Week Hot newz

Ni uchawi wa Uturuki, Oman Mkwakwani

WAKATI mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Yanga, wakitarajiwa kushuka kwenye dimba la Mkwakwani jijini Tanga kuwavaa wenyeji Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ leo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limewataka mashabiki watakaosafiri kwenda huko kuhakikisha wanakamilisha kununua tiketi za elektroniki.
Yanga iliyotoka kusaka makali
nchini Uturuki inajitupa Mkwakwani kuwavaa Wagosi wa Kaya waliotoka kusaka mavumba Oman, katika pambano linalotabiriwa kuwa na ushindani na kuvuta mashabiki wengi kutoka Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, ambapo TFF imewataka kuhakikisha wanaepuka usumbufu kwa kusafiri wakiwa na tiketi zao mkononi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa mauzo ya tiketi za mechi hiyo yalianza juzi na ni vema mashabiki hao wakanunua watokako, kuliko kutarajia kwenda kununulia Tanga.
“Uzoefu unaonyesha kuwapo kwa mambo yanayochangia usumbufu katika ununuzi wa tiketi za elektroniki, hivyo tunawaomba mashabiki wa Dar, Morogoro na Arusha ambako vituo vya mauzo vipo, kununulia huko, kuliko kutarajia kwenda kununulia kule,” alisisitiza Wambura.
Aliongeza kuwa TFF, Bodi ya Ligi na wazabuni wa mfumo mpya wa tiketi hizo, benki ya CRDB, wanatambua uwepo wa changamoto miongoni mwa mashabiki katika kuuelewa, lakini akasisitiza kuwa wako tayari kukabiliana nazo kwa kutoa elimu kuliko kuufuta.
“Tunatambua ugumu uliopo, ndiyo maana tunawaomba wadau wetu kuhakikisha wanajifunza taratibu na hatimaye wataelewa na kuutumia vizuri. Kwa sasa msisitizo wetu ni kuwa mashabiki wasio na tiketi wasiende viwanjani, kwani haziuzwi huko,” alisema Wambura.
Alitaja viingilio katika pambano kati ya Coastal na Yanga kuwa ni sh 5,000 na 15,000, kwa tiketi moja zinazopatikana kupitia M-Pesa, CRDB SIMBanking na CRDB Fahari Huduma.
Mechi nyingine zitakazopigwa leo, Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, ambako viingilio ni sh 10,000 na sh 5,000 huku Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar watawaalika wakata miwa wenzao, Mtibwa Sugar ya Manungu Turiani, Morogoro, viingilio vikiwa ni sh 5,000 na 3,000.

Nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kule Chamazi Mbagala, Azam FC watakuwa nyumbani Azam Complex kuumana na Rhino Rangers ya Tabora, viingilio vikiwa sh 10,000 na 3,000

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni