Na Paskal Linda http://batarokota.blogspot.com/
Kweli, aliyekubuhu katika uovu anaweza kumfunda mwana awe malaika? Au mwalimu juha wa mazuzu anaweza kuandaa na kutoa mwanafunzi gwiji? Jambazi anathubutu kumkemea kibaka?
Kweli, aliyekubuhu katika uovu anaweza kumfunda mwana awe malaika? Au mwalimu juha wa mazuzu anaweza kuandaa na kutoa mwanafunzi gwiji? Jambazi anathubutu kumkemea kibaka?
Kweli fukara aliyejifahari katika hali yake anaweza kumuongoza mjasiriamali katika umaridadi wa kutafuta neema?
Haya ni baadhi ya maswali wengi tumekuwa tunajiuliza kwa kutafakari
mitihani inayotukabili. Maswali kama haya tumeyasikia yakiulizwa kwa
namna mbalimbali katika semi, methali na hata vioja vya kisa mkasa.
Uchaguzi huu pia una vioja vyake. Kutokana na uchu wa kusaka kura
kuna mambo tunayashuhudia ambayo hakika yanaibua maswali mengi, tena
sana.
Hivi karibuni mgombewa wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward
Lowassa, ameshutumiwa na hasimu wake kwa kutoa ahadi ambayo
inatafsiriwa kuingilia uhuru wa mahakama na kubashiria kuivunja katiba
ya nchi. Mgombea huyo, pamoja na mambo mengine, aliahidi kumwachia huru
mtu fulani aliyetiwa hatiani na mahakama wapo atachaguliwa kuwa Rais.
Naye mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, amekuwa akimwaga ahadi
ambazo baadhi zinaelekea kuvunja sheria na haki za wengine. Miongoni
mwake ni ahadi ya kunyang’anya watu mali zao au kuwapa wananchi faida
ambayo huna mamlaka nayo.
Kwa lugha za wachambuzi ni kwamba wagombea wa aina hii wanakosolewa
kwa kutoa, bila haya, ahadi hewa wakati wakitambua fika kuwa
unachokisema hatotenda. Hawa ndio aina ya watu waliokomaa kuturubuni
watuongoze, sisi wananchi ambao tunasaka bado masihi wa kutuvusha
kuelekea kwenye Tanzania tarajiwa, Tanzania yenye neema.
Wapo miongoni mwetu waliohoji ombwe ama uhaba/ukavu wa uongozi
nchini Tanzania. Tutakuaje na viongozi bomba kama desturi imekuwa
kuongoza kwa njia ambazo ni za kihuni, yaani ambazo hazifikii wala
kukidhi viwango vya ustaarabu?