
Katuni.
Nafasi zinazowaniwa na wagombea hao ni za udiwani, ubunge na urais.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichoko madarakani katika serikali
inayomalizika muda wake, kimemteua Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli,
kupeperusha bendera yake kwa nafasi ya urais.
CCM imejipanga kuzindua kampeni zake Jumapili wiki hii katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Rajabu Luhwavi, alikaririwa
juzi na gazeti hili akisema baada ya uzinduzi huo jijini Dar es Salaam,
itafanya kampeni zake katika maeneo yote ya nchi na imepanga kufanya
mikutano 1,000 sawa na wastani wa mikutamo 15 kwa siku moja.
Aidha, alisema chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinawafikishia
watu wote ujumbe unaokusudiwa katika takriban siku 63 za kampeni.
Kwa upande wa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa, chama hicho kilipanga kuzindua kampeni zake
kesho Jumamosi katika Uwanja wa Taifa.
Hata hivyo, serikali imezuia shughuli za kisiasa kufanyikia katika
uwanja huo wa kisasa wenye uwezo wa kubeba watu waliokaa kwenye viti
60,000.
Hivyo, hadi kufikia jana, Ukawa walikuwa hawajatangaza rasmi mahali gani jijini Dar es Salaam watazindulia kampeni zao.
Nipashe linapenda kutoa rai kwa vyama vyote vya siasa
vinavyoshiriki uchaguzi mkuu katika nafasi yoyoye ile ya uongozi,
kuhakikisha kwamba kampeni zinafanywa kistaarabu.
Tunatarajia wagombea watajikita zaidi kuelezea ilani za vyama vyao
jinsi vilivyojipanga kuwaletea wananchi maendeleo na si kusimama
majukwaani na kuporomosha matusi ama vijembe visivyo na tija.
CCM tayari imetangaza timu yake ya kampeni ilivyosheheni makada 32 wenye sifa za kila aina.
Watanzania wanatarajia kuwasikia makada hao wakimwaga sera za chama chao kiungwana ili kuwashawishi wawapigie kura wagombea wao.
Kama ilivyo kwa CCM, basi pia Watanzania watapenda kusikia sera za
kutoka upande wa upinzani zikielezwa kwa lugha ya kistaarabu ili kutoa
nafasi kwa wananchi kuzipima na hatimaye ifikapo Oktoba 25, mwaka huu,
watumie haki yao ya kikatiba kuwapata viongozi wao kutoka katika vyama
hivyo.
Watanzania yatupasa kufahamu kwamba amani iliyopo ikitoweka, ni kazi kubwa kuirejesha.
Ni kwa msingi huo ndipo tunapowasihi wagombea wa vyama vyote kuacha
kufanya kampeni za kukamiana na kutumia lugha za matusi kati ya
wagombea wenyewe kwa wenyewe ama vyama kwa vyama.
Nec nayo inapaswa kuhakikisha kwamba inapanga vizuri mikutano ya
kampeni pasipo kuingiliana kwa ratiba ama viwanja vya mikutano kwani
hali hiyo yaweza kuwa mwanzo wa uvunjifu wa amani.