Mpendwa,
unayeitegea sikio Radio Vatican, leo Mama Kanisa anasherehekea sherehe
ya Mama wa Mungu ambayo huja daima kila tarehe mosi ya mwezi Januari. Ni
sherehe ya amani kwa maana Mama Maria ni Mama wa amani. Amemzaa
Mkombozi mfalme wa amani na hivi Mama Kanisa anaona ni vema tukasali
tukimwomba Mungu kwa njia ya Mama huyu kwa ajili ya amani ya ulimwengu.
Sherehe hii ya kuombea amani duniani iliwekwa rasmi na Papa Paulo VI
kunako mwaka 1968. Kwa namna ya pekee kabisa, Kanisa linaadhimisha
Sherehe hii katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kanisa
linamkumbuka Bikira Maria kama Tabernakulo ya kwanza ya huruma na
upendo wa Mungu na Sanduku la Agano kati ya Mungu na binadamu.
Salaam Mama Mtakatifu wa Mungu
uliyemzaa mfalme mwenye kutawala mbingu na dunia daima na milele. Hii
ndiyo salaam yetu kwa Mama mpendelevu Mama asiye na doa, katika sherehe
hii tukufu tunapofungua mwaka mpya.