Week Hot newz

Oktoba 25,2015 Tanzania tutavuna tulichopanda

Na Paskal Linda    http://batarokota.blogspot.com/

Kweli, aliyekubuhu katika uovu anaweza kumfunda mwana awe malaika? Au mwalimu juha wa mazuzu anaweza kuandaa na kutoa mwanafunzi gwiji? Jambazi anathubutu kumkemea kibaka?
 
Kweli fukara aliyejifahari katika hali yake anaweza kumuongoza mjasiriamali katika umaridadi wa kutafuta neema? 
 
Haya ni baadhi ya maswali wengi tumekuwa tunajiuliza kwa kutafakari mitihani inayotukabili. Maswali kama haya tumeyasikia yakiulizwa kwa namna mbalimbali katika semi, methali na hata vioja vya kisa mkasa. 
 
Uchaguzi huu pia una vioja vyake. Kutokana na uchu wa kusaka kura kuna mambo tunayashuhudia ambayo hakika yanaibua maswali mengi, tena sana.
 
Hivi karibuni mgombewa wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa, ameshutumiwa na hasimu wake kwa kutoa ahadi ambayo inatafsiriwa kuingilia uhuru wa mahakama na kubashiria kuivunja katiba ya nchi. Mgombea huyo, pamoja na mambo mengine, aliahidi kumwachia huru mtu fulani aliyetiwa hatiani na mahakama wapo atachaguliwa kuwa Rais.
 
Naye mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, amekuwa akimwaga ahadi ambazo baadhi zinaelekea kuvunja sheria na haki za wengine. Miongoni mwake ni ahadi ya kunyang’anya watu mali zao au kuwapa wananchi faida ambayo huna mamlaka nayo. 
 
Kwa lugha za wachambuzi ni kwamba wagombea wa aina hii wanakosolewa kwa kutoa, bila haya, ahadi hewa wakati wakitambua fika kuwa unachokisema hatotenda. Hawa ndio aina ya watu waliokomaa kuturubuni watuongoze, sisi wananchi ambao tunasaka bado masihi wa kutuvusha kuelekea kwenye Tanzania tarajiwa, Tanzania yenye neema.
 
 Wapo miongoni mwetu waliohoji ombwe ama uhaba/ukavu wa uongozi nchini Tanzania. Tutakuaje na viongozi bomba kama desturi imekuwa kuongoza kwa njia ambazo ni za kihuni, yaani ambazo hazifikii wala kukidhi viwango vya ustaarabu?
 
Kwani nani asiyejua kuwa ingawa nje Tanzania inajinadi kuwa ni taifa lenye amani, utawala wake ni wa kimabavu? Utawala wake na watawala wake kwa kiwango kikubwa ndio vinara wa kuvuka mipaka katika kutoheshimu sheria, taratibu, haki na hata maadili ya msingi.
 
Waswahili wanasema, unavuna ulichokipanda! Sasa kama sisi tunapanda na kukuza viongozi ambao kimsingi wamesheheni kasoro katika hayo misingi ya uongozi, tutarajie miujiza gani katika aina ya wagombe wanaojitokeza? Labda mfano halisi utasaidia kuakisi kinachosisitizwa hapa.
ajibisha Naibu Waziri yeye kaona namna nzuri ya kumaliza tofauti zilizojitokeza katika mjadala ni
 
Hivyo, tusishangae kuwa miezi michache baadaye mtu huyu huyu alipohisi amehujumiwa au amezidiwa katika pukurushani za kugombania kura alitumia hekima hiyo hiyo ya kupigana katika kupata mradi wake na kumaliza tatizo lililokuwa linamsibu. 
 
Na hilo si tukio adimu au la bahati mbaya. Hata aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge lilopita naye kanaswa katika kanda moja akiwa kaghadhabika na akitembeza mkongojo wake kuwatandika aliokuwa akihitilafiana nao. 
 
Kama ‘viongozi’ hawaoni tabu ‘kuzipiga’ kwa nini tustaajabu pale wafuasi wao, wengi wakiwa vijana nao wakitafutana kufanyiana fujo na kuingiliana maungoni? Kwanini tushangae kama wapo waandishi wanaotumiwa vitisho kutoka wafuasi wa kambi fulani iwapo makala zao zikionekana kuwa hasi kwa mgombea wao? Kwanini tujaribu kuwazuia watu kujieleza hata kwa kuwadhuru?