Week Hot newz

Watakatifu wapya, miamba ya huruma ya Mungu !

Baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, Jumapili tarehe 27 Aprili 2014 katika Ibada iliyohudhuriwa na maelfu ya watu waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na viunga vyake, watakatifu hawa wapya watakumbukwa kila mwaka mwezi Oktoba kadiri ya Kalenda ya Liturujia ya Kanisa.

Kadiri ya Kalenda ya Liturujia ya Kanisa kwa ajili ya kumbu kumbu ya Watakatifu, Yohane XXIII atakumbukwa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba. Hii ni siku maalum ambayo, kwa takribani miaka hamsini iliyopita, Yohane XXIII alikuwa anafungua rasmi maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, tukio ambalo limeleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Hili ni tukio la kishujaa lililomstahilisha Papa Yohane XXIII kuitwa Mtakatifu.

Mtakatifu Yohane Paulo II atakumbukwa kila mwaka ifikapo tarehe 22 Oktoba. Hii ni siku ambayo Papa Yohane Paulo II alipoanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, akaendeleza maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na kukazia umuhimu wa Mama Kanisa kujikita katika mchakato wa Umissionari na Uinjilishaji Mpya. Mwezi Oktoba ni mwezi wa shughuli na mikakati ya kimissionari ndani ya Kanisa.

Tangu sasa waamini na watu wenye mapenzi mema wanaweza kuwaenzi watakatifu hawa wapya kwa maadhimisho ya: Ibada, Liturujia pamoja na kuwaweka kuwa walinzi na wasimamizi wa shughuli mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II atakuwa ni msimamizi wa Siku za Vijana Duniani.


Papa Francisko anawaalika vijana kutoka kimasomaso kukutana na Yesu Mfufuka!


Vijana wanaalikwa kumwangalia kwa namna ya pekee kabisa yule kijana tajiri anayesimuliwa kwenye Maandiko Matakatifu aliyemwendea Yesu akiomba ushauri ili aweze kuurithi uzima wa milele. Mitume wengi walikuwa ni vijana na walifurahia sana walipokutana na kuzungumza na Yesu, kiasi hata cha kuwabadilishia mwelekeo wa maisha, kwani waliweza kusikiliza ufafanuzi wa Neno la Mungu kwa kina na mapana!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa video kwenye maadhimisho ya Siku ya Vijana Kikanda nchini Argentina, iliyoadhimishwa, Jumamosi tarehe 26 Aprili 2014 nchini Argentina, katika mkesha wa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, anawauliza vijana, jinsi walivyojisikia kwa mara ya kwanza walipokutana na Yesu katika hija ya maisha yao ya kiroho, Anawaalika kuwaangalia Mitume waliokutana na Yesu kwa mara ya kwanza katika maisha yao.

Yesu alionesha upendo wa pekee kwa yule kijana tajiri aliyejitahidi katika maisha yake kushika Amri za Mungu, lakini akisoka ndani mwake ufukara wa maisha ya kiroho, ndiyo maana anapoambiwa kwenda kuuza vyote alivyonavyo na kuwapatia maskini, kisha amfuate Yesu, anashikwa na huzuni kubwa katika moyo wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maandiko Mataktifu yamesheheni mifano ya vijana wa kina aina. Anawakumbusha yule kijana aliyeomba urithi kutoka kwa Baba mwenye huruma, kisha akatokomea mjini kwenda kuponda mali na baadaye akakiona cha mtema kuni kwa kukumbana na uso kwa uso na baa la njaa! Hapa akajifunza kutubu na kuongoka, ili kukimbilia tena huruma ya Mungu. Daima Baba yake alikuwa anamsubiri kwa hamu kubwa, kuona kijana wake akirudi tena nyumbani. Siku ile aliporejea nyumbani, akamkumbatia na kumwonjesha tena huruma na upendo usiokuwa na kifani.

Baba Mtakatifu amewakumbusha vijana wa Argentina kuhusu yule kijana wa Naini aliyekuwa amefariki dunia baadaye akafufuliwa na Yesu, kwa kumwonea yule mama mjane huruma? Baba Mtakatifu anawauliza vijana wao wanajisikia kuwa sehemu gani kati ya vijana wanaosimuliwa kwenye Injili? Je, wanaonesha ari na shauku ya kuwashirikisha wengine ushuhuda wa kukutana na Yesu? Au wamekata tamaa na kujikunyata? Au pengine tayari wamekwisha kupoteza maisha ya kiroho ndani mwao?

Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha vijana kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kutolea ushuhuda wa imani katika matendo, ili kujenga na kuimarisha amani na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na kukumbatia Injili ya maisha pamoja na kuguswa na mahangaiko ya wengine kama alivyofanya Bikira Maria kwenye arusi ya Kana na mwishoni akasimama chini ya Msalaba wa Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wasichana kuiga mfano wa Bikira Maria na wanawake watakatifu wanaosimuliwa katika Injili kwa kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, wakimwachia Yesu nafasi ya kuwaongoza, ili waweze kukua na kukomaa, tayari kuwahudimia Watu wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu amewatakia kheri na baraka vijana hao katika maadhimisho ya Siku ya Vijana wa Argentina Kikanda, ili wapate nafasi ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao, bila kuwa na woga wala makunyanzi, bali wangalie Yesu na Bikira Maria, ili waweze kusonga mbele, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake.

Woga na mashaka ni sumu ya imani



Katika dominika hii ya pili ya Pasaka, Injili inatuletea aina mbili za mazingira yaliyo tofauti:Mazingira ya kwanza, Yesu anawatokea wafuasi jioni ya siku ileile ya Pasaka, wakiwa chumbani pindi mtume mmoja aitwaye Thomas hakuwepo. Mazingira ya pili, ni siku nane baadaye Yesu anawatokea tena wafuasi chumbani sasa akiwepo hata Thomas. Mazingira ya kutokea-tokea kwa Yesu baada ya ufufuko wake ni tofauti hasa ukikumbuka alivyomtokea mara ya kwanza Maria Magdalena asubuhi ileile ya Pasaka.

Mazingira aliyomtokea nayo yalikuwa ni ya nje kwenye bustani karibu na kaburi. Lakini kwa mitume ilikuwa ni jioni tena chumbani milango ikiwa imefungwa kutokana na woga wa wanafunzi. Mwinjili anataka kutuonesha kwamba Yesu anafika katika ulimwengu kwa namna ambayo si ya kiyakinifu, ni yeye lakini siyo yuleyule. Kitu cha muhimu zaidi kukiepa hapa ni matumizi ya neno hili “kutokea”, kwa sababu neno hili halijatumika kabisa na mwinjili. Fasuli inasema, Yesu alikuja na kusimama katikati. “Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwa wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi: akaja Yesu akasimama katikati, akawaambia, “Amani iwe kwenu.” (Yoh. 20:19).

Siku ya Pasaka na siku nane baadaye Bwana anakuja na kukaa katika jumuia yake iliyokusanyika pamoja, na kama ilivyokuwa kwa wafuasi wale wa mwanzo siku ya Pasaka kadhalika waumini siku ya Pasaka. Waumini hao hawana budi kufungua sana macho yao, lakini siyo macho ya kiyakinifu, yanayoangalia kwa udadisi na kuanisha mambo, bali kwa macho safi, macho ya imani yanayoweza kuona mambo yasiyoweza kuonekana kwa macho ya kawaida.

Ndivyo inavyotufundisha Injili ya leo jinsi ya kufungua macho ya imani na kuangalia Yesu mfufuka anayefika na kukaa kati ya jumuia iliyokusanyika pamoja. Wafuasi wanashangaa kwa kutokewa na Bwana kwani walikuwa na woga sana. Wamekusanyika pamoja siyo kutokana na upendo waliokuwa nao kati yao, la hasha, bali kutokana na woga, kwa vile wanaye adui mmoja wanayemwogopa yaani wayahudi.

Angalia watu wengine wanaotembea nje, wanawaacha tu hawa wafuasi wajifungie humo chumbani, wao hawana wasiwasi wowote kwani ni kesi binafsi ya mitume walioingiwa na wasiwasi kutokana na yaliyotokea. Hawa wanao woga kwa vile hawajamwona Bwana mfufuka na kuhuishwa na roho ya mfufuka, hivi wanao woga. Woga huo unawapata pia wakristu wowote katika jumuia kama endapo wanakuwa hawana mang’amuzi ya Kristu mfufuka. Hali hiyohiyo inaweza kumkumba kila mkristu mkereketwa na Kristu kama anakosa mang’amuzi ya Kristu mfufuka katikati ya ndugu zake.

Woga huo wa Mkristu unatokana na mambo mawili: Mosi, kuogopa kifo. Mkristu aliyemwona Kristu anayeingia katika utukufu wa Baba hawezi kuwa na woga wowote ule wa kifo. Anaweza kuwa na woga wa homa, ugonjwa, mateso, lakini siyo wa kifo. Mtu huyo atasubiri kama “mlinzi akeshavyo akisubiri kuchomoza kwa jua la asubuhi”.

Kuingia kwake makaoni kwa Baba yake ambako ni lengo la wote, hakuwezi kumpatia woga wa kifo. Hata kama woga huo unabaki kutokana na kuachana na wapenzi wake na vitu mbalimbali ambavyo Mungu ametupatia. Kwa hiyo hapa unauona woga wa wanafunzi, ambao walikuwa bado hawajamwona Kristu mfufuka.

Woga wa pili, unakuwa dhidi ya wengine ambao hawakuyapokea mapendekezo haya ya Yesu hadi wakataka kumfifisha kabisa. Wenye woga aina hiyo hawawezi kuwa wanafunzi wa kweli, kwani Yesu anawatuma wafuasi wake kama vile kondoo kati ya mbwa mwitu. Kama unao woga kwa mbwa mwitu, basi ni bora kutoroka na kwenda mbali kujificha.

Kadhalika woga ni ni kitu kibaya kupita kila kitu kingine katika imani, kwa sababu unawafanya wafuasi wa dini kuwa wenye msimamo mkali, hawaambiliki, hawataki majadiliano, ni wagomvi, ni wachokozi, wanapiga makelele, wanapenda zogo katika kuitangaza imani yao.

Kwa sababu kama imani yao na wanachokisadiki kingekuwa cha ukweli na wanakiamini kwa dhati, basi wasingekipigia makelele, badala yake wangekitangaza kwa furaha na kwa utulivu. Pengine ingekuwa pia njia ya kujisaidia wao wenyewe ya kuuona mwanga wa Pasaka. Kwa hiyo yatubidi tujiangalie sana, kwani woga unatuingiza katika hatari ya kujifungia katika ukweli wetu usio na msingi wa kuchochewa tu na mapokeo wa mambo yale tuliyozoea kuyatenda, tunakuwa viziwi mbele ya hali halisi na hivi kujikuta unajihami mbele ya kosoo ya imani yako, na unakuwa mwoga wa mambo mapya.

Katika kipindi fulani cha historia ya Wakristu, Kanisa lilikuwa na hofu kubwa sana wakati Biblia ilipokuwa inamilikiwa na Waprotestanti. Kulikuwa pia woga wa demokrasia, na ule woga wa kukutana na utamaduni au mila nyingine ngeni. Woga aina hiyo ni sawa na ule wa mitume wa kujifungia ndani ya chumba. Yaani unakuwa na woga na mambo ya nje.

Huku kujitenga na kujifungia ndani ya chumba katika nyumba moja, kuna maana pia ya kiteolojia: Yohane anataka kuonesha kwamba mbele ya ulimwengu, wanafunzi wanajisikia katika mazingira mageni, wanayo thamani ambayo si sawa na zile za ulimwengu. Yesu anasema, ninyi mpo katika ulimwengu lakini si wa ulimwengu huu. Ndiyo maana wanakuwa na woga.

Aidha, endapo mmoja anajitangazia kwamba amemwona Kristu mfufuka, anatangaza imani yake, hivi anaogopa kueleweka kuwa ni kichaa, yaani ni mtu anayeishi nje ya ulimwengu, kwa sababu watu wamefungwa na mtindo wa maisha ya ulimwengu huu hawaoni namna nyingine ya maisha. Kwa mfano Mtakatifu Paulo anapozungumza juu ya ufufuko, watu wanamcheka na kumwambia waziwazi kwamba “juu ya suala hilo tutakusikiliza tena wakati mwingine”.

Ni ngumu sana kushuhudia imani yako hadharani. Hata mapadre, usiku wa Pasaka, hatuwi hata na uso wa furaha wa kuona mwanga wa ufufuko. Kwamba Yesu yuko na alifika kusimama mbele ya wafuasi. Yaani mwanzo mpya wa kudumu wa uwepo wa Yesu. Amefufuka na kuonesha mikono yake na kuwa katikati yao. Anaonesha mikono iliyofanya kazi na ubavu wake, hiyo ndiyo kadi yake ya utambulisho. Mikono iliyotenda mema na kupigiliwa misumari na moyo wake uliochomwa mkuki ilipotokea damu kuonesha maisha na maji kuonesha Roho mtakatifu, maisha yaliyomwagwa duniani maisha ya Roho yaliyotolewa ulimwengu. Hii ndiyo ID ya Yesu.

Mazingira ya pili, aliyotokea Yesu ni ya siku nane baada ya ufufuko. Tomasi hakuwepo pale alipotokea Yesu mara ya kwanza. Huyu Tomasi anaitwa Didimo maana yake Pacha, “Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomas, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. .. Basi, baada ya siku nane wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomas pamoja. Akaja Yesu na milango imefungwa akasimama katikati , akasema, “Amani iwe kwenu.”(Yoh. 20: 24, 26). Mwinjili anasisitiza sana jina hili Pacha (Didimo). Yaonekana kuwa huyu ndiye pacha wa kila mmoja wetu. Kwa sababu hata sisi tutapita safari hiyohiyo ya jinsi ya kumfuata Kristu mfufuka.

Katika Injili, Thomasi anajitokeza mara tatu: Mara ya kwanza ni pale Yesu anapotaka kwenda Yudea, alikokufa Larazo, Thomas anasema twende tukafe sote huko: “Basi Tomas, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, “Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.” (Yoh. 11:16). Kwa hiyo ni kweli Tomasi anayo mang’amuzi ya kifo tu, bali mang’amuzi ya ufufuko hana kwa sababu hajayashuhudia. Amebakiwa na wazo lake lilelile, “Twendeni tukafe naye”. Nafasi nyingine ni kwenye karamu ya mwisho, pale Yesu anapowaambia wanafunzi kwamba kule ninakoenda ninyi mnafahamu njia. Tomasi anasema, sisi hatujui unakoenda, tutawezaje kuijua njia? “Nami niendako mwaijua njia.” Tomas akamwambia, “Bwana, sisi hatujui uendako, nasi twaijuaje njia?” (Yoh. 14:4-5) Huyu ndiye ndugu yetu Tomas, pacha wetu (Kurwa), kwa sababu anataka kujua. Kuna wakristu wengi wanaopata taabu ya kuelewa mambo yote katika imani. Anaye pacha wa Tomasi atauliza, “utuoneshe njia.” Kwani baada ya kuuliza Yesu anaweza kujieleza: “Mimi ni njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” (Yoh. 14:6).

Hebu tuangalie ni katika vipengee vipi Tomas anaweza kuwa ni pacha wako.
Hoja ya mojawapo yaweza kuwa Tomas alikuwa haelewi ni kwa nini wenzake wamejifungia chumbani. Yeye ameondoka na kwenda kuzubaa sijui wapi kwa sababu hajisikii kuwa na woga wowote ule. Katika kipengee hiki, Tomas ni pacha au kurwa wa mtu yule ambaye hajisikii kuwa wa maana au bora zaidi kuliko wengine, yaani, haelewi ni kwa nini wengine wamejifungia ndani.

Ni dhahiri kwamba Tomas siyo pacha wa wale wanaojitenga na jumuia ya kikristu kwa sababu labda wanachekwa na kudharauliwa na wengine; wanaojisikia bora zaidi na kuwahukumu wengine wasio katika jumuia au hata wanaowahukumu wale walio katika jumuia kwamba ni waovu kuliko wengine, au kama wale wanaoacha dini yao na kuingia nyingine.

Tomas hahukumu, wala kudharau wengine bali yawezekana anajiona kama amedanganyika kidogo au amekwazika na jumuia ile. Yaani ni kama wakristu wale wanaoona ndani ya kanisa kuna makwazo au mambo ya aibu, hivi wanajisikia kukwazika na kuteseka mioyoni mwao. Hivi wanaona ni bora kujiweka kidogo pembeni.

Aina ya nyingine ya kuwa pacha wa Tomas ni pale wale ambao wamedanganyika na muundo wa kanisa, na uendeshaji wa mambo ya kanisa, kukosa mpango mzuri. Hakuna uinjilishaji wa kutosha, au kuna utawala wa kibabe, kuna kujionesha ukuu unaotegemea mali, na hivi wanaona afadhali kujiepusha kidogo. Waumini wasioamini kama mambo yanaweza kubadilika katika kanisa. Hawa ni pacha wa Tomas.

Anapofika Tomas wenzake wanamhabarisha: “Tumemwona Bwana.” Kwa tamko hili walikuwa wanataka kummweleza kwamba mambo yamebadilika, si kama alivyodhani au kama alivyoyaacha. Tomas anataka kuhakikisha yeye mwenyewe kama kweli mazingira aliyoyaacha yamebadilika.

Hapa sasa tunakutana na pacha mwingine, yaani wale wanaotaka kuhakikisha kwa kuona na kugusa. Pacha wa Tomas ni wale wasiomwona Yesu wa Nazareti lakini wameitwa kumwamini ili kumshuhudia kwa ndugu zao. Pacha ni wale wasioelewa. Yaani hao pia wameitwa ili kuelewa lakini wanayo namna mbili ya kuelewa. Kimwili, kuamini kwao ni kama kule Tomas, lakini ndani yao kuna haja na hamu ya kuamini ambayo wanataka kuihakikisha.

Aliye na mang’amuzi haya ya ndani, ajue kwamba Tomas ni pacha wake. Na kwamba tusiwe na woga wa kuungama mashaka yetu ambayo ni kama ya Tomas, kama tunaweza kugusa kama Tomas hatuwezi kuwa na mashaka. Lakini kugusa huko kwetu hakuwezekani.

Kwa hiyo ni vyema kabisa kuwa ndani yetu tunaye huyo pacha wetu Tomas wa kuona mashaka kwamba huyo aliyetoa maisha kwa kufa kwake kama mtumwa ameingia katika utukufu wa Baba. Kwa hiyo fundisho kuu tunalopata hapa kwa huyu pacha wetu ni hili: Yesu anapofika siku ya nane anaonesha majeraha yake na anamwita Tomas kuja kuhakikisha.

Huo ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kuweka mikono yetu ubavuni pake. Kualikwa na Yesu Mfufuka kuweka mikono yako ubavuni mwake maana yake pale unapoweka mikono yako, shughuli zako zote, na hasa ukijiweka wewe mwenyewe, kujiaminisha na kujitoka kabisa maisha yako kwa upendo kama ya Yesu hapo umeingia katika ulimwengu wa Mungu na wa utukufu wa ufufuo.

Upacha mwingine na Tomas ulio mzuri sana, ni pale Yesu anapomwalika Tomas kuyatupa maisha yake kwenye mapendekezo ya mwalimu: “Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.” (Yoh. 20: 27), naye Tomas anapojibu: “Bwana wangu na Mungu wangu!” (Yoh. 20:28). Hilo ni ungamo la imani katika Mungu wa kweli imani inayojidhihirisha katika ufufuko wa Kristu. Imani kwa Mungu anayetoa maisha yake kwa ajili ya upendo.

Tomas aliyekuwa na mashaka, ndiye wa kwanza kushuhudia imani iliyo safi ya wakristu wa kwanza. Ni yeye aliyeona uthibiti wa msulibiwa katika ufufuko. Haamini juu ya Mungu anayeadhibu, anayezawadia, anayewapenda wema tu, amemwamini katika Kristu aliyetoa maisha Mungu wa kweli ambaye hawezi kuwa mwingine isipokuwa yule aliyesulibiwa kwa ajili ya upendo.

Uhakika kwamba ameona na kugusa mikono na ubavu wa Mungu, uhakika ule anaweza kuwa nao tu kwa mtazamo wa imani. Mtazamo unaotakiwa kuufungua daima pamoja na jumuia. Sisi tunasikia sauti ya Bwana na katika mkate wa Ekaristi sisi tunagusa mapendekezo yake ya maisha ya kujifanya mkate kwa ajili ya kutupenda.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

Utakatifu wa maisha!


Utakatifu ni hija ya maisha inayotekelezwa hatua kwa hatua kama walivyofanya Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II watakaotangazwa kuwa watakatifu, Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Huu ndio utakatifu ambao watu wanaendelea kuushuhudia katika maisha na utume wa Wenyeheri hawa.

Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican akiwa ameambatana na wahusika wakuu katika mchakato wa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu: Padre Giovangiuseppe Califano pamoja na Monsinyo Slawomir Oder, Jumanne, tarehe 22 Aprili 2014, wamepembua maana ya utakatifu mintarafu maisha ya wenyeheri hawa wawili.

Yohane XXIII katika maisha yake kama Padre, Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro alijiwekea nadhiri ya kuwa karibu na Yesu, kujificha katika Moyo wake Mtakatifu, Kusali Rozari na kumpatia nafasi ya pekee katika maisha yake. Haya ni mambo yaliyojionesha kwa namna ya pekee katika maisha na utume wake kama Mchungaji na Baba.

Ni kiongozi aliyeyasimika maisha yake katika furaha na ukarimu kiasi cha watu wengi kumwita kuwa ni Papa mwema! Alikazia umuhimu wa mshikamano katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuitisha Sinodi ya Jimbo kuu la Roma na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ni kiongozi aliyeonesha upendo na uelewa katika shughuli za kichungaji; akawa kweli ni mtu wa msamaha na faraja kwa wote waliomkimbilia. Alikazia utii na amani ya kweli duniani.

Monsinyo Slawomir Oder anasema, utakatifu wa Mwenyeheri Yohane Paulo II ulianza kuonekana tangu alipokuwa bado Chuo Kikuu, kiasi kwamba, baadhi ya wanadarasa wake waliandika chumbani kwake, "Mtakatifu mtarajiwa", kutokana na na moyo na bidii ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na maisha adili. Yote haya yalimwilishwa kwa njia ya matendo ya huruma.

Alikuwa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, akawa na ujasiri wa kukabiliana na changamnoto za maisha kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa, kwani daima aliuona mkono wa Mungu ukiyaongoza maisha yake! Watu wengi walitambua kuwa kweli Yohane Paulo II alikuwa ni mtu wa Mungu aliyekuwa ni chemchemi ya maisha yake yote, kiasi cha kujikita katika Uinjilishaji Mpya, ili wote waweze kuwa ni watakatifu kwa kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Jumapili ya Huruma ya Mungu!


Tunaendelea tena katika tafakari yetu masomo Dominika ya II ya Pasaka mwaka A. Ni kipindi cha furaha kwa sababu ya ushindi dhidi ya kifo kwa njia ya ufufuko. Neno la Mungu, linakazia na kuahidi furaha ya kweli kwa wale ambao hata kama hawakumwona Bwana wanayo imani na tumaini la kweli katika yeye. RealAudioMP3

Katika Somo la kwanza, kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume latuonesha furaha na tabia ya jumuiya ya kwanza ya Yerusalemu. Kwa nini tunaoneshwa jambo hilo? Ni kwa sababu tunaalikwa kuishi mtindo uleule wa jumuiya ya mwanzo katika mazingira yetu. Mambo msingi ya Jumuiya ya I yalikuwa utii na usikivu wa watu kwa Neno la Mungu lililohubiriwa na Mitume. Aidha waliweka mali yao na moyo wao pamoja kwa faida yao na kasi ya Injili.

Ili kuimarisha mambo haya waliadhimisha pamoja Ekaristi Takatifu na kusali pamoja kwa upendo. Mambo haya msingi yalifungamana na furaha, uchangamfu, ushirikiano ambavyo vilikuwa vivutio kwa jumuiya nyingine nje ya Yerusalemu. Ndiyo kusema waliishi na kukishuhudia kile walichohubiri katika maisha yao, yaani waliuishi ufufuko ambao ndilo chimbuko la haya yote.

Mpendwa msikilizaji, wito kwetu hivi leo katika jumuiya zetu ni kuanza polepole kupalilia nguvu ya ufufuko, ndiyo kusema tunaalikwa kushuhudia daima kwa maisha yetu yakuwa Kristu ni mfufuka. Mpendwa, katika mantiki hiyo katika jumuiya zetu lazima tabia za jumuiya ya kwanza zijitokeze na kukua na hivi kuwa kielelezo cha mapendo kwa watu wa mataifa. Yafaa kukomaza ile tabia ya kushirikishana tulichonacho hata kama ni kidogo. Tujifunze kuwa na kile kinachotufaa na kinachobaki kiwe kwa ajili ya wale waliowahitaji katika jumuiya zetu.

Kumbuka usemi wa Mtakatifu Basil akisema “kama mmoja wetu angechukua kwa ajili yake kinachohitajika na kingine kikawa kwa ajili ya ndugu yake maskini, basi kusingekuwa na tajiri wala maskini katika jumuiya”. Hii ni falsafa ya mgawanyo sawa ambayo tungepaswa kuifikia kama kweli tunataka kumfuasa Bwana kwa ukamilifu! Mpendwa msikilizaji inaonekana kuna ugumu katika kushirikishana mali tulizonazo, na hasa kuwapeni maskini, je toka tukiamini na kuendelea katika ugumu huu twaweza kusema tunaishi na tunashuhudia ufufuko? Tafakari sana jambo hili!

Katika somo la Pili toka barua ya kwanza ya Mtakatifu Petro tunakumbushwa siku ya ubatizo wetu. Kwa njia ya ubatizo tulipata kuingia katika furaha isiyo na mwisho. Ndiyo kusema Mt Petro anataka hata kama kuna madhulumu na taabu mbalimbali tusisahau furaha ya milele. Anasema mateso ni ya kitambo kidogo tu na baadaye yanapita cha msingi ni kutazama mbele tukiendelea kukua katika neema ya ubatizo.

Mtakatifu Petro anatukumbusha kuwa mkristu katika ulimwengu huu ni mgeni na hivi yuko safarini kwenda nchi ya ahadi yaani mbinguni. Tunakumbushwa kuwa hakuna mateso yanayoweza kuzima moto wa furaha na mapendo uliowashwa wakati wa ubatizo. Wakristo ni kama dhahabu ambayo ili itengeneze kitu cha thamani lazima ipitie moto ili ichomwe na kusafishwa tayari kwa kito cha thamani.
Katika somo la Injili, hali ya maisha ya jumuiya inajionesha wazi. Wanafunzi wako pamoja ingawa wanahofu! Bwana anawakuta wakiwa pamoja na kuwatakieni amani. Anawaonesha alama za madonda na wanafurahi na kusema tumemwona Bwana! Ni katika jumuiya hiyo Bwana anawavuvia Roho Mtakatifu ili wapate kuondolea dhambi. Ni siku hii anaweka sakramenti ya kitubio katika Kanisa na kisha anawatuma wakaende kutangaza habari njema. Kumbe Toba ni mlango wa kazi ya kimisionari, ni mlango wa imani, ni mlango wa wokovu. Analikabidhi kanisa ufunguo wa kufunga na kufungua katika mambo yamhusuyo Mungu katika uhusiano wake na mwanadamu.
Jumuiya wakati fulani zinakuwa na watu walio na mashaka katika imani. Hali hii inajionesha leo pia. Ndiyo kusema, kumbe Mtume Tomaso ambaye hakuwapo pamoja na wenzake siku ya kwanza haamini, bado ana mashaka kuhusu ufufuko! “Siamini mpaka nitie vidole vyangu katika makovu ya Bwana! Baada ya siku nane tukio hilo la kitaalimungu, Bwana anawatokea tena Mitume na wakati huo Tomaso yupo.
Bwana anamwambia lete mikono yako na uweke kidole chako katika ubavu wangu na usiwe asiyeamini! Tomaso anajibu, Bwana wangu na Mungu wangu! Mpendwa, Mtume Tomaso anapokiri udhaifu wake anatufundisha kuwa watu wa Imani na unyenyekevu mkubwa na hivi baada ya ufufuko hakuna mashaka tena kinachobaki ni kwenda kutangaza habari ya furaha kwa mataifa.
Mpendwa leo hii wapo watu wa namna hii katika jumuiya zetu, kumbe wanaalikwa na Bwana kusadiki pasipo kuona, na kwa namna hiyo Bwana anatangaza heri kwa wasioona wakasadiki na si kwa wanaosadiki kwa sababu ya kuona. Mwishoni mwa sehemu ya Injili ya Dominika hii, Mwinjili anatuambia pia zipo ishara nyingi ambazo hazikuandikwa na hivi mtu asishangae ishara nyingine ambazo hazimo katika Biblia lakini ni muhimu kwa imani yetu na maisha ya Kanisa.
Nakutakieni furaha tele katika kipindi chote cha Pasaka na Mungu azidi kuwa nawe, nawe ukitekeleza mapenzi yake katika Jumuiya kama Jumuiya ya kwanza ya Waamini. Tukutane tena Dominika ijayo. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.

Maisha ni mchaka mchaka, vinginevyo utachakachuliwa!


Daima ni mchakamchaka. Tabia ya watu wa ulimwengu wa leo ni ile ya mchakamchaka. Kila kitu kinaenda kwa kasi. Taarifa zinaenda kwa kasi kwa njia ya pembejeo za mawasiliano ya haraka, barabara nzuri na za mikato, na wenzetu walioendelea ndiyo wana magarimoshi yanayoenda kwa umeme kwa mwendo wa kasi.

Tuna kila kitu tunachokitaka kwa haraka, daima tuko katika mchakamchaka na kiherehere cha kufanya mambo kama vile tuna wasiwasi wa kutofika tunakotaka kufika au kutofanikiwa kufanya kwa wakati wake kile tunachotaka kukifanya. Ama kweli ni mchakamchaka wa maisha. Mtu yupo katika kupiga mbio za maendeleo katika maisha. Mtu anapiga mbio kwa vile hana uhakika wa kuwasili au kufikia juu kijamii au kiuchumi au hata kuwazidi wengine. “Tukimbie wakati wengine wanatembea!”

Hali hii ya mchakamchaka na ya mbiombio ndiyo unayoikuta katika Injili ya leo. Mtakatifu Yohani anaposimulia kuhusu kaburi wazi lililokutwa asubuhi ile ya ufufuko, anawaonesha wahusika wote wa tukio lile wakiwa katika mbiombio na mchakamchaka: Maria Magdalena ndiye mwanakiherehere aliyefungia. Alikurupuka asubuhi sana kungali bado giza kwenda kaburini. Alipolikuta jiwe lililofunika kaburi limeondolewa hapo ndipo ilipoanza patashika ya mchakamchaka. Akaenda mbio kwa wanafunzi. Nao wale wanafunzi Simon Petro na Yohane wakaanza mchakamchaka.

Tunaambiwa wakaondoka mbio wote wawili kwenda kaburini. Yohane akamzidi mbio Petro akafika wa kwanza kaburini. Kulikoni? Yaonekana mbio hizo zilipigwa kutokana na wasiwasi, na kiherehere cha kujua kumetokea kitu gani. Budi ieleweke kwamba katika mazingira kama haya, binadamu anakuwa amepagawa na kitu anachokuwa na uhakika nacho kwamba kinaweza kikatokea. Yaani, kinakuwa ni kituko kipya kabisa anachotegemea kukiona au kukipata, kitu kitakachotokea au kilichoishatokea kabla. Katika mantiki hiyo mtu huwa haweza kutulia au kujidanganya kutulia. Wasiwasi na kiherehere chake ni kutaka kukiona au kukijua ni kitu gani ambacho ni budi kitokee lakini hakijui.

Endapo kwa hawa wanafunzi wawili wangemwona Yesu kuwa si kitu cha maana au si kitu cha kukijali, hapo tungewaona wametulia na kufanya mambo kitulivu. Wangeenda kaburini kitulivu tena kwa ajili ya udadisi tu, siyo zaidi. Injili ya Yohani inatafuta kutuingizia vionjo vya wanafunzi hawa wawili, Petro na Yohani wanaokimbia kwenda kaburini. Nafikiri pengine, kwa wote wawili kuna woga labda kuna kitu siyo kwamba hakikwenda sawa, bali wanaonja kwamba imani yao inalazimika kukua ili kutobaki katika woga wa kumtamani tu Bwana wao aliyekufa na sasa hayuko tena. Mbio yao inadhihirisha imani yao. Siyo imani kama ya yule aliye na uhakika bila wasiwasi, la hasha, vinginevyo wangekuwa wamepoozwa, na kukosa mwelekeo na hivi kuchanganyikiwa na miguu kutetemea. Wangekosa nguvu kabisa ya kukimbia, hivi daima wangekuwa wanajikwakwaa na kuanguka. La hasha, kuna kitu!

Mbio na kiherehere cha Mkristu
Mkristu ni yule anayekimbia, anayepiga mbio katika maisha. Mbio za mkristu siyo zile zitokanazo na kutokuwa na uhakika wa kuwasili au kufikia juu kijamii au kiuchumi au kupiga mbio za kuwazidi wengine, bali anakimbia kwa vile anajisikia kuwa ni muhimu kuonja uwepo wa Mungu katika maisha yake binafsi.

Tunajitambua katika mbio hizi? Tuna wasiwasi hata sisi katika kumwelewa Kristu angalao kidogo Kristu ambaye wakati mwigine tunaamini amekufa na kuzikwa katika maisha na katika maisha ya jamii?

Tunakubaliana na kupokea hatari ya kuanguka na kujikwaa katika mwendo wetu wa imani? Tunasadiki kwamba kuwa na imani kunamaanisha kwenda mbele katika kutafiti na kuhitaji kupanua uelewa wetu wa imani. Au tunatafuta kwa mbinu na gharama zozote zile kutafuta au kubaki mahali pamoja penye kutupatia uhakika na usalama? Kanisa (tuko wote humo ndani) wakati mwingine hupunguza kasi, au mwendo na kutamani au kutulia katika uhakika na usalama wa hali tuliyofikia.

Petro na Yohane, wakiwa wameambukizwa na kasi ya Magdalena wanaanza kukimbia pamoja.
Tuanze hata sisi mchakamchaka wa kumtafuta Yesu, tuwahusishe katika mchakamchaka huo hata wale walio karibu nasi, labda wamezuiwa na matatizo fulani au na harakati za maisha ya leo.

Heri sana kwa Pasaka yenye mbio… ili maisha yasikwame.

Ijumaa Kuu Papa kuongoza Ibada ya Njia ya Msalaba- Koloseo




Ijumaa Kuu Baba Mtakatifu Francisko majira ya saa tatu na nusu za usiku, ataongoza Ibada ya njia ya Msalaba katika eneo la magofu ya Koloseo ya mjini Roma. Tafakari katika za Ibada hii zimeandaliwa na Askofu Mkuu Giancarlo Bregantini wa JImbo Kuu la Campobasso Boiano.

Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, Ijumaa kuu 2014


Askofu mkuu Giancarlo Maria Bregantini wa Jimbo kuu la Campobasso- Boiano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya matatizo ya kijamii, kazi, haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ndiye aliyepewa dhamana ya kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka magofu ya Colosseo, Ijumaa kuu tarehe 18 Aprili 2014 Ibada hii inatarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia saa 3:15 Usiku kwa majira ya Ulaya, baadaye atatoa baraka zake za kitume. RealAudioMP3

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha kwa ufupi, tafakari ya Njia ya Msalaba iliyoandaliwa na Askofu mkuu Bregantini.

Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua kuwa anasema ukweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana haya yalitukia ili andiko litimie: hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko lingine lanena: watamtazama yeye waliyemchoma. Hivi ndivyo Askofu mkuu Bregantini anavyoanza tafakari ya Njia ya Msalaba, kwa kuonesha kwamba, Yesu alipanda kwenda Mlimani Golgota bila kusita, kama kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa na akawaruhusu watesi wake kumtendea jeuri bila kulalama!

Yesu, Mwana wa Maria alipenda kubeba mabegani mwake, matendo ya giza yanayomwandama mwanadamu katika hija yake ya maisha, ili kuweza kumkirimia mwanga, unaoleta nuru katika moyo wake. Mateso na mahangaiko ya Kristo ni chemchemi ya wokovu wa mwanadamu; machozi yake yanaonesha upendo wa Mungu. Yesu amesamehe dhambi za binadamu ili kwa njia ya maisha yake, aweze kuwaonesha njia ya wokovu kutokana na mateso pamoja na mahangaiko wanayokabiliana nayo katika maisha, pasi na kukata tamaa.

Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anajisadaka bila ya kujibakiza, kwa ajili ya wadhambi ambao kwa haki kabisa walistahili kutundikwa pale juu Msalabani. Kiu inayooneshwa na Yesu pale Msalabani ni chemchemi ya matumaini yaliyo wazi na mikono iliyo tayari kumpokea mdhambi anayetubu na kumwongokea Mungu. Askofu mkuu Bregantini anamwomba Yesu Msulubiwa kuwakirimia watu huruma yake isiyokuwa na kifani, kwa kuwaonjesha harufu nzuri iliyoujaza mji wa Bethania, mwanzo wa maisha mapya. Kwa kifo cha Kristo Msalabani, Yesu awajalie waamini maisha ya uzima wa milele.

Katika tafakari yake, Askofu mkuu Bregantini anagusia mashitaka yanayoendelea kujitokeza ulimwenguni kwa kujikita katika ubaguzi wa rangi, hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu, kielelezo cha dhamiri mfu, inayoonesha jinsi watu wanavyoshindwa kuwajibika na ukweli kutawala, changamoto ya kusimama kidete kutetea wanyonge na kulinda ukweli.

Msalaba wa athari za myumbo wa uchumi kimataifa unazidi kuwaelemea watu wengi kwa kukosa fursa za ajira, mshikamano wa upendo na udugu; matumaini na imani thabiti. Msalaba unaweza kuwa rahisi, ikiwa kama watu watajifunza kuubeba pamoja na Yes una kwamba, kwa njia ya udhaifu wa kibinadamu, watu wajifunze kujenga na kudumisha moyo wa ukarimu, kwani sura ya wote wanaoteseka, inaonesha pia ile sura ya Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kati ya watu wake.

Kuna akina Mama na wanawake wanaoendelea kuwalilia watoto wao wanaofariki dunia kutokana na sababu mbali mbali; watoto kupelekwa mstari wa mbele vitani; watoto wanaofariki kwa saratani kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira; watoto wanaotumbukizwa kwenye utumwa mamboleo na matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia. Kwa kushikamana na Bikira Maria, hakuna hata chozi moja linaweza kupotea, kwani Bikira Maria ni Mama wa wote.

Kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu, kwa kuguswa na mateso na mahangaiko ya jirani, daima lengo likiwa ni kutafuta mafao na ustawi wa wengi, ili kushinda vikwazo vya chuki, uhasama na kuonea wivu. Tafakari ya Njia ya Msalaba inamwonesha Veronika, mwanamke mwenye huruma anayethubutu kupangusa uso wa Yesu na hivyo kushiriki katika mateso yake. Yesu anatambua upendo na ukarimu wa Veronika, changamoto ya kuguswa na wale wanaoishi katika upweke hasi unaoweza kuwasababishia kifo!

Wafungwa ni kundi la watu wanaoendelea kuteseka kutokana na ukosefu wa haki jamii na mifumo duni ya maisha kwa kuishi hata kinyume kabisa cha ubinadamu, hawa wanaendelea kuvikwa taji la miiba viwachani wao. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza watu wanaojitolea kutoa huduma mbali mbali za kiroho na kimwili kwa wafungwa gerezani.

Katika tafakari hii, wanawake wakweli na waaminifu wanaoneshwa wakimsindikiza Yesu katika Njia ya Msalaba, wanataka kumsalimia na kumfariji, changamoto ya kuendelea kuwa imara katika imani na matumaini; kwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Yesu anapoanguka mara kadhaa kwa kuelemewa na uzito wa Msalaba, anawalika waamini kujibidisha kushinda tabia chafu zinazowaangusha daima dhambini. Waamini wajenge umoja na mshikamano, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kwa kujikita katika upatanisho, kwa kuwamngalia Yesu anayetundikwa Msalabani.

Watu wajenge utamadni wa kuwaheshimu, kuwajali na kuwahudumia wagonjwa badala ya kuwatelekeza na kuwatafutia njia ya mkato ya kumaliza mahangaiko yao kwa kifo laini. Yesu hakushuka Msalabani, aliendelea kupenda na kusamehe. Ugonjwa unaweza kuwa ni shule ya hekima ya kimungu, mahali pa kukutana na Mungu mpole na mvumilivu, mwaliko wa kupambana na magonjwa katika mwanga wa Pasaka na mafao ya familia na Jamii kwa ujumla.

Maneno saba ya Yesu Msalabani ni chemchemi ya upendo na kwamba, kifo cha Kristo kinafungua ukurasa mpya kwa kuonesha kwamba, kifo hakina tena nguvu! Msamaha unaponya na kupyaisha; unawaunda watu katika maisha mapya, mwaliko wa kuondokana na falsafa ya vita, kwani upendo na mshikamano ni mambo yenye nguvu zaidi kuliko hata kifo! Huu ni mwaliko wa kuchuchumilia huduma ya upendo kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Fundisho kuu ambalo Yesu amewaachia wafuasi wake ni kupenda bila ya kujibakiza, ndiyo maana Bikira Maria anathubutu kupokea maiti ya mwanaye kwa imani na matumaini makubwa! Mwanadamu anakumbushwa kwamba, hapa duniani ni mpita njia, iko siku ataungana na Muumba wake. Katika kimya kikuu pale bustanini kulikokuwa na kaburi la Yesu, waamini wajitaabishe kusikiliza sauti ya Yesu ikisema, mimi niko pamoja nanyi hadi ukamilifu wa dahali.

Kwa ufupi, haya ndiyo mawazo makuu yanayochambuliwa na Askofu mkuu Giancarlo Maria Bregantini katika tafakari yake ya Njia ya Msalaba, Ijumaa Kuu kuzunguka magofu ya Colosseo, mjini Roma.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Papa kuongoza Karamu ya Mwisho ya Bwana katika kituo cha Walemavu


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamis Kuu majira ya jioni, saa 11:30, ataadhimisha Karamu ya Mwisho ya Bwana, na liturujia ya kuosha miguu watu kadhaa kama ishara ya unyenyekevu na huduma, akiwa katika Kituo walemavu cha Shirika la Mtakatifu Maria wa Kudra ya Mungu, cha Shirika la la Don Gnocchi, cha mjini Roma. Shirika hili hufadhili watu wapatao elfu tatu wenye ulemavu na tegemezi nchini kote Italia, Rome kukiwa na vituo vyake 12 ambavyo hufadhili wageni wahitaji wanaoingia jiji la Roma, kati ya vituo vya 29 vinavyofanya kazi katika mikoa tisa ya Italia.

Baba Mtakatifu Francisko anasubiriwa kwa hamu na wagonjwa na familia zao katika cha kituo cha Mtakatifu Maria wa Kudra ya Mungu , mtaa wa Via Casal Marmo 401, Roma , ambako watu wa kujitolea huhudumia wagonjwa na familia zao. Alhamis Kuu ya mwaka jana Papa Francisko aliadhimisha pia Ibada ya Alhamis Kuu akiwa katika gereza la watoto la mjini Roma.
Kwa Alhamis Kuu hii, taarifa zinaeleza kwamba, tukio hili la Baba Mtakatifu, kukitembelea Kituo cha Waelmavu cha Don Gnocchi, linafanyika baada ya kupita wiki chache kwa shirika hili kuadhimisha sherehe kubwa ya kupita kwa miaka mitano tangu mwanzilishi wa shirika Don Gnocchi kutajwa Mwenye Heri Februari , sherehe iliyohudhuriwa na waelfu ya waamini, kama sehemu ya mipango kwa ajili ya maadhimisho ya miaka tano ya Don Carlo Gnocchi , kutajwa Mwenye Heri. Sherehe zilizo hamasisha mwamko mpya wa utamaduni wake wa muda mrefu na huduma maalum, isiyoweza kusahaulika, inayoonyesha kupandwa kwa Mbegu ya mshikamano na umoja kwa jirani katika utendaji wa Papa, " baba wa vilema ".

Kituo cha Mtakatifu Maria wa Kudra ya Mungu , ambacho zamani kilifanya kazi kwa jina la Mama Nasi, nyumba ndogo ya Maongozi ya Mungu ya Cottolengo, ilifanywa kuwa Shirika la Don Gnocchi Foundation Septemba 2003 na kwa sasa lina jumla ya 150 vitanda, ambamo kuna makazi kwa ajili ya huduma ya Afya kwa Watu wenye ulemavu 60 vitanda, ambao hawahitaji kuunganisha na vifaa vya aina hospitali au vituo vya ukarabati ); na pia kuna idara ya kisasa ya ukarabati wa mwili “ neuromotor” wa ngazi ya juu, wanaotumia vitanda 60 , ambao pia hupokea huduma ya mazoezi ya mwili, , huduma ya tiba , tathmini saidizi teknolojia na ushauri nasaha, nasaha za kisaikolojia na elimu kwa shughuli zinazo husiana na hali ya wagonjwa hao. Na vitanda 30 vilivyo baki , ni kwa ajili ya wanaotoa huduma kwa wagonjwa.

Mbali na huduma hiyo ya ndani pia huhudumia wagonjwa walemavu kama wagonjwa wa nje kila siku, ambao hupewa tiba na ushauri wa ukarabati na huduma za nyumbani .

Rais wa Shirika la Don Gnocchi, Mosinyori Angelo Bazzari , akizungumzia Papa Francisiko kuendesha Ibada ya Karamu ya Bwana katika kituo hicho cha Mtaa wa Via Casal Marmo , amesema ni furaha kubwa kwao na wanamkaribisha Baba Mtakatifu kwa furaha kubwa ndani mwao. Na kwamba, ishara ya kuosha miguu ni wazi inayoonyesha kwamba Kanisa tangu kuanzishwa kwake, daima limeitwa kuhudumia kwa unyenyekevu hasa watu masikini na dhaifu. Ni huduma ya upendo wa Papa katika ulimwengu wa mateso na ishara ya huruma ya Kiiinjili, ambayo husaidia kukumbuka kwamba , kiwango cha ustaarabu wa jamii kinapaswa kuwa kipimo katika uwezo wake wa kutembea pamoja na watu dhaifu.

Upendo huu wa kuhudumia dhaifu na wanyonge katika jamii, ni karama ya Don Gnocchi , aliyowaachia kama urithi wafanyakazi zaidi ya elfu tano wa Shirika lake, ambayo hufanya kazi kila siku kwa majitoleo ya bila kujibakiza , kwa uaminifu na kama msimamo kila siku , katika dhamira yao ya uwezo, nia, huduma na uendelezaji wa maisha ya maelfu ya watu wanaotafuta huduma katika vituo vya shirik, kwa ajili ya Utafiti wa Afya , mshikamano na huduma.

Papa atoa zawadi ya Injili kwa wafungwa

Papa Francisko atatoa vItabu vya Injili vidogo vinavyoweza kuwekwa mfukoni, vipatavyo elfu moja mia mbili, kama zawadi ya Pasaka kwa wafungwa katika Gereza Kuu la Malkia wa Mbingu la Roma. Zawadi ya Papa itawasilishwa Jumatano hii, na Askofu Mkuu Konrad Krajewski wakati atakapo tembelea jengo la Gereza katika mtaa wa Lugara Roma.
Kitabu hicho kidogo cha Injili chenye kuwa pia waraka wa Matendo ya Mitume, Jumapili iliyopita pia kiligawiwa kwa waamini waliofika kumsikiliza Papa wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, na pia kwa waliohudhuria Ibada ya Misa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu George Mkuu la Magliana Roma.

Na Jumapili ya tarehe 4 Mei, Papa ana mpango wa kufanya ziara ya Kichungaji katika Kanisa la Mtakatifu Stanslao la Botteghe la Roma.
Kisha 18 Mei 2014 , majira ya saa kumi za jioni , Papa Francesko atafanya hija katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Upendo wa Mungu, ambayo yako katika Mtaa wa Via Ardeatina nell’Angola Romano , nje kidogo ya jiji la Roma. Hija inayopendwa na watu wa Roma.
Madhabau ya Bikira Maria wa upendo wa Mungu, ya Mtaa wa Via Ardeatina , yako kiasi cha umbali wa kilomita 12 Roma, katika kanda ya Agro Romano katika jengo la Castel di Leva. ambalo kwa mara ya kwanza liliteuliwa na Papa Gregoria V11 kwa barua yake ya kitume ya mwaka 1081, kama mali ya Abassia ya Mtume Paulo . Na mwaka 1268, mali hiyo ililithishwa kwa Kanisa la Mtakatifu Sabina na baadaye kupewa Wana shirika wa Orsinina mwaka 1295na tena kuhamishiwa kwa Wasaveli.
Na baada ya kupitia katiak mbadiliko mbalimbali, Desemba 1938, Madhabahu hayo yalifanywa kuwa Parokia ikiongozwa na Paroko wa kwanza Don Umberto Terenzi ambaye mwaka 1942 alianzisha Shirika la Mabinti wa Maria wa Upendo wa Mungu na mwaka 1962, madhabahu hayo yakawekwa chini ya usimamizi wa Shirika la Oblates hadi leo. Simulizi juu ya madhabahu hayo, huelezea tukio la mwaka 1740, juu ya muujiza uliotokea kwa muhujaji mmoja aliyekuwa akisafiri kwenda Roma kuhiji ambaye alipofika katika eneo hilo, kulitokea kundi la mbwa mwitu wakali walotaka kushambulia, lakini mara aliomba msaada wa Mama Bikira Maria na ghafla mbwa wao walizuiwa na kitu kisichoonekana na kutoweka zao. Aidha watu wa Roma wanasadiki, Sanamu ya Bikira Maria wa Upendo wa Mungu iliyo katika eneo hili iliweza kuuokoa mji wa Roma dhidi ya kuanguka katika mikono ya maadui wakati wa vita kuu ya pili ya dunia.

Ushuhuda wa kuokelewa na Bikira Maria wa Upendo wa Mungu, ndiyo asili ya hija katika eneo hili ambako waamini wanapenda kwenda kuomba msaada wa kwa Bikira Maria kutatua shida zao mbalimbali na pia kwa ajili ya kutoa shukurani zao kwa mambo mbalimbali waliyofanikisha.



Maadhimisho ya Juma kuu ili kuadhimisha Fumbo la Pasaka




Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, Kanisa linamshangilia Kristo alipoingia Yerusalemu kwa shangwe na watoto wa Wayahudi wakatandaza nguo zao njiani. Hii ni siku ya vijana kijimbo, inayoongozwa na kauli mbiu, "Heri maskini wa roho maana ufalme wa mbingu ni wao".

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kubariki matawi, umati wa vijana ulianza maandamano kuelekea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, huku wakiimba kwa shangwe. Baba Mtakatifu katika Ibada hii ametumia Fimbo ya Kiaskofu aliyozawadiwa na wafungwa kutoka gereza la Sanremo, Italia. Huu ni mwanzo wa maadhimisho ya juma kuu, Kanisa linapokumbuka mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anatawaka waamini kujitafakari kwa kuangalia hali yao mbele ya Yesu, kama wako kweli na hamasa ya kuonesha furaha na kumshangilia, au wamejikunyata na kumwangalia tu kama "nyanya mbichi". Katika shida na mahangaiko ya Yesu, waamini wanajisikia namna gani na wako upande gani? Je, ni kati ya kundi la wakuu wa Makuhani na Waandishi waliokuwa wanasubiri fursa ya kumkamata na kumsulubisha Yesu?

Je, wao pia ni sehemu ya akina Yuda Iskarioti waliomuuza Yesu kwa vipande thelathini vya fedha? Au ni kati ya Mitume waliokuwa wanauchapa usingizi wakati Yesu anakabiliana na mateso makali? Baba Mtakatifu anawauliza waamini ikiwa kama wanataka njia ya mkato kwa kutumia upanga kama ambavyo alitaka kufanya Mtakatifu Petro? au Yuda aliyemsaliti Yesu kwa busu la unafiki? Au Wazee wa Baraza wanaofanya kila mbinu kwa kutafuta mashahidi wa uwongo ili kumtia Yesu hatiani kwa kudhani kwamba ni kwa ajili ya mafao ya wengi?

Baba Mtakatifu anaendelea kuwauliza waamini ikiwa kama wanafanana na Pilato anapoona kwamba, "maji yamezidi unga" ana nawa mikono ili kukwepa wajibu wake kwa kuwashirikisha wengine. Katika hali ya kuchanganyikiwa na vurugu, Je, hata waamini nao wanaendelea kupiga kelele wakitaka Barabara afunguliwe na Yesu ahukumiwe kifo ili kuwafurisha watu na kumdhalilisha Yesu au kama wale Askari waliomdhihaki, wakampiga mijeledi na kumtemea mate usoni?

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake ambayo yalikuwa ni tafakari inayomshirikisha mwamini binafsi anawauliza ikiwa kama kweli wamekuwa na ujasiri wa Simoni wa Kirene aliyeshurutishwa kumsaidia Yesu kubeba Msalaba wake naye kwa upendo mkubwa akatekeleza dhamana hii! Kuna watu waliokuwa wanapita mbele ya Msalaba wakimdhihaki Yesu kwa vile alijiaminisha kuwa ni Mwana wa Mungu. Baba Mtakatifu anawauliza waamini, Je, hata wao wanajisikia kuwa na jeuri hata kumdhihaki na kumkejeri Mwana wa Mungu?

Bikira Maria na baadhi ya wanawake wajasiri, walisimama chini ya Msalaba kwa ujasiri mkubwa, wakateseka pamoja na Yesu katika hali ya ukimya!, Je, waamini nao wanaendelea kuteseka na Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku, tayari kama Yusufu wa Arimatayo kwenda kuchukua Mwili wa Yesu ili kuuzika au wanawake waliokuwa wanalia mbele ya kaburi la Yesu au wale Askari walioomba ulinzi mkali kwenye Kaburi la Yesu aliyekuwa ametangaza kwamba, baada ya Siku tatu angefufuka kutoka katika wafu? Hawa ni watu waliokuwa wanataka kuzuia maisha mapya kwa njia ya ufufuko wa Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ni maswali msingi ambayo yanaweza kuwasaidia waamini katika tafakari ya maadhimisho ya Juma kuu, Kanisa linapotafakari Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo.

Amepanda Punda na wala si Prado, lakini Yesu anafunika! Wamemkubali!



Katika ulimwengu wa leo suala la maandamano limeshamiri karibu katika kila nchi. Maandamano hayo yanakuwa ya jamii fulani inayodai haki yake, mathalani yanaweza kuwa maandamano ya wanawake wanaodai haki zao za kijinsia, wafanyakazi, wanafunzi, waganga nk.

Maandamano mengine yanakuwa ya kufanya kampeni ya uongozi, na mengine ni ya shamrashamra za sikukuu fulani za kidini au arusi nk. Maandamano yoyote yanakuwa na sehemu mbili maalumu yaani pahala pa kuanzia na pa kumalizikia, sehemu hizo zaweza kuwa hospitalini, shuleni, uwanjani, ikulu au hata kanisani nk.

Leo tutayaona maandamano ya namna yake yanayoendeshwa na Yesu. Maandamano hayo siyo ya kufanya mgomo wa madai ya masilahi toka serikalini, la hasha, bali tungeweza kuuingiza kwenye aina kama vile ya kampeni ya kupigania sera zake za uongozi. Maandamano hayo yalikusanya watu wengi sana, wakiwepo wanafunzi wake, mashabiki wengi na wapambe kibao mpaka mji ukatikisika. Yerusalemu hapakutosha! Mapato yake hata viongozi wa dini na wa serikali walipoyaona maandamano hayo wakataharuki na kuulizana: “Ni nani huyu?”

Maandamano ya leo yalianza pahala palipoitwa Bethfage na yakaishia mjini Yerusalemu tena ndani ya Hekaluni. Humo hekaluni, Yesu anahitimisha maandamano siyo kwa kutoa hotuba refu ya ahadi hewa, hapana, bali kwa kuwashughulikia watu waliokuwa wanachenji hela na kufanya biashara ndogondogo hekaluni, halafu siku ya pili yake anapokuwa na njaa anaulaani mtini usiozaa matunda.

Sasa hebu tupaone kwanza pahala palipoanzia na palipoishia maandamano hayo, yaani Bethfage na Yerusalemu. “Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni.” Bethfage, ipo upande wa Mashariki ya mlima wa Mizeituni, baada tu ya Bethfage kuna mlima wa Mizeituni ambako ukisimama juu yake unaweza kuangalia vizuri sana mji wa Yerusalemu ulio chini yake. Neno hili Bethfage ni muunganiko wa maneno mawili, Beth (Bayet) ni nyumba; na Fage ni matunda ya tini yasiyokomaa. Kwa hiyo Bethfage ni nyumba ya matunda ya tini yasiyokomaa.

Jambo la kushangaza ni kwamba baada ya kuingia Yerusalemu na kuwasambaratisha wafanyabiashara hekaluni, linafuata simulizi la mfano ule ambao unonesha kitu gani Mungu anakitegemea toka kwa Taifa lake, yaani kitendo cha Yesu kwenda kutafuta matunda kwenye mti wa mtini na bila kukuta kitu isipokuwa majani matupu, anaulaani. “Mtini ukanyauka mara.” Tendo lile la Yesu ni mfano hai unaolingana na kile anachokitegemea Mungu toka kwa watu wake kifanyike ndani ya hekalu au katika ibada zao, lakini anakikosa.

Mungu anategemea kupata matunda ya upendo, ya haki, ya kuwajali maskini, wajane, yatima na watoto, wageni, badala yake ndani ya hekalu anakuta majani, yaani, liturjia, nyimbo za kupendeza, madhehebu marefu, chetezo, ubani na mishumaa kwa wingi. Vitu hivi havisemi chochote kile mbele ya Mungu kama havizai matunda. Hivyo siyo sadaka ambazo Mungu anategemea kuziona toka kwa watu, kwake Mungu vitu hivyo ni kama majani tu, au ni kama Bethfage tu (matunda yasiyokomaa).

Baada ya kuona maana ya mandhali ya maandamano, sasa tuwaone wahusika wakuu wa maandamano hayo. Anapofika Bethfage anawaagiza wanafunzi wake wamletee usafiri: “Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, ‘Bwana ana haja nao,’” Maagizo haya ni ya muhimu sana na umuhimu wake unaonekana jinsi masimulizi yanavyorudi mara mbili. Mosi, pale anapowaagiza mitume wake: “mtaona Punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee.” halafu inarudiwa tena inaposemwa. “Wale wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaamuru (kuwafungua), wakamleta yule punda na mwanapunda”. Msisitizo upo katika kuwafungua hao punda na kuwaleta ili waweze kutumika kwa kazi atakayoitaka Yesu waifanye. Endapo maandamano haya ni ya kampeni za uongozi, basi yaonekana siri na sera za uongozi huo zimelala katika Punda hao. Kwa hiyo Punda ndiyo wasanii wakuu wa maandamano ya leo.

Kazi ya wanafunzi waliotumwa ni kuwafungua punda. Wanyama hawa punda wana maana gani katika Biblia? Mfalme wa enzi za Wayahudi aliwastaajabia sana Farasi na wapanda Farasi waliojulikana kuwa hodari kwa kupigana vita. Kwa mfano, tunasikia kuwa askari wa Farao Farasi na wapanda Farasi wao wote waliangamizwa baharini. Hivi hata Wafalme wa kiyahudi walikuwa wanatamani sana kuwa na farasi na wapanda farasi. Katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati, mfalme Salomoni anaonywa asiongeze idadi ya Farasi, na asiuze ndugu zake kwa Wamisri kwa ajili ya kuwa na Farasi na wapanda Farasi (askari). Kutembea juu ya farasi ni alama ya ukuu, uongozi, utawala, ufalme, utajiri na ufahari. Namna ya usafiri unaonesha hadhi ya mtu.

Siku za leo, tunaweza kupata picha ya magari ya gharama na ya fahari wanayotembelea marais, mawaziri, wabunge, makardinali, maaskofu, matajiri, maofisa, nk Itakuwa ni kichekesho na haiwezekani kabisa kumwona kiongozi wa hadhi kama hizo kusafiri kwa lori la mkaa, kwa Bajaji au kwa bodaboda, au baiskeli nk. Katika kampeni za uongozi wa kisiasa, wagombea wanasafiri kwa magari ya gharama za kutisha, kama vile gari aina ya Prado, VX, Helikopta. Hii ndiyo hadhi yao.

Kumbe, katika maandamano ya kampeni za Yesu, anamchagua Punda jike na mwanapunda kuwa prado ya kuingia nayo rasmi mjini Yerusalemu. Hii ndiyo sera mpya ya utawala na uongozi anaotaka Yesu kuuingiza ulimwenguni. Ni kiongozi pekee anayefanya hivyo. Marko anasema kwamba hakukuwahi kutokea mtu mwingine yeyote yule aliyewahi kumpanda yule Punda kabla: “Mtamwona mwanapunda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado” (Mk. 11:2). Tamko hilo la Marko ni muhimu sana, likimaanisha kwamba, hakujawahi tokea mfalme au rais yeyote yule hapa duniani, aliyewahi kujionesha, katika hali kama hii ya utumishi. Yesu ni mfalme wa kwanza na wa mwisho anayependekeza aina hii mpya ya utawala.

Ili kuelewa vizuri ujumbe tunaoletewa hapa hatuna budi kuangalia mwishoni mwa kitabu cha Mwanzo ambako Yakobo anatoa baraka yake kwa watoto wake kumi na wawili, anapotoa baraka kwa Yuda, ambaye ni mtoto wake wa kwanza na atakayekuwa kiongozi wa kabila la Israeli, anasema: “Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, wala mfanya sheria kati ya miguu yake, hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, ambaye mataifa watamtii. Atafunga punda wake katika mzabibu, na mwanapunda wake katika mzabibu mzuri.” (Mwanzo 49:10-11). Sisi hapa tuko mbele ya kituko hicho cha Yesu anayemfungua punda na mwanapunda kama rejea ya Yuda, yaani yule ambaye ataingiza sera za uongozi, utawala mpya ambao hautakuwa na mwisho. Sasa amefika yule ambaye ni kiongozi mpya wa taifa.

Yesu anasema: ‘Wafungueni mniletee’ Wasanii wakuu tunaoletewa hapa leo, wanayo tabia ya pekee sana. Mnyama huyu anafugwa na kuthaminiwa na binadamu hasa kutokana na tabia yake ya kufanya kazi. Kutokana na tabia hiyo, mnyama huyu anayo majina mengine mengi sana yanayowakilisha udundaji wake wa kazi, wengine wanamwita, Nsikiri, Kihongo, Daqwai, Mbunda au Punda nk. Ukitaka kumsifia mtu anayefanya kazi sana wanasema: “Anafanya kazi kama kihongo.”

Hivi Punda ni alama ya kazi, utumishi, na uvumilivu, hachoki kamwe, daima yuko tayari kubeba mizigo. Tabia hii ya Punda ndiyo ilimvutia Yesu hadi akamchagua kuwa mfano wa kuigwa na kipeo cha utumishi ambao unawakilishwa katika nafsi ya kila mtu. Sisi tunashangaa tunapomwona Yesu anajilinganisha na Punda. Kumbe, yeye alitaka daima ajioneshe kama mtu wa kutumikia. Kwa hiyo anapoagiza “wafungueni Punda” anamaanisha kuwa, Punda hao walikuwa wamefungwa, na katika hali hiyo ya kufungwa hawawezi kufanya kazi. Ilibidi kwanza wafunguliwe ili waweze kufanya kazi.

Kila mmoja wetu anao uwezo wa kufanya kazi na uwezo wa kutumikia. Tunayo hali hiyo kutokana na kufanana kwetu na Mungu katika upendo. Upendo ni zawadi kwa maisha yetu maana yake ni kuwajali wengine, yaani kutumikia. Ndani yetu sisi tunaye huyu Punda, Kihongo, Nsikiri nk. Kwa hiyo, endapo punda hao ni sisi, basi yabidi tufunguliwe tuwe huru kufanya kazi yaani, kutumikia, kuvumilia, kunyenyekea, kuwa tayari daima... Yaani tunao uwezo wa kutumikia, lakini daima tumejifunga hatutaki kujifungua ili tuwe huru kutumikia, badala yake tunataka daima kutumikiwa.

Yesu anawapa wanafunzi wake kazi: “Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, mtaona Punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee”. Kazi ya wanafunzi ni kuamsha nguvu ya kutumikia iliyo ndani yetu, kuifungua na kumpelekea Yesu.

Yesu anaongeza kusema: “na kama mtu akiwaambia neno, semeni, ‘Bwana ana haja nao’”. Maana yake akitokea mtu fulani anakataza au anaonesha kupinga. Mtu huyo si mwingine bali ni mimi ninayesema: Tafadhali uniache huru, Usimfungue punda aliye ndani mwangu. Lakini Yesu anakuhitaji anasema: “Nina haja nawe,” kwa sababu kwa njia ya ushirikiano wetu, Yesu anaweza kuanzisha utawala wake duniani kwa kishindo, lakini siyo utawala wa kukandamiza, bali wa utumishi, wa upendo, na wa haki. Yesu anahitaji mchango wa kura ya moyo wako kwa kadiri ya uwezo wako yaani ujifungue, uwe huru, ujiruhusu, kuwa na haki na upendo wa kutumikia, kuwa tayari kusaidia wengine kusudi kuunda uongozi mpya.

Nabii Zakaria anasema: “Tazama, (Yerusalemu) mfalme wako anakuja kwako, mpole, naye amepanda Punda, na mwana Punda, mtoto wa Punda.” Nabii anasema, mfalme huyo haendi vitani kama mpanda-farasi, bali amepanda punda ambaye ni kwa ajili ya kazi ya kutumikia. Kwa hiyo mfalme (kiongozi) huyo anakuja kutumikia. Wanyofu ndiyo watakorithi ulimwengu huu mpya.

Baada ya kuipata sera ya Yesu kutokana na aina ya usafiri aliotumia katika kampeni yake, sasa tuwaone waandamaji katika msafara huu wa Yesu. Punda walipowasili, “wanafunzi wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake. Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani: wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.” Vifaa hivi na matendo ya waandamaji ni muhimu sana katika maandamano haya. Hebu tuyafuatilie.

Tafsiri halisi ya nguo hapa ingekuwa mgolole au shuka, yaani ni nguo ya binafsi inayomsitiri mtu anapoivaa au hata kujifunika anapolala. Kadhalika kwa Myahudi, hiyo ilikuwa ni nguo yake binafsi. Ni sawa na vazi binafsi ambalo mtu huwezi ukalitoa kwa yeyote. Unaweza ukagawa kitu kingine lakini siyo shuka ya kujifunika au mgolole wa kujitanda. Kwa hiyo nguo hizo ni alama ya utu wa mtu, nafsi yake, uwepo wake na kila kitu chake.

Wanafunzi wanaweka au kutandika shuka na migolole yao juu ya Kihongo na mtoto wake, inamaanisha kwamba wao wanayatoa maisha yao na kila kitu ikiwemo utajiri wao, kwa utumishi unaopendekezwa na Yesu kutokana na tabia ya huyo Kihongo. Yesu anaikalia hiyo migololi ya wanafunzi hao kuonesha kuwa wako chini ya utawala ambao Yesu ndiye mfalme wake. Wanakubaliana na uongozi huu pamoja na sera zake. Yesu mwenyewe akiwa mnyofu, mnyenyekevu, mpole na mtii anasafiri juu ya Punda aliye mvumilivu, mfanya kazi, mtumishi tu na anakaa juu ya migololi hii ya wanafunzi. Wamepokea, na kuukubali uupya wa masiha huyu, mtumishi na mleta amani. Ndiyo maana ya kuweka migololi yao juu ya Punda.

Watu wengine wengi pia wanajitokeza kushangilia: Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani: wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.”

Watu hao wanafanya mambo tofauti na wanavyofanya wanafunzi. Wanafunzi wanatandika migololi yao juu ya punda kuonesha kwamba wao ndio wanaoendeleza sera za mtindo huo wa uongozi. Watu wengine kumbe wanatandaza nguo zao njiani au barabarani. Kiutamaduni ilikuwa kwamba, wakati wa kumtawaza kiongozi, watu walikuwa wanatandaza nguo ardhini na kushangilia ikiwa na maana kwamba walikuwa wanakubali kujitoa na kujiweka chini ya uongozi wa huyo mfalme.

Katika nafasi hiyo watu walikuwa wanashabikia na kupiga vigelegele lakini mara nyingi hawakuelewa sera za uongozi huo. Katika kundi la maandamaji wa leo yaonekana kulikuwa na wapambe wengi sana: “Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani, na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza wauti wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarakiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.” Watu hawa wote walikuwa wanamshabikia mfalme huyu lakini pengine kadiri ya sera walizokuwa wanazifikiria wao.

Wanampokea lakini kadiri wanavyoelewa wao aina ya Mfalme wanayemtegemea. Ni tofauti na mitume wanaoweka nguo zao juu ya punda. Hata katika mazingira yetu ya sehemu mbalimbali yaweza kutokea wachache wanaoelewa maana ya utumishi ya kumfuata Yesu na watu wengine wakabaki ni wapambe na mashabiki tu. Watu hao wanakata na matawi ya miti kushangilia.

Kuhusu matawi ya miti, kunakumbushia Sikukuu ya Vibanda. Siku hiyo waliyakata matawi ili kusherekea kumbukumbu ya kukombolewa toka utumwani Misri. Hapa sasa wanakata matawi kuonesha kuwa sasa wanao uhuru kwa sababu Masiha amefika. Lakini Masiha huyo wanayemdhani ni wa aina gani? Hapo tunaona ukweli wa usemi kwamba “katika msafara wa mamba kenge nao hawakosekani.” Watu waliendelea kuimba “Mwana wa Daudi” lakini ni mwana wa Daudi wanayemtegemea wao.

Katika sikukuu hii ya Matawi tunaalikwa kujihoji upya ushirika wetu na Kristu. Endapo tunataka kidhati kuwa washiriki wa ufalme mpya anaotupendekezea Yesu yabidi tumfungue punda aliye ndani mwetu ili kuwa na uwezo wa kupenda ambao Mungu ametupatia. Tuwe Punda, Kihongo au Nsikiri aliyefunguliwa na kukubali kumbeba Kristu, yaani kutumikia kwa upendo.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

BATAROKOTA AOMBA KURA ABEBE TUZO YA KILI

Na Dina Ismail, Dar es Salaam
MSANII wa muziki wa asili nchini, Pascal linda maarufu kama Batarokota amewaomba mashabiki wa muziki nchini kumpigia kura kwa wingi ili aweze kushinda tuzo za kili mwaka 2014.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY, msanii huyo alisema kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho kumefanikushwa na mashabiki hao hivyo amewaomba kuendelea kumpa ushirikiano kwa kumpigia kura kwa wingi.
Batarokota anaomba kura zenu

"Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sintowashukuru wadau wa muziki hivyo nawaomba waendelee kunisapoti kwa kunipigia kura",alisema
Batarakota ambaye wimbo wake wa Kwejaga Nyangisha umeteuliwa kuwania tuzo hizo kupitia kipengele cha wimbo wenye vionjo vya kitanzania amewaomba mashabiki kumpigia kura kwa kuandika ab1 kwenda no 15440.
Aidha msanii huyo mzaliwa wa Mwanza akifanya kazi zake nchini Kenya, anaimba nyimbo zake akitumia lugha za Kisukuma, Kinyamwezi na Kinyakyusa ambapo kwa sasa yupo mbioni kukamilisha albamu yake ya kwanza.
Batarokota katikati akiwa na rafiki zake Wazungu

Jumapili ya Matawi



Mpendwa mwana wa Mungu karibuni katika kipindi cha tafakari tunapoadhimisha Dominika ya Matawi, Dominika ambayo ni mwanzo wa Juma Kuu, Juma la Pasaka. Kabla ya Misa Takatifu daima tunaanza kwa maandamano ambayo ni ishara ukumbusho wa kuingia kwa Yesu Kristu Yerusalemu.

Ni ishara ya utukufu kwa Mungu juu mbinguni. Mwaliko ambao Mama Kanisa anatupa ni ule wa kumshangilia Bwana na kuandamana tukimsindikiza kuelekea Yerusalemu. Kwa kawaida yaweza kuonekana tunafanya kumbukumbu tu lakini si hivyo bali tunashika imani na tunamsindikiza na kupata neema zote alizozitoa wakati ule na tunashika njia yetu ya kumfuasa yeye tukielekea Pasaka ya Mbinguni.

Ewe msikilizaji, kwa kawaida tunajua kuwa Kristu aliteswa, akafa na kisha kufufuka, kumbe kwa njia hiyo tunapata tumaini na tunaalikwa kufuata nyayo zake daima mpaka kufa kwetu. Kwa jinsi hiyo njia ya Bwana ni njia yetu sote. Mama Kanisa ametuwekea mateso makali ya Bwana mbele yetu ambayo yaweza kuwa ni tishio na hivi kujenga woga katika safari, hata hivyo hatuogopi maana ikiwa Bwana ambaye hakustahili alivumilia, je sisi ambao twasitahili twaweza kukwepa wajibu huo? Si hilo tu bali pia matunda ya mateso makali ya Bwana tumeona ni wokovu wa ulimwengu.

Bwana anapokaribia kuingia Yerusalemu ili kumalizia njia yake ya mateso anapanda mwanapunda, hii ni ishara ya unyenyekevu, ishara ya kuwa yeye si mfalme wa mabavu bali anayetumia upendo kujibu ubaya wa ulimwengu. Hii haina maana kuwa hana uwezo, bali uwezo wake ni kwa ajili ya wokovu wa watu na si wa mapigano ya kivita.

Watu wote wanatandaza nguo na majani ya mitende wanaimba Hosana Mwana wa Daudi, hili ni shangilio kwa Mungu wa mbinguni, ni kiitikio cha utukufu na ushindi wa Bwana. Kwa hakika ni mwendelezo wa shangilio ambalo malaika walilitoa kwa Mwana wa Mungu alipozaliwa pangoni Betlehemu, (Lk 2:14). Jibu la shangilio hili tumpalo Bwana ni amani yangu nawapa, yaani amani iliyo zawadi kwetu, (Yn 14:27).

Nabii Isaya anapoagua juu ya Masiha anatuwekea Masiha aliye mvumilivu, anayetukanwa anayekubali kupigwa na hata kung’olewa ndevu lakini hajibu mapigo, bali ametulia na kuweka tumaini kwa Mungu wake. Jambo hili linakamilika katika Bwana wetu Yesu Kristo, anapoingia Yerusalemu. Mwinjili Matayo anasema tazama maaskari wa Pilato wanavyomdhihaki Yesu Mkombozi” (Mt. 27:27-31). Kwa jinsi hii Nabii Isaya anamtangaza Masiha mshindwa, mteswa, asiyeua lakini anayehuisha kwa upendo na kuleta wokovu.

Mpendwa msikilizaji, Mtume Paulo anawaonya Wafilipi na kisha kuwaimarisha katika kuiga na kujifunza kwa Bwana. Katika familia ya Wafilipi kuna chuki, ugomvi na fitina na hivi anawapa wosia akisema kila mmoja amthamini mwenzake na kwa kukazia wosia huu anaweka mbele yao Yesu Kristu Masiha aliyejishusha mpaka kuwa mwanadamu na si ubinadamu tu bali hata kuteswa na Warumi! Chukua muda kidogo tafakari na fikiri juu ya upeo wa jambo hili!

Fikirini mtu bilionea akijishusha na kukaa na maskini! Kwa hakika mbele ya ulimwengu atakuwa wa ajabu lakini wa maana zaidi mbele ya Mungu. Kristu kwa umwilisho wake hakupoteza Umungu wake bali ulibaki umejificha na hivi Mungu Baba akamwadhimisha mno kwa unyenyekevu wake. Basi mwaliko kwako ni amani na utulivu daima, na Mungu atakuadhimisha mno!

Katika Injili ya Marko katika historia ya mateso anatuwekea Yesu Kristu asiyejibu ubaya wowote unaoelekezwa kwake au kwa wengine kwa nguvu za kivita bali kwa neno la upendo. Tazama dhihaka ya Yuda Iskariote, tazama Mtume Petro anapotumia upanga kukata sikio la mtu aliye kinyume na Bwana. Yote haya anayajibu kwa utulivu na unyenyekevu wa hali ya juu akisema, rudisha panga alani!

Katika Injili ya Matayo tunamwona mwinjili akiweka mbele yetu msisitizo wa ukamilifu wa yale yaliyoaguliwa na manabii hapo kale juu ya Masiha, yakwamba atateswa na kisha kufa. Tunasoma hili katika aya ya 24: wakati wa karamu ya mwisho akishatangaza atakayemsaliti anamalizia akisema, “Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama maandiko matakatifu yasemavyo”.

Katika aya ya 56, pale Getsemane wanapomkamata, yeye mwenyewe anasema tena, “lakini haya yote yametendeka ili maandiko ya manabii yatimie, kisha wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia”. Mwinjili Matayo anaweka mkazo katika hili kwa sababu anawaandikia Wayahudi akilenga kuweka vizuri dhana ya Masiha yakwamba tegemeo lao la Masiha mwenye utukufu na nguvu za kivita hayupo, bali mpole na mnyenyekevu wa moyo.

Anawajibu wale wote waliokwazwa na tendo la Masiha kuteswa, akileta hoja ya Agano la Kale ya kwamba ilikwishatangazwa na Manabii kwamba angetendewa hivyo. Mpendwa msikilizaji wewe uko upande gani? Upande wa Masiha mwenye siraha za kivita au mpole na mteswa? Tafakari!

Kwa kukaa katika upande wa Masiha mteswa basi unakubaliana na fundisho la Matayo akinukuu maneno ya Bwana, yaani rudisha panga alani. Jambo hili anaambiwa Mt. Petro, wakati huohuo Bwana mwenyewe anarudisha sikio la aliyekatwa. Masiha anamwambia Mt Petro asitumie upanga kamwe maana atumiaye upanga atakufa kwa upanga. (Mt. 26:52) Katika hili Bwana anatangaza amani na upole wa moyo mbele ya madhulumu. Kumbukeni mafundisho ya Origen katika karne za kwanza: “sisi wakristu hatuchukui mapanga tena, hatujifunzi tena kupigana vita kwa maana kwa njia ya Kristu Yesu tumekuwa watu wa amani”

Tunapata kusikia tu, katika Injili ya Matayo kifo cha Yuda Iskariote 27: 3-10). Yuda ni alama ya wafuasi wa Bwana ambao ni wa muda tu wakitarajia ushindi na mafanikio katika mipango yao na hivi Bwana anapoonesha kushindwa basi hukimbia na kumtafuta bwana mwingine ambaye kwa hakika ni kifo. Yuda anakata tamaa, haoni kwamba Bwana ni huruma upeo, kiasi kwamba angeweza kuomba msamaha kama yule mwizi wa msalabani.

Mpendwa msikilizaji, tukio jingine ambalo tunalikuta katika Injili ya Matayo tu, ni lile la kuwekwa walinzi katika kaburi la Bwana, Mt. 27:62-66) Hawa ni alama ya ushindi wa shetani. Yesu anaonekana kushindwa kabisa, na kupatilizwa katika kaburi. Hata hivyo Mungu ataingilia kati na kuonesha ushindi wa Mwanae wa pekee Mt. 28:4. Walinzi watashtushwa na mwanga mkali wa Pasaka na Bwana ataibuka kidedea akiwa mfufuka na mshindi wa vita dhidi ya shetani.

Mpendwa msikilizaji Mwinjili Matayo pamoja na Wainjili wengine wanatuwekea alama ya kupasuka kwa pazia la hekalu vipande viwili toka juu hadi chini akitaka kutuambia kuwa kwa njia ya kifo cha Bwana mipaka kati yetu na Mungu imeondolewa na si tu kati ya Mungu nasi bali kati yetu sisi kwa sisi. Tangu siku anakufa msalabani wote tu wana wa familia moja ya Mungu.

Mpendwa mwanatafakari ukiyakumbuka mateso ya Bwana na kuyaweka moyoni na kisha kuyaunganisha mateso yako na yake basi Pasaka kwako ni Ufufuko kweli. Ninakualika basi umsindikize Bwana katika Juma hili Kuu kwa furaha na utulivu mkamilifu ili mwisho wa mateso tupate matunda ndiyo uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako toka Padre Richard Tiganya C.PP.S.

Siku za Vijana Duniani zinapania kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari

Baba Mtakatifu Francisko ana matumaini makubwa katika maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani kama nyenzo msingi inayopania kuasha na kukuza ari na moyo wa kimissionari miongoni mwa vijana ndani ya Kanisa. Ni maneno ya Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa la Walei, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa wakurugenzi wa utume wa vijana, unaofanyika mjini Roma kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 13 Aprili 2014. Mikutano hii ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Krakovia, Poland, kunako mwaka 2016.

Mkutano huu unahudhuriwa na wajumbe 250 kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki 90 na Jumuiya za Kitume 45 sanjari na Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani Rio de Janeiro na Kamati kutoka Jimbo kuu la Krakovia. Kardinali Rylko anasema, katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo, itakayofanyika Jumapili ya Matawi, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko atawakabidhi rasmi vijana kutoka Poland Msalaba wa Siku ya Vijana Duniani, uliotembezwa nchini Brazil kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Brazil.

Tukio hili ni muhimu sana kwa mwaka huu, kwani Mama Kanisa anaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka thelathini, tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, kunako Mwaka 1984 wakati wa Siku kuu ya Pasaka sanjari na kufunga rasmi Mwaka wa Ukombozi, alipowakabishi vijana Msalaba wa Mwaka wa Ukombozi. Ni Msalaba ambao umetembezwa sehemu mbali mbali za dunia kwa kuwasindikiza vijana katika shida na mahangaiko yao bila kusahau furaha na matumaini yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Msalaba wa Mwaka wa Ukombozi, umekuwa ni alama ya toba na wongofu wa ndani, chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba ni Msalaba ambao kweli umekuwa ni kikolezo cha imani na matumaini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kama alivyosema Baba Mtakatifu Francisko nchini Brazil ni maadhimisho ya imani na udugu na kwamba, hii ni zawadi kubwa kwa Mama Kanisa.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 yatafanyika nchini Poland, miaka 25 tangu yalipofanyika kwa mara ya kwanza nchini Poland kunako mwaka 1991 mara tu baada ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin. Hapo dunia ikashuhudia nguvu na jeuri ya vijana waliomiminika kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kuungana katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kwa pamoja wakaimba, ule wimbo maarufu "Abbà, Padre", unaoendelea kuvuma sehemu mbali mbali za dunia.

Tangu wakati huo anasema Kardinali Rylko, kumekuwepo na mabadiliko makubwa sana ulimwenguni na ndani ya Kanisa. Kuna mabadiliko makubwa katika ulimwengu wa vijana wanaoogelea katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kumbe, maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni kikolezo cha ari na mwamko wa kimissionari, kwa kutafuta na kuibua mbinu mkakati kwa ajili ya utume wa Mama Kanisa kwa vijana.

Kwa namna ya pekee, wakati huu, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia umuhimu wa upendo na huruma ya Mungu; toba na wongofu wa ndani. Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha tukio la kihistoria kwa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu hapo tarehe 27 Aprili 2014. Kanisa katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani itakayofanyika nchini Poland kunako mwaka 2016, itamkumbuka Papa Yohane Paulo II muasisi wa Siku za Vijana na Msimamizi wa maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani.

Mwenyeheri Yohane Paulo II kwa vijana ataendelea kuwa ni Baba na Rafiki; Mlezi na Msimamizi wa vijana mbinguni. Mkutano huu umefanya pia tathmini ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika Rio de Janeiro, Brazi, pamoja na kuangalia matunda ya shughuli za kichungaji yaliyopatikana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani nchini Brazil kwa njia ya ushuhuda na taarifa mbali mbali zilizowasilishwa na wajumbe.



Usilete mzaha, ananuka!

Manamuziki Remmy Ongala anakilalamikia kifo pasipo kutushauri tukikabilije: “kifo kifo kifo hakina huruma! Ukitaka kujua ubaya wa kifo, pita hospitalini, utakuta wengine wanalia. Wengine hawana miguu tena, wengine wana vidonda, wengine wana vipele, wengine wana ukurutu, wengine wamezaa watoto wamekufa shauri yako wewe kifo, kifo kwa nini unatusumbua. Tumezaliwa shauri ya kuishi. Ulimwengu bila watu siyo ulimwengu tena. Kifo we! Kifo kifo kifo hakina huruma…. Kifo ni kiboko yao!”

Ni ukweli kabisa, kifo hakina huruma, kifo kinatia uchungu, kifo kinakatisha tamaa ya maisha. Mbele ya kifo watu tunalia machozi. Ongala anakilaani kifo kiasi kwamba anaona hata magonjwa na ajali yanasababishwa na kifo. Ninakipongeza kifo kwa sababu kinatufanya watu wote tulingane! Kinamvaa kila mtu, bila kujali umri, cheo, ukuu, kabila, dini, jinsia. Kifo hakipokei rushwa. Ama kweli kifo ni kiboko kikali! Bahati mbaya na nzuri ya kifo kinawafanya wafiwa wengi wachanganyikiwe na kuanza kumlaani na kumtukana Mungu, kwa wafiwa wengine kinawakomaza kiimani na kimaadili. Hata kama tukilia na kulalalmika namna gani kifo kinabaki palepale na msimamo wake! Kifo ni suala nyeti. Je, haiwezekani kufanya appointment ya kukutana na kifo na kujadiliana naye suala hili nyeti?

Jumapili iliyopita tulitafakari “Ishara” jinsi anavyoita Mwinjili Yohana kuhusu uponyi wa upofu. Jinsi kipofu anavyozawadiwa mwanga au anavyofunguka macho. Ishara ile ilikuwa kama aina mpya ya uumbaji anaofanya Kristo. Lakini hata baada ya huko kufunguka macho, tunabakiwa bado na maswali dodoso ya kujihoji juu ya maisha. Mosi, Kristu anatufungua macho ili tuone nini au twende wapi? Pili, je, lengo la kutufungua macho ni kwa ajili ya kuona tu mambo hapa duniani halafu mwisho wake iwe nini?

Aidha, hata kama Yesu ananifungua macho na kuniwezesha kutembea vyema humu ulimwenguni, Je, maisha haya yana maana gani endapo hayana hatima? Je uzee usioisha na unaoendelea tu bila kwisha utauita ni ushindi dhidi ya kifo? Halafu hali hiyo ya uzee itaishia wapi wakati ulimwengu unaendelea kudumu tu hata bila ya mimi? Je, maisha hayo yanayoendelea tu yatakuwa na maana gani ndani yangu? Maswali kama haya ndiyo tutakayoyatafakari katika injili ya leo.

Tukitaka kuelewa vizuri hali halisi ya maisha tunayoyaishi, hatuna budi kuangalia kwa makini upi ni mwisho wake. Ni sawa na usafiri wa mguu usianze tu kusafiri kichwakichwa bila kujua wapi unaenda na umbali wake. Tunaposema mwisho wa maisha tunamaanisha kifo. Yaani, yabidi kukitafakari kifo, vinginevyo maisha yetu yote yanakuwa ni kutorokatoroka na kukikimbikimbia kifo, kwa kuogopa kukabili ukweli huo wa maisha ambao hatuna budi kuukabili.

Ni utamaduni wa binadamu ambao mara nyingi matendo ya maisha yetu yanajaribu kuepa kupanga ratiba ya kukutana na kifo. Kumbe, unaona kifo kinaendelea kututia wazimu hadi kutukosesha raha kabisa. Muziki wa Ongala unatupa hali halisi ya woga wa binadamu mbele ya kifo. Ni woga mkuu usioleta matumaini. Ama kweli “usilolijua litakusumbua.”

Ni ukweli dhahiri kwamba sisi binadamu tumeumbwa kwa ajili ya maisha ambayo hayana kikomo. Kwa hiyo ni vyema kukumbuka maneno ya mzaburi anayosema: “Ee Bwana utufundishe kuhesabu siku zetu, tujipatie hekima ya moyo” (Zab. 90:12). Tuwe na busara kutambua siyo kwa woga kwamba maisha yetu ni mafupi sana na tujaribu kuyapangilia vizuri.

Leo tumebahatika kuwa na mihadi (appointment) ya majadiliano na kifo kilichomwingia mwenzetu Lazaro. Msemaji mkuu katika mazungumzo hayo ni Yesu pamoja na wafiwa ambao ni dada wa damu wa mfu.

Tukifuatilia kwa makini mazungumzo hayo tutagundua uhondo uliomo katika ishara hiyo na kuelewa kifo ni nini na kina faida au hasara gani kwetu. Awali ya yote tuelewane juu ya matumizi ya msamiati wa neno kufufuka na tunavyolitumia kwa Lazaro. Hilo neno hapa siyo pahala pake kwa sababu neno kufufuka linamaanisha hali ya kupita toka ulimwengu huu na kuingia mbinguni kwenye maisha ya milele ya kukaa na Mungu Baba. Kwa mfano tunazungumza juu ya kufufuka kwa Yesu ikiwa na maana kwamba ameingia mbinguni na kuketi pamoja na Mungu Baba.

Kwa hiyo Yesu amefufuka yaani amepita toka ulimwengu huu na kuingia ulimwengu wa Baba. Kufika mbinguni na kumwona Mungu ni kikomo komesha na “Hakuna aliyemwona Mungu akarudi tena duniani.” Kwa hiyo kama Yesu alimfufua Lazaro ambaye alishaingia katika ulimwengu wa Baba basi alimkatishia mwenzake uhondo wa kukaa na Mungu. Kwa hiyo tunapozungumzia juu ya Lazaro, tusitumie neno kufufuliwa bali tutumie neno kuhuisha. Lazaro alihuishwa kwa sababu hakuwa ameingia katika maisha ya milele mbinguni.

Lazaro alirudishiwa uhai wake na akaendelea kuishi tena hapa duniani, ingawaje hatujui alikuwa wapi kipindi kile alichokufa na kuzikwa. Kati ya miujiza mingi aliyoyaifanya Yesu tendo hili la kuhuisha lilikuwa la pekee sana kwa watu waliolishuhudia, kwani watu walimwona Lazaro ameshafariki na kunuka. Mwinjili Yohani analichukua tendo hili la Yesu kuwa kama ishara, ili kuonesha jinsi gani Yesu ni Bwana wa maisha haya ya kibiolojia.

Hoja ya Yesu kumrudisha tena Lazaro katika ulimwengu huu wa maisha mapya ambayo hayakuwa yameguswa na aina ile ya maisha yenye malengo, yenye hatima, yaani maisha ambayo hayaishii hapa tu, bali yanaendelea na kuishia kwenye maisha ya Baba wa mbinguni. Huu ndio ujumbe mmojawapo ambao mwinjili anataka kutuletea katika ishara anayoifanya Yesu leo.

Sasa tuione kwa karibu ishara hii ya kuhuishwa kwa Lazaro. Masimulizi yanaanza hivi: “Kulikuwa na mtu aitwaye Lazaro.” Huyu Lazaro, alikuwa mwanafamilia ya namna yake. Kwa sababu katika familia hii hatuwaoni wazazi, yaani baba na mama. Tunaona tu kuna kaka na dada wawili Maria na Marta. Maana yake tunaoneshwa jumuia ya wana ndugu, au tungeweza kusema, jumuia ya kikristu. Jumuia ya kaka na dada ambao yabidi wakabiliane na hali halisi ya maisha. Hali halisi ya maisha tuionayo ni ya homa halafu kifo nk.

Katika familia hii tunasikia kuwa kaka mtu anaumwa homa kali inayopelekea kifo. Kabla mambo hayajawaharibikia, akina dada hawa wanatuma ujumbe kumtaarifu Yesu wakiwa na matumaini kuwa angemponya. Wakamwambia: “Bwana, yeye umpendaye hawezi.” Majibu ya Yesu hayaeleweki kirahisi, anaposema: “Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu.” Maana yake, kwa njia ya homa hii kutafumbuliwa kile ambacho Mungu anauwezo nacho na anachotaka kutufundisha. Kwa maneno haya Yesu anataka kusema kwamba yaonekana kuna ugonjwa unaopelekea kifo, na ugonjwa mwingine haupelekei kifo.

Ugonjwa unaopelekea kwenye kifo, ni ule unaoharibu maisha ya kweli ya mtu, yaani maisha yale yasiyo na mwisho. Kama vile isemavyo kwenye kitabu cha Mwanzo. Ukifanya uchaguzi wa mambo kinyume cha yale anayokuagiza Mungu utakufa: “Msile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” (Mwa 2:1) Kama hufanyi mambo kadiri alivyoagiza Mungu, unaharibu maisha yako halisi, maisha ya utu, ya binadamu. Huko ndiko kunakoitwa kufa-basi! Lakini kuna homa ambayo inakupeleka kwenye kifo cha kimwili tu (kibaolojia).

Kifo cha kimwili ni kile ambacho Mungu alishakipanga kwa ajili ya binadamu. Kifo cha aina hiyo hatuwezi kamwe kukikwepa. Hiki siyo kifo anachomaanisha Yesu. Ukweli Yesu aliipenda sana familia hii tena ni mapendo ya Kristu yanayotakiwa katika juimuia ya kikristu. Lakini unaona kuwa Yesu anaposikia kwamba Lazaro anaumwa, anabaki alipo na kuchelewa kwa siku mbili zaidi hadi Lazaro anakufa. Je upendo wa Mungu upo wapi pindi anatuacha tufe? Yesu anampenda Lazaro lakini anapomwacha afe anataka kutupa ujumbe. Hapa linaingia suala la ukuu wa Mungu.
Sisi tungependa kwamba Mungu aturuhusu tu tuingie paradisini pasipo kufa. Je, Mungu anaweza kuruhusu jambo hilo? Jibu ni hapana! Mungu angeweza kuruhusu hilo, lakini ingekuwa kama kutudanganya na kutuchanganya, kwamba Mungu anatupatia uhai huu ili aturudishie tena mwili huu wa kibinadamu tuendelee nao bila kwanza kuubadili kidogo. Tatizo ni kwamba, maisha yetu ya kibaolojia, yanahusu ulimwengu huu, lakini kwa vile ndani mwetu tuna maisha ya Kimungu, tunapopaswa kuingia katika maisha ya Mungu, kwa hiyo maisha haya budi yakome. Anayeshiriki maisha ya kimungu hawezi kufa, hawezi kupambana na kifo kile cha kibaolojia. Hadhi yetu ya kibidamu ipo kwa ajili ya kufa ili kuendelea na maisha ambayo Mungu ametuandalia.

Kwa kumwacha Lazaro afe, Yesu anataka kutuonesha waziwazi kwamba yeye hajafika kuzuia kifo hiki cha kibaolojia. Yesu anaacha mambo yafuate mfumo wake wa kimaumbile (wa kibaolojia). Mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe anapowalilia wanamuziki waliofariki, anakubali kwamba kifo ni njia ya kila binadamu, anaimba: “Wanamiziki na wanamichezo wote hapa nchini Tanzania, hujiwa na majonzi kila mara tunapowakumbuka waliotutoka. Rambirambi zetu ziwafikie wanandugu. Kifo ni njia ya kila binadamu. Hatuna budi tutoe masikitiko na imani zetu kwa yao mazuri.” Kwa vile “Kifo ni njia ya kila binadamu”, Basi lengo la Yesu likatimia, kwani anapofika Bethania Lazaro alishafariki kitambo na kuzikwa siku nne zimeshapita.

Mandhali anayoikuta Yesu ni ya msiba. Hivi kulikuwa na watu wengi waliofika kuwatuliza wafiwa. Hapa unaalikwa kuvuta taswira (picha) kidogo ya hali halisi inayokuwa msibani, na ya watu wanaotuliza wafiwa. Mara nyingi watuliza wafiwa wanasema: “Poleni na msiba! Mtulizike ni mapenzi ya Mungu! Kazi ya Mungu haina makosa! Marehemu atabaki daima kwenye kumbukumbu ya mioyo yetu! Pengo lake haliwezi kuzibika tena! Sisi tulimpenda, lakini Mungu alimpenda zaidi! Bwana alitoa, na Bwana ametwaa, jina la Bwana na libarikiwe! nk.

Wakati mwingine inawekwa kanda ya muziki wa nyimbo za maombolezo. Pengine zinachapishwa hata kadi za ukumbusho na kuvaliwa sare za msiba nk. Yote hii ni kwa ajili ya kutuliza wafiwa. Lakini hata hivyo unaona wafiwa hawatuliziki sana wanazidi kuwa na majonzi na kubujika machozi. Hiyo ndiyo hali halisi inayoletwa na kifo. Kumbe ingefaa zaidi katika mazingira kama hayo kukitafakari kifo. Na katika misiba ya kikristu yatakiwa kutafakari kuhusu mwanga huu anaotupatia Kristu, yaani tumaini la ufufuko.

Hebu sasa tumfuatilie Yesu anapofika msibani anakabilianaje na mazingira haya magumu ya uchungu na huzuni? Atawatulizaje wafiwa hawa? Aidha wafiwa wenyewe wanamtazamaje Yesu aliyechelewa kufika licha ya kuambiwa hali ya mgonjwa kabla hajafa? Vituko anavyovionesha Marta kwa Yesu vinawakilisha vituko na fikra za wengi wanapokabiliwa na msiba au matatizo mazito. Mara nyingi tunasikia hata watu wa dini wanapokuwa katika matatizo, wanakosa imani, wanamkasirikia Mungu, wanakatishwa tamaa ya kuamini.

Angalia sasa Yesu anapofika pale msibani Marta anaanza kumvaa na kumgombeza bila hata ya kumwamkia: “Bwana kama ungalikuwapo hapa ndugu yangu hangalikufa.” Yesu anamwelewa vizuri tu Marta anajaribu kumtuliza kwa maneno aliyozoea kuyasikia mfiwa kadiri ya fikra za wengi ili aweze baadaye kuyatolea maelezo ya kina anamwambia: “Usijali ndugu yako atafufuka.” Kwa jibu hilo la Yesu, Marta anazidi kuchafuka nyongo tu, kwani haoni jipya kwa sababu alishakeremishwa ukweli huo kwenye imani ya mafarisayo juu ya ufufuko ujao kwa hiyo mara moja anamdakiza Yesu: “Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.” Ni dhahiri kwamba uelewa huu wa ufufuko ujao hauna maana yoyote.

Ufufuko utakaokuwepo sijui lini, yaani Mungu atuache tufe kisha baada ya kupita miaka mingi aturudishie tena maisha haya. Imani ya mtindo huu haiwezi kumtuliza mtu. Kutokana na udhaifu huo wa hoja ya ufufuko wa siku ya mwisho, Yesu anaongeza maneno yanayoleta maana na yanauyotuliza anamwambia kwa mkazo: “Mimi ndimi huo ufufuo na uzima.” Kumbe kama tuko gizani, basi tunahitaji mwanga toka nje unaoweza kutuangaza. Kujijulisha namna hii kwa Yesu kunafanana na kule alikomwambia yule Msamaritana pale kisimani: “Mimi ninayesema nawe, ndiye.”

Ni mimi niliye hapa ndiye ninayeweza kuhuisha mambo, ninayeweza kuwatuliza, wale waliokata tamaa ya maisha. Hapa mpangilio wa maneno unaanza na ufufuo halafu Uzima. “Mimi ndimi ufufuo na uzima”. Yaani kwanza kuwekwa huru halafu kuishi milele. Ufufuo ndiyo kitu cha muhimu zaidi katika maisha yetu ya sasa. Ufufuo ni mwito hasa kwa walio wazima kimwili halafu kwa waliokufa. Sisi tumeshakuwa wafufuka anavyosema Paulo: “Hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu, alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, mmeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.” (Efeso 2:5-6). Ni kwamba mtu huyu amepata maisha au uzima ambao hauwezi kumtoka kutokana na kufa kibaolojia.

Maisha ya mbinguni ni bora zaidi kuliko maisha ya duniani. Jaribu kupata picha ya watoto pacha walio bado tumboni mwa mama. Humo tumboni watoto hao wanalishwa chakula toka mwilini mwa mama yao. Inapotokea kwamba mmoja anatangulia kuzaliwa, yule aliyebaki tumboni anaweza kuwaza kwamba mwenzangu amekufa. Lakini yule aliyezaliwa na kuona mwanga anaufurahia uso wa mama yake ambao kabla yake hakuujua ulivyo ingawaje mama yake huyo ndiye aliyekuwa anampa uhai alipokuwa bado tumboni. Sasa anauona laivu uso wa mama yake. Vivyo hivyo Yesu anaposema anayenisadiki mimi hatakufa anamaanisha kwamba baada ya maisha haya kuna maisha mengine utakayoyaona laivu.

Dada mwingine, Maria naye anafika kwa mtindo wake. Yeye anafika huku analia. Yesu anapomwona Maria analia anamwelewa kwamba hayo ni mapato ya kifo ndiyo yanayofanya mtu alie. Lakini kilio cha Maria na cha waombolezaje wengine ni kile cha sauti na cha kukata tamaa. Tofauti na kilio cha Yesu baada ya kuuliza: “Mmemweka wapi?” Yesu analia, lakini kilio chake hakikuwa cha kukata tamaa bali yasemwa yalikuwa yanamtoka tu machozi. Kwa hiyo hata mtu mwenye imani yatamtoka tu machozi mbele ya kifo. Baada ya kuelewana hivyo juu ya ufufuo na uzima, sasa Yesu anaanza kufanya vitu vyake ambavyo ndiyo ishara inayoonesha kuwa yeye ni ufufuo na uzima. Hapa Kifo kinakatwa kilimilimi.

Yesu anaagiza kuliondoa jiwe lililofunika pango alimowekwa mfu. Kuliweka jiwe juu ya pango maana yake ni kuliziba. Kitendo hiki cha kufunika kinatafsiriwa kuwa ni cha kusahau. Kwamba kesi ya mtu aliyekufa imeisha. Hebu ifunike! “Funika kikombe mwanaharamu apite”. Kumbe Yesu anaagiza: “Liondoeni jiwe.” Kwa sababu haina maana kuufunika kwa jiwe ulimwengu wa wazima katika shimo la “sahau” na kumtenga na ulimwengu wa watu walio paradizini. Martha anapata bado shida ya kuelewa maana ya kutoa jiwe lile wakati mambo yameishaharibika kabisa na yananuka.

Bado ana mashaka, akdhani kwamba mambo yataweza kumzidi Yesu. Anadadisi: “Ananuka kwa vile amekaa humo siku nne.” Marta hajui kwamba kunuka ndiyo pia ni hali halisi ya kifo. Yesu anamwambia: “Marta kama unasaidiki, utaona utukufu wa Mungu.” Baada ya kufunguka macho yabidi kuangalia mambo kwa undani zaidi na kuona mambo ambayo macho ya kawaida hayawezi kuyaona. Maana yake, kama unasadiki utaweza kuona.

Toka hapa sasa kunafuata mahitimisho ambayo ndiyo uhondo wa Injili yote ya leo. Yesu analia kwa sauti kuu: “Lazaro njoo huku nje.” Hiyo sauti ni kilio cha ushindi. “Mfu akatoka,” huyo anatamkwa jina la mfu na siyo kwa jina la Lazaro. Mfu alitoka aliyeviringishwa sanda miguuni, mikononi na uso umefungwa leso. Mfu huyo hatuoni wala sisi hatumwoni. Ameviringishwa nguo na kufunikwa leso kama vile mtoto mchanga aliyezaliwa.

Hapa ni dhahiri kwamba tunaletewa fundisho muhimu sana la kiteolojia, kwamba hata Lazaro amezaliwa toka tumbo la kaburi. Ni ukweli usiopingika kwamba Yesu amemhuisha Lazaro. Mwinjili anataka kurudia tena ishara ambayo Yesu ameitoa katika kitendo hiki cha kumfufua Yesu kuwa ni Bwana wa maisha, Bwana wa uzima siyo uzima huu wa kibaolojia wa kurudishia uhai Lazaro, la hasha, bali mwuujiza huo tuuchukulie kuwa ni ishara au kichokoo tu cha kutuonesha au kutushirikisha uzima mwingine ambao Yesu amekuja kutuletea hapa ulimwenguni. Mfu anakuwa mzima anazaliwa upya na anabaki katika hali ya mfu ameviringishwa vitambaa. Yaani mfu ambaye Yesu anamwita toka kaburini (pangoni) anabaki bado na alama zote za mzikwa wa kaburini. Kisha Yesu anasema: “Mfungueni, mkamwache aende zake.” Usemi huu nao ni muhimu sana. Tamko hili ni fumbo, kwani Yesu hasemi, “twendeni naye pamoja anakoenda huko”.

Baada ya tamko hili la Yesu na kumfungua mfu na kumwacha aende zake, tungetegemea kuona vituko vingine husika vikiendelea kuorodheshwa. Yaani tungemtegemea Yesu anaendelea kutoa maagizo yafuatayo: “Mfungueni halafu akisha jiweka sawa, ataweza kuja kutusimulia mambo yalivyokuwa kuzimuni alikokuweko siku hizi nne. Kisha tutaenda kumnywea na kufanya sherehe. Ratiba nyingine itaendelea jinsi mambo yatakavyojitokeza.”

Pengine hata Lazaro mwenyewe angeenda kumkumbatia Yesu ikiwa kama ishara ya shukrani. Lakini kumbe Yesu anasema tu “mfungueni na mkamwache aende zake.” Lazaro anaondoka na kwenda zake kimyakimya bila ya kuwahamasisha, au kuwachangamsha waliokuwa wanahuzunika.

Ndiyo mwisho! Ndivyo anavyotutendea Mungu, anayetuumba, anatuacha mahuru tuendelee na maisha bila kutufunga. Hii ni ishara kubwa katika maisha yetu ya kidini, kutomfunga Mungu katika imani, bali kumwacha huru. Ishara hiyo pia ni mwito kwa ndugu wanaolia na kuhuzunika kwa kuondokewa na ndugu, rafiki na mpenzi wao, lakini utakuwa ni ubinafsi mkubwa sana kumshikilia na kumtaka marehemu aendelee kubaki nao.

Yabidi kumwacha “kumfungua na kumwacha aende kwa raha zake.” Ingependeza sana kutanguzana naye kwenda pamoja huko aendako. Kumbe haiwezekani! Sisi tubaki tu kumsindikiza kwa jicho la imani katika hatua mbalimbali za maisha yake. Tumwache aende kwa uhuru wake wote. Ama kweli mwisho wa maisha ni mwanzo wa maisha.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB



Kanisa linapania kushiriki kikamilifu katika kudumisha amani na majadiliano ya kidini huko Mashariki ya Kati!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni tarehe 7 Aprili 2014 amekutana na kuzungumza na Mfalme Abdullah wa Pili wa Yordan pamoja na ujumbe wake, ambao walipokelewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, aliyekuwa ameandamana na viongozi kadhaa kutoka Vatican.

Baba Mtakatifu na mgeni wake wamefanya mazungumzo yao kwenye Hostel ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican. Mazungumzo haya kadiri ya taarifa ya Padre Lombardi yamefanyika wakati viongozi hawa wawili wakiwa wanaendelea kupata chai ya jioni na kwamba, yamedumu kwa takribani dakika arobaini na tano.

Safari ya kikazi iliyofanywa na Mfalme Abdallah wa pili mjini Vatican ni sehemu ya maandalizi ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko huko katika Nchi Takatifu, ambako atapata fursa kwanza kabisa ya kutembelea na kuzungumza na wananchi wa Yordan na kwamba, wananchi wengi wa Yordan wanasubiri kwa hamu hija hii ya kichungaji, itakayomwezesha Baba Mtakatifu kujionea hali halisi ya wananchi wa Yordan.

Kwa upande wake, Baba Mtakatifu ameonesha utashi na nia ya kimaadili ya kutaka kushiriki kikamilifu katika mchakato unaopania kupata amani ya kudumu huko Mashariki ya kati pamoja na kudumisha majadiliano ya ya kidini, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amesalimiana na wajumbe waliokuwa kwenye msafara wa Mfalme Abdallah wa pili wa Yordan