Week Hot newz

GOtv Cecafa Senior Challenge Cup:Uganda, Sudan wafuzu robo fainali


Na Paskal Linda,Kenya
Mabingwa watetezi Uganda na Sudan walikuwa mataifa ya kwanza kukata tiketi za robo fainali kwenye dimba linaloendelea la GOtv Cecafa Senior Challenge Cup baada ya wote kuandikisha ushindi Jumatatu.
Uganda walianza mechi yao dhidi ya Eritrea kwa kumkaribisha nahodha wao Emmanuel Okwi aliyerejea baada ya kupata nafuu kutokana na Malaria yaliomfanya kukosa mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Rwanda.
Mshambuliaji wa mabingwa wa Ligi Kuu Kenya, Gor Mahia, Dan Sserunkuma na Okwi waliunganisha kupatia Uganda uongozi dakika kumi baada ya mechi kuanza.
Hamis Kiiza aliongeza la pili kupitia mkwaju wa penalti baada ya Sserunkuma kufyekwa ndani ya eneo la hatari.
Straika huyo wa Gor aliendelea kuwa nyota wa kikosi chake baada ya kubuni nafasi iliyopelekea Uganda kupata lao la tatu.
Sserunkuma alitimuka wingi ya kushoto kabla ya kutuma pasi iliyofunikwa na Okwi kupatia Uganda uongozi wa 3-0 katika mapumziko.
Serak Beyene na Muner Ahmed walikumbana na mwamba kwenye lango la Uganda pale goli kipa Benjamin Ochan alipokabiliana na mikwaju yao huku Eritrea wakitishia kufunga katika kipindi cha lala salama.
Kwenye mechi ya awali, Sudan walilaza mabingwa wa 2009 Rwanda 1-0 kupitia nyota wao Sala Ibrahim aliyetia kimyani katika dakika ya 29 na kombora kali kutoka hatua 30.
Ibrahim sasa anaongoza orodha ya wafungaji na mabao matatu.
Baada ya kuzoa alama sita kila mmoja, Uganda na Sudan watamenyana Alhamisi ili kutafuta nani ataongoza kundi hilo kwenye mechi za mwisho za makundi.
Rwanda wamebaki na kibarua cha kucharaza Eritrea na watumai kuwa watukuwa miongoni mwa timu zitakazo fuzu kama bora zaidi katika nafasi ya tatu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni