Papa amesema, uhalisi huu wa kuonekana wenyewe peke yake, ni fumbo linaonyesha upendo na fadhila nyingi za Mungu zilizofichika ndani mwake ambazo hutekelezwa na waumini wa Kanisa duniani kote. Na ili kuelewa uhusiano kati ya yale yanayoonekana na yale yanayofanyika katika kipimo cha kiroho ndani ya mwili wa Kristo, yaani Kanisa, tunahitaji kumtazama Yesu mwenyewe, kama Mungu na Mwanadamu.
Katika ubinadamu, Kristo anatimiza Mpango Mtakatifu wa Mungu wa kumkomboa binadamu. Na hivyo katika macho ya imani , tunaweza kuelewa jinsi Kanisa linavyo onekana katika mwelekeo wake wa kuzamisha ukweli kamili wa kiroho. Na kwa njia ya sakramenti zake na ushuhuda wake kwa Kristo, katika dunia yetu, Kanisa hutafuta kutangaza upendo wa Mungu na huruma yake kwa watu wote, hasa kwa maskini na wahitaji.
Katika mafundisho yake Papa, amesema, kwa mara nyingi tunasikia watu wakilalamikia Kanisa halijafanya hiki, halijafanya kile. Lakini, Papa akahoji , Kanisa ni nani hasa? , Je ni Mapadre au Maaskofu au Papa? Hapana , Kanisa ni wabatizwa wote. Waamini wote wa Kristo huunda Kanisa. Kanisa linaloonekana si tu la Mapadre, Maaskofu au Watawa, au Papa, bali ni mjumuiko wa waamini wote wabatizwa, wake kwa waume wa pande zote za dunia , ambao hutangaza kwa vitendo upendo wa Mungu usiokuwa na kipimo. Ni familia zilizo simama imara katika imani , ni wazazi wanaoieneza imani kwa watoto wao , ni wagonjwa wanao yatolea mateso yao kwa Bwana wa Kanisa. Huo ndiyo ulikuwa ujumbe wa Papa katika Katekesi hii.