea kwa mvua hizo.
“Mvua hizo hutokea pale kiwango cha joto kinapoongezeka kwa kiasi
kikubwa kwenye bahari na mpaka sasa tumeona joto limeongezeka kwa kiasi
kikubwa katika bahari ya Pacific,” alisema Kijazi. Alisema baada ya
kuangalia mifumo ya hali ya hewa katika eneo la Afrika Mashariki,
wataalamu watarudi katika nchi zao na kuangalia mifumo ya hali ya hewa
katika maeneo yao na kutoa utabiri kwa wananchi husika kwa kipindi
Septemba mpaka Desemba.
“Hapa kwetu Tanzania tutatoa utabiri wa mvua kwa miezi mitatu yaani
Septemba mpaka Desemaba ifikapo Septemba Mosi mwaka huu,” aliongezea
kusema. Kijazi alitoa wito kwa wananchi na wadau wa hali ya hewa
kufuatilia utabiri utakaotolewa Septemba Mosi, mwaka huu ili kujua hali
itakavyokuwa.
CHANZO:
NIPASHE