Week Hot newz

Mwaka Mmoja watimia Baba Mtakatifu Benedikto 16, alipotangaza rasmi kung'atuka

Ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alipotangaza rasmi kwamba, kwa hiyari yake mwenyewe na utashi kamili ameamua kung'atuka kutoka madarakani, ili kutoa nafasi kwa Makardinali kuweza kumchagua Khalifa mwingine wa Mtakatifu Petro.

Maneno haya yakaushangaza ulimwengu. Kwa Kanisa hili likawa ni tukio la kinabii, ili kutoa nafasi kwa Mama Kanisa kuendelea kufanya mageuzi ya kina katika maisha na utume wake, Mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza; waamini wakijikita kutangaza Habari Njema ya Wokovu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Akachaguliwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameamua kuendeleza mageuzi yaliyokuwa yameanzishwa na Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika maisha na utume wa Kanisa kwa kukazia uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, bila kumezwa na malimwengu, mambo ambayo yamelisababishia Kanisa kujikuta linaandamwa na kashfa mbali mbali. Maaskofu mahalia wamepewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanatekeleza utume wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ujasiri na moyo mkuu.

Kuna waamini ambao bado wana madonda makubwa katika mioyo yao, jambo la msingi kwa Kanisa ni kujikita katika mchakato wa uponyaji na upatanisho, ili Kanisa liweze kusonga mbele kwa ari kubwa zaidi katika azma yake ya kuwatangazia watu Injili ya Furaha.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliona kashfa ya matumizi haramu ya fedha iliyokuwa inalinyemelea Kanisa kwa kutumia migongo ya wajanja wachache ndani ya Kanisa. Vatican ikatunga na kuridhia sheria inayopiga vita utakatishaji wa fedha haramu inayoweza kutumika kugharimia vitendo vya kigaidi. Papa Francisko anaendelea kukazia umuhimu na dhamana ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa.

Kanisa linamshukuru na kumpongeza Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kwa ujasiri na uamuzi wake wa busara wa kung'atuka kutoka madarakani, ili aweze kupata nafasi kubwa zaidi ya kusali na kutafakari.



Papa mstaafu Benedikto XVI kwa sasa ana utume wa sala na tafakari; uamuzi wake ni ushuhuda wa kinabii!

Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican, anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa sasa anautumia muda wake mwingi kwa ajili ya kusali na kutafakari na kwamba, uamuzi wake wa kung'atuka kutoka madarakani ni wazo ambalo alilitafakari, akasali na kulipembua kwa kina na mapana yake, hatimaye,

Mradi wa miaka 5 kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi wazinduliwa nchini Tanzania

Mfuko wa Msamaria mwema, unaosimamiwa na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya kwa kushirikiana na Idara ya afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Kampuni ya Gilead Sciences kutoka Marekani, wamekubaliana kimsingi kusaidia juhudi za kupambana na ugonjwa wa Ukimwi mkoani Shinyanga, kwa kusaidia juhudi za kupima virusi vya Ukimwi kwa wananchi 120, 000 pamoja na kuwapatia dawa za kurefusha maisha wale watakaokuwa wameathirika.


Makubaliano hayo yamefikiwa Jijini Dar es Salaam, tarehe 11 Februari 2014 katika Maadhimisho ya Siku ya 22 ya Wagonjwa Duniani. Huu ni mradi wa miaka mitano kwa ajili ya kupima virusi vya Ukimwi na kutoa dawa za kurefusha maisha. Ni mradi unaozingatia taaluma, maadili, usafi pamoja na mafunzo kwa walengwa watakaofaidika na mradi huu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watoto yatima.

Mradi huu utaendelea kuongeza nguvu katika kuwahudumia wagonjwa wa Ukimwi, juhudi zinazofanywa na Jimbo Katoliki la Shinyanga katika Vituo vya Afya vya: Ngokolo, Bugisi, Buhangija na Mija. Mradi utatoa ufadhili kwa ajili ya mafunzo ya hali ya juu kwa wahudumu wa sekta ya afya, ili kuweza kutekeleza wajibu wao barabara pamoja na kuendelea kujikita katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi na maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto.

Wananchi watakaogundulika kuwa na maambukizi ya Ukimwi watapewa dawa za kurefusha maisha anasema Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya. Mradi unapania pamoja na mambo mengine, kudhibiti maambukizi ya virusi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto, kama sehemu ya huduma makini inayotolewa na Kanisa katika kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili, kama sehemu ya mwendelezo wa agizo la Kristo katika kuwahudumia wagonjwa.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, amemkumbuka kwa namna ya pekee, Marehemu Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga, aliyefariki dunia mwezi Novemba 2012. Aliamini kuhusu mafanikio ya mradi huu katika kuwahudumia watanzania waliokuwa wameathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi. Ni mradi wa pekee, unaojumuisha Mfuko wa Msamaria Mwema, Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na Kampuni ya Gilead.

Lengo li kuhakikisha kwamba, Kanisa Katoliki linashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi ambao umekuwa ni chanzo cha vifo na upotevu wa nguvu kazi nchini Tanzania.

Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, yalianzishwa kunako mwaka 1992 na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, ambaye hapo tarehe 27 Aprili 2014 anatarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu. Siku ya Wagonjwa Duniani inalenga pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, wagonjwa wanapata huduma bora pamoja na kuishirikisha Familia ya Mungu katika huduma kwa wagonjwa, kwani wagonjwa bado wanayo nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa.

Kanisa linawahamasisha watu wa kujitolea, ili waweze kuwashirikisha jirani zao upendo, kwa kuwaonjesha upendo. Kanisa linapania pia kutoa majiundo makini ya kitaaluma na kimaadili kwa wahudumu wa sekta ya afya.