
Meno ya tembo yaliyokamatwa
POLISI nchini Tanzania wamesema
shehena ya meno ya tembo yaliyokamatwa katika bandari ya Zanzibar ni
sawa na tembo mia tatu na watano, yakiwa na thamani ya karibu shilingini
bilioni nane, sawa na karibu dola milioni tano za Kimarekani.
Watu wawili wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma
za kuhusika na meno hayo, huku maafisa wawili wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania, TRA, na mmoja wa Mamlaka ya Bandari pia wamekamatwa kuhusiana
na tukio hilo.Meno hayo ya tembo yalikuwa yamefichwa kwenye kontena la urefu wa mita 40, tayari kwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Serikali ya Tanzania iko katika kampeni kamambe ya kupambana na ujangili ili kunusuru wanyama pori ambao wako hatari kutoweka kutoka na kushamiri kwa biashara ya meno ya tembo na vipusa vya faru.
Iliripotiwa kuwa wastani wa tembo 30 huuawa kila siku nchini Tanzania, hali iliyoilazimisha serikali kukabiliana na mtandao wa ujangili, ambao unatuhumiwa kuunganisha watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wawindaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wakubwa ndani na nje ya nchi.
Hivi karibuni raia watatu wa China walikamatwa nchini Tanzania kwa kukutwa na meno 706 ya tembo, sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini humo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni