RAIS John Magufuli amewasili mkoani Dodoma kwa mara ya kwanza tangu
achaguliwe kuongoza Tanzania akiwa ametumia njia ya barabara huku akiwa
na siri moyoni ya nani atakuwa Waziri Mkuu wake. Njia aliyotumia kufika
Dodoma imewashangaza wengi kutokana na ukweli kwamba marais
waliotangulia wamekuwa wakitumia usafiri wa ndege.
Baada ya kuwasili Ikulu Ndogo ya Rais iliyopo Wilaya ya Chamwino
mkoani Dodoma akitokea jijini Dar es Salaam, alipokewa na viongozi
mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Chamwino Ikulu, Joseph
Seganje, wananchi wamefarijika kuona Rais huyo akiishi kwenye Ikulu hiyo
kama alivyokuwa ameahidi. “Tayari tumempokea Rais wetu na wananchi wana
furaha isiyo na kifani,” alisema Seganje.
Wakizungumza mapema wiki iliyopita, baadhi ya wakazi wa Chamwino
Ikulu walisema itakuwa ni faraja kubwa kwa Rais kuishi kijijini hapo.
Alice Chidong’oi alisema Dk Magufuli ni kiongozi anayeonesha nia ya
dhati ya kuwatumikia watu wake kwa kujali zaidi wanyonge kama ilivyokuwa
kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Tunaamini akiishi hapa atakuwa sehemu ya jamii ya Wana Chamwino na
hilo litasaidia hata kuboreshwa kwa huduma za jamii ikiwemo maji,”
alisema Chidong’oi. Alisema hiyo itakuwa fursa nzuri kwa wakazi wa eneo
hilo kufanya biashara, kwani uwepo wake ndani ya wilaya hiyo utaongeza
idadi ya wageni.
Mkazi mwingine, Stanley Richard, alisema vijana wa Chamwino wanapenda
kazi na Dk Magufuli akiwa hapo itakuwa ni kazi tu. “Ni mtu ambaye
anapenda kazi na sisi vijana tunapenda kufanya kazi, tutampa ushirikiano
mkubwa katika kipindi chote atakachokuwa madarakani,” alisema.
Alisema alifurahi alipochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwani alijua nchi imepata kiongozi ambaye yuko tayari kuwaletea
wananchi wake mabadiliko. Tayari Serikali mkoani hapa imepiga marufuku
kufanyika kwa mikutano ya hadhara na maandamano wakati wa vikao vya
Bunge vikiendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa, alisema amri hiyo ya kuzuia
mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa bado inaendelea ili
kuweka utulivu muda wote wa vikao vya Bunge.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Bunge, kesho Alhamisi, Bunge
litapokea na kuthibitisha kwa kupiga kura jina la Waziri Mkuu wa 11 wa
Tanzania ambalo Dk Magufuli atakuwa ameliwasilisha kwa Spika Job Ndugai.
Kwa hiyo, Dk Magufuli atakuwa ametua mjini hapa akiwa na siri yake
moyoni ya nani atakuwa Waziri Mkuu wake kwa miaka ya mwanzo ya utawala
wake inayokoma mwaka 2020.
Mbali ya kutoa jina la Waziri Mkuu, Dk Magufuli anatarajia
kulihutubia Bunge, Ijumaa alasiri baada ya kuwa amemwapisha Waziri Mkuu
asubuhi. Hotuba yake itakuwa dira ya utawala wake kwa miaka mitano
ijayo.