Week Hot newz

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Tunaendelea katika safari yetu ya tafakari masomo Dominika ya nne ya kipindi cha mwaka. Neno la Mungu latualika kuwachagua maskini. Katika kuwachagua maskini yatulazimu kuwa maskini wa roho tukitambua kuwa ufalme wa mbinguni unajifungamanisha na heri hiyo.
Katika somo la kwanza, Nabii Sefania anawaalika walio wacha Mungu, kutafuta daima haki na unyenyekevu, maana ni kwa njia hiyo katika siku ya hukumu Mungu atawahurumia. Anasema kwa hakika wale wote walioonewa na kutumainia jina la Mungu watabakizwa na hawatasahauliwa kamwe.

Nabii Sefania anakuja na mahubiri haya akisukumwa na hali ya maisha ya wakati wake katika kipindi kabla ya uharibifu wa Hekalu la Yerusalemu, na hasa mawazo juu ya mali. Katika kipindi hicho mali ilikuwa ni kipimo cha baraka toka kwa Mungu. Aidha, mtu alionekana kuwa wa maana kwa kuwa na mali. Basi Nabii Sefania na Manabii wengine, wanaona wakati fulani mali hupatikana kwa sababu ya unyonyaji wa maskini, na hivi wanaanza kukemea hali hiyo. Umaskini haukuwa tokeo la dhambi, bali tokeo la madhulumu toka kwa matajiri.

Nabii Sefania anakemea kwa nguvu zote jambo hili pamoja na kwamba alikuwa amezaliwa toka familia tajiri. Anawaalika watu kutambua ujio wa adhabu ya Mungu kama wataendelea na unyonyaji kwa maskini. Ndiyo kusema anawaalika kurudi kwa Mungu kwa njia ya toba na kutenda haki. Nabii anaona kufanya toba lazima kujikite katika kuwa maskini wa roho, kuwa wanyenyekevu daima kama karama msingi kwa ajili ya maisha ya kumpendeza Mungu.

Kwa njia ya Nabii tunatambua, nini maana ya umaskini wa roho, kumbe si hali ya mtu au nafasi ya mtu katika jumuiya bali njia ya kiroho, hali ya ndani ya mtu anayetafuta wokovu. Umaskini wa roho ni kutokuwa na hali ya kujitegemea na kwa namna hiyo kumtegemea Mungu. Ndiyo kusema, mwaliko kwetu hivi leo ni kutafuta namna ya kujinasua toka mali kwa ajili ya uzima wa milele.

Katika somo II toka barua ya Mt. Paulo kwa Wakorinto tunamwona Mungu anavyochagua mambo dhaifu ili kuaibisha wenye hekima. Mungu anachagua maskini wa roho badala ya wanaojigamba. Kumbe Paulo anawaalika Wakorinto waliochaguliwa na Mungu kwa njia ya Kristo, hekima ya Mungu, haki na shime yao kuwa makini katika hilo. Kwa nini Paulo anakuja na fundisho hili? Ni kwamba jumuiya ya Wakorinto ilijawa na utengano kwa sababu ya madaraka na utajiri. Utengano huu ulileta maudhi hasa kwa maskini!

Mt Paulo sasa anawaonya kwa maneno makali na hata yanayoweza kufanya mtu afikiri kuwa hekima si ya maana. Hekima na akili ni vya maana lakini lazima viwe kwa ajili ya huduma kwa watu na kwa Mungu. Mungu anachagua maskini na si fukara, kumbe umaskini wa roho, unaojali maisha ya watu na kumweka Mungu katikati ya safari ya wokovu wa wanajumuiya wanaoishi na kusafiri pamoja wakielekea mbinguni.

Katika somo la Injili, toka Injili ya Matayo, tunapata kutafakari Heri Nane za mlimani. Kwa kifupi Heri Nane ni ufupisho wa mafundisho mazima ya maisha ya kiroho na mwongozo wa namna ya kufika mbinguni. Mungu anawachagua walio maskini wa roho, yaani wale ambao huweza kuchagua njia ya unyenyekevu, huruma, msamaha, furaha, haki, utakatifu, amani, uvumilivu wakati wa taabu itokayo na utafutaji wa haki pamoja na taabu itokayo na dhuluma, kama ndio warithi wa uzima wa milele.
Mpendwa, yafaa kujiuliza, hivi Mungu apendezwa na umaskini? Mbona Injili yatualika kufanya bidii ili kuondoa umaskini katika maisha yetu? Ni kweli, Mungu hapendezwi na umaskini bali apendezwa na umaskini wa roho ambao huleta wokovu. Kuhusu mali, Bwana hatofautiani na manabii waliomtangulia, yaani haoni mali kama alama ya baraka toka kwa Mungu, lakini pia habezi mali. Sasa ataka nini!

Yafaa twende kuangalia neno mali kama lilivyotumiwa na Matayo na matumizi ya mali tuliyonayo! Tukitazama Injili ya Lk 16:9 tunaona neno mali hupata maana sahihi kiroho pale tunapogawanya mali hiyo kwa maskini. Hata hivyo Bwana huona hatari itokanayo na mali tunapoelekea mbinguni, angalia Lk 14:33 akisema hakuna anayeweza kuwa mfuasi wangu kama atashikama na mali. Fundisho la Bwana latudai kujibandua toka mali ili kumfuasa yeye na ndio msingi wa kuweza kuelewa nini maana ya kuwa maskini wa roho.

Mpendwa msikilizaji, mwaliko katika fundisho ni kujipatia uwezo wa kushirikishana mali tulizojaliwa na Mungu. Bwana hapendezwi na ufukara ambao huja bila kuchagua bali hupendezwa na umaskini ambao mtu anauchagua kwa ajili ya huduma ya Injili. Ndiyo kusema furaha kwa wale wanaochagua umaskini kwa ajili ya kujitoa kwa waliowahitaji ni tele na ya uhakika. Umaskini mwingine tofauti na huo si heri na si njia ya kiroho bali njia ya uvivu na kwa hivi hakuna furaha. Aidha umaskini wa roho unaokuja kwa njia ya uchaguzi wa ndani katika mlengo wa Injili ni mwito kwa ajili ya wakristu wote na si kwa tabaka fulani kati ya waamini.

Tukiitazama heri II yaani wanaheri wale wenye huzuni, tunapata kujiuliza swali, je Mungu apendezwa na huzuni? Kwa hakika hapana, kumbe heri hii ni kwa wale ambao wanahuzuni kwa sababu wanateswa kwa ajili ya imani yao. Heri inakuja kwa maana hali yao hiyo itaondolewa na watafarijiwa, na Mungu. Bwana akisonga mbele anatangaza tena heri kwa walio wapole maana watairithi nchi. Wapole ni wale wastahimilivu na wanyenyekevu. Bwana hasifu unyenyekevu na uvumilivu wa asili, yaani zawadi za Mungu kwa mtu tangu kuzaliwa kwake bali asifu upole na uvumilivu wa kiroho ambao mtu hujipatia mbele ya madhulumu ya haki zake, akionesha uvumilivu, akimtegemea Mungu pasipo kupambana kwa njia ya vita!

Mpendwa, katika msingi uleule wa upole Bwana anatangaza heri kwa wenye njaa na kiu ya haki kwa maana watashibishwa. Kwa heri hii, ataka tutambue na tupiganie haki kwa ajili ya wote kama ambavyo mtu hutafuta chakula kwa ajili ya kuishi. Ndiyo kusema, kama ilivyo njaa ya chakula basi ijengeke njaa na kiu ya haki. Mpendwa msikilizaji, Bwana anasonga mbele akitangaza heri wenye huruma, akitaka tuwe na huruma, huruma ambayo hujihusisha katika kuwasaidia wengine, yaani isiyoishia katika kusamehe bali katika kuhakikisha wengine wanapata kuishi na kuokoka. Heri hii inakuja kwa maana ufalme wa Mungu utakapokuwa umetimia nao watapata mmojawapo wa kuwasaidia na kuwafariji. Kristu katika hili anatangaza maisha mpya ambamo ubinafsi na magomvi si vitu vya maana bali mapendo na rehema kwa wengine.

Bwana anasonga mbele katika mafundisho yake akikazia usafi wa moyo kama kigezo cha kuweza kumwona Mungu. Katika heri hii, Bwana hazungumzii useja bali unyoofu na ukweli unaomfanya mtu asihangaikie fikira potofu kinyume na mapenzi ya Mungu. Huyu mwenye usafi wa moyo hagawanyi upendo wake na maisha yake kwa wafalme wawili yaani Mungu na shetani bali tu kwa Mungu. Ni kwa jinsi hiyo basi moyoni mwake hukaa mawazo na mapendo ya kimungu ambayo ndiyo umletea heri na furaha daima. Kilele cha heri hii ni kumwona Mungu.

Katika mambo msingi ambayo mwanadamu anayahitaji ni amani. Amani ni tunda la Roho Mtakatifu. Ni tokeo la kuzaliwa Mwana wa Mungu, kumbuka utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema. Bwana anatangaza heri kwa watenda na watafuta amani, yaani wapatanishi kwa ujumla. Neno amani katika Biblia halina maana tu ya kutokuwepo kwa vita bali hulenga ustawi wa watu, haki, furaha, afya njema na maisha maelewano. Mpendwa msikilizaji, maisha ya namna hii hujengwa na hivi Bwana anatangaza heri na baraka kwa wale watakaojishughulisha na ujenzi wa amani katika taifa la Mungu.

Mpendwa msikilizaji, Bwana akimalizia mafundisho yake pale mlimani anakuja na tangazo la heri kwa wale ambao katika kutenda heri hizi na hasa wakitafuta haki wataudhiwa na kudhulumiwa, akisema ufalme wa mbinguni ni wao. Kwa hakika awaye yote anayetafuta kutenda haki, atadhulumiwa na kunyanyaswa. Ndiyo kusema wadhulumaji huogopa ujio wa ukombozi na hivi kujiweka katika mapambano kinyume na ufalme huo. Bwana akijua hilo anatangaza heri kwa awaye yote atafutaye amani yakwamba akibaki imara atapata furaha na baraka za Mungu.

Tukumbuke pia kwamba, Bwana aliteswa, lakini alivumilia kiasi kwamba Mungu akamwadhimisha mno na kumpa jina lipitalo kila aina ya jina. Mpendwa, kupokea heri za Mungu si jambo jepesi, ladai kuzama katika maisha ya kiroho ili polepole kukuza roho ya mapendo na utii kwa Mungu. Tunaitwa kuwa watakatifu kama Baba yetu aliye mbinguni.

Mpendwa mwana wa Mungu nikutakie baraka na heri za mbinguni sasa na daima na milele. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C. PP.S.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni