PAMBANO la kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi
mwaka 2018 kati ya timu ya soka ya Tanzania `Taifa Stars’ dhidi ya
Algeria, linalotarajiwa kupigwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
limekuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa soka ndani na nje ya nchi.
Aidha, idadi kubwa ya mashabiki katika `vijiwe’ vya soka, wameonesha
dhamira ya dhati ya kutaka kuiunga mkono Stars. Ujio wa Mbwana Samatta
na Thomas Ulimwengu wa Stars wanaochezea klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na pia taarifa za Rais, Dk John Magufuli
kuwa atajitokeza kuishangilia timu ya taifa ya Tanzania `Mwanzo Mwisho’,
kwa pamoja vimechangia kuongeza hamasa ya mchezo huo.
Samatta na Ulimwengu wametoka kuweka historia ya kuwa wa wanasoka wa
kwanza wa Tanzania kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya
klabu yao kufanya hivyo mwishoni mwa wiki, huku Samatta akiongeza taji
jingine la ufungaji bora.
Aidha, kwa Magufuli, hilo litakuwa pambano lake la kwanza kushuhudia
akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu alipoapishwa
kuchukua nafasi ya Rais Jakaya Kikwete, mwanamichezo aliyeondoka
madarakani baada ya kumaliza muda wake wa uongozi kwa mujibu wa Katiba
ya nchi.
Tayari waamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Mali, Keita Mahamadou,
Diarra Bala, Niare Drissa Kamory na mwamuzi wa akiba Coulibaly Harouna
wameshawasili nchini tangu jana asubuhi, huku mtathimini wa waamuzi
Attama Ibrahim Boureima kutoka nchini Niger naye akiwa tayari nchini
tangu juzi usiku.