Neno Kwaresima linatokana na neno la lugha ya kilatini Quadragesima; maana yake, namba arobaini. Kwa hiyo, Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini katika Mwaka wa Liturjia au Mwaka wa Kanisa. Mwaka wa Kanisa ni maadhimisho ya mafumbo ya Ukombozi kwa njia ya Kristo, pamoja na Kristo na ndani ya Kristo katika Kanisa. Mwaka wa Kanisa una vipindi vikuu vitano; Majilio, Noeli, Kwaresima, Pasaka na dominika au jumapili za kawaida. Noeli na Pasaka ndivyo vipindi maalum katika Mwaka wa Kanisa na kabla ya kuadhimishwa hufanyika maandalizi maalum. Noeli huandaliwa kwa kipindi cha Majilio; na Pasaka huandaliwa kwa kipindi cha Kwaresima. Kwaresima huanza siku ya jumatano kwa Ibada ya Jumatano ya Majivu na huisha alhamisi jioni inapoanza Misa ya Karamu ya Bwana ya Alhamisi Kuu ambapo Siku Kuu Tatu za Pasaka huanza. Kwaresima ni kipindi pekee katika Mwaka wa Kanisa ambacho huanza kwa amri ya Kanisa (amri ya pili ya Kanisa): “Shiriki liturjia ya Jumatano ya Majivu, ambayo ni siku ya kufunga chakula; na Ijumaa Kuu iliyo siku ya kutokula nyama.”
Maana ya Kwaresima
Kwaresima ni kipindi muafaka cha
kufanya toba. Toba ni sharti la msingi kabisa katika kuutafuta uzima wa milele
au ufalme wa mbinguni. Mwenyezi Mungu ndiye anayemwalika mwanadamu ashiriki katika
ufalme wake; basi mwanadamu naye anaitikia mwaliko huo kwa kufanya toba. Kwa
hiyo toba ni kielelezo cha mwanadamu anayekubali mwaliko wa kuingia katika
maisha ya imani ili ashiriki katika ufalme wa Mungu (Mk. 1:15): .....Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari
Njema ya Mungu akisema, “Wakati umetimia
na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini Injili.”
Mwaliko wa Yesu kumtaka mwanadamu
afanye toba ndiyo mwanzo wa historia mpya ya uhusiano kati ya Mungu na
wanadamu. Tendo la toba linajikita katika maana kuu tatu za msingi:
1) Kuacha njia potovu. Mtu anapotambua
kuwa maisha yake ni kinyume na nia ya Mungu na hivyo anakubali na kuamua
kubadilika. Hili ni tendo la toba linalompelekea mtu kubatizwa; na kwa mkristo
humpelekea kurudi katika maisha ya kushiriki sakramenti za Kanisa.
2) Kuacha fikra potovu. Ni
mabadiliko ya dhati kwa wakristo wenye fikra potovu kuhusu ukombozi. Baadhi ya
wakristo wanapotea kwa kuamini kuwa ubatizo peke yake watosha ili kuokoka.
Ubatizo ni mwanzo wa maisha ya kumfuasa Kristo na ni ufunguo wa kuingilia
kwenye haki na wajibu wa kikristo.
Kuokoka ni tendo la kuishinda dhambi na kuingia mbinguni. Kwa hivyo
basi, si sahihi mtu kusema kuwa ameokoka angali bado yuko hapa duniani. Duniani
tunaishi kwenye dhambi na wakati wowote tunaweza bado kuanguka katika dhambi
hata kama tumeshabatizwa.
3) Kuongoka. Ni tendo la kila
siku kwa mkristo mwenye fikra sahihi juu ya ukombozi. Kuongoka ni kutambua
udhaifu wa kibinadamu na kuitumia vema huruma ya Mungu kwa kuungama dhambi.
Dhambi ipo duniani na ina nguvu kuliko sisi wanadamu. Lakini, neema ya Mungu
ipo pia na ina nguvu kuliko dhambi. Kufanya toba maana yake ni kuitambua dhambi
yako na kuiungama kwa Mungu ili upate neema. Neema ya Mungu inatupatia nguvu ya
kupambana na dhambi na inatusaidia kukwepa nafasi ya kutenda dhambi tena.
Kwaresima na Pasaka
Uhalisia wa Kwaresima haupo tu katika
toba bali hasa upo katika fumbo la Pasaka. Pasaka ndiyo kiini cha Mwaka wa
Kanisa; na ndiyo sherehe kubwa kuliko sherehe zote katika liturjia. Ni sherehe
inayoadhimisha ukombozi wa wana wa Mungu kutoka katika utumwa dhambi na
kufanyika kwa taifa jipya la Mungu. Kimsingi, Kwaresima ni kipindi cha siku
arobaini za toba zinayoitayarisha Pasaka. Pasaka huadhimishwa kila mwaka mara
baada ya Kwaresima; na huendelea kuadhimishwa kila jumapili kwa mwaka wote
(Jumapili zote zilizo ndani ya kipindi cha Kwaresima hazihesabiwi kati ya siku
arobaini). Kila jumapili ni Pasaka, ni siku ya Bwana Mfufuka (dominika) ambapo
taifa la Mungu hukusanyika ili kusherehekea ukombozi. Kwa umuhimu wake, Pasaka ya
kila mwaka ni lazima itayarishwe kwa kipindi maalum; yaani Kwaresima. Pasaka na
Kwaresima ni vipindi vinavyotegemezana. Kwaresima ndiyo inayotuandaa ili
tustahili kusherehekea Pasaka.
Nguzo za Kwaresima
Siku arobaini za Kwaresima ni
kielelezo cha utimilifu wa maandalizi ya Pasaka. Kadiri ya desturi za kibiblia,
namba 1, 3, 7, 10, 12, 40 na 50 huitwa namba kamili. 40 ni namba kamili
inayoashiria utimilifu wa kitu fulani. Kwa mfano; Musa alikaa siku arobaini
mlimani sinai akisubiri kupewa Amri Kumi za Mungu, waana wa Israeli walisafiri jangwani
kuelekea nchi ya ahadi kwa miaka arobaini, Yesu alifunga chakula siku arobaini
jangwani kabla ya kuanza kuhubiri Habari Njema, Yesu alipaa mbinguni siku ya
arobaini baada ya ufufuko wake. Matukio hayo na mengine mengi kuhusu namba 40
yanaashiria ukamilifu wa jambo fulani katika umuhimu na umaana wake.
Utimilifu wa siku arobaini za
Kwaresima hujengwa katika nguzo kuu nne: Neno la Mungu, Sala na Sakramenti,
Mfungo, na Matendo Mema.
1) Neno la Mungu: Kipindi cha
Kwaresima ni fursa nzuri ya kujipa muda wa kutosha kwa ajili ya kusoma na
kutafakari Neno la Mungu. Tukisoma Biblia tutamjua zaidi Mungu wetu, tutajijua
sisi wenyewe na hasa tutaijua nia ya Mungu kwetu ili tuweze kuyafanya mapenzi
yake.
2) Sala na Sakramenti: wakati wa
Kwaresima ni vema kusali zaidi sala binafsi na sala za Kanisa ili
kujitakatifuza na kuzibariki shughuli zetu za kila siku. Tushiriki Misa
Takatifu, tushiriki ibada ya Njia ya Msalaba, tushiriki katika jumuiya zetu,
tushiriki sakramenti za Kanisa (hasa Kitubio na Ekaristi Takatifu).
3) Mfungo: Kwaresima ni wakati
muafaka wa kujinyima vitu na mambo ya ziada. Kielelezo kikubwa zaidi ni kufunga
chakula. Maana ya kufunga haiishii tu kwenye chakula bali pia ni kuacha mazoea
mbalimbali yasiyo ya lazima na yasiyofaa. Kujinyima kunatuwezesha kupata fursa
ya kusoma Neno la Mungu, kusali na kufanya matendo mema.
4) Matendo Mema: Kila mmoja wetu
ana shida fulani na anahitaji msaada wa mwenzake. Lakini pia wapo wenzetu
wengine wenye shida zaidi kuliko sisi. Kile nilichojinyima kwa kufunga ndicho
nimpatie mwenye shida zaidi kuliko mimi. Tuwatembelee wafungwa na wanaoishi
katika upweke, tuwatibu wagonjwa, tuwazike wafu, tuwasaidie wazee, yatima na
wajane, tuwashauri na kuwaombea wanaopotoka.
Umuhimu wa Kwaresima
Amri ya pili ya Kanisa inamtaka kila mkristo kushiriki
kipindi cha Kwaresima tangu siku ya kwanza, yaani Jumatano ya Majivu. Toba
ndiyo roho ya Kwaresima iliyojengwa juu ya Neno la Mungu, kusali, kushiriki
sakramenti, kufunga na kufanya matendo mema. Siku arobaini za Kwaresima ni
kielelezo kamili kinachotufundisha kuwa toba ni tendo la kila siku katika
maisha ya mkristo. Wakati wa Kwaresima toba husisitizwa zaidi na kwa namna ya
pekee ili kumjenga mkristo katika wajibu wa kuiishi imani. Katika kuiishi imani
yetu tunapambana na shetani ambaye nia yake ni kuharibu mpango wa Mungu wa
ukombozi. Silaha kubwa ya kupambana na shetani ni kuiishi roho ya toba
inayojikita katika Neno la Mungu, sala na sakramenti, mfungo na matendo mema. Bwana
wetu Yesu Kristo alifunga jangwani kwa siku arobaini kama maandalizi ya kufanya
matendo mema ya kumkomboa mwanadamu.
Kwa siku arobaini alifunga na kusali akamshinda shetani kwa kulitumia
vema Neno la Mungu (Mt. 4:1-11). Kwa
mfano huo wa Yesu, mkristo anatakiwa kuiishi toba wakati huu wa Kwaresima ili astahili
kuishiriki Pasaka. Mkristo anatakiwa kuiishi kwa dhati toba ya kila siku ili amshinde
shetani na hatimaye aingie kwenye Pasaka ya milele mbinguni.Makala haya yameandaliwa na;
Dk. Padri Leonard Maliva Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustimo Stella Maris Mtwara. simu namba 0754666908
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni