Week Hot newz

Tafakari ya neno la Mungu, Jumapili ya VI ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa

Ninakuleteeni tena ujumbe wa Neno la Mungu katika Dominika ya VI ya kipindi cha mwaka A. Neno la Mungu latukumbusha kuwa Kristu Mwana wa Mungu hakuja kutangua Torati bali kuikamilisha. Kristo ni sheria mpya na hivi analeta ukamilifu wa sheria ya Mungu. Katika Somo la kwanza toka kitabu cha Yoshua bin Sira, Mungu anatangaza uhuru kamili kwa mwanadamu.

Anamtaka mwanadamu aamue mwenyewe kumchagua Mungu au kumchagua shetani! Anatumia alama za moto na maji, uzima au mauti akitaka mtu aone katika uhuru wake mwenyewe wajibu wa kuchagua jema au baya. Kwa hakika ni alama yakwamba mwanadamu alizaliwa akiwa huru na hivi matendo yote ya nje hayawi ya kutenda tu bali mwanadamu anawajibika kuchagua kwa kuwa anao uwezo huo. Kama anataka maisha ya kiroho basi atachagua amri za Mungu, kama anataka kifo cha kiroho basi atachagua rushwa na vionjo vya mwili!

Katika somo la II mtume Paulo anaendelea kuwasisitizia Wakorinto juu ya hekima ya Mungu yakuwa ni siri ambayo haikufunuliwa kwa watawala wa dunia bali ilifunuliwa kwa Mitume. Kwa kuthibitisha hilo anasema kama wangalipewa hekima hiyo wasingalimtundika msalabani Mwana wa Mungu. Ndiyo kusema hekima waliyonayo wakristu si hekima ya kawaida ya kidunia bali hekima ya kimungu. Ni hekima ambayo inakuja kwetu kwa njia ya mpango wa Mungu ulio wa milele. Siri ya hekima hii ni kwamba wanaijua wale waliokomaa katika imani na tumaini la kweli katika Kristo Yesu.

Katika somo la Injili , Mwinjili Matayo akinukuu maneno ya Bwana anasema sikuja kuondoa hata yodi moja wala nukta moja bali kuifanya sheria ya Mungu iweze kueleweka vizuri zaidi katikati ya watu. Nimekuja kuifanya sheria iwe kwa ajili ya watu wa Mungu yaani kuwajengea uhuru kamili.

Mpendwa msikilizaji, Bwana anao uwezo wa kutafsiri sheria katika mtazamo wa mapendo kwa watu. Ona jinsi anavyowapenda wanadamu na hata akathubutu hata kuivunja Sabato. Anachotafuta kwa uhakika ni kuipa sheria uwezo wa ndani unaozaa mapendo kwa mwanadamu. Sheria iliyokuwa kavu anaipa nyama na hivi inaweza kutafunwa kwa urahisi!

Anakazia pia maana na namna ya kutafsiri sheria, akitaka tusiishie katika kile kilichoandikwa katika mwonekano wa kawaida, mfano usiue, kwa namna ya kutambua kuua kama ile hali ya kuondoa maisha kimwili, bali tutazame ndani na kugundua kuwa hata wale walio na lugha chafu, hasira, chuki wanashiriki katika mauaji ya wenzao.

Anatoa mfano wa kunawa hata viwiko ulio utamaduni wa Wayahudi kabla ya kwenda Hekaluni kwa ajili ya kutolea sadaka, hili kwake halina maana kama mmoja haangalii moyo wake. Matendo haya ya kilitrujia hayatoshi kama hayaambatani na toba ya ndani na upatanisho na wenzetu. Bwana akisonga mbele na mafundisho yake anakazia amri ya ndoa yakwamba kadiri ya mpango wa Mungu ndoa haitenganishwi. Ndiyo kusema katika mantiki ya ndoa ya kudumu, yafaa kukazia maisha ya unyenyekevu ili kuweza kuhimili vitimbwi nyemelezi dhidi ya familia. Hii haina maana yakwamba wale walioanguka katika utengano wadharauliwe katika jumuiya bali waombewe daima kwa ajili ya mabadiliko yao ya ndani.

Mpendwa mwanatafakari, Bwana anazidi kufunua namna ambavyo mkristu anapaswa afanye anapojikuta mbele ya kutoa ahadi na kiapo. Anawaalika wakristu daima wawe ni watu wa kusema ukweli daima. Maneno yao yawe ya unyoofu, wasiishi undumilakuwili yaani katika mazingira fulani ndiyo na katika mazingira tofauti siyo kwa jambo lilelile. Hii ni sumu kwa familia na jumuiya kwa ujumla, ni sumu wa serkali na utawala wa nchi.

Basi mpendwa jaribu kufuata hatua kwa hatua mafundisho ya Bwana kwa ajili ya kukua kiroho katika tumaini la kweli litakalokupa uzima wa milele. Nikutakie furaha na matumaini katika kushika mausia ya Bwana ambayo ndiyo sasa dira kamilifu na itupayo uhuru kamili wa wana wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S

Majibu ya Papa Francisko kwa wanandoa watarajiwa!



Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya Wapendanao Duniani kwa Mwaka 2014 amewataka vijana kukuza na kujenga ndani mwao upendo unaodumu hadi kifo kitakapowatenganisha; wajitahidi kumwilisha ndani mwao mtindo wa maisha ya wanandoa ili kukabiliana na changamoto za maisha ya ndoa na familia pamoja na kuthamini adhimisho la Sakramenti ya Ndoa ya Kikristo, kwani hapo wanajichotea neema na baraka katika mchakato wa utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anasema, upendo wa maisha ya ndoa ni wa kudumu hadi pale kifo kitakapowatenganisha kwani haya ni mahusiano kati ya Bwana na Bibi, yanayokuwa na kukomaa hatua kwa hatua, kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni upendo unaowashirikisha wanandoa kazi ya uumbaji na kamwe si upendo mpito usioguswa na mahangaiko ya mwenzi wake. Upendo huu hauna budi kurutubishwa kwa kukutana na Yesu kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu na Matendo ya huruma.



Ubora wa ndoa unajikita katika udumifu wake, changamoto kubwa kwa wanandoa Wakristo. Pale wanandoa wanapohisi kwamba, wamepungukiwa na divai ya upendo na udumifu wasisite kumshirikisha Kristo katika upendo wao wa kila siku; ili wapendane na kutakiana mema.

Baba Mtakatifu anawaambia wanandoa watarajiwa kwamba, kuishi kwa pamoja ni sanaa na hija inayohitaji uvumilivu, inapendeza na kushangaza; ni safari inayojikita katika maneno: tafadhali, asante na samahani. Huu ni urithi ambao wanandoa wanapaswa kuwarithisha watoto wao. Ikumbukwe kwamba, unyenyekevu ni fadhila inaondoa chuki na kujenga upendo.

Si rahisi sana watu kujenga utamaduni wa kushuruku, lakini wanandoa wajenga na kuimarisha utamaduni wa kushuruku kwani mwenzi wako ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kukosa na kukoseana ni ubinadamu, kusamehe na kusahau ni kuanza hija ya utakatifu wa maisha. Wanandoa wajifunze kutambua mapungufu yao ya kibinadamu na kuwa tayari kukiri makosa yao, tayari kuanza tena upya. Wajenge utamaduni wa kusikilizana kwa makini, ili kujenga na kuimarisha familia ya Kikristo.

Baba Mtakatifu anasema hakuna Familia inayoweza kujidai kwamba ni kamilifu na takatifu; wala hakuna Bwana au Bibi ambaye ni mkamilifu, kila mtu ana fadhila na kasoro na mapungufu yake, changamoto ya kujenga utamaduni wa kuomba na kutoa msamaha kila siku na kwa njia hii Ndoa zinaweza kudumu daima.

Maadhimisho ya Sakramenti ya Ndoa Kanisani yazingatie umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa na kiasi bila kumezwa mno na malimwengu. Watambue uwepo wa Yesu Kristo anayeendelea kufanya miujiza kwa wanandoa kama alivyofanya takribani miaka elfu mbili iliyopita kwenye Arusi ya Kana. Kila kitu kiwe na kiasi na kielelezo cha furaha ya ndani na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanandoa wawashirikishe jirani zao ile furaha na kumbu kumbu ya maisha yao ya ndoa.

Haya ndiyo yaliyojiri katika Maadhimisho ya Siku ya Wapendanao Duniani kwa Mwaka 2014, tukio ambalo litakumbukwa na wanandoa hawa watarajiwa katika hija ya maisha yao ya ndoa na familia. Mji wa Roma, umefurika umati wa vijana na wasichana wanaotembea huku wameshikana mikono na maua ya waridi mikononi mwao alama ya upendo!

Friday, February 14, 2014 HISTORIA FUPI YA SIKU YA WAPENDANAO


Sikukuu ya wapendanao inasherekewa kila ifikapo tarehe 14 mwezi wa pili kila mwaka.
Watu wengi wanaosherekea siku hii kwa Nchi za Afrika Mashariki ni vijana walio kati ya miaka 18 hadi 35.
Historia ya sikukuu hii inaanzia miaka mingi jijini, Roma, Italia ikiwa inahusishwa na mtakatifu Valentine au Valentinus aliyekuwa akiishi jijini humo katika karne hiyo. Wakati wa maisha ya mtakatifu Valentine Roma ilikuwa ikitawaliwa na Kaisari, Claudius II, ambaye alipata hisia wakati huo kuwa askari mkakamavu na bora zaidi ni yule asiyekuwa na mke wala familia. 
Claudius alilifanyia kazi wazo lake na aliamua kupiga marufuku ndoa zote kwa askari wa nchi hiyo, jambo ambalo halikukubaliwa na mtakatifu, Valentinus. Hivyo Valentinus alichukua jukumu la kukaidi amri ile na kuendelea kuwafungisha ndoa kwa siri maaskari waliokuwa wakitaka kufungishwa ndoa.
 
Haikuchukua muda mrefu, taarifa zilimfikia mfalme, Claudius na alipopata habari hizo aliamuru kukamatwa na kufungwa gerezani na kisha Valentinus aliuawa kwa amri ya Kaisari. Kuna taarifa zinadai kuwa kabla ya kuuawa kwa Valentine wakati huo akiwa amefungwa, mtakatifu Valentine aliandika barua ya salamu kwa binti aliyekuwa amekwenda  kumsalimia gerezani. Na mwisho wa barua kulisomeka maneno yaliyoandikwa ‘From your Valentine’.
Tangu hapo Valentine akawa anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na siku hii ikawa inaadhimishwa duniani kote.
Baada ya kufariki kwa mtakatifu huyo ndipo wananchi wengi duniani wakaamua kuadhimisha siku hii kama sherehe ya kumkumbuka Mtakatifu Valentinus

Baraza la Kipapa tarehe 18 hadi 20 Februari 2014 litaadhimisha Kongamano la Kimataifa



Baraza la Kipapa la Ibada na nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kuanzia tarehe 18 hadi 20 Februari 2014 litaadhimisha Kongamano la Kimataifa, kuhusu Jubilee ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu Liturujia ya Kanisa "Sacrosanctum Concilium", litakaloongozwa na kauli mbiu Waraka wa Liturujia, shukrani na dhamana kwa ajili ya mabadiliko ya Kikanisa".

Kongamano hili litawashirikisha wadau kutoka sehemu mbali mbali za dunia na utakuwa ni muda muafaka kwa ajili ya kusali, kutafakari, kuabudu na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Ni kipindi cha kuonjeshana uzoefu na mang'amuzi ya Liturujia ya Kanisa, tayari kutwika hadi kilindini kwa ajili ya