
Kutajwa kwa msanii Diamond Platnumz kuwania tuzo
sita za Kilimanjaro 2014, hakujatosha kumfunga mdomo msanii huyo
asizungumzie kutofurahishwa kwake na maamuzi ya kutoswa katika tuzo hizo
kwa nyimbo za wasanii Snura, Madee na Jux.
Nyimbo za wasanii hao 'Nimevurugwa', 'Tema Mate Tuwachape' na 'Uzuri Wako', zimepigwa marufuku kuonekana katika televisheni na kuondolewa katika kinyang'anyiro cha tuzo hizo na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kutokana na video zake "kukosa maadili" ya Mtanzania.
Kupitia kurasa za mitandao yake ya kijamii, Diamond ambaye ameingia katika tuzo hizo kupitia wimbo wake wa 'My Number One', aliandika: "Ikiwa kweli tuna lengo la kutoipotosha kimaadili jamii yetu na vizazi vyetu pendwa, nafikiri ni vyema tungeanza kuzuia video na nyimbo za kutoka nje, kuliko kuzuia nyimbo na video za nyumbani ambazo uchafu wake haufikii hata robo ya uliopo kwenye nyimbo zinazopewa kipaumbele kutoka nje... Hii ni sawa na kuzidi kuukuza muziki wa nje huku tukiudidimiza na kuua muziki wetu... Mikakati ya kufikia malengo yetu itafanikiwa kweli?? #Ni_mtazamo_tu"
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni