RAIS Dk John Pombe Magufuli amewaapisha wakuu wa mikoa aliowateua hivi karibuni na kuwapa maagizo mazito. Rais amewaambia wakafanye kazi ya kutatua kero za wananchi na sio kwenda kufanya siasa.
Katika hotuba yake fupi kwao, Rais amewapa wakurugenzi wa halmashauri siku 15 wawatoe katika Orodha ya Malipo ya Mshahara (Pay Roll) wafanyakazi hewa wote katika halmashauri zote nchini.
Ameonya kuwa halmashauri yoyote baada ya muda huo itakayokuwa na mfanyakazi hewa, mkurugenzi wake atakuwa amejifuta kazi mwenyewe.
Vilevile Rais amewaagiza mawaziri wokati wowote kuwaeleza watendaji wao wawaondoe wafanyakazi hewa wote ndani ya kipindi hicho cha siku 15 na kubainisha kuwa watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo watafukuzwa kazi kwani sheria ni msumeno.
Rais ameeleza matumaini yake kuwa kupitia kwa wakuu hao wa mikoa, kero nyingi zitamalizwa na wananchi watakuwa huru katika nchi yao. Baadhi ya kero ambazo Rais amezigusia ni migogoro ya wafugaji na wakulima, ukosefu wa usalama barabarani hadi mabasi kusindikizwa na polisi pamoja na tatizo la njaa.