
Wakati Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden
Rage akitarajiwa kutua nchini tarehe 22/11/2013 jioni, bodi ya wadhamini ya klabu hiyo
imetangaza kusitisha maamuzi ya kamati yao ya utendaji ya kumwengua
katika nafasi uenyekiti.
Jumanne Kamati ya Utendaji ya Simba iliyokutana Jumatatu bila uwapo kwa mwenyekiti (Rage) aliyekuwa Marekani, ilitangaza kumsimamisha Rage na makocha wa timu yao, Abdallah 'King' Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelu 'Julio'.
Kamati hiyo iliamua timu kwa sasa iwe chini ya kocha wa timu ya vijana, Simba B, Seleman Matola ambaye atakuwa pia Msaidizi wa Kocha Mkuu mpya wa kigeni, Zdravok Logarusic, raia wa Croatia atakayetambulishwa Desemba Mosi, mwaka huu.
Akizungumza jana jijini, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa klabu hiyo, Hamisi Kilomoni, alisema katika kikao hicho cha bodi kilichohudhuriwa na wajumbe wawili (Kilomoni na Ramesh Patel), kilisitisha maamuzi ya kumsimamisha Rage kwa sababu kikao kilichokaa na kutoa maamuzi hayo kilikuwa ni batili.
Kilomoni alisema pia kuwa, wameamua kusitisha maamuzi hayo ili kuiepusha klabu hiyo na migogoro ambayo inaweza kuanza kutokana na hatua hiyo ya kumsimamisha mwenyekiti wao.
Mwenyekiti huyo alisema katika kikao chao kilichofanyika Jumanne Novemba 19, mwaka huu waliitaka Kamati hiyo ya Utendaji kuwasilisha muhtasari wa kikao walichokifanya, kuorodhesha majina ya wajumbe waliohudhuria na maamuzi waliyoyafanya baada ya kukutana.
"Katika kikao chetu tulimuita Kinesi (Joseph Itang'are- kaimu makamu mwenyekiti), tukamhoji na kukubaliana waahirishe maamuzi yao, hatutaki vurugu, hatupendi na hatutaki wagawanyike," alisema mwenyekiti huyo.
Alieleza kuwa kikao hicho hakikuwa halali kwa sababu hakikuitishwa na mwenyekiti (Rage) kama katiba inavyoelekeza au kingekuwa halali endapo makamu mwenyekiti angeachiwa baraka za kuitisha kikao hicho.
Alisema lengo la kutaka kuwasuluhisha viongozi hao na mwenyekiti wao ni kuleta suluhu kwenye klabu na vile vile kuwataka wakae madarakani hadi muda wao utakapomalizika kikatiba.
"Sisi ndio wasuluhishi tunaotambulika katika ibara ya 18 (3) ambayo inaeleza kuwa viongozi wakishindwa kupatana waje kwetu kabla ya kwenda nje," Kilomoni aliongeza.
Kauli ya TFF
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, alisema kuwa tayari shirikisho hilo limeshapokea taarifa za kusimamishwa kwa Rage na kamati ya utendaji ya klabu hiyo.
Malinzi alisema suluhisho la maamuzi hayo yaliyotolewa na viongozi wa Simba litajulikana mapema wiki ijayo kufuatia uongozi wake kutangaza wajumbe wapya wa Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji.
Rage
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tabora mjini (CCM), anatarajiwa kurejea nchini.
Mara baada ya kuwasili, Rage, anatarajiwa kuweka wazi msimamo wake kufuatia maamuzi yaliyofanywa na wajumbe wake wa kamati ya utendaji.
Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa klabu hiyo waliofika kwenye makao makuu ya klabu yao leo asubuhi, walionekana kugawanyika kufuatia maamuzi hayo yaliyotolewa ya kumsimamisha Rage.
Rage alikaririwa na vyombo vya habari akisema, "maamuzi yaliyofanywa dhidi yangu ni batili" huku akiahidi kulifanyia kazi suala hilo pindi atakaporejea nchini akitokea Marekani."
Mapema mwaka huu, baadhi ya wanachama walikusanyika jijini Dar es Salaam na kutangaza kuung’oa uongozi mzima wa Rage, wakati akiwa nchini India kwa ajili ya matibabu, lakini baadaye likatokea kundi kubwa la wanachama kumpokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa maandamano ya kishujaa ambapo alisisitiza yeye ndiye mwenyekiti wao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni