
Changamoto hizo zimesababisha wagonjwa hao kukata tamaa ya kuendelea na matibabu na kuamua kukatisha dozi na kurudi majumbani mwao.
Hali hiyo hutokea baada ya kuchoka kuhangaika kutafuta fedha za kumudu gharama za dawa huku wakizidi kunyanyasika wakiwa ugenini kwa kuja hospitali ya Ocean Road (ORCI) ambayo inashughulikia tiba na uchunguzi wa ugonjwa huo.
Changamoto kubwa ambayo waathirika wengi wanaomba kusaidiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa aina ya Chemotherapy ambayo hupewa kama tiba katika hospitali hiyo.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa Chama cha Matumaini ya Mwanamke, mmoja wa wagonjwa hao, Bihuda Shaiza, anasema huwa wanaambiwa dawa hizo ni bure lakini wanapoziulizia mara nyingi huambiwa zimeisha hivyo hulazimika kununua kwenye maduka ya nje ambako huuzwa ghali.
“Nimelipia dozi hiyo mzunguko wa kwanza kwa shida sana kwa gharama ya Sh 200,000 baada ya kuambiwa dawa hiyo haipatikani hospitalini, hapa nilipo sijui dozi ya pili na ya tatu nitaipata vipi,”anasema Shaiza.