Baba
Mtakatifu Francisko ameondoka mjini Roma asubuhi, tarehe 24 Mei 2014
tayari kwa hija ya kitume huko Yordani, Palestina na Israeli kama kilele
cha maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana,
akazungumza na kusali pamoja na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu, huu
ukawa ni mwanzo mpya wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene.
Baba
Mtakatifu katika Uwanja wa ndege wa Fiumicino, Roma amesindikizwa na
viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali ya Italia. Ametumia nafasi
hii kuwasalimia mmoja mmoja na kuwatakia kheri na baraka. Kama desturi,
Baba Mtakatifu alibeba mkoba wake mweusi tayari kuanza safari ya kitume
Nchi Takatifu.
Baba Mtakatifu amewaandikia wakuu wa Nchi ya
Italia, Ugiriki, Cyprus na Israeli ujumbe wa matashi mema wakati
alipokuwa anasafiri kuelekea mjini Amman, kituo cha kwanza cha hija yake
ya kitume! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Rais
Giorgio Napolitano wa Italia, anamwambia kwamba, anaelekea Nchi Takatifu
ili kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana na
Patriaki Anathegoras wa Yerusalem pamoja na kusali kwa ajili ya kuombea
haki, amani pamoja na kukoleza majadiliano ya kiekumene na kidini.
Anawatakia kheri na baraka wananchi wa Italia, anawaomba pia kumkumbuka
katika sala zao.
Naye Rais Giorgio Napolitano wa Italia
amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa ina
matumaini makubwa katika hija hii ya kitume huko Nchi Takatifu, mahali
ambapo kuna kinzani kubwa katika historia yake na ulimwengu kwa ujumla.
Ni matumaini ya Rais Napolitano kwamba, hija hii itakuwa ni cheche za
matumaini kwa wale wanaotaka kusimama kidete kuendeleza amani na
utulivu. Rais Napolitano anamtakia mafanikio mema katika hija hii ya
kitume.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Rais
Karolos Paoulias wa Ugiriki anamtakia mafanikio mema katika kukuza na
kudumisha misingi ya haki na amani, anawaombea baraka tele kutoka kwa
Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko akimwandikia Rais Nicos
Anastasides wa Ugriki anasema, anawatakia kheri na baraka tele wananchi
wa Ugiriki na kwamba, anawaombea furaha na amani kutoka kwa Mwenyezi
Mungu.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia pia ujumbe
Rais Shimon Peres wa Israel kwa kumtakia matashi mema na wananchi wote
wa Israeli na kwamba, ana matumaini ya kukutana naye Nchi Takatifu
wakati wa hija yake ya kichungaji. Anawatakia wote baraka tele!
Baba
Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 23 Mei 2014 asubuhi na mapema,
aliondoka kutoka mjini Vatican na kwenda kusali kwenye Kanisa kuu la
Bikira Maria mkuu lililoko mjini Vatican, kuomba ulinzi na tunza ya
Bikira Maria kabla ya kuanza hija yake ya kichungaji Nchi Takatifu
itakayomwezesha kutembelea: Yordan, Palestina na Israeli kama sehemu ya
maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana,
akazungumza na kusali na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu.
Baba
Mtakatifu Francisko alipokuwa anatangaza hija hii ya kitume aliwaambia
waamini waliokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican kwamba, hija hii itafikia kilele chake wakati viongozi
wawakilishi wa Makanisa watakaposali kwa pamoja kwenye Kaburi Takatifu,
mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe
wamoja!
Baba
Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 19 Mei 2014 amekutana na
kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico kwa kuwataka kujenga na
kudumisha utamaduni wa watu kukutana pamoja na kujenga amani. Ili
Kanisa liweze kuendelea kuwajengea watu imani na matumaini, halina budi
kushikamana na wahanga wa biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na
maskini!
Baba Mtakatifu anasema, hakuna sababu ya Kanisa kuogopa
au kutishwa na nguvu za giza, bali linapaswa kusimama kidete na kwa
ujasiri pamoja na watu wanaoendelea kuteseka, kwa kutetea haki zao
msingi pamoja na kushiriki katika mchakato wa kuwaletea maendeleo
endelevu yanayomlenga mtu mzima: kiroho na kimwili. Mambo haya
yanajikita katika mchakato wa Uinjilishaji pamoja na kutafuta mafao ya
wengi.
Baba
Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi
Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba
2014 hapa mjini Vatican, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Changamoto za
kichungaji kuhusu familia mintarafu Uinjilishaji" ameandika barua kwa
familia zote duniani ili kukazia dhamana ya Kanisa kuendelea kutangaza
Injili kwa kukabiliana kinaga ubaga na changamoto mpya zinazohusu
familia.
Baba Mtakatifu anasema, maandalizi haya yanawahusu Watu
wote wa Mungu kwa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu kwa kutoa
mawazo pamoja na kusindikiza mchakato mzima kwa njia ya sala, jambo
muhimu sana kutoka kwa familia zote. Sinodi hii ni maalum kwa ajili ya:
wito na utume wa Kanisa na Jamii; matatizo yanayowakabili wanandoa;
maisha ya kifamilia, elimu na malezi kwa watoto; dhamana na utume wa
familia katika maisha ya Kanisa.
Baba Mtakatifu anazialika
familia kusali na kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwaangazia Mababa
wa Sinodi katika kutekeleza wajibu wao huu nyeti. Sinodi hii maalum,
itafuatiwa tena na Sinodi ya kawaida ya Maaskofu itakayojadili kuhusu
tema ya familia mwaka 2015 sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Familia
Kimataifa itakayofanyika mwezi septemba, mjini Philadelphia, nchini
Marekani.
Baba Mtakatifu anawaalika wanafamilia pamoja na watu
wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kufanikisha matukio haya
makuu ndani ya Kanisa, ili liweze kung'amua na kupata mikakati
itakayosaidia familia ili kukabiliana na changamoto kadiri ya mwanga na
nguvu ya Kiinjili.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, ameitunga
barua hii wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Siku kuu ya kutolewa
Bwana Hekaluni. Ni tukio ambalo liliwakutanisha Mzee Simeoni na Anna
kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wakamtambua Yesu kuwa ni Masiha. Mzee
Simeoni akamshukuru Mungu kwa kuwa ameuona wokovu na Anna kwa upande
wake akasimulia matendo makuu ya Mungu licha ya uzee wake.
Inafurahisha
kuona kwamba, wazee wawili na vijana wawili wanakutanishwa na Yesu. Hii
inaonesha kwamba, Yesu ana uwezo wa kukutanisha na kuunganisha vizazi,
kwani Yeye ni chemchemi ya upendo inayovuka ubinafsi, upweke na
masikitiko. Baba Mtakatifu anasema, familia katika hija ya maisha yao
wanashirikishana na kumegeana mambo mengi mema: chakula na mapumziko;
kazi za nyumbani, starehe, sala, safari na hija ya maisha ya kiroho
pamoja na matendo ya huruma.
Pale panapokosekana upendo, hapo
kutakosekana furaha na kwamba, upendo wa kweli unabubujika kutoka kwa
Kristo kwa njia ya Neno lake ambalo ni mwanga katika mapito ya waamini;
anawapatia Mkate wa maisha ya uzima wa milele, unaowasaidia waamini
kupambana na changamoto za maisha ya kila siku.
Baba Mtakatifu
anahitimisha barua yake kwa familia kwa kuhimiza kwamba, mchango wao wa
sala ni muhimu sana katika Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu
Familia. Anawaomba pia kumwombea ili aweze kuwahudumia Watu wa Mungu
katika ukweli na upendo. Baba Mtakatifu anawaombea ulinzi na tunza
kutoka kwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, ili waweze kutembea huku
wakiwa wameshikamana katika upendo na huduma.
Kwa
mara ya kwanza katika historia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia,
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 19 Mei 2014 amefungua mkutano
wa sitini na sita kwa kuwataka kutambua kwamba, wao ni wachungaji wa
Jumuiya ya Kristo Mfufuka. Wao ni wachungaji wa Fumbo la Mwili wa Kristo
yaani Kanisa, wachungaji wanaoendeleza ujio wa Ufalme wa Mungu kati ya
watu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa familia, maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Baba Mtakatifu Francisko
katika hotuba yake ya ufunguzi amewataka Maaskofu Katoliki Italia
kushikamana na Kristo pamoja na Kanisa lake, ili aweze kuwaimarisha
katika imani, matumaini na mapendo, kwa kuendelea pia kuwa ni waaminifu
katika utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wao.
Kanisa
ni Jumuiya ya Kristo Mfufuka inayojikita katika imani ambayo
inarutubishwa kwa Neno na Sakramenti za Kanisa, changamoto na mwaliko wa
kuepukana na vishawishi vinavyoweza kuwasonga na hivyo kushindwa
kutekeleza wajibu wao kikamilifu: kwa kutokuwa na mikakati makini ya
kichungaji, kwa kujiamini sana na kutoona umuhimu wa kumtegemea Kristo
katika maisha na utume ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu anawaalika
Maaskofu kumtegemea Kristo na kumkaribisha ili aweze kutenda pamoja nao,
ili waweze kuwa kwelini watakatifu na mifano bora ya kuigwa.
Maaskofu
ni wachungaji wa Kanisa ambalo ni Fumbo la Mwili wa Kristo,
linalowashirikisha kwa namna ya pekee Fumbo la Pasaka na huduma
inayowawajibisha kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na
ukarimu, bila kumezwa na malimwengu wala kuwadharau wengine. Huu ndio
mfano bora uliooneshwa na Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II.
Mama
Kanisa anapojiandaa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI hapo
tarehe 29 Oktoba 2014 kuwa Mwenyeheri, Maaskofu wanakumbushwa maneno
yake aliyowataka Maaskofu Katoliki Italia kujisadaka kwa ajili ya ujenzi
wa umoja wa kitaifa, kwa kuondokana na udhaifu unaoweza kujitokeza kwa
kutokuwa na mawasiliano makini, kwani kinzani na utengano ndani ya
Kanisa ni kashfa kubwa na hakuna mtu anayeweza kuhalalisha kitendo hiki.
Baba
Mtakatifu anawakumbusha kwamba, umoja na mshikamano wao unapata
chimbuko lake katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; kwa
kujenda na kudumisha amani na utulivu hata katika nyakati ngumu.
Tasahufi ya Ekaristi takatifu inajenga mshikamano, majadiliano, udugu,
uhuru na uwezo wa mtu kuchangia kadiri ya Roho Mtakatifu
anavyowakirimia. Baraza la Maaskofu linapaswa kuwa ni kwa ajili ya
huduma ya umoja, mahusiano ya dhati, mahali pa kubadilishana na
kushirikishana mang'amuzi na changamoto katika shughuli za kichungaji.
Baba
Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwa karibu na Mapadre wao katika maisha
na utume wao; kwa kuwapatia majiundo makini ya awali na endelevu katika
maisha ya kiutu, kitamaduni, kiroho na kimahusiano. Mkutano mkuu wa
Baraza la Maaskofu utakaofanyika mwezi Novemba, 2014 utajikita katika
maisha ya Mapadre, changamoto ya kufanya maandalizi makini.
Maaskofu
wawasaidie watawa kutekeleza utume wao ndani ya Kanisa na kuishi kadiri
ya kweli za Kiinjili, ili waweze kuwa ni mashahidi wa Injili ya Furaha.
Maaskofu wajenge utamaduni wa kusikiliza watu wao, wawaimarishe katika
imani, wawasaidie waamini walei katika maisha na utume wao wa
kuyatakatifuza malimwengu. Wawapatie mikakati itakayowawezesha waamini
walei kutangaza Neno la Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao na
Katekesi. Utume wa Kanisa unajikita katika umoja na upatanisho kama
kielelezo cha unabii katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, matendo ya huruma ni muhimu sana katika
ujenzi wa Ufalme wa Mungu kati ya watu. Kanisa liguswe na matatizo
yanayowakabili watu katika hija ya maisha yao hapa duniani, lisaidie
kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Kanisa linatumwa
kutangaza ukweli kuhusu Kristo na huruma kwa waja wake, kwa kutambua
kwamba, upendo katika ukweli ni kikolezo cha maendeleo endelevu katika
familia ya binadamu, tunu zinazopaswa kumwilishwa katika matendo!
Maaskofu
wawe ni wachungaji wasiomezwa na malimwengu, watu wanaopenda na kuishi
ufukara, kwa kuonesha huruma na unyenyekevu katika maisha. Wawe ni watu
huru wanaweza kuwakaribia watu kwa upendo na kuwasindikiza wale
wanaotembea katika upweke na giza la uvuli wa maisha, ili hatimaye watu
hawa waweze kuonja tena utu, matumaini pamoja na kuwa na maisha mapya.
Hapa
Familia zinapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa
Kanisa, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu bora za
maisha ya kifamilia. Familia ni kiini cha Jamii na ushuhuda wa uzuri wa
maisha. Hapa ni mahali ambapo watu wanapaswa kufundishwa namna ya
kukumbatia Injili ya Uhai, kwa kuwasaidia wazazi katika mchakato wa
malezi ya watoto wao, kwa kuwaganga wale waliopoteza dira na mwelekeo wa
maisha.
Baba Mtakatifu Francisko anawaambia Maaskofu wa Italia
kwamba, waoneshe mshikamano wa upendo na watu wasiokuwa na fursa za
ajira au wale ambao wamepoteza ajira kutokana na sababu mbali mbali,
watu ambao kwa sasa maisha na utu wao uko mashakani. Wawafungulie
milango wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta faraja na kutaka kusalimisha
maisha yao kutoka kwenye vita, nyanyaso na dhuluma, kwani upendo ni
kielelezo kikuu cha ushuhuda wa ukarimu, kwani hii Injili itaenea sehemu
mbali mbali kwa kuonesha mvuto na mashiko!
Baba Mtakatifu
anasema kuna haja ya kuwa na sera mbadala katika mikakati ya maendeleo
ya kiuchumi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji
yake msingi, kwa kulinda na kuboresha mazingira sanjari na kuwajengea
watu matumaini wakati huu wanapopambana na athari za myumbo wa uchumi
kimataifa; mmong'onyoko wa kimaadili na utu wema pamoja na watu kupoteza
mwelekeo katika maisha ya kiroho. Hapa kuna haja ya kuwa na mikakati
makini kwa kuona ukweli wa mambo, ili kujenga na kudumisha, udugu na
mshikamano.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaomba Maaskofu
wa Italia kumsindikiza katika hija yake ya kitume huko Nchi Takatifu,
kama sehemu ya maadhimisho ya jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI
alipokutana, akazungumza pamoja na kusali na Patriaki Anathegoras wa
Yerusalemu. Anakwenda huko ili kuwaonjesha mshikamano wa Kanisa kwa
ajili ya watu wanaoishi katika eneo ambalo limebarikiwa na Yesu kwa kufa
na kufufuka kwake!
Mahakama
moja nchini Sudan imemkuta na hatia Meriam Yahya Ibrahim Ishaq,
mwanamke mwenye umri wa miaka 27 ya kukufuru na kuzini kwa kuwa ameolewa
na raia mmoja Mkristo kutoka Sudan ya Kusini na hivyo kuhukumiwa
kuchapwa viboko mia moja na kunyongwa hadi kufa!
Adhabu hii
imewashtua watetezi wa haki msingi za binadamu, kwa kuitaka Serikali ya
Sudan kuheshimu uhuru wa kuabudu kadiri ya Katiba ya nchi iliyotungwa
kunako Mwaka 2005.
Mahakama hiyo imetumia "Sharia" za dini ya
Kiislam zilizoingizwa nchini humo kunako mwaka 1983 zinazopiga rufuku
kwa mwamini wa dini ya Kiislam kuoa au kuolewa na Mkristo. Viongozi
mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa wameitaka Serikali ya Sudan
kuingilia kati ili kusitisha utekelezaji wa adhabu hii ambayo ni kinyume
cha haki msingi za binadamu.
Ninaendelea
tena kuwa nawe katika kipindi cha Liturujia ya Neno la Mungu, tukiwa
tayari Dominika ya V ya Pasaka. Ujumbe wa Neno la Mungu umezama katika
kuamini kina katika Bwana na kisha kutoa huduma katika jumuiya kama njia
ya kukamilisha unachoamini na hivi baadaye kukuwezesha kufika mbinguni.
Bwana anaenda huko kutayarisha makao ya kutosha kwa ajili yetu. 
Katika
somo la kwanza: (Mdo, 6:1-7), tunakutana na ongezeko la wanafunzi
katika jumuiya ya kwanza, na katika ongezeko hili, kunatokea malalamiko
ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu ya huduma pungufu
kwa wajane. Basi Mitume wakishauriana na kusali wanaona kuwa haipendezi
wao kuacha huduma ya Neno la Mungu na kuhudumu mezani.
Uamuzi
unaotolewa ni kuwaambia wanajumuiya ya wa jumuiya ya kwanza wakisema
chagueni kati yenu watu 7 wenye karama ya wema, wenye kujawa na roho na
hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili na sisi tutadumu katika kuomba na
kuhudumia lile Neno”. Baada ya ushauri huo wakachaguliwa watu 7 kati
yao alikuwako Stefano aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, wakasali na
wakawawekea mikono na tayari wakawa mashemasi katika Kanisa.
Mpendwa
msikilizaji kwa nini kunatokea malumbano na mikingamo katika Jumuiya ya
kwanza? Kwa nini mwandishi anaweka jambo hili mbele yetu? Jambo la
kukumbuka katika simulizi hili ni kwamba hapo mwanzo Jumuiya ilikuwa na
Waebrania tu na polepole kadiri ya kazi ya kimisionari ilivyokuwa
ikisonga mbele, wakajiunga hata Wayahudi wa Kiyunani ambao walikuwa
wakitumia lugha ya Kigriki. Wayahudi wa Kiyunani walikuwa na
mchanganyiko wa tamaduni kwa maana walikuwa wakiishi nje ya Palestina.
Waebrania
ambao hawakuwa na mchanganyiko, wao waliendelea kutumia lugha ya
Kiebrania kama kawaida! Basi jumuiya ilivyozidi kuongezeka vilianza
kujitokeza vijidharau vya hapa na pale dhidi ya Wayahudi wa Kiyunani na
hasa wajane na yatima wao kuhusiana na ugawanyaji wa mali za jumuiya!
Kumbuka kuwa, tangu mwanzo walikuwa wameweka mali pamoja. Mambo haya
yalianza kujitokeza baada ya miaka 3 hivi. Kilele cha dharau ni
malumbano na madai ya kutaka Mitume washiriki katika kuhudumu mezani,
ili kuweka haki katika maisha ya jumuiya kila siku.
Basi, shauri
hilo likiwafikia Mitume, na Mitume wataamua kwa hekima ya kimungu
kuwaweka wakfu watu saba kwa ajili ya huduma hiyo. Mpendwa msikilizaji
hiki ndicho chanzo cha ushemasi katika Kanisa Moja,Takatifu, Katoliki na
la Mitume.
Mpendwa mwana wa Mungu, tunajifunza nini katika hili?
Jambo la kwanza tunajifunza kuwa tangu mwanzo Kanisa limekuwa
likikumbwa na matatizo na hivi kuonesha sura mbili za Kanisa: Kanisa la
wema na wadhambi. Kumbe hata hivi leo inapotokea purukushani fulani
katika Kanisa tusishangae, ni hali ya mwanadamu tangu mwanzo. Wajibu na
jambo la kufanya ni kusali na kuomba kwa ajili ya kupatikana suluhu kwa
njia ya amani.
Jambo la pili Mitume wametupa mfano bora yaani
wakati Kanisa linakua nao wanaona ni vema kushirikisha madaraka
waliyokabidhiwa na Mungu kwa wengine, kwa ajili ya faida ya Taifa la
Mungu. Wanapoamua jambo hili wanashirikisha jumuiya yote; huu ndio umoja
wa Kanisa, ndicho Bwana anachotaka katika kuwa mchungaji mwema. Mitume
wanabaki na lengo moja yaani utume wa Neno la Mungu.
Katika somo
la Pili: (1Mt Petro 2:4-9) Mt Petro awaalika watu wote kumwendea Yesu
Kristu jiwe hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule.
Jiwe hili ndo lile jiwe kuu la pembeni ambalo Mungu ndiye mjenzi wake.
Mungu anapojenga nyumba yake akisha kuweka jiwe kuu anasonga mbele
akitumia mawe mengine, yaani wanadamu ambao Mt Petro anasema “Katika
yeye nasi tunaitwa kuwa nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu tena
tunaalikwa kutolea daima dhabihu njema zinazokubaliwa na Mungu. Ndiyo
kusema Mungu, anajenga nyumba yake kwa kutumia mawe yaliyohai, yaliyojaa
upendo! Hawa ni wabatizwa wanaomkubali Kristu na hivi kujenga nyumba ya
kiroho yaani Kanisa la Mungu.
Mpendwa msikilizaji yafaa
kujiuliza ujenzi huu ulianza lini? Kwa hakika ujenzi umeanza wakati wa
ufufuko wa Bwana, maana waashi walilikataa jiwe hai na Mungu akalifanya
kwa njia ya ufufuko kuwa jiwe kuu la pembeni. Jambo hili lilishaaguliwa
na manabii wa kale “tazama naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni,
teule lenye heshima”. Ni kwa jinsi hiyo basi uaguzi huu umekamilika
katika ufufuko wa Bwana. Mpendwa msikilizaji kwa kuwa mawe hai ya nyumba
ya Mungu, Bwana anatuita daima kuachana na giza na tunaalikwa
kuzitangaza fadhili zake daima kwa mataifa ili waweze kuingia katika
nuru yake ya ajabu.
Katika Injili: (Yn 14:1-12) Mwinjili anaweka
mbele yetu mafundisho ya Bwana aliyoyatoa katika chakula cha jioni siku
iliyotangulia kuteswa kwake. Ndiyo kusema anawaachia wosia Mitume na
vizazi vyote. Mmoja anaweza kuuliza hivi kwa nini Mama Kanisa ameweka
somo hili baada ya Pasaka? Ni kwa sababu moja ya kawaida kwamba wosia
husomwa baada ya mwenye kuandika wosia anapokuwa ameondoka duniani!
Katika
mafundisho ya Bwana tunaona jinsi Bwana mwenyewe akiwatayarisha
wanafunzi wake kwa ajili ya Kupaa kwake. Anasema wasifadhaike bali wawe
na imani katika Mungu na yeye mwenyewe, na kisha wakumbuke anaenda
kuwatayarishia makao tele ili atakapokuwepo nao wawepo. Jambo la kwenda
kutayarisha makao linashangaza kidogo kwa sababu kuna mawazo kwamba
tayari pamekwishaandaliwa! Ni kweli, lakini ataka kutuambia suala la
kusafiri na ugumu wake linahitaji maandalizi. Kwa sababu hiyo basi,
Bwana ataongeza neno akisema huko niendako mwaijua njia!
Mpendwa
mwanatafakari, kwa kuwa njia na makao tunayopaswa kuyafikia ni kazi
nyeti, mara moja Tomaso atasema hatujui njia! Bwana mkarimu na Mchungaji
mwema anamjibu “mimi ndimi njia na ukweli na uzima; mtu haji kwa Baba
ila kwa njia ya mimi”. Hili maana yake nini? Jambo hili lamaanisha
lazima kufuata njia ya mapendo, njia ya mateso hadi msalabani na kisha
hapo kutakuwa na ufufuko.
Kumbe, matayarisho ya makao yanaanza
na msalaba wake na kisha ufufuko furaha ya milele na Baba mbinguni. Ili
tuweze kupita katika njia ya Bwana tunahitaji msaada wake na ndiyo maana
alisema, nitaenda na kisha nitarudi kuwachukua pamoja nami! Katika
kutangaza makao, Bwana ansema nyumbani mwa Baba yake, kuna makao mengi.
Bwana ataka kusema nini katika hili? Ataka kusema tukikubali kumfuasa
yeye basi kuna wajibu na shughuli za kutosha kama tuonavyo leo katika
Kanisa. Nyajibu hizi tunaalikwa kuzifanya kwa mapendo tukishirikiana
katika raha na taabu mpaka kufikia mwisho wa nyakati na hapa ndipo kuna
kumwona Baba.
Wakati Bwana anatangaza kuwa yeye ni njia ya kwenda
kwa Baba, mara moja Filipo anauliza utuoneshe Baba yatutosha! Ombi hili
linamwendea Bwana na hata sisi wakristu wa leo. Kwa upande wake Bwana
anajibu akisema aliyeniona mimi amemwona Baba, kwa kuwa mimi ni ndani ya
Baba na Baba yu ndani yangu. Kwa upande wetu tunapaswa kusema daima
aliyemwona Kristu amemwona Baba. Baada ya fundisho hilo lililo gumu
kwao, Bwana atawaalika kusadiki hilo na kama hawasadiki basi wasadikini
kwa sababu ya kazi zenyewe!
Mpendwa, kwa kumtambua na kumjua
Baba haina haja ya kujenga falsafa ya pekee bali ni kuitikia kile
ambacho Bwana anasema. Ndiyo kusema inatosha tu kumtazama Kristu yaani
Mwana, ambaye ni sura kamilifu ya Mungu. Inatosha kumtazama Mwana,
yamaanisha na yatulazimu kusoma Neno la Mungu na kutafakari, kusikia
kile anachofundisha kwa njia ya Kanisa, kupambanua namna yake ya kupenda
yaani mpende adui yako, namna yake ya kukosoa kunapokuwa na shida au
dhambi na mwishoni kuyashika yale yote mema aliyoliachia Kanisa la
Kitume.
Mpendwa msikilizaji, katika kusadiki yaani, kuamini
kuliko kina Bwana anafungamanisha zawadi, yaani anasema kama mmoja
akisadiki ataweza kufanya mambo makubwa katika maisha yake. Hili ni
kweli nami nasadiki.
Nakutakieni furaha tele katika Dominika hii
ya Pasaka na Mungu azidi kuwa nawe, ukitekeleza mapenzi yake katika
maisha yako. Tukutane tena Dominika ijayo. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari
hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.
Ndugu
msikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, tulianza maandalizi
ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu
kwa kukufanualia maeneo muhimu katika historia na maisha ya Yesu.
Tumekwishatembelea Bethlehemu mahali alipozaliwa Yesu, tukavuka ng'ambo
ya pili ya Mto Yordan, mahali alipobatizwa na leo tuko chumba cha juu,
mahali alipoweka Ekaristi Takatifu na kuwataka wanafunzi wake wawe ni
watu wa huduma! 
Karibu
Wainjili wote wanatupatia maelezo ya karamu ya mwisho. Katika chumba
kilicho juu. Wainjili wanasema kwamba karamu hiyo ilikuwa ya Agano Jipya
na la milele.
Katika mazingira hayohayo ya kula Yesu akawaosha
miguu wafuasi wake. Kila mwenjili anajitahidi kutoa fundisho la pekee
kadiri anavyoona yeye. Hapa sisi tufuate maelezo ya mwinjili Luka. Sote
tunafahamu kilichotokea siku ile ya karamu ya mwisho. Maneno ambayo Luka
anayoyatumia na ambayo yabidi kuyafanyia tafakuri ni yake tunayoyasikia
katika kila misa: “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” Ni mwinjili Luka
peke yake anayesema maneno hayo.
Lengo la Yesu lilikuwa ni
kuwaalika wafuasi wake wote kumkumbuka Yeye, yaani daima kurudia kufanya
kitendo hicho. Lakini zaidi pia aliwataka wamege mkate na kula ikiwa
kama alama ya msingi katika imani yetu. Tendo la kumega mkate ni
ufupisho wa maisha yake yote toka kuzaliwa hadi kufa kwake. “Mimi
nimejifanya chakula ili kuyalisha maisha.” Ni kama vile angekuwa
Bethlehemu inayotembea (mobile bakery).
Luka anataka kutuambia
kuwa mnapokuwa katika karamu hii, au mnapokula chakula hiki, mnafanya
uchaguzi kama wangu wa kujitoa na kujitolea. Huo ni mwaliko wa kuwa kama
Kristu, wa kuwa mkate na kujigawa kwa wengine. Kwa hiyo haitaeleweka
kabisa kumwona mkristu baada ya kuadhimisha ekaristi, anashindwa
kusaidia wengine.
Hali halisi nyingine inayoonekana humo
chumbani, wakati wa sherehe hiyo kuliibuka mabishano mazito hasahasa
tungeweza kuyaita mahojiano makali kati ya mitume. Kisa walikuwa
wanabishana juu ya ukuu, juu ya kuwa na heshima na cheo kati yao “ni
nani anayehesabiwa kuwa mkuubwa.” Yesu akawaambia: “Wakuu wa mataifa
huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu
ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye
kuongoza kama yule atumikaye. Mimi niko kati yenu kama atumikaye.” Haya
tena ni maneno yanayoletwa na Luka peke yake wakati huu wa mlo. Ni
maneno kwa ajili ya kila mtu hasahasa yule anayejiita mkristu. Hayo
ndiyo mambo yanayoharibu jumuia za kiristu siku za leo. Kazi ya mtu
aliyeshiba ni kutafuta cheo.
Mahojiano hayo ya mitume hayakuishia
kwao tu. Mabishano hayo yameletwa hapa kuonesha kuwa yanaweza kumpata
kila mmoja katika maisha yake. Hasa kuhusu kujihoji wewe mwenyewe kuhusu
kuchagua mambo. Hali kadhalika Yesu Kristu katika maisha yake hapa
duniani alikabiliwa na changamoto hii ya kujihoji nafsini mwake.
Mahojiano
hayo ya Yesu tutayaona baada ya karamu ya mwisho akiwa kwenye mlima wa
Mizeituni. Tunaambiwa kuwa alipatwa na uchungu sana ambao katika Injili
ya Kiswahili wanafasiri kuwa ni dhiki. “Yesu akatoka akaenda mpaka mlima
wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; ...akajitenga na mitume
wake… huko akasali... kwa vile alikuwa katika dhiki... hari yake ikawa
kama matone ya damu yakidondoka nchi.”
Alikuwa katika katika
dhidi au tuseme alikuwa na hali mbaya sana. Yaani ni kama hali ile
anayokuwa nayo mtu kabla ya kufa. Neno hili uchungu pia limetokea katika
injili ya Luka peke yake, kwa kiingereza ni "Agony". Maana halisi ya
neno hilo agoni lamaanisha mapambano, mashindano au mahojiano makali.
Hasa mashindano kama yale ya wanariadha. Yesu aliingia katika mashindano
kama hayo.
Toka mwanzo wa maisha yake, Yesu ilimbidi aingie
katika mapambano na mashindano na nguvu za shetani. Mapambano hayo
hayakwisha katika vishawishi, yaani pale shetani alipomjia Yesu jangwani
mara tu baada ya kubatizwa. La hasha, baada ya vishawishi vile
tunasikia kuwa shetani alimwacha Yesu kwa muda. “Basi alipomaliza kila
jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.” (Lk. 4:13). Shetani
anakuja tena akijua kwamba hapa sasa ni lala salama!
Hapa kuna
mapambano makali ya roho yanayomdai Yesu kuwa mwaminifu na inabidi
kuyashinda. Yesu anashinda! Kuonesha kwamba hayo yalikuwa ni mashindano
makali, Yesu anatoka jasho, hilo kama vile jasho linalomtoka mwanariadha
wakati wa mashindano. Kwa hiyo "agony" siyo uchungu bali ni mapambano,
kuvutana, ukinzani, ugomvi ndani ya mtu. Mapigano yaliyoko ndani ya mtu.
Katika mapambano hayo Yesu anajiandaa kwa kujitenga na kusali.
“Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti
akaomba.” Anajiweka katika mahusiano na Mungu ili kuweza kuiona mipango
ya Mungu. Anajiweka katika mahusiano na Mungu, ili kujua Mungu anao
mpango gani kwa ajili yake. Yesu alisali sana na akawahimiza mitume wake
kukesha na kusali. “Alipofika mahali pake aliwaambia: ‘ombeni kwamba
msiingie majaribuni. Ondokeni, mkaombe msije mkaingia majaribuni.” Sala
inamsaidia Yesu. Kisha wanafika malaika kumliwaza. Hiyo ni alama ya kuwa
na mawazo ya ndani ya Mungu. Endapo alifikiria kutoroka maisha,
kutoroka mateso sasa anaimarika, na kuhiari kuurekebisha ulimwengu. Kwa
hiyo ili kushinda mapambano ya ndani ya mtu, yabidi kusali sana.
Kuunganisha mipango yako na mipango ya Mwenyewe Mungu.
Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican inakutakia hija njema na Baba Mtakatifu
Francisko huko Nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014
kwa kuongozwa na kauli mbiu " Wote wawe wamoja".
Imetaraishwa na
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
Jina
hili Bethlehemu linatokana na maneno mawili ya Kiebrania, Bet ni nyumba
na Lehem (lexem) ni mkate, kwa hiyo Beth-Lehem au bet-lexem maana yake
nyumba ya mkate. 
Kwa
lugha ya kigiriki cha zamani walitamka Bethleem. Ziko sehemu nyingi
zenye nyumba ya mkate mathalani Beth-lehem-ephratah, Bethlehemjudah,
lakini Bethlehemu iliyokuwa kusini karibu na Yerusalemu ndiyo iliyokuwa
inaitwa Bethlehemu katika mji wa Daudi. Hapo ndipo alipozaliwa Yesu. Ni
mji ambao toka zamani wameishi wakristu wengi, lakini sasa wanaishi pia
watu wa dini mchanganyiko. Sehemu hii wanafurika wahaji na watalii wengi
sana hususani wakati wa Kipindi cha Noeli.
Kisa cha kujulikana
Betlehemu kilianza na safari ya Yosefu na Maria aliyekuwa na baraka
tumboni. Walienda huko kwa ajili ya senza. Katika pilikapilika za
kutafuta mahali pa kulala mama akajifungua mtoto wake hapo Betlehemu mji
wa Daudi (Lk. 2:4). Baada ya kuzaliwa, mtoto huyo akaviringishwa nguo
za mtoto mchanga na kulazwa kwenye hori la kulishilia wanyama.
Hii
ndiyo alama ambayo malaika waliwapa maelezo wachungaji na kuwaagiza
waende huko kumwona mtoto. Malaika wakawaambia wachungaji: “Leo katika
mji wa Daudi amezaliwa kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristu Bwana. Na
hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto,
amelala katika hoi ya kulia ng’ombe.”
Kumbe yawezekana malaika
walikuwa wa kwanza kufika hapo Betlehemu na kushuhudia mambo yalivyo
kabla ya kwenda kuwahabarisha wachungaji. Tunaambiwa pia kwamba mara tu
baada ya malaika kuondoka, wachungaji nao wakaambizana wenyewe, Jamani
tusiilazie damu taarifa hii ya malaika: “Twendeni mpaka Betlehemu,
tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.” (Lk. 2:15). Baada ya
kumwona mtoto wakaanza nao wakaanza kutawanya habari: “Walipomwona
(mtoto Yesu) wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Halafu wote
waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.” (Lk 2:27).
Malaika walipoona utukufu umetua Bethlehemu, hawakuuacha utulie
tu pale pangoni, bali wakaondoka kwenda kuutangaza kwa wachungaji. Kwa
hiyo utukufu haukuhusu pango ila unawahusu wachungaji wanaowakilisha
wanyonge wote. Wachungaji ndiyo wanaodhihirisha utukufu wa Mungu. Mungu
anajidhihirisha na kutukuzwa pale tu ambapo wanyonge, fukara
wanapofurahi. Huo ni utukufu wa Mungu.
Wachungaji wanafurahi kwa
sababu kutokana na hali halisi ya unyonge wao, walijisikia kama watu
waliolaaniwa, kwa hiyo hawakutegemea kabisa kupata mawasiliano na Mungu.
Kumbe amezaliwa mchungaji mwenzao, anayejua unyonge wao. Hawakujiamini
wenyewe, na mara moja wakaanza kushauriana wenyewe na kuchukua maamuzi
ya kwenda kushuhudia na baadaye kutoa ushuhuda.
“Twendeni mpaka
Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.” Wanaenda
haraka, kushuhudia utukufu wa Mungu, ambao ni kutaka watu wapate furaha
haraka. Kwetu sisi tungetegemea kusikia mambo ya ajabu zaidi au hata
kusikia muujiza. Hakuna maelekezo zaidi, ni kama vile amezaliwa mtoto wa
kawaida. Maisha ya kawaida yanaendelea. Yesu kuwa Mungu hakutegemei
muujiza wa pekee, bali yeye mwenyewe jinsi alivyo. Yeye ni kama sisi,
Mungu amekuwa mwenzetu. Anayemtegemea Mungu wa kufanya miujiza, ujue
mungu aina hiyo ni mungu wa kipagani.
Wachungaji wanaenda
Betlehemu na wanamwona mtoto aliyeviringishwa nguo. Hiyo ndiyo picha
mpya ya Mungu anayejidhihirisha kwa binadamu. Watoto waliviringishwa
nguo ili kuwakinga na baridi lakini pia inayo maana ya kidini. Mtoto ni
safi, hivi huwezi kumshika tu kwa mikono, lakini kuna maana pia muhimu
ya kiroho, hasa mwinjili anaposisitiza jinsi mtoto alivyoviringishwa
nguo, hoja kubwa ni kusudi mtoto huyo aweze kuguswa, kushikwashikwa na
kubebwa na watu wote.
Aidha imeandikwa mara tatu kuwa aliwekwa
katika hori la kulishia chakula wanyama (ng’ombe). Kwa hiyo msisitizo
huo unahusu chakula. Mtoto aliviringishwa nguo, kama vile mkate
unavyoviringishwa karatasi au majani na kuwekwa kwenye nyumba ya mkate
(Bethlehemu). Kwamba Yesu anadhihirishwa hapa kama mkate yaani chakula.
Malaika wanawaelekeza wachungaji kwenda kwenye nyumba ya mkate
(bethlehemu) huko watauona mkate umeviringishwa.
“Na hii ndiyo
ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala
katika hoi ya kulia ng’ombe.”Yesu aliishi na kuhitimisha historia ya
maisha yake hapa duniani akijionesha mwenyewe daima kuwa ni mkate utokao
mbinguni. Maisha yake yote akayatolea hadi chembe ya mwisho ya mkate.
“Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha
Bwana.”
Wachungaji wanapofika pangoni wakamwona Maria, Yosefu na
mtoto mchanga amelala horini. Hawaoni cha pekee zaidi. Kisha wakatoa
taarifa juu ya kile walichoambiwa juu ya huyo mtoto. “Walipomwona (mtoto
Yesu) wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Halafu wote
waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.” Nadhani
watu wote walishangazwa na taarifa hizo kwani ni Mungu aina gani
anayeweza kuwatokea watu wanyonge kama wachungaji. Kama ndivyo basi hayo
ni maajabu.
Tunaambiwa jambo jingine lililotokea pale Bethlehemu
ni kuwa Maria akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.
Neno kufikiri, siyo tafsiri sahihi, kwa kigiriki “sinmbalus” inamanisha
kuweka mambo pamoja na kutafakari, hasa kule ambako mmoja unapoona mambo
lakini unashindwa kuyaelewa. Maria anatulia, anaangalia, anaunganisha
mambo anaweka pamoja mambo yanayomtukia. Atakuja kufahamu atakapokuwa
amesimama chini ya Msalaba.
Wachungaji wanaondoka wakimshukuru na
kumsifu Mungu – wameyaona maisha mapya. Wamemwona Mungu aliyejifanya
binadamu na kulingana na watu. Wamemwona Mungu anayejiacha
kushikwashikwa na watu wenye mikono michafu, watu wanaonuka, yaani
wanyonge, maskini, wazee, wenye dhambi, walalahoi. Watu hawa wanyonge
wameona na wanafurahi, wanamshukuru na kumsifu Mungu, kisha
wanamshuhudia.
Kumbe, watu hawa wanyonge tu ndiyo wanaoweza
kutambua na kushabikia sera hii kubwa ya Mungu kujifanya mtu. Ni watu
kama hawa ndiyo wanaoweza kuwa na furaha, na kusifu na kumshukuru Mungu.
Kwa wataalamu, wakuu, matajiri sera hii haiingii akili na mioyoni mwao.
Ni muhimu hata kwetu kwamba badala ya kujihoji na kufikri nini
tufanye nini katika maisha, baada ya kumwona Kristu tubaki tu kufurahi.
Tumeona tendo kuu la upendo alilotufanyia Mungu. Huo ndiyo mwanzo wa
uchumba kati ya Mungu na binadamu, kati ya Yesu na Kanisa lake. Sisi
tunafunganishwa na Yesu katika upendo. Ndiyo mwanzo wa maisha ya upendo
na ya furaha. Wanaopendana daima wanashika simu mkononi wakisubiri
”message au kupib”, au kuitwa na mpendwa wao ili kuongeana.
Sisi
tukitaka kugundua utukufu na upendo huo wa Mungu tuanza Bethlehemu, na
kuendelea mbele hadi kwenye majitoleo kamili ya Yesu kule Kalvari. Kwa
hiyo ndugu zangu “twendeni na Papa mpaka Betlehemu” tukirudi toka huko
tuwapagawaze watu kwa tutakayoyaona. Hebu sasa tutoke Bethlehemu
kuongozane na Papa hadi mto Yordani.
Imeandaliwa na
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
Katika
dini nyingi iko desturi nzuri ya kiroho ya kufanya hija pahala
patakatifu au sehemu za kihistoria za dini hiyo. Hija hiyo mara nyingi
hufanyika kama moja ya kuadhimisha tukio fulani muhimu linalomhusu mtu
binafsi ili kujichumia neema anayohitaji mhiji au alhaji. 
Papa
pia hufanya hija sehemu mbalimbali kama vile Lourdes, Fatima, Loreto,
Namugongo, Nchi Takatifu, nakadhalika. Hija ya Papa haiwi kwa ajili yake
binafsi tu, bali hasa ni kuchuma neema kwa ajili ya kanisa zima, pia
inakuwa kwa ajili ya kuimarisha mahusiano ya kuletesha haki, amani na
upendo kati ya nchi na nchi.
Mwaka huu kuna jubilei za dhahabu
kadhaa za kikanisa zitokanazo na Mtaguso wa pili wa Vatican. Zaidi pia
ni mwaka wa 50 tangu Papa Paulo VI alipohiji nchi ya ahadi na kuzungumza
na Patriaki Anathagora wa Yerusalemu. Papa Fransis atahiji nchi ya
ahadi ikiwa ni kuadhimisha jubilei ya dhahabu ya hija hiyo ya Papa Paulo
VI. Katika hija hiyo, Papa atakutana na viongozi muhimu wa serikali na
dini, atakutana pia na waumini wenzetu walioko huko.
Papa
atazuru sehemu chache muhimu. Mosi, ataenda Bethlehemu kuzuru na kusali
pahala alipozaliwa Yesu. Ataenda kuzuru na kusali kando ya mto Yordani
alikobatizwa Yesu. Mwisho ataenda kuangalia chumba ambacho Yesu alikula
Karamu ya Mwisho na mitume wake. Chumba hicho ni mandhali ya mwisho
aliyokuwa Yesu kabla ya kuteswa na kufa kwake.
Kwa hiyo, Wakristu
wote na watu wote wenye mapenzi mema tunaalikwa mosi, kuiombea hija hii
ya Papa, kusudi asafiri salama, aende akatuombee na kufanikisha
makusudio aliyojipangia kwa faida yake, na kwa manufaa ya kanisa zima na
ulimwengu kijumla, na hatimaye arudi salama, kusudi Mungu atukuzwe
katika yote.
Pili tunaalikwa sisi sote kutanguzana na Papa kwenda
katika hija hiyo, usikose kuwepo katika msafara huo wa Baba Mtakatifu.
Kutokana na msongamano wa watu na hasa kupanda gharama ya maisha, siyo
wote watafanikiwa kwenda hiyo hija. Tunaalikwa kukata tiketi ya kiroho
ambayo gharama yake ni bure sanasana inategemea uhuru wako mwenyewe, na
mkatishaji tiketi ni Roho Mtakatifu mwenyewe ambaye hata Yeye mwenyewe
ataenda kwenye hija hiyo ya awali tangu atoke huko alipokufa Yesu
Msalabani. “Akainama kichwa akaitoa Roho yake”.
Kwa watakaoenda
huko kwa tiketi ya Roho Mtakatifu, mnaalikwa kusoma ramani hii au
mwongozo ufuatao, utakaowasaidia kujua sehemu mbalimbali mtakazotembelea
na kuzihiji pindi mnaongozana na Papa. Hizo ni sehemu muhimu ambazo
kulifanyika mambo makuu na mazito yahusuyo ukombozi wetu. Katika
mwongozo huu tutajaribu kuzieleza kwa kifupi sana sehemu hizo
kijiografia na kiteolojia. Tutaona pia matukio yaliyotokea sehemu hizo,
yahusuhuyo Yesu au mitume wake na sisi tunaweza kupata fundisho gani
toka sehemu hiyo.
Hebu twendeni kwanza Betlehemu alikozaliwa
Yesu tuhimizane kwenda huko kwa maneno ya Wachungaji waliokuwa
wanahimizana kwenda huko baada ya kupata taarifa toka kwa malaika:
“Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha
Bwana.” (Lk 2:15).
Imeandaliwa na
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
Kuna
msemo ulioshamiri sana kwa Waswahili, hasa ikiwa mtu anayo matumaini ya
kupata kitu katika biashara na anakikosa anaambiwa: “Imekula kwako”.
Usemi huu ungeweza pia kutumika kwa mitume baada ya kifo na kuzikwa kwa
Yesu. Mitume na wafuasi waliweka matumaini yao yote kwa Yesu, lakini
sasa baada ya kufa kwake na kupita siku mbili tatu, wanakata tamaa na
kujisikia “imekula kwao.”
Wengi wao waliingiwa na woga na
kujifungia kwenye vyumbani, ili mradi tu kwamba walikuwa wameishiana na
mradi wa kumfuata Yesu. Wengine baada ya kwisha tu sikukuu ya Pasaka ya
kiyahudi siku iliyofuata kila mmoja akaanza kuchukua njia zake. Wafuasi
wawili walitanguzana mmoja hatajwi jina na mwingine anaitwa Kleopa
wakachukua zao kurudi kijijini Emmaus. Wamepoteza muda mrefu wa
kutumaini, wa kujitoa, myaka mitatu ya ushindi mkuu, miaka ya imani, ya
kusubiri, ya uzuri, miaka utamu ya mwanga. Lakini kifo kile cha Yesu
ndicho kilichochafua kila kitu. Ama kweli imekula kwao!
Wafuasi
hawa wawili walijisikia kuwa kama miali ya moto inayokaribia kuzimika.
Hebu tuone jinsi Bwana mfufuka anavyoihuisha tena: Wafuasi hao
wanatembea kwenye barabara kuu wanayopita watu wote, wakiwa katika
huzuni kubwa, katika upweke, wakijadiliana. Yesu hawaiti toka mbali na
kuwasimamisha, bali anawasogelea kama mtu mwenye haraka lakini anayetaka
kutanguzana nao. Wao wanageuka na kugundua kwamba kuna mtu anawafuata.
Hapa Yesu amejionesha kama msafiri wa kawaida tu ila mwenye haraka. Yeye
mfufuka angeweza kusafiri kwa mwendo wa kasi sana, kumbe anatanguzana
nao, anapima hatua zao zilingane na mwendo wao wa kuchoka, mwendo wa
waliojeruhiwa.
Wanaelekea Emmaus, yaani anatanguzana nao katika
kuchanganyikiwa kwao na katika matatizo na uchungu wao. Ndivyo Yesu
anavyokutana na watu mbalimbali hapa duniani na kutanguzana nao katika
safari yao ya maisha. Kila mmoja anamkuta akiwa na hali fulani ya pekee.
Tunasikia kwamba Magdalena alimkuta akiwa analia, kwa wale kumi
na mmoja kule kwenye ziwa jumapili ijayo, anawakuta wana uchungu na
wamechanganyikiwa baada ya kukesha usiku mzima wakivua bila kupata kitu,
wakati Tomaso jumapili iliyopita alimkuta katika hali ya kutoamini.
Wafuasi hawa anawakuta katika lindi la uchungu na la upweke. Wako wawili
tu, lakini sasa wanakuwa wasafiri watatu.
Katika uchungu wao huo
wanajadiliana na kuhubiriana juu ya suala zito na muhimu la maisha.
Wanaongeana juu ya jambo linalowakereketa kabisa ndani ya mioyo yao.
Wafuasi hawa wanazungumza juu ya Upendo. Yaonekana amewakimbilia, na
kuwakuta ili kuwapa moyo, kuwahimiza na kuwangaza. Hawakatishi
mazungumzo yao: Anatafuta mwanya wa kujiingiza katika mazungumzo yao kwa
utulivu, kwa utamu kwa kuuliza swali jepesi na rahisi tu.
Tena
anauliza kama vile mtu mjinga asiyefahamu kilichotokea. “Ni maneno gani
haya mnayosemezana hivi mnapotembea?” Kwa swali hili Yesu anaonesha
kuujali sana uchungu wao.
Swali hilo linamfanya Kleopa na
mwenzake waanze kumshangaa. Yaani msafiri mwenzao aliyetokea upande
wanakotokea wao kuwa hajavisikia vituko vilivyotokea huko Yerusalemu.
Habari
hizo zimevuma mji mzima na watu wote wanavizungumzia sana.
“Inawezekanaje, wewe unayetoka sasa hivi huko mjini usisikie habari hii
ya kusikitisha?”
Angekuwa mtu mwingine yeyote angeweza
kuwasimamisha na kuwaambia: “Kaeni chini hapa niwaeleze kinaganaga cha
mambo yalivyotokea.” Kumbe Yesu ameanza kwa kuwaamshia hamu ya kujieleza
zaidi hadi wanamgeuzia kibao: “Hivi wewe peke yako ni mgeni asiyejua…”.
Huwezi kujua ni jinsi gani Yesu alilipokea swali hilo la wafuasi. Swali
hilo la wafuasi linaonesha waziwazi vionjo vilivyokuwa vimejaa ndani ya
mioyo yao. Hadi hapo ilimtosha kabisa Yesu kujisikia kuaminiwa na watu
hawa. Kleopa aliyekuwa katika hali mbaya ya kukata tamaa, na aliyejaa
jazba, amefanikiwa kujimwaga mbele ya mgeni huyu.
Yesu anawaacha
waendelee kujimwaga. Bila kujitambua wakaendelea kujieleza hadi kufikia
kuzungumza mambo ya kiroho waliposema: “Mambo ya Yesu wa Nazareti,
aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za
Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu
walivyomtia katika hukumu yak ufa, wakamshulibisha… Tena wanawake kadha
wa kadha wa kwetu walitushitusha waliokwenda kaburini asubuhi na mapema,
wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika
waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda
kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye
hawakumwona.” (Lk 24:19-20, 22-24).
Hapa unaona kama vile
wamechanganyikiwa. Yaani, wanaonekana kwa upande mmoja kama vile
wanasadiki lakini halafu kwa upande mwingine hawasadiki. Watu hawa
wanateseka sana kisaikolojia lakini walikuwa bado na imani mioyoni
mwao. Kwa hiyo Yesu anawaambia: “Enyi wenye mioyo mizito ya kuamini yote
waliyoyasema manabii!” (Lk.24:25).
Yaani, hawa walikuwa watu wa
kutibiwa, siyo wa kuwalaani, watu wa kuwasahihisha na siyo kuwaachilia
tu, watu wa kuwapoza siyo kuwagombeza! Baada ya kuwatulia kidogo, Yesu
anaanza kuwapa dawa ya tiba. Anaanza kuwaelezea historia ya mambo
yaliyokuwa kadiri ya Maandiko matakatifu hadi wanakaribia kijiji cha
Emmaus.
Baadaa ya kumaliza kuwaeleza, Yesu angeweza kusema:
“Sasa jamani baada ya kuwaeleza haya yote, tafadhali rudini Yerusalemu
na mkawahabarishe wenzenu haya niliyowaambia ili msikose tena imani.
Yesu hafanyi hivi badala yake anajifanya kama vile anapitiliza na
kuendelea na safari zake. Hahitaji chochote, wala haulizi chochote, na
wala hategemei chochote toka kwao. Ndiyo maana hawa wasafiri wawili
wanaamua kumshawishi: “Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana
unakwisha.” (Lk 24:29). “Mgeni afike mwenyeji apone”. Je, sisi tumwambie
nani “Kaa pamoja nasi”?
Tunaweza kumwambia mtu aliyetutendea
jema fulani “kaa nasi”, au mgeni yule ambaye hatutii hasara, mtu
asiyekuwa mzigo. Wageni namna hiyo wako wachache sana na pengine hawako
kabisa. Kumbe Yesu aliye Mungu hahitaji chochote. Yesu aliyesukumwa na
upendo mtupu hataki kumtuliza tu mtu. Hatukani mtu, hasemi maneno yasiyo
na maana, huyu mgeni alitoa maneno ya kuhuisha. Aligusa hata mioyo yao,
aliwatia moyo, hadi wanamkaribisha kwao.
“Wakakikaribia kile
kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea
mbele.” (Lk 24: 28). Katika nafasi nyingine Yesu aliwapita wanafunzi
wake: Mathalani kwenye mto Yordani, au mbele ya Yohane Mbatizaji kule
Genesareti, au usiku ule wa dhoruba. Anapita pembeni ya Kanani bila
kusimama. Anampita kipofu bila kumponya. Yesu anafanya hivi ili mmoja
uweze kumtafuta, au uweze kumwita. Yesu anapenda kuitwa. Wakati mwingine
anaweka hata mazingira ya kuja kwake na matendo yake ili aweze kuitwa
na binadamu. Anavuvia, anadokeza, anashawishi, anahimiza lakini
anasubiri. Wanafunzi wanamwomba atulie, abaki akae nao.
Wao
wanahoja zao kinyume na ukweli ule wa ndani kabisa. Hoja wanayotoa ya
kumshawishi abaki ni kwamba: “kumekuchwa, na mchana unakwisha.” Badala
ya kumwambia kwamba tunapenda kuwa na wewe. Tumeshakupenda, licha ya
kutukosoa na kutusahihisha, na hasa kutokana na hilo tunataka ubaki
nasi. Yesu alilazimisha kwa wema. Alikuwa yeye wa kwanza kuwajongelea.
Sasa wamekuwa wao kutaka kumshikilia asiondoke. Anaingia na katika tendo
la kumega mkate, wanamtambua. Mioyo yao inafunguka: “Ni Yeye” wakasema.
Lakini kabla hawajafanikia kuwasiliana naye, akawa ameshatoweka machoni
pao.
Kumbe, ili aweze kutambulika, haoneshi vyeti vyake vya
utambuilisho, na vyeti vya shule. Anajitambualisha kwa kumega mkate.
Tendo ambalo wanafunzi wake wanamtambua mara moja. Yawezekana walimzoea
akifanya hivyo kila walipokuwa wanakula pamoja. Aidha tendo hilo
alilirudia karibuni tu kwenye karamu ya mwisho alipowaambia: “Fanyeni
hivi kwa kunikumbuka mimi.” (Lk. 22:19).
Hapo hapo wale
wanafunzi wawili wakaanza safari ya kurudi Yerusalemu, wale ambao
walipokuwa wanakuja Emaus walikuwa wamechoka, na kuchanganyikiwa. Sasa
wanarudi kwa mbio wakiwa na kiherehere cha kwenda kuwasimulia wenzao
kwamba Yesu amefufuka, anaishi, na kwamba wao wameonana naye. Waliochoka
kutembea sasa wanakimbia.
Kumbe umoja aina hii na Kristu unaleta nguvu mpya na ari mpya. Tunaalikwa kutanguzana na Kristu katika maisha yetu.
P. Alcuin Nyirenda
Mpendwa
mwana wa Mungu ninakuleteeni tena furaha ya Pasaka kwa njia ya tafakari
ya Neno la Mungu tukiwa tayari Dominika ya tatu ya Pasaka. Ujumbe wa
Neno la Mungu Dominika hii ni ule usemao, "Wakamtambua katika kuumega
Mkate". Katika somo la kwanza toka Kitabu cha Matendo ya Mitume tunapata
kukutana na sehemu ya mahubiri ya Mtakatifu Petro. 
Katika
mahubiri haya Mtakatifu Petro akiwa amejawa na Roho wa Mungu na nguvu
ya Pasaka anatangaza kuwa Kristu aliyedhihirishwa kwetu na Mungu na
kuteswa na kisha kutundikwa msalabani, amefufuliwa na Mungu. Jambo hili
ni la kweli na hakika, kwa maana sisi tu mashahidi. Mtakatifu Petro
anashuhudia hilo akisema tulikula, na tukanywa pamoja naye na si hilo tu
bali tumeshuhudia na kufuata mafundisho yake hadi anapofufuka.
Mpendwa
msikilizaji, Mt Petro analenga kufundisha na kusimika imani katika
Bwana mfufuka na tokea pale kuweza kusonga mbele katika utume kadiri
Bwana alivyoagiza.
Mpendwa mwana wa Mungu, Mtakatifu Petro
anasonga mbele akijaribu kuweka wazi mpango wa Mungu uliojificha katika
kifo cha Bwana. Anakazia na anasema ni kweli kifo chake kilikuwa ni
sehemu ya mpango wa Mungu. Katika hoja hii anajaribu kujibu maswali ya
wale walioona kifo cha Kristu kama kikwazo na hasa wanapofikiri na
kutambua kuwa yeye alikuwa Masiha! Anasema kile kinachoonekana kwetu
kama makwazo na madhulumu kwa Mungu ni ishara ya ushindi! Kwa njia ya
kifo kuna maisha mapya, yaani maisha ya ufufuko.
Katika somo II
toka barua ya Mt Petro, (1Pet. 1:17-21) tunakutana na mwendelezo wa
mafundisho juu ya ubatizo. Anawaambia wabatizwa wapya kwamba sasa wanao
uwezo na nguvu za kumwita Mungu “Baba” kwa sababu wamepokea maisha mapya
toka yeye. Ni zawadi kubwa na nono lakini pia inayo sehemu ya wajibu
mkubwa nao ni kuwa mpya na daima kukaa katika hali ya utu upya!
Mtakatifu Petro anasonga mbele akisema kwa kupata zawadi ya ubatizo na
yote yaambatanayo na zawadi hiyo, mfano kumwita Mungu “Abba” kunatupasa
kutambua kuwa kuna mmoja ambaye amelipia fidia.
Ndiyo kusema si
kwa fedha wala dhahabu bali kwa DAMU YA MWANA WA MUNGU!, Damu ya Kristu
mpakwa mafuta wa Bwana! Damu isiyo na doa la dhambi. Kumbe tumekombolewa
kwa Damu ya thamani kuu mno! Yule kondoo ambaye Waisraeli walikuwa
wakimchinja wakati wa sherehe za Pasaka ilikuwa ni kiashilio cha Kristu
kondoo wa AJ ambaye anajitoa kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu.
Katika
somo III toka Mwinjili Luk 24:13-35, tunapata simulizi la wanafunzi 2
wa Emmaus. Mmoja wa wanafunzi hawa anaitwa Kleopa na mwingine jina lake
halijulikani. Habari njema imewekwa katika mtindo wa katekesi, Ni Kristu
mfufuka anafundisha watu wake na ndio sisi wenyewe na mafundisho ni juu
ya ufufuko wake. Mwinjili Luka anamtaja mwanafunzi mmojawapo kuwa
Kleopa ambaye kadiri ya tafiti za kibiblia alikuwa ni kaka yake na
Yosefu, baba yake mlishi wa Yesu Kristu yaani Bwana.
Mwingine
hatajwi jina, Luka akitaka kuacha nafasi kwa ajili yetu sisi ambao
tunaalikwa kufuata nyayo zake tukimwelekea Bwana Mfufuka. Hawa wanafunzi
wanakimbia toka Yerusalemu kwa maana matarajio yao hayakutimia.
Walitarajia Masiha mshindi, mwenye nguvu, na mwenye kuishi maisha marefu
na badala yake wanamwona akishindwa na kufa akiwa na miaka 33!.
Mpendwa
msikilizaji, ndugu hawa wakiwa katika majadiliano ghafla Bwana
ataingilia majadiliano yao na kuwauliza mnajadiliana nini? Hawa
wanafunzi wawili wanasimama na kukasilika wakishangaa mtu huyu ni nani
asiyejua kilichotokea Yerusalemu? Atawauliza tena kwani kumetokea nini?
Basi
wanafunzi hawa watahadithia habari za Yesu Mnazareti jinsi alivyokuwa
na uwezo mkuu lakini wakuu wa walimtia nguvuni na kumsulubisha!
Wanafunzi hawa wanasema kwa kweli hatuoni tumaini tena na ndiyo maana
tunakimbia! Mara kadhaa hata sisi tunalo tumaini fulani katika maisha,
lakini inapojitokeza hatufaulu basi ni kuanza kulalamika na kukata tamaa
kama ndugu hawa na hata wengine kuliacha Kanisa.
Angalia hali
ya kisiasa kunakuwa na tumaini fulani kwa watu fulani na
wanaponyamazishwa basi matumaini yetu huanguka pia! Hata hivyo mpendwa
unayenisikiliza, mkristu anayeamini katika ufufuko hawezi kukatishwa
tamaa na mikasa inayojitokeza katika maisha bali anasonga mbele kama
Kristu mpaka Kalvari ambapo ndipo kuna ufufuko!
Mpendwa katika
Bwana, wanafunzi wa Emmaus walikuwa na ujuzi juu ya Bwana lakini ujuzi
wao uliishia katika kifo cha Bwana tu, hawakuweza kuendelea mbele!
Hawakutambua kuwa Bwana alikuwa amefufuka na hiki ndicho kisa cha kukata
tamaa, maana kama ni kifo tu, kwa hakika kinatisha na kukatisha tamaa.
Ndiyo kusema nasi wakati fulani tunapoanza safari ya kumtafuta Bwana
tunaishia kwenye kifo pasipo kwenda mpaka ufufuko na hapa ndo kuna taabu
na mikato ya tamaa isiyohesabika! Tunaalikwa kwenda mbele mpaka
ufufuko.
Hatupaswi kuishia katika kumwona Bwana kama mwana
mapinduzi bali kama mwokozi wetu. Tunaalikwa kwenda mpaka ufufuko ambao
huwezi kuufafanua kwa mahesabu bali kwa imani na hapa ndipo kuna hekima
ya Kimungu. Wanafunzi wa Emmaus wana huzuni kwanza kuacha jumuiya yao
ambamo wangeweza kupata majibu ya wasiwasi wao.
Shida nyingine
hawakutaka kufanya utafiti juu Ya kile kilichosemwa na akina mama
waliokwenda makaburini siku ya ufufuko. Pengine waliona kwa kuwa
kimahesabu haiwezekani kukifafanua na hivi wanazama katika dharau na
hili ni ukosefu wa imani! Leo hii katika Jumuiya yetu ya Kanisa kuna
watu ambao kukitokea shida kidogo ni kuanza kukimbia wakifikiria
wataweza kupata majibu na badala yake ni kukumbana na mkato wa tamaa na
udhaifu wa kiroho kukua na kuongezeka. Fundisho katika hili ni kwamba
yafaa siku zote kukaa na jumuiya na kutafuta suluhisho la matatizo yetu
na ya Kanisa ndani ya Jumuiya yetu.
Mpendwa katika Bwana pamoja
na kwamba ndugu hawa wawili wamekata tamaa na wanaujuzi nusunusu juu ya
Bwana, Bwana hawaachi anaambatana nao na kuwasaidia polepole ili waweze
kuelewa nini kilitokea na kwa nini ilikuwa vile. Hata kwetu hivi leo
Bwana anatupa company tunapokuwa katika hali ya kukimbia matatizo na
kukata tamaa. Ndiyo kusema nasi tuwape company kaka na dada zetu wakiwa
katika taabu.
Mpendwa msikilizaji, ndugu hawa pamoja na kwamba
Bwana amewasaidia katika shida yao ya kutoelewa vema maandiko matakatifu
bado wanamwona kama msafiri mwenzao, mwenye shida kama wao. Mpendwa
yatupasa kukazia lengo letu katika maisha, maana yake tukilipoteza hata
mmoja anapojaribu kutueleza akili haipokei haraka.
Katika shida
kama hii Bwana atafanyaje? Kwa hakika anaanza kuwafafanulia maandiko
matakatifu kuanzia AK mpaka AJ linalomhusu yeye mwenyewe na hasa juu ya
mateso hadi ufufuko wake. Ndiyo kusema Kwa njia ya Neno la Mungu mtu
huweza kutambua mafumbo ya Mungu. Hata hivyo pamoja na hilo hawakuweza
kuelewa kitu na Bwana atawakemea kwa mioyo migumu hiyo. Kwa hakika hata
hivi leo shida ya kutoelewa na hasa kutoguswa na Neno la Mungu ipo,
yafaa kuomba sana nguvu ya Roho Mtakatifu kwa ajili hiyo.
Mpendwa
Bwana akiendelea na katekesi yake inafika jioni na anataka kuendelea
mbele wakati wanafunzi wamefika. Basi wanamkaribisha nyumbani walipokuwa
wanaenda na kisha ataketi chakulani pamoja nao na KUUMEGA MKATE na
kuwapatia. Kwa tendo la kuumega mkate macho yalifunguka na wakamtambua
kuwa ni BWANA MFUFUKA na mara atatoweka! Swali linawajia kwa nini
hatukumtambua alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu? Basi mara
moja ndugu hawa walirudi Yerusalemu kwa furaha bila wasiwasi tena na
kutangaza habari njema wakisema tumemwona Bwana mfufuka na kweli
amefufuka.
Mpendwa katika Bwana simulizi la wanafunzi wa Emmaus
kadiri ya Mt. Yustini ni chimbuko la mpango wa Misa Takatifu. Waamini
kuingia mapema katika ibada, hii ni sawa na wanafunzi wa Emmaus kuwa
njiani tokea Yerusalemu, kuingia kwa Padre kwa maandamano ni ishara ya
kuingia kwa Kristu masiha katika majadiliano ya wanafunzi hawa. Mahubiri
ni ishara ya ufafanuzi wa Neno la Mungu uliofanywa na Bwana mfufuka na
Litrujia ya Ekaristi Takatifu yaturudisha katika ishara ya Kristu
kuumega mkate na kuwapa wanafunzi wa Emmaus.
Mwishoni mwa Misa
Padre huondoka kwa maandamano toka kwenye Misa kabla ya waamini wengine,
hii yaturudisha katika lile tendo la Bwana kutoweka mara baada ya
kumega mkate na kuwapatia. Wanafunzi wa Emmaus walipoelewa haya,
walirudi Yerusalemu wa furaha kutangaza furaha ya ufufuko. Mpendwa, wewe
je baada ya kuumega mkate waondoka katika Misa kwa furaha kwa ajili ya
kutangaza kwa wengine au warudi nyumbani kwa huzuni? Tafakari hili!
Nakutakieni
furaha tele katika kipindi chote cha Pasaka na Mungu azidi kuwa nawe,
nawe ukitekeleza mapenzi yake katika Jumuiya ukienda kutangaza habari ya
ufufuko wa Bwana kwa furaha kuu. Tukutane tena Dominika ijayo. Tumsifu
Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya
C.PP.S.
JANA ilikuwa Siku
kuu ya Wafanyakazi Duniani, maarufu kama Mei Mosi ni fursa inayotolewa
na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka kwa wafanyakazi kufanya tathimini ya
kina kuhusu kazi walizotenda, ufanisi na tija katika shughuli za
uzalishaji na utoaji wa huduma pamoja na kujiwekea malengo kwa siku za
usoni kwa kukazia umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau mbali mbali katika
kazi.
Katika mazingira ya utandawazi usiojali mateso na
mahangaiko ya watu, kuna haja ya kuanzisha na kuimarisha mshikamano wa
kidugu unaojengeka katika vyama vya ushirika miongoni mwa wafanyakazi,
kwa kutambua na kuendelea kudumisha sheria, kanuni na usalama kazini.
Mishahara mizuri, mazingira safi na bora ya kazi pamoja na vitendea kazi
vizuri ni mambo ambayo yanaweza kuchangia katika maboresho na ufanisi
kazini sanjari na ukuzaji wa pato la wafanyakazi.
Ubadhirifu wa
mali ya umma, ufisadi, wizi na hujuma kazini ni mambo ambayo daima
yamekwamisha ufanisi kazini na matokeo yake ni watu kuendelea kukomaa
katika ubinafsi na utandawazi wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya
jirani. Siku kuu ya Wafanyakazi Duniani, iwe ni fursa ya kukuza na
kuimarisha sheria za kazi, utawala bora na usalama kazini.
Siku
kuu ya Wafanyakazi imewekwa chini ya ulinzi wa Mtakatifu Yosefu
Mfanyakazi. Siku kuu hii ndani ya Kanisa ilianzishwa kunako mwak 1955 na
Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili. Lengo ni kutambua heshima ya
kufanya kazi kama sehemu ya utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Huu
ni mwendelezo wa kuutiisha ulimwengu, ili uweze kuwa ni mahali pazuri
zaidi pa kuishi. Watu wanapaswa kutambua kwamba, kazi ni sehemu muhimu
sana katika maisha ya mwanadamu kwani ni sehemu ya ubinadamu na matokeo
ya kazi.
Utu na heshima ya mwanadamu ndicho kipimo sahihi cha
heshima ya kazi. Kazi ni wajibu na utambulisho mwa wanadamu na kwamba,
nguvu kazi ina kipaumbele cha kiasili zaidi ya mtaji, kumbe, kuna haja
ya kuwa na uhusiano unaokamilishana kati ya kazi na mtaji, lakini utu na
heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza.
Baada
ya Baba Mtakatifu Francisko kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na
Yohane Paulo II kuwa watakatifu, Jumapili tarehe 27 Aprili 2014 katika
Ibada iliyohudhuriwa na maelfu ya watu waliokuwa wamefurika kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na viunga
vyake, watakatifu hawa wapya watakumbukwa kila mwaka mwezi Oktoba kadiri
ya Kalenda ya Liturujia ya Kanisa.
Kadiri ya Kalenda ya
Liturujia ya Kanisa kwa ajili ya kumbu kumbu ya Watakatifu, Yohane XXIII
atakumbukwa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba. Hii ni siku maalum
ambayo, kwa takribani miaka hamsini iliyopita, Yohane XXIII alikuwa
anafungua rasmi maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, tukio
ambalo limeleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa
katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Hili ni tukio la
kishujaa lililomstahilisha Papa Yohane XXIII kuitwa Mtakatifu.
Mtakatifu
Yohane Paulo II atakumbukwa kila mwaka ifikapo tarehe 22 Oktoba. Hii ni
siku ambayo Papa Yohane Paulo II alipoanza utume wake kama Khalifa wa
Mtakatifu Petro, akaendeleza maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa
Vatican pamoja na kukazia umuhimu wa Mama Kanisa kujikita katika
mchakato wa Umissionari na Uinjilishaji Mpya. Mwezi Oktoba ni mwezi wa
shughuli na mikakati ya kimissionari ndani ya Kanisa.
Tangu sasa
waamini na watu wenye mapenzi mema wanaweza kuwaenzi watakatifu hawa
wapya kwa maadhimisho ya: Ibada, Liturujia pamoja na kuwaweka kuwa
walinzi na wasimamizi wa shughuli mbali mbali katika maisha na utume wa
Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II atakuwa ni
msimamizi wa Siku za Vijana Duniani.
Vijana
wanaalikwa kumwangalia kwa namna ya pekee kabisa yule kijana tajiri
anayesimuliwa kwenye Maandiko Matakatifu aliyemwendea Yesu akiomba
ushauri ili aweze kuurithi uzima wa milele. Mitume wengi walikuwa ni
vijana na walifurahia sana walipokutana na kuzungumza na Yesu, kiasi
hata cha kuwabadilishia mwelekeo wa maisha, kwani waliweza kusikiliza
ufafanuzi wa Neno la Mungu kwa kina na mapana!
Baba Mtakatifu
Francisko katika ujumbe wake wa video kwenye maadhimisho ya Siku ya
Vijana Kikanda nchini Argentina, iliyoadhimishwa, Jumamosi tarehe 26
Aprili 2014 nchini Argentina, katika mkesha wa kuwatangaza Wenyeheri
Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, anawauliza vijana,
jinsi walivyojisikia kwa mara ya kwanza walipokutana na Yesu katika hija
ya maisha yao ya kiroho, Anawaalika kuwaangalia Mitume waliokutana na
Yesu kwa mara ya kwanza katika maisha yao.
Yesu alionesha upendo
wa pekee kwa yule kijana tajiri aliyejitahidi katika maisha yake kushika
Amri za Mungu, lakini akisoka ndani mwake ufukara wa maisha ya kiroho,
ndiyo maana anapoambiwa kwenda kuuza vyote alivyonavyo na kuwapatia
maskini, kisha amfuate Yesu, anashikwa na huzuni kubwa katika moyo wake.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, Maandiko Mataktifu yamesheheni mifano ya
vijana wa kina aina. Anawakumbusha yule kijana aliyeomba urithi kutoka
kwa Baba mwenye huruma, kisha akatokomea mjini kwenda kuponda mali na
baadaye akakiona cha mtema kuni kwa kukumbana na uso kwa uso na baa la
njaa! Hapa akajifunza kutubu na kuongoka, ili kukimbilia tena huruma ya
Mungu. Daima Baba yake alikuwa anamsubiri kwa hamu kubwa, kuona kijana
wake akirudi tena nyumbani. Siku ile aliporejea nyumbani, akamkumbatia
na kumwonjesha tena huruma na upendo usiokuwa na kifani.
Baba
Mtakatifu amewakumbusha vijana wa Argentina kuhusu yule kijana wa Naini
aliyekuwa amefariki dunia baadaye akafufuliwa na Yesu, kwa kumwonea yule
mama mjane huruma? Baba Mtakatifu anawauliza vijana wao wanajisikia
kuwa sehemu gani kati ya vijana wanaosimuliwa kwenye Injili? Je,
wanaonesha ari na shauku ya kuwashirikisha wengine ushuhuda wa kukutana
na Yesu? Au wamekata tamaa na kujikunyata? Au pengine tayari wamekwisha
kupoteza maisha ya kiroho ndani mwao?
Baba Mtakatifu Francisko
anawahamasisha vijana kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa
lake, kwa kutolea ushuhuda wa imani katika matendo, ili kujenga na
kuimarisha amani na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa
lake sanjari na kukumbatia Injili ya maisha pamoja na kuguswa na
mahangaiko ya wengine kama alivyofanya Bikira Maria kwenye arusi ya Kana
na mwishoni akasimama chini ya Msalaba wa Kristo.
Baba Mtakatifu
Francisko anawataka wasichana kuiga mfano wa Bikira Maria na wanawake
watakatifu wanaosimuliwa katika Injili kwa kutolea ushuhuda wa imani yao
kwa Kristo na Kanisa lake, wakimwachia Yesu nafasi ya kuwaongoza, ili
waweze kukua na kukomaa, tayari kuwahudimia Watu wa Mungu katika medani
mbali mbali za maisha.
Baba Mtakatifu amewatakia kheri na baraka
vijana hao katika maadhimisho ya Siku ya Vijana wa Argentina Kikanda,
ili wapate nafasi ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao, bila
kuwa na woga wala makunyanzi, bali wangalie Yesu na Bikira Maria, ili
waweze kusonga mbele, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa
watu wake.
Katika
dominika hii ya pili ya Pasaka, Injili inatuletea aina mbili za
mazingira yaliyo tofauti:Mazingira ya kwanza, Yesu anawatokea wafuasi
jioni ya siku ileile ya Pasaka, wakiwa chumbani pindi mtume mmoja
aitwaye Thomas hakuwepo. Mazingira ya pili, ni siku nane baadaye Yesu
anawatokea tena wafuasi chumbani sasa akiwepo hata Thomas. Mazingira ya
kutokea-tokea kwa Yesu baada ya ufufuko wake ni tofauti hasa ukikumbuka
alivyomtokea mara ya kwanza Maria Magdalena asubuhi ileile ya Pasaka.
Mazingira
aliyomtokea nayo yalikuwa ni ya nje kwenye bustani karibu na kaburi.
Lakini kwa mitume ilikuwa ni jioni tena chumbani milango ikiwa imefungwa
kutokana na woga wa wanafunzi. Mwinjili anataka kutuonesha kwamba Yesu
anafika katika ulimwengu kwa namna ambayo si ya kiyakinifu, ni yeye
lakini siyo yuleyule. Kitu cha muhimu zaidi kukiepa hapa ni matumizi ya
neno hili “kutokea”, kwa sababu neno hili halijatumika kabisa na
mwinjili. Fasuli inasema, Yesu alikuja na kusimama katikati. “Ikawa
jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwa wanafunzi, milango
imefungwa kwa hofu ya Wayahudi: akaja Yesu akasimama katikati,
akawaambia, “Amani iwe kwenu.” (Yoh. 20:19).
Siku ya Pasaka na
siku nane baadaye Bwana anakuja na kukaa katika jumuia yake
iliyokusanyika pamoja, na kama ilivyokuwa kwa wafuasi wale wa mwanzo
siku ya Pasaka kadhalika waumini siku ya Pasaka. Waumini hao hawana budi
kufungua sana macho yao, lakini siyo macho ya kiyakinifu, yanayoangalia
kwa udadisi na kuanisha mambo, bali kwa macho safi, macho ya imani
yanayoweza kuona mambo yasiyoweza kuonekana kwa macho ya kawaida.
Ndivyo
inavyotufundisha Injili ya leo jinsi ya kufungua macho ya imani na
kuangalia Yesu mfufuka anayefika na kukaa kati ya jumuia iliyokusanyika
pamoja. Wafuasi wanashangaa kwa kutokewa na Bwana kwani walikuwa na woga
sana. Wamekusanyika pamoja siyo kutokana na upendo waliokuwa nao kati
yao, la hasha, bali kutokana na woga, kwa vile wanaye adui mmoja
wanayemwogopa yaani wayahudi.
Angalia watu wengine wanaotembea
nje, wanawaacha tu hawa wafuasi wajifungie humo chumbani, wao hawana
wasiwasi wowote kwani ni kesi binafsi ya mitume walioingiwa na wasiwasi
kutokana na yaliyotokea. Hawa wanao woga kwa vile hawajamwona Bwana
mfufuka na kuhuishwa na roho ya mfufuka, hivi wanao woga. Woga huo
unawapata pia wakristu wowote katika jumuia kama endapo wanakuwa hawana
mang’amuzi ya Kristu mfufuka. Hali hiyohiyo inaweza kumkumba kila
mkristu mkereketwa na Kristu kama anakosa mang’amuzi ya Kristu mfufuka
katikati ya ndugu zake.
Woga huo wa Mkristu unatokana na mambo
mawili: Mosi, kuogopa kifo. Mkristu aliyemwona Kristu anayeingia katika
utukufu wa Baba hawezi kuwa na woga wowote ule wa kifo. Anaweza kuwa na
woga wa homa, ugonjwa, mateso, lakini siyo wa kifo. Mtu huyo atasubiri
kama “mlinzi akeshavyo akisubiri kuchomoza kwa jua la asubuhi”.
Kuingia
kwake makaoni kwa Baba yake ambako ni lengo la wote, hakuwezi kumpatia
woga wa kifo. Hata kama woga huo unabaki kutokana na kuachana na wapenzi
wake na vitu mbalimbali ambavyo Mungu ametupatia. Kwa hiyo hapa unauona
woga wa wanafunzi, ambao walikuwa bado hawajamwona Kristu mfufuka.
Woga
wa pili, unakuwa dhidi ya wengine ambao hawakuyapokea mapendekezo haya
ya Yesu hadi wakataka kumfifisha kabisa. Wenye woga aina hiyo hawawezi
kuwa wanafunzi wa kweli, kwani Yesu anawatuma wafuasi wake kama vile
kondoo kati ya mbwa mwitu. Kama unao woga kwa mbwa mwitu, basi ni bora
kutoroka na kwenda mbali kujificha.
Kadhalika woga ni ni kitu
kibaya kupita kila kitu kingine katika imani, kwa sababu unawafanya
wafuasi wa dini kuwa wenye msimamo mkali, hawaambiliki, hawataki
majadiliano, ni wagomvi, ni wachokozi, wanapiga makelele, wanapenda zogo
katika kuitangaza imani yao.
Kwa sababu kama imani yao na
wanachokisadiki kingekuwa cha ukweli na wanakiamini kwa dhati, basi
wasingekipigia makelele, badala yake wangekitangaza kwa furaha na kwa
utulivu. Pengine ingekuwa pia njia ya kujisaidia wao wenyewe ya kuuona
mwanga wa Pasaka. Kwa hiyo yatubidi tujiangalie sana, kwani woga
unatuingiza katika hatari ya kujifungia katika ukweli wetu usio na
msingi wa kuchochewa tu na mapokeo wa mambo yale tuliyozoea kuyatenda,
tunakuwa viziwi mbele ya hali halisi na hivi kujikuta unajihami mbele ya
kosoo ya imani yako, na unakuwa mwoga wa mambo mapya.
Katika
kipindi fulani cha historia ya Wakristu, Kanisa lilikuwa na hofu kubwa
sana wakati Biblia ilipokuwa inamilikiwa na Waprotestanti. Kulikuwa pia
woga wa demokrasia, na ule woga wa kukutana na utamaduni au mila
nyingine ngeni. Woga aina hiyo ni sawa na ule wa mitume wa kujifungia
ndani ya chumba. Yaani unakuwa na woga na mambo ya nje.
Huku
kujitenga na kujifungia ndani ya chumba katika nyumba moja, kuna maana
pia ya kiteolojia: Yohane anataka kuonesha kwamba mbele ya ulimwengu,
wanafunzi wanajisikia katika mazingira mageni, wanayo thamani ambayo si
sawa na zile za ulimwengu. Yesu anasema, ninyi mpo katika ulimwengu
lakini si wa ulimwengu huu. Ndiyo maana wanakuwa na woga.
Aidha,
endapo mmoja anajitangazia kwamba amemwona Kristu mfufuka, anatangaza
imani yake, hivi anaogopa kueleweka kuwa ni kichaa, yaani ni mtu
anayeishi nje ya ulimwengu, kwa sababu watu wamefungwa na mtindo wa
maisha ya ulimwengu huu hawaoni namna nyingine ya maisha. Kwa mfano
Mtakatifu Paulo anapozungumza juu ya ufufuko, watu wanamcheka na
kumwambia waziwazi kwamba “juu ya suala hilo tutakusikiliza tena wakati
mwingine”.
Ni ngumu sana kushuhudia imani yako hadharani. Hata
mapadre, usiku wa Pasaka, hatuwi hata na uso wa furaha wa kuona mwanga
wa ufufuko. Kwamba Yesu yuko na alifika kusimama mbele ya wafuasi. Yaani
mwanzo mpya wa kudumu wa uwepo wa Yesu. Amefufuka na kuonesha mikono
yake na kuwa katikati yao. Anaonesha mikono iliyofanya kazi na ubavu
wake, hiyo ndiyo kadi yake ya utambulisho. Mikono iliyotenda mema na
kupigiliwa misumari na moyo wake uliochomwa mkuki ilipotokea damu
kuonesha maisha na maji kuonesha Roho mtakatifu, maisha yaliyomwagwa
duniani maisha ya Roho yaliyotolewa ulimwengu. Hii ndiyo ID ya Yesu.
Mazingira
ya pili, aliyotokea Yesu ni ya siku nane baada ya ufufuko. Tomasi
hakuwepo pale alipotokea Yesu mara ya kwanza. Huyu Tomasi anaitwa Didimo
maana yake Pacha, “Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomas, aitwaye
Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. .. Basi, baada ya siku nane
wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomas pamoja. Akaja Yesu na
milango imefungwa akasimama katikati , akasema, “Amani iwe kwenu.”(Yoh.
20: 24, 26). Mwinjili anasisitiza sana jina hili Pacha (Didimo).
Yaonekana kuwa huyu ndiye pacha wa kila mmoja wetu. Kwa sababu hata sisi
tutapita safari hiyohiyo ya jinsi ya kumfuata Kristu mfufuka.
Katika
Injili, Thomasi anajitokeza mara tatu: Mara ya kwanza ni pale Yesu
anapotaka kwenda Yudea, alikokufa Larazo, Thomas anasema twende tukafe
sote huko: “Basi Tomas, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe,
“Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.” (Yoh. 11:16). Kwa hiyo ni
kweli Tomasi anayo mang’amuzi ya kifo tu, bali mang’amuzi ya ufufuko
hana kwa sababu hajayashuhudia. Amebakiwa na wazo lake lilelile,
“Twendeni tukafe naye”. Nafasi nyingine ni kwenye karamu ya mwisho, pale
Yesu anapowaambia wanafunzi kwamba kule ninakoenda ninyi mnafahamu
njia. Tomasi anasema, sisi hatujui unakoenda, tutawezaje kuijua njia?
“Nami niendako mwaijua njia.” Tomas akamwambia, “Bwana, sisi hatujui
uendako, nasi twaijuaje njia?” (Yoh. 14:4-5) Huyu ndiye ndugu yetu
Tomas, pacha wetu (Kurwa), kwa sababu anataka kujua. Kuna wakristu wengi
wanaopata taabu ya kuelewa mambo yote katika imani. Anaye pacha wa
Tomasi atauliza, “utuoneshe njia.” Kwani baada ya kuuliza Yesu anaweza
kujieleza: “Mimi ni njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa
njia ya mimi.” (Yoh. 14:6).
Hebu tuangalie ni katika vipengee vipi Tomas anaweza kuwa ni pacha wako.
Hoja
ya mojawapo yaweza kuwa Tomas alikuwa haelewi ni kwa nini wenzake
wamejifungia chumbani. Yeye ameondoka na kwenda kuzubaa sijui wapi kwa
sababu hajisikii kuwa na woga wowote ule. Katika kipengee hiki, Tomas ni
pacha au kurwa wa mtu yule ambaye hajisikii kuwa wa maana au bora zaidi
kuliko wengine, yaani, haelewi ni kwa nini wengine wamejifungia ndani.
Ni
dhahiri kwamba Tomas siyo pacha wa wale wanaojitenga na jumuia ya
kikristu kwa sababu labda wanachekwa na kudharauliwa na wengine;
wanaojisikia bora zaidi na kuwahukumu wengine wasio katika jumuia au
hata wanaowahukumu wale walio katika jumuia kwamba ni waovu kuliko
wengine, au kama wale wanaoacha dini yao na kuingia nyingine.
Tomas
hahukumu, wala kudharau wengine bali yawezekana anajiona kama
amedanganyika kidogo au amekwazika na jumuia ile. Yaani ni kama wakristu
wale wanaoona ndani ya kanisa kuna makwazo au mambo ya aibu, hivi
wanajisikia kukwazika na kuteseka mioyoni mwao. Hivi wanaona ni bora
kujiweka kidogo pembeni.
Aina ya nyingine ya kuwa pacha wa Tomas
ni pale wale ambao wamedanganyika na muundo wa kanisa, na uendeshaji wa
mambo ya kanisa, kukosa mpango mzuri. Hakuna uinjilishaji wa kutosha,
au kuna utawala wa kibabe, kuna kujionesha ukuu unaotegemea mali, na
hivi wanaona afadhali kujiepusha kidogo. Waumini wasioamini kama mambo
yanaweza kubadilika katika kanisa. Hawa ni pacha wa Tomas.
Anapofika
Tomas wenzake wanamhabarisha: “Tumemwona Bwana.” Kwa tamko hili
walikuwa wanataka kummweleza kwamba mambo yamebadilika, si kama
alivyodhani au kama alivyoyaacha. Tomas anataka kuhakikisha yeye
mwenyewe kama kweli mazingira aliyoyaacha yamebadilika.
Hapa sasa
tunakutana na pacha mwingine, yaani wale wanaotaka kuhakikisha kwa
kuona na kugusa. Pacha wa Tomas ni wale wasiomwona Yesu wa Nazareti
lakini wameitwa kumwamini ili kumshuhudia kwa ndugu zao. Pacha ni wale
wasioelewa. Yaani hao pia wameitwa ili kuelewa lakini wanayo namna mbili
ya kuelewa. Kimwili, kuamini kwao ni kama kule Tomas, lakini ndani yao
kuna haja na hamu ya kuamini ambayo wanataka kuihakikisha.
Aliye
na mang’amuzi haya ya ndani, ajue kwamba Tomas ni pacha wake. Na kwamba
tusiwe na woga wa kuungama mashaka yetu ambayo ni kama ya Tomas, kama
tunaweza kugusa kama Tomas hatuwezi kuwa na mashaka. Lakini kugusa huko
kwetu hakuwezekani.
Kwa hiyo ni vyema kabisa kuwa ndani yetu
tunaye huyo pacha wetu Tomas wa kuona mashaka kwamba huyo aliyetoa
maisha kwa kufa kwake kama mtumwa ameingia katika utukufu wa Baba. Kwa
hiyo fundisho kuu tunalopata hapa kwa huyu pacha wetu ni hili: Yesu
anapofika siku ya nane anaonesha majeraha yake na anamwita Tomas kuja
kuhakikisha.
Huo ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kuweka mikono
yetu ubavuni pake. Kualikwa na Yesu Mfufuka kuweka mikono yako ubavuni
mwake maana yake pale unapoweka mikono yako, shughuli zako zote, na hasa
ukijiweka wewe mwenyewe, kujiaminisha na kujitoka kabisa maisha yako
kwa upendo kama ya Yesu hapo umeingia katika ulimwengu wa Mungu na wa
utukufu wa ufufuo.
Upacha mwingine na Tomas ulio mzuri sana, ni
pale Yesu anapomwalika Tomas kuyatupa maisha yake kwenye mapendekezo ya
mwalimu: “Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono
wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.” (Yoh.
20: 27), naye Tomas anapojibu: “Bwana wangu na Mungu wangu!” (Yoh.
20:28). Hilo ni ungamo la imani katika Mungu wa kweli imani
inayojidhihirisha katika ufufuko wa Kristu. Imani kwa Mungu anayetoa
maisha yake kwa ajili ya upendo.
Tomas aliyekuwa na mashaka,
ndiye wa kwanza kushuhudia imani iliyo safi ya wakristu wa kwanza. Ni
yeye aliyeona uthibiti wa msulibiwa katika ufufuko. Haamini juu ya Mungu
anayeadhibu, anayezawadia, anayewapenda wema tu, amemwamini katika
Kristu aliyetoa maisha Mungu wa kweli ambaye hawezi kuwa mwingine
isipokuwa yule aliyesulibiwa kwa ajili ya upendo.
Uhakika kwamba
ameona na kugusa mikono na ubavu wa Mungu, uhakika ule anaweza kuwa nao
tu kwa mtazamo wa imani. Mtazamo unaotakiwa kuufungua daima pamoja na
jumuia. Sisi tunasikia sauti ya Bwana na katika mkate wa Ekaristi sisi
tunagusa mapendekezo yake ya maisha ya kujifanya mkate kwa ajili ya
kutupenda.
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
Utakatifu
ni hija ya maisha inayotekelezwa hatua kwa hatua kama walivyofanya
Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II watakaotangazwa kuwa
watakatifu, Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican. Huu ndio utakatifu ambao watu wanaendelea
kuushuhudia katika maisha na utume wa Wenyeheri hawa.
Padre
Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican akiwa ameambatana na wahusika
wakuu katika mchakato wa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane
Paulo II kuwa watakatifu: Padre Giovangiuseppe Califano pamoja na
Monsinyo Slawomir Oder, Jumanne, tarehe 22 Aprili 2014, wamepembua maana
ya utakatifu mintarafu maisha ya wenyeheri hawa wawili.
Yohane
XXIII katika maisha yake kama Padre, Askofu na Khalifa wa Mtakatifu
Petro alijiwekea nadhiri ya kuwa karibu na Yesu, kujificha katika Moyo
wake Mtakatifu, Kusali Rozari na kumpatia nafasi ya pekee katika maisha
yake. Haya ni mambo yaliyojionesha kwa namna ya pekee katika maisha na
utume wake kama Mchungaji na Baba.
Ni kiongozi aliyeyasimika
maisha yake katika furaha na ukarimu kiasi cha watu wengi kumwita kuwa
ni Papa mwema! Alikazia umuhimu wa mshikamano katika maisha na utume wa
Kanisa kwa kuitisha Sinodi ya Jimbo kuu la Roma na Mtaguso mkuu wa Pili
wa Vatican. Ni kiongozi aliyeonesha upendo na uelewa katika shughuli za
kichungaji; akawa kweli ni mtu wa msamaha na faraja kwa wote
waliomkimbilia. Alikazia utii na amani ya kweli duniani.
Monsinyo
Slawomir Oder anasema, utakatifu wa Mwenyeheri Yohane Paulo II ulianza
kuonekana tangu alipokuwa bado Chuo Kikuu, kiasi kwamba, baadhi ya
wanadarasa wake waliandika chumbani kwake, "Mtakatifu mtarajiwa",
kutokana na na moyo na bidii ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na
maisha adili. Yote haya yalimwilishwa kwa njia ya matendo ya huruma.
Alikuwa
na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, akawa na
ujasiri wa kukabiliana na changamnoto za maisha kwa imani na matumaini
pasi na kukata tamaa, kwani daima aliuona mkono wa Mungu ukiyaongoza
maisha yake! Watu wengi walitambua kuwa kweli Yohane Paulo II alikuwa ni
mtu wa Mungu aliyekuwa ni chemchemi ya maisha yake yote, kiasi cha
kujikita katika Uinjilishaji Mpya, ili wote waweze kuwa ni watakatifu
kwa kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Tunaendelea
tena katika tafakari yetu masomo Dominika ya II ya Pasaka mwaka A. Ni
kipindi cha furaha kwa sababu ya ushindi dhidi ya kifo kwa njia ya
ufufuko. Neno la Mungu, linakazia na kuahidi furaha ya kweli kwa wale
ambao hata kama hawakumwona Bwana wanayo imani na tumaini la kweli
katika yeye. 
Katika
Somo la kwanza, kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume latuonesha
furaha na tabia ya jumuiya ya kwanza ya Yerusalemu. Kwa nini tunaoneshwa
jambo hilo? Ni kwa sababu tunaalikwa kuishi mtindo uleule wa jumuiya ya
mwanzo katika mazingira yetu. Mambo msingi ya Jumuiya ya I yalikuwa
utii na usikivu wa watu kwa Neno la Mungu lililohubiriwa na Mitume.
Aidha waliweka mali yao na moyo wao pamoja kwa faida yao na kasi ya
Injili.
Ili kuimarisha mambo haya waliadhimisha pamoja Ekaristi
Takatifu na kusali pamoja kwa upendo. Mambo haya msingi yalifungamana na
furaha, uchangamfu, ushirikiano ambavyo vilikuwa vivutio kwa jumuiya
nyingine nje ya Yerusalemu. Ndiyo kusema waliishi na kukishuhudia kile
walichohubiri katika maisha yao, yaani waliuishi ufufuko ambao ndilo
chimbuko la haya yote.
Mpendwa msikilizaji, wito kwetu hivi leo
katika jumuiya zetu ni kuanza polepole kupalilia nguvu ya ufufuko, ndiyo
kusema tunaalikwa kushuhudia daima kwa maisha yetu yakuwa Kristu ni
mfufuka. Mpendwa, katika mantiki hiyo katika jumuiya zetu lazima tabia
za jumuiya ya kwanza zijitokeze na kukua na hivi kuwa kielelezo cha
mapendo kwa watu wa mataifa. Yafaa kukomaza ile tabia ya kushirikishana
tulichonacho hata kama ni kidogo. Tujifunze kuwa na kile kinachotufaa na
kinachobaki kiwe kwa ajili ya wale waliowahitaji katika jumuiya zetu.
Kumbuka
usemi wa Mtakatifu Basil akisema “kama mmoja wetu angechukua kwa ajili
yake kinachohitajika na kingine kikawa kwa ajili ya ndugu yake maskini,
basi kusingekuwa na tajiri wala maskini katika jumuiya”. Hii ni falsafa
ya mgawanyo sawa ambayo tungepaswa kuifikia kama kweli tunataka kumfuasa
Bwana kwa ukamilifu! Mpendwa msikilizaji inaonekana kuna ugumu katika
kushirikishana mali tulizonazo, na hasa kuwapeni maskini, je toka
tukiamini na kuendelea katika ugumu huu twaweza kusema tunaishi na
tunashuhudia ufufuko? Tafakari sana jambo hili!
Katika somo la
Pili toka barua ya kwanza ya Mtakatifu Petro tunakumbushwa siku ya
ubatizo wetu. Kwa njia ya ubatizo tulipata kuingia katika furaha isiyo
na mwisho. Ndiyo kusema Mt Petro anataka hata kama kuna madhulumu na
taabu mbalimbali tusisahau furaha ya milele. Anasema mateso ni ya
kitambo kidogo tu na baadaye yanapita cha msingi ni kutazama mbele
tukiendelea kukua katika neema ya ubatizo.
Mtakatifu Petro
anatukumbusha kuwa mkristu katika ulimwengu huu ni mgeni na hivi yuko
safarini kwenda nchi ya ahadi yaani mbinguni. Tunakumbushwa kuwa hakuna
mateso yanayoweza kuzima moto wa furaha na mapendo uliowashwa wakati wa
ubatizo. Wakristo ni kama dhahabu ambayo ili itengeneze kitu cha thamani
lazima ipitie moto ili ichomwe na kusafishwa tayari kwa kito cha
thamani.
Katika somo la Injili, hali ya maisha ya jumuiya inajionesha
wazi. Wanafunzi wako pamoja ingawa wanahofu! Bwana anawakuta wakiwa
pamoja na kuwatakieni amani. Anawaonesha alama za madonda na wanafurahi
na kusema tumemwona Bwana! Ni katika jumuiya hiyo Bwana anawavuvia Roho
Mtakatifu ili wapate kuondolea dhambi. Ni siku hii anaweka sakramenti ya
kitubio katika Kanisa na kisha anawatuma wakaende kutangaza habari
njema. Kumbe Toba ni mlango wa kazi ya kimisionari, ni mlango wa imani,
ni mlango wa wokovu. Analikabidhi kanisa ufunguo wa kufunga na kufungua
katika mambo yamhusuyo Mungu katika uhusiano wake na mwanadamu.
Jumuiya
wakati fulani zinakuwa na watu walio na mashaka katika imani. Hali hii
inajionesha leo pia. Ndiyo kusema, kumbe Mtume Tomaso ambaye hakuwapo
pamoja na wenzake siku ya kwanza haamini, bado ana mashaka kuhusu
ufufuko! “Siamini mpaka nitie vidole vyangu katika makovu ya Bwana!
Baada ya siku nane tukio hilo la kitaalimungu, Bwana anawatokea tena
Mitume na wakati huo Tomaso yupo.
Bwana anamwambia lete mikono yako
na uweke kidole chako katika ubavu wangu na usiwe asiyeamini! Tomaso
anajibu, Bwana wangu na Mungu wangu! Mpendwa, Mtume Tomaso anapokiri
udhaifu wake anatufundisha kuwa watu wa Imani na unyenyekevu mkubwa na
hivi baada ya ufufuko hakuna mashaka tena kinachobaki ni kwenda
kutangaza habari ya furaha kwa mataifa.
Mpendwa leo hii wapo watu wa
namna hii katika jumuiya zetu, kumbe wanaalikwa na Bwana kusadiki
pasipo kuona, na kwa namna hiyo Bwana anatangaza heri kwa wasioona
wakasadiki na si kwa wanaosadiki kwa sababu ya kuona. Mwishoni mwa
sehemu ya Injili ya Dominika hii, Mwinjili anatuambia pia zipo ishara
nyingi ambazo hazikuandikwa na hivi mtu asishangae ishara nyingine
ambazo hazimo katika Biblia lakini ni muhimu kwa imani yetu na maisha ya
Kanisa.
Nakutakieni furaha tele katika kipindi chote cha Pasaka na
Mungu azidi kuwa nawe, nawe ukitekeleza mapenzi yake katika Jumuiya kama
Jumuiya ya kwanza ya Waamini. Tukutane tena Dominika ijayo. Tumsifu
Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya
C.PP.S.