Week Hot newz

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima 2014

Mama Kanisa anakianza kipindi cha Kwaresima, yaani siku arobaini za toba na wongofu wa ndani; kusali na kufunga; kusoma na kulitafakari Neno la Mungu pamoja na kumwilisha imani katika matendo, kwa Jumatano ya Majivu. Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini watarudi tena.

Hizi ni nyakati za toba na zimewekwa na Mama Kanisa kwa ajili ya mazoezi ya maisha ya kiroho; zinajikita katika liturujia ya toba, kuhiji kama ishara ya toba, kujinyima kwa hiyari kama sehemu ya kufunga na kutoa sadaka kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; ni mwaliko wa kushiriki kidugu kazi za mapendo na kimissionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa.

Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2014 unaongozwa na kauli mbiu “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, Jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba, ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”. Huu ni mwaliko kwa waamini kuonesha moyo wa ukarimu kwa jirani zao kama ilivyokuwa nyakati za Mtakatifu Paulo aliyewahimiza Wakorintho kuwasaidia ndugu zao waliokuwa wanateseka mjini Yerusalemu.

Baba Mtakatifu katika tafakari hii anaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu ambaye ni tajiri na mwingi wa rehema kwa njia ya Yesu Kristo, Mwanaye wa pekee amejinyenyekesha na kuwa maskini, ili aweze kuwa karibu na binadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Hiki ni kielelezo cha upendo wa Mungu ambao ni neema na baraka inayotolewa kwa binadamu anayependwa na Mwenyezi Mungu, kiasi cha hata Kristo kujisadaka maisha yake.

Huu ndio upendo unaoshirikisha, unajenga na kuimarisha umoja na udugu kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu amefikiri na kutenda kama binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi.

Kwa njia ya umaskini wa Yesu, Mwenyezi Mungu amependa mwanadamu aweze kutajirika, hii ndiyo mantiki ya Fumbo la Umwilisho na Fumbo la Msalaba. Alibatizwa mtoni Yordani si kwa vile alikuwa anahitaji toba, wongofu wa ndani na msamaha, bali alipenda kuonesha mshikamano wa dhati na binadamu mdhambi kwa kujitwika dhambi zake mabegani mwake, ili aweze kuwafariji, kuwaokoa na kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka huu anasema, Yesu alijifanya kuwa jirani na Msamaria mwema, kwa kuguswa na mahangaiko ya binadamu, ili hatimaye, aweze kumwonjesha huruma na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Utajiri wa Yesu unajionesha kwa namna ya pekee kwa kumtegemea Baba yake wa mbinguni, katika kutekeleza mapenzi yake na hatimaye kuvikwa taji la utukufu. Yesu anatambua kwamba, ni Mwana pekee wa Mungu, Masiha anayewaalika wafuasi wake kujitajirisha kutoka kwake na kushiriki udugu na kujitahidi kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa kuishi kama watoto wa Mungu na ndugu zake Kristo.

Kila wakati Mwenyezi Mungu anaendelea kumkomboa mwanadamu kutoka katika umaskini wake kwa njia ya umaskini wa Yesu, kwa kuonja na kuguswa na umaskini wa jirani zao tayari kujifunga kibwebwe kusaidia kupambana na umaskini: wa hali, kipato na maadili. Umaskini ni kielelezo cha kukosa imani, mshikamano na matumaini. Umaskini wa kipato unawakumba wote wanaoishi katika mazingira ambayo ni kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu.

Hawa ni watu wanaopokonywa haki na mahitaji msingi kama vile: chakula, maji, malazi, huduma bora za afya, fursa za kazi na ajira, maendeleo na ukuaji wa kitamaduni. Kanisa linaendelea kujisadaka kwa ajili ya kupambana na umaskini wa kipato katika mikakati yake ya kichungaji inayopania kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linaiona na kuitambua sura ya Kristo miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa linapania kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya binadamu vinaendelea kupewa kipaumbele cha pekee kwa kukomesha ubaguzi ambao wakati mwingine ni chanzo kikuu cha umaskini. Kanisa linahimiza matumizi bora ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Jamii iongozwe katika misingi ya haki, usawa, kiasi na ushirikiano.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna umaskini wa kimaadili, unaomfanya mwanadamu kuwa ni mtumwa wa dhambi, ulevi wa kupindukia, mcheza kamari na mtazamaji wa picha za ngono. Hili ni kundi la watu lililopoteza dira na mwelekeo wa maisha kwa kukata tamaa! Ni watu wanaoogelea katika utupu kwa kukosa fursa za ajira pamoja na kuendelea kudhalilishwa utu na hehima yao kama binadamu: wanakosa chakula na malazi; hawana haki ya kupata huduma bora katika sekta ya elimu, afya na maendeleo. Matokeo yake ni watu kuelemewa mno na umaskini wa kimaadili kiasi hata cha kutema zawadi ya maisha!

Umaskini huu ni chanzo kikuu cha myumbo wa uchumi kimataifa na matokeo yake ni umaskini na utupu wa maisha ya kiroho. Hali hii inajionesha pale mwanadamu anapomn’goa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vyake, kiasi hata cha kutema upendo na huruma yake. Hapa mwanadamu anadhani kwamba, anaweza kujitegemea mwenyewe na wala haitaji msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini ikumbukwe kwamba, ni Mungu peke yake anayeweza kukomboa na kumwokoa mwanadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Injili ni dawa inayoponya umaskini wa maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa kila Mkristo kuhakikisha kwamba, anashiriki kutangaza Injili ya Kristo katika medani mbali mbali za maisha, ili watu waonjeshe upendo na huruma ya Mungu; ili hatimaye, waweze kushirikishwa maisha ya uzima wa milele. Waamini wawe ni watangazaji amini wa Injili ya Furaha inayojikita katika huruma na matumaini; mwanga na faraja kwa wote wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti. Ni mwaliko wa kumfuasa Kristo aliyethubutu kuwaendea maskini; akaonesha sifa ya kuwa mchunga mwema kwa kumwendea Kondoo aliyekuwa amepotea, ili kumwonjesha upendo wake. Kwa kushikamana na Yesu, waamini wanaweza kuwa na ujasiri wa kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya na maendeleo endelevu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi hiki cha Kwaresima anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha ushuhuda wa pekee kwa maskini wa hali, maadili na maisha ya kiroho wanaokutana nao kila siku ya maisha yao, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Kwaresima ni muda muafaka wa kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia wengine, kwa kutambua kwamba, kwa njia hii pia tunafanya toba.

Waamini wanaweza kuwatajirisha jirani zao na hivyo kushiriki katika mchakato wa kuganga na kuponya umaskini unaomwandama binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini wataweza kukitumia kipindi hiki cha Kwaresima ili kupata neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe!

Ujumbe huu umehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.



KWARESIMA: Muarobaini wa Maisha ya Kikristu


Neno Kwaresima linatokana na neno la lugha ya kilatini Quadragesima; maana yake, namba arobaini. Kwa hiyo, Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini katika  Mwaka wa Liturjia au Mwaka wa Kanisa. Mwaka wa Kanisa ni maadhimisho ya mafumbo ya Ukombozi kwa njia ya Kristo, pamoja na Kristo na ndani ya Kristo katika Kanisa. Mwaka wa Kanisa una vipindi vikuu vitano; Majilio, Noeli, Kwaresima, Pasaka na dominika au jumapili za kawaida. Noeli na Pasaka ndivyo vipindi maalum katika Mwaka wa Kanisa na kabla ya kuadhimishwa hufanyika maandalizi maalum. Noeli huandaliwa kwa kipindi cha Majilio; na Pasaka huandaliwa kwa kipindi cha Kwaresima. Kwaresima huanza siku ya jumatano kwa Ibada ya Jumatano ya Majivu na huisha alhamisi jioni inapoanza Misa ya Karamu ya Bwana ya Alhamisi Kuu ambapo Siku Kuu Tatu za Pasaka huanza. Kwaresima ni kipindi pekee katika Mwaka wa Kanisa ambacho huanza kwa amri ya Kanisa (amri ya pili ya Kanisa): “Shiriki liturjia ya Jumatano ya Majivu, ambayo ni siku ya kufunga chakula; na Ijumaa Kuu iliyo siku ya kutokula nyama.”

Maana ya Kwaresima
Kwaresima ni kipindi muafaka cha kufanya toba. Toba ni sharti la msingi kabisa katika kuutafuta uzima wa milele au ufalme wa mbinguni. Mwenyezi Mungu ndiye anayemwalika mwanadamu ashiriki katika ufalme wake; basi mwanadamu naye anaitikia mwaliko huo kwa kufanya toba. Kwa hiyo toba ni kielelezo cha mwanadamu anayekubali mwaliko wa kuingia katika maisha ya imani ili ashiriki katika ufalme wa Mungu (Mk. 1:15): .....Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu akisema, “Wakati umetimia na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini Injili.”

Mwaliko wa Yesu kumtaka mwanadamu afanye toba ndiyo mwanzo wa historia mpya ya uhusiano kati ya Mungu na wanadamu. Tendo la toba linajikita katika maana kuu tatu za msingi:
1)    Kuacha njia potovu. Mtu anapotambua kuwa maisha yake ni kinyume na nia ya Mungu na hivyo anakubali na kuamua kubadilika. Hili ni tendo la toba linalompelekea mtu kubatizwa; na kwa mkristo humpelekea kurudi katika maisha ya kushiriki sakramenti za Kanisa.
2)    Kuacha fikra potovu. Ni mabadiliko ya dhati kwa wakristo wenye fikra potovu kuhusu ukombozi. Baadhi ya wakristo wanapotea kwa kuamini kuwa ubatizo peke yake watosha ili kuokoka. Ubatizo ni mwanzo wa maisha ya kumfuasa Kristo na ni ufunguo wa kuingilia kwenye haki na wajibu wa kikristo.  Kuokoka ni tendo la kuishinda dhambi na kuingia mbinguni. Kwa hivyo basi, si sahihi mtu kusema kuwa ameokoka angali bado yuko hapa duniani. Duniani tunaishi kwenye dhambi na wakati wowote tunaweza bado kuanguka katika dhambi hata kama tumeshabatizwa.
3)    Kuongoka. Ni tendo la kila siku kwa mkristo mwenye fikra sahihi juu ya ukombozi. Kuongoka ni kutambua udhaifu wa kibinadamu na kuitumia vema huruma ya Mungu kwa kuungama dhambi. Dhambi ipo duniani na ina nguvu kuliko sisi wanadamu. Lakini, neema ya Mungu ipo pia na ina nguvu kuliko dhambi. Kufanya toba maana yake ni kuitambua dhambi yako na kuiungama kwa Mungu ili upate neema. Neema ya Mungu inatupatia nguvu ya kupambana na dhambi na inatusaidia kukwepa nafasi ya kutenda dhambi tena.

Kwaresima na Pasaka
Uhalisia wa Kwaresima haupo tu katika toba bali hasa upo katika fumbo la Pasaka. Pasaka ndiyo kiini cha Mwaka wa Kanisa; na ndiyo sherehe kubwa kuliko sherehe zote katika liturjia. Ni sherehe inayoadhimisha ukombozi wa wana wa Mungu kutoka katika utumwa dhambi na kufanyika kwa taifa jipya la Mungu. Kimsingi, Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za toba zinayoitayarisha Pasaka. Pasaka huadhimishwa kila mwaka mara baada ya Kwaresima; na huendelea kuadhimishwa kila jumapili kwa mwaka wote (Jumapili zote zilizo ndani ya kipindi cha Kwaresima hazihesabiwi kati ya siku arobaini). Kila jumapili ni Pasaka, ni siku ya Bwana Mfufuka (dominika) ambapo taifa la Mungu hukusanyika ili kusherehekea ukombozi. Kwa umuhimu wake, Pasaka ya kila mwaka ni lazima itayarishwe kwa kipindi maalum; yaani Kwaresima. Pasaka na Kwaresima ni vipindi vinavyotegemezana. Kwaresima ndiyo inayotuandaa ili tustahili kusherehekea Pasaka.

Nguzo za Kwaresima
Siku arobaini za Kwaresima ni kielelezo cha utimilifu wa maandalizi ya Pasaka. Kadiri ya desturi za kibiblia, namba 1, 3, 7, 10, 12, 40 na 50 huitwa namba kamili. 40 ni namba kamili inayoashiria utimilifu wa kitu fulani. Kwa mfano; Musa alikaa siku arobaini mlimani sinai akisubiri kupewa Amri Kumi za Mungu, waana wa Israeli walisafiri jangwani kuelekea nchi ya ahadi kwa miaka arobaini, Yesu alifunga chakula siku arobaini jangwani kabla ya kuanza kuhubiri Habari Njema, Yesu alipaa mbinguni siku ya arobaini baada ya ufufuko wake. Matukio hayo na mengine mengi kuhusu namba 40 yanaashiria ukamilifu wa jambo fulani katika umuhimu na umaana wake.

Utimilifu wa siku arobaini za Kwaresima hujengwa katika nguzo kuu nne: Neno la Mungu, Sala na Sakramenti, Mfungo, na Matendo Mema.
1)    Neno la Mungu: Kipindi cha Kwaresima ni fursa nzuri ya kujipa muda wa kutosha kwa ajili ya kusoma na kutafakari Neno la Mungu. Tukisoma Biblia tutamjua zaidi Mungu wetu, tutajijua sisi wenyewe na hasa tutaijua nia ya Mungu kwetu ili tuweze kuyafanya mapenzi yake.
2)    Sala na Sakramenti: wakati wa Kwaresima ni vema kusali zaidi sala binafsi na sala za Kanisa ili kujitakatifuza na kuzibariki shughuli zetu za kila siku. Tushiriki Misa Takatifu, tushiriki ibada ya Njia ya Msalaba, tushiriki katika jumuiya zetu, tushiriki sakramenti za Kanisa (hasa Kitubio na Ekaristi Takatifu).
3)    Mfungo: Kwaresima ni wakati muafaka wa kujinyima vitu na mambo ya ziada. Kielelezo kikubwa zaidi ni kufunga chakula. Maana ya kufunga haiishii tu kwenye chakula bali pia ni kuacha mazoea mbalimbali yasiyo ya lazima na yasiyofaa. Kujinyima kunatuwezesha kupata fursa ya kusoma Neno la Mungu, kusali na kufanya matendo mema.
4)    Matendo Mema: Kila mmoja wetu ana shida fulani na anahitaji msaada wa mwenzake. Lakini pia wapo wenzetu wengine wenye shida zaidi kuliko sisi. Kile nilichojinyima kwa kufunga ndicho nimpatie mwenye shida zaidi kuliko mimi. Tuwatembelee wafungwa na wanaoishi katika upweke, tuwatibu wagonjwa, tuwazike wafu, tuwasaidie wazee, yatima na wajane, tuwashauri na kuwaombea wanaopotoka.
Umuhimu wa Kwaresima
Amri ya pili ya Kanisa inamtaka kila mkristo kushiriki kipindi cha Kwaresima tangu siku ya kwanza, yaani Jumatano ya Majivu. Toba ndiyo roho ya Kwaresima iliyojengwa juu ya Neno la Mungu, kusali, kushiriki sakramenti, kufunga na kufanya matendo mema. Siku arobaini za Kwaresima ni kielelezo kamili kinachotufundisha kuwa toba ni tendo la kila siku katika maisha ya mkristo. Wakati wa Kwaresima toba husisitizwa zaidi na kwa namna ya pekee ili kumjenga mkristo katika wajibu wa kuiishi imani. Katika kuiishi imani yetu tunapambana na shetani ambaye nia yake ni kuharibu mpango wa Mungu wa ukombozi. Silaha kubwa ya kupambana na shetani ni kuiishi roho ya toba inayojikita katika Neno la Mungu, sala na sakramenti, mfungo na matendo mema. Bwana wetu Yesu Kristo alifunga jangwani kwa siku arobaini kama maandalizi ya kufanya matendo mema ya kumkomboa mwanadamu. Kwa siku arobaini alifunga na kusali akamshinda shetani kwa kulitumia vema Neno la Mungu (Mt. 4:1-11). Kwa mfano huo wa Yesu, mkristo anatakiwa kuiishi toba wakati huu wa Kwaresima ili astahili kuishiriki Pasaka. Mkristo anatakiwa kuiishi kwa dhati toba ya kila siku ili amshinde shetani na hatimaye aingie kwenye Pasaka ya milele mbinguni.
Makala haya yameandaliwa na;
Dk. Padri Leonard Maliva Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustimo Stella Maris Mtwara. simu namba 0754666908