Week Hot newz

Basata yalitoa kifungoni shindano la Miss Tanzania


 

Dar es Salaam.
Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) limemfungulia mwandaaji wa shindano la urembo la Miss Tanzania, Lino International Agency baada ya kuomba radhi na kufanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza na kutekeleza masharti aliyopewa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo,  Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Godfrey Mngereza amesema  LINO International Agency imepewa kibali cha muda kisichozidi miezi minne kwa ajili ya maandalizi ili kukamilisha usajili wa mawakala katika ngazi husika.
Mngereza amesema kuwa mapungufu yaliyobainishwa ni pamoja na kutofuata sheria ,kanuni za uendeshaji matukio ya sanaa nchini ,kutokuwakilisha nyaraka mbalimbali za shindano lake na mikataba ya washirki,kutumia  mawakala ambao hawajasajiliwa na kupewa vibali na Baraza la sanaa la Taifa.
Amesema miongoni mwa mapungufu yaliyofanyiwa kazi na Kampuni ya Lino ni mchakato wa kusajili mawakala  na kufanyia marekebisho kanuni na taratibu za uendeshaji wa mashindano ya urembo ya Miss Tanzania.

Rais huchaguliwa kwa kura, si maandamano

mafuriko
MAANDALIZI ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka huu ni ya kipekee kutokana na kupambwa na mbwembwe nyingi ikiwamo misafara na maandamano makubwa ya wagombea urais. Ni jambo la kujivunia kuona kwamba wananchi wengi wameonyesha mwamko mkubwa wa ushabiki wa kisiasa.
 Hadi sasa dalili za awali zinaonyesha kwamba ushindani mkubwa wa kinyang’anyiro cha urais utakuwa kati ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 Misafara na maandamano makubwa ya wagombea urais hao vinazidi kuteka akili za wananchi wengi waliogawanyika katika makundi mawili yanayoelekea kulingana; kundi linalomshabikia Lowassa na jingine linalomuunga mkono Dk. Magufuli.
Kutokana na misukumo mikubwa ya hisia za kisiasa, kuna wananchi ambao ukiwambia kuwa Dk. Magufuli ndiye rais ajaye wanaweza kukutoa roho! Vivyo hivyo, wapo wengine ambao wakikusikia unasema njia ya Lowassa kuelekea Ikulu ni nyeupe wanaweza kukutenga katika jamii.
Ukiuliza sababu za wanaoamini kwamba Lowassa atashinda urais watakwambia ni misafara na maandamano makubwa ya watu wanaoonekana kumshabikia. Hata kwa upande wa Dk. Magufuli jibu ni hilo hilo!
Lakini kwa upande mwingine, wapambe wa Lowassa wanamuelezea kwamba ni mwajibikaji na mwenye uamuzi mgumu katika masuala ya umma, hivyo anafaa kukabidhiwa uongozi wa nchi kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania kiuchumi na kijamii.
Wengine wanaamini kwamba Dk. Magufuli ndiye anafaa kukabidhiwa mikoba ya Ikulu ya Tanzania baada ya Rais Jakaya Kikwete. Kwamba mgombea huyo ni msafi asiye na kashfa za ufisadi, lakini pia hayumbishwi katika kusimamia misingi ya uwajibikaji kwa umma na kutetea maslahi ya Taifa.
Kimsingi hakuna wa kuwalaumu mashabiki wa pande hizo mbili maana wanatekeleza haki yao ya kikatiba na kidemokrasia ilmradi hawavunji sheria za nchi.
Lakini pamoja na haki hiyo, mashabiki hawa wanapaswa kutafakari vizuri juu ya misimamo yao ya kuamini kwamba misafara ya kifahari na maandamano makubwa ya watu ni kielelezo tosha cha ushindi kwa mgombea urais.
Si sahihi kutumia takwimu za idadi kubwa ya watu katika misafara na maandamano kuwa ndiyo kigezo cha ushindi kwa mgombea, maana mbwembwe za aina hiyo hazimchagui rais. Kinachomchagua rais ni kura zinazopigwa kwa utaratibu uliowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), si vinginevyo.
Tukumbuke kwamba mtu yeyote ana uhuru wa kushiriki maandamano ya wagombea urais, ubunge na udiwani bila kuulizwa kitambulisho. Lakini haruhusiwi kupiga kura za kuchagua viongozi wa nafasi hizo kama hana kitambulisho husika na iwapo atakiuka maelekezo ya NEC.
Hii ni sawa na kusema kwamba katika Tanzania hii, kila mtu, yaani mwenye kitambulisho cha kupiga kura, asiye nacho, mtoto na hata mgonjwa wa akili, wote wana uhuru wa kushiriki maandamano ya wagombea, jambo ambalo ni tofauti na utaratibu wa kupiga kura za kuchagua viongozi wa kisiasa.
 Ikumbukwe hata wakati wa ziara ya Rais Barack Obama wa Marekani hapa Tanzania Julai 2013 maelfu ya watu walijitokeza kumlaki, kumwona na kusikia anachosema, ingawa si kweli kwamba wote walikuwa wanampenda wala kumkubali na kumfurahia. Miongoni mwao walikuwapo wanafiki waliochukizwa na ziara hiyo wakiamini kimakosa kwamba alikuja kusaini mikataba ya kuuziwa nchi yetu!
Misafara na maandamano ya wagombea ni sawa na kokoro ambalo wakati mwingine hubeba viumbe wasiohitajika. Kuna watu wanashiriki misafara na maandamano ya aina hiyo wakiwa na dhmira ya kweli ya kuwaunga mkono wagombea, lakini wengine wanakwenda kufanya kazi zisizo za kisiasa kama vile kulinda usalama, kupiga picha, kurekodi video na sauti.
 Kwa hiyo, kuamini au kujitumainisha kwamba idadi kubwa ya watu kwenye misafara na maandamano ya wagombea ndiyo kigezo cha ushindi, ni sawa na ndoto za mchana kweupe ambazo daima hazitimii.
Itakuwa jambo la maana kama mashabiki na wapambe wa kisiasa watazingatia umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kupiga kuza za kuwachagua wagombea wanaowataka kuliko kujiridhisha na wingi wa watu katika maandamano ambayo hayana nafasi ya kuchagua viongozi.
Kuamini kwamba idadi kubwa ya watu kwenye misafara na maandamano ya wagombea ndiyo kigezo cha ushindi ni dhana potofu na matokeo yake mwisho wa siku upande unaoshindwa katika uchaguzi hudhani umeibiwa kura, na wakati mwingine hugeuka kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani usiyo wa lazima.
Jambo la msingi zaidi kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ni kuongeza juhudi za kuhamasishana (kwa wenye vitambulisho waliojiandikisha kwenye dafrari la kudumu la wapigakura) kujitokeza kwa wingi kupiga kura za kuchagua viongozi tunaowataka siku ya Jumapili Oktoba 25, mwaka huu.
Sambamba na hilo, wananchi wote tunapaswa kushiriki mikutano ya kampeni za wagombea kutoka vyama mbalimbali vya siasa ili kuwachuja na kubaini wanaofaa kutuongoza baada kusikia sera na ilani za vyama vyao.
Ingawa baadhi ya wananchi imani zao zimejikita kwenye vyama, lakini ni vizuri zaidi kuchagua mtu kwanza, chama baadaye kwa sababu maendeleo na mabadiliko tunayoyataka yataletwa na viongozi watu, siyo vyama ambavyo daima haviwezi kufanya chochote.
 Lakini pia, tushirikiane kuuombea Uchaguzi Mkuu ujao baraka za Mungu ili ufanyike kwa uhuru na haki. Tuombe tukitambua kwamba mshindi wa uchaguzi huo atakuwa ni yule aliyepigiwa kura nyingi kwa utaratibu halali, si vinginevyo. Mungu ubariki Uchaguzi Mkuu Tanzania 2015.

Nani akinusuru Chuo cha Ualimu Korogwe?


Chuo cha Ualimu Korogwe
S.L.P. 533, Korogwe
NDUGU Mhariri,
Sisi ni watumishi wazalendo katika Chuo cha Ualimu Korogwe, mkoani Tanga. Tunasikitishwa na uendeshaji mbovu wa chuo chetu.
Uongozi wa juu wa chuo umekuwa dhaifu katika kuchukua uamuzi wa kiutawala ili kulinda hadhi ya chuo hiki kitaifa na kimataifa. Tumejitahidi bila mafanikio kukabili uzembe wa kiuongozi chuoni hapa.
Juhudi zetu ni pamoja kuripoti katika mamkala husika, ikiwamo ngazi ya wizara. Tunaamini kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha za chuo, kuanzia fedha za michango, miradi ya chuo na hata zile zinazoletwa chuoni kutoka wizarani.
Wapo wenzetu waliodiriki kuhoji hadharani, kumuandikia nyaraka mbalimbali na hata kushauri uongozi wa juu wa chuo bila mafanikio. Maarifa yote ya kiutaratibu na kikanuni yalifuatwa bila mafanikio na wengine ilibidi siku moja kumfungia mkuu wa chuo ofisini kama hatua ya kumshinikiza aondoe uozo chuoni.
Hatua zote hizo zimekuwa zikilenga kuwezesha mabadiliko ya kimfumo chuoni na kujibu hoja za msingi, ikiwamo kuitishwa kwa vikao vya ripoti za mapato na matumizi.
Athari za uongozi mbovu chuoni zimeanza kujitokeza ambazo ni pamoja na kuporomoka kwa kiwango cha taaluma chuoni. Kwa mfano, matokeo ya watahiniwa wa mtihani wa taifa kwa mwaka 2012 ni mabaya, zaidi ya watahiniwa 310 wanatakiwa kukariri masomo waliyofeli hapo mwakani wakati wenzao watakapokuwa wanafanya mtihani mingine, pia wapo wanachuo 67 waliofeli kabisa hivyo hawana sifa za kuwa walimu popote pale.
Gharama serikali inazoingia kumsomesha mwanachuo mmoja kwa miaka miwili si chini ya milioni sita (ukijumuisha mishahara ya watumishi, na gharama nyingine za uendeshaji).
Wakufunzi wamekuwa wakiomba vikao vya kujadili hali ya kitaaluma, kwa mfano, kujadili matokeo hayo mabovu lakini kutokana na maovu ya uongozi, imekuwa vigumu vikao hivyo kufanyika.
Tunaamini vikao haviitishwi kwa sababu uongozi utabanwa kuhusu mwenendo wake mbovu. Kero mbalimbali zimekithiri chuoni, kuanzia hali duni ya maktaba ambayo huchangiwa Sh. 10,000 na kila mwanachuo tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000 hadi leo lakini hali ya jengo la maktaba si ya kuridhisha.
Hakuna vitabu vya kutosha maktaba, chumba cha maktaba kilichopo hali yake ni mbaya, maabara ya kompyuta si ya kuridhisha. Kuna madai kwamba fedha zinazotoka wizarani kwa ajili ya ukarabati zimekuwa zikitafunwa sambamba na fedha za michango ya Sh. 10,000 kila mwaka ya wanafunzi.
Mashine za kudurufu ni tatizo, wino kwa ajili ya mashine hizo hakuna na wanafunzi hujigharimia ili angalau kujitafutia elimu bora. Inafikia mahali hata barua za mkuu wa chuo zinakaa kwa karani wake zaidi ya wiki mbili bila kuchapwa kisa eti wino hakuna! Hii ni aibu kwa chuo kikubwa kama hiki.
Ndugu mhariri, chuo kina miradi na huduma kadhaa ambazo ni sehemu ya vyanzo vya mapato bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini. Baadhi ya vyanzo vya mapato vya chuo ni pamoja na fedha zinazotokana na huduma ya chakula kupitia mradi wa “Domestic Science” (DS).
Mradi huu unaendeshwa zaidi wakati wa kazi mbalimbali maalumu zinazofanyika eneo la chuo, kwa mfano shughuli za Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) au shughuli nyingine kama semina.
Mradi huu ni miongoni mwa miradi mikubwa inayokiingizia chuo fedha nyingi lakini hali ya chuo haiendani na mamilioni ya shilingi yanayopatikana kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato.
Upo mradi wa mnara wa simu, mradi mdogo wa kantini ya chakula, mradi wa huduma ya mafunzo ya muda mfupi kwa wanafunzi wa sekondari maarufu kwa jina la TAI (Teachers Academic Initiatives) na wale wa elimu ya awali ambao nao unaingiza fedha. Tunaamini mapato ya miradi hii hayafanani na taarifa zilizopo na kwa kweli tunashangazwa na wakaguzi wa hesabu wanaofika chuo hapa na kuondoka kimya kimya bila kuwapo na ripoti kuhusu hali halisi.
Chuo chetu kimepoteza mvuto kwa sababu ya uongozi mbovu, miaka ya nyuma chuo kilikuwa kikipokea wanafunzi zaidi ya 1500 lakini leo hii hata 200 ni vigumu kuwapata. Wakati mwingine tunadhani ni njama zinazohusisha hata vyuo binafsi ili wanafunzi wakasome huko badala ya chuo hiki chenye sifa ya kipekee nchini.
Haturidhiki na mbinu zinazotumiwa na uongozi wa chuo katika kukabili matatizo haya kwa sababu uongozi ni sehemu ya matatizo haya.
Uongozi wenye tuhuma katika miradi ya chuo ukiwamo mradi wa majoho kwa ajili ya mahafali ya wanachuo haupaswi kuaminika kuongoza chuo cha kitaaluma, tena taaluma nyeti ya ualimu. Uongozi unaojihusisha na michango ya fedha za wanafunzi katika hali ya shaka kubwa haupaswi kuongoza chuo hiki.