Week Hot newz

SAUTI ZA BUSARA: Ni zaidi ya Tamasha la burudani

TAMASHA la Sauti za Busara ni miongoni mwa machache ambayo yamejenga historia kutokana na kuutangaza na kuuendeleza muziki wa Tanzania nje ya mipaka yake, ambako mwaka huu litafanyika kuanzia Februari 13 hadi 16. Mbali na burudani, Tamasha la Busara ambalo ni la 11 mwaka huu tangu kuanzishwa, limekuwa kiunganishi kizuri kwa wasanii wa hapa nyumbani na wale wa kimataifa, jambo linalotoa nafasi ya kubadilishana ujuzi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Sauti za Busara Promotions, Simai Said Mohamed, anasema lengo la kuandaa tamasha hilo ni kuwaleta watu pamoja na kuonyesha utajiri wa muziki wa kisasa, ambao umebuniwa katika nchi za Afrika Mashariki, nchi nyingine kutoka barani Afrika na kwingineko duniani.

Mohamed anasema, tamasha hilo linalojulikana kama ‘Tamasha Rafiki Katika Sayari’ ni la kimataifa linalosherehekea muziki wa Kiafrika kila mwaka na kwamba vikundi 32 vitafanya maonyesho jukwaani ndani ya Ngome Kongwe visiwani Zanzibar.
Anasema vikundi hivyo vimechaguliwa kutokana na maombi zaidi ya 560 na vinawakilisha nchi 19, zikiwemo za Afrika Mashariki, Afrika Kusini na Magharibi, maeneo ya Mto Nile, pia kutoka Puerto Rico na inatarajiwa zaidi ya wasanii 200 watafika Zanzibar kufanya maonyesho ya muziki.
Mwenyekiti huyo anawataja miongoni mwa wasanii maarufu kutoka Tanzania watakaoshiriki Tamasha la Sauti za Busara 2014 kuwa ni pamoja na Jhiko Manyika ‘Jhikoman’, mwanamuziki anayejulikana kwa muziki wake wa reggae, ambaye atazindua ziara yake ya kuitembelea dunia jukwaani wakati wa onyesho lake.

Wasanii wengine kutoka hapa nchini ni Ashimba,Batarokota, Swahili Vibes, Hoko Roro, Seven Survivor, Abantu Mandingo, Segere Original na Kazimoto, anayemshirikisha Jackie Kazimoto kutoka ‘The Internationally-Acclaimed’, Jagwa Music.
Anasema tamasha hilo pia litamkaribisha mwanamuziki mkongwe aliyefanikiwa kimuziki kutoka nchini Ghana, Ebo Taylor, pia atakuwepo Sona Jobarteh, mwanahistoria kutoka Gambia na ‘Jupiter and Okwess International’ mwanamuziki mwenye mafanikio kutoka Jamhuri ya Watu wa Congo, ambaye anapasua anga katika fani ya muziki Afrika na kwingineko duniani.
Mwenyekiti huyo anawataja wasanii watakaopamba tamasha hilo na nchi zao kwenye mabano kuwa ni Jhikoman, Ashimba, Hoko Roro, Seven Survivor, Abantu Mandingo, Segere Original, Kazimoto (Tanzania),  Swahili Vibes, Baladna Taarab, Tausi Women’s Taarab, Rajab Suleiman & Kithara ft. Derya Takkali (Zanzibar),  Joel Sebunjo ft. Lenna Kuurmaa (Uganda), Moyize (Rwanda),  Ricky na Marafiki (Kenya).

Wengine ni Ebo Taylor (Ghana na Ujeruman),   Jupiter & Okwess International (DRC),  Joe Driscoll and Sekou Kouyate (USA na Guinea),  The Nile Project (Nile Basin), Noumoucounda Cissoko (Senegal), Oy (Ghana na Uswisi), Addis Acoustic Project (Ethiopia), Sona Jobarteh (Gambia na Uingereza), Tarabband (Misri na Sweden), Majestad Negra (Puerto Rico), HAJAmadagascar and The Groovy People ft. Werner Puntigam (Madagascar, Ufaransa na Australia), Tritonik (Mauritius), Kara Sylla Ka (Senegal na Uswisi), Dizu Plaatjies & The Ibuyambo Ensemble (Afrika Kusini), Street Rat and Body Mind & Soul (Malawi),  Moyize (Rwanda), Ricky na Marafiki (Kenya), Waldemar Bastos (Angola na Portugal) na wengineo wengi kutoka nchi mbalimbali.

Mohamed anaongeza kuwa kwa upande mwingine, mwaka huu burudani ya muziki itajumuisha ‘paredi’ siku ya ufunguzi, pia kutakuwa na ‘Movers & Shakers’ (kongamano la wataalamu), na uonyeshaji wa filamu ndefu za muziki za Kiafrika ambazo zimeshinda tuzo mbalimbali.
“Kwa kushirikiana na wafadhili wa miradi HIVOS, pia tutautambulisha mradi mpya unaojulikana kama ‘Santuri Safari’, mradi ambao utaangalia zaidi jukumu la DJ kwa wakati huu na kuangalia jinsi ya utamaduni wa DJ katika kukuza muziki wa Afrika Mashariki,” anasema.
Mohamed anasema DJ waalikwa, wazalishaji wa muziki, wataalamu wa sauti, waandaaji wa matamasha na wataalamu wa sanaa kutoka ukanda wa Afrika, watajumuika pamoja Zanzibar na kufanya kazi pamoja na kupata mafunzo.

“Tunaona hii ni fursa adimu kushirikiana na kuangalia kuibuka kwa vitu vya kisasa vinavyotokea katika muziki wa elektroniki na utamaduni wa MaDj, na kuangalia jinsi ya kuukuza muziki kikanda na katika anga la kimataifa kwa wakati huu na kwa miaka ijayo,” anasema.
Anasema, kutakuwa na muziki kipindi cha jioni wakati wa jua kuzama maeneo ya mjini na Ijumaa na Jumamosi kutakuwa na burudani ya muziki Ngome Kongwe baada ya kumalizika kwa maonyesho ya moja kwa moja jukwaani.
Anasema, pia tamasha hilo linakuza mambo mbalimbali kupitia ‘Buasara Xtra’ kwa kujumuisha matukio ya maonesho, ambako kwa pamoja hutoa fursa kwa wasanii wazawa kuonyesha kazi zao na kuwafanya wageni watembelee maeneo mengine ya Kisiwa cha Zanzibar.
Anasema zaidi ya Watanzania 150 huajiriwa kila mwaka kama wafanyakazi wa tamasha na pia kwa upande wa kukuza na kulinda muziki na utamaduni wa Zanzibar, Sauti za Busara inatumia nafasi iliyonayo katika kuuthamini muziki wa Bara zima la Afrika, kukuza amani, kujenga jamii ya pamoja Afrika Mashariki na kukuza utalii wa kitamaduni.
“Kwa kila siku kiingilio katika tamasha ni bure kabla ya saa 11 jioni kwa Watanzania wote, na baada ya hapo kiingilio ni sh 5,000 pia ukitaka maelezo zaidi, unaweza kutembelea www.busaramusic.org na kwamba
Busara Promotions ni taasisi inayowezeshwa kwa mwaka mzima na Ubalozi wa Norway,” anasema.
Mohamed, anatoa shukurani kwa Bodi ya wadhamini na wafadhili kama Hivos, Goethe-Institut, the Embassy of the United States of America, Swiss Agency for Development and Cooperation, African Music Festivals Network, Zanzibar Unique, Memories of Zanzibar, Ultimate Security, Ubalozi wa Ufaransa, Southern Sun Hotel, Azam Marine, Ubalozi wa Ujerumani na SMOLE II.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni