Week Hot newz

Waangalizi wa ndani na mwenendo wa uchaguzi mkuu


Mwanaharakati, Martina Kabisama.

Katika kipindi cha uchaguzi, vyombo mbalimbali zikiwamo asasi mbalimbali za kiraia hufanya kazi ya uangalizi wa mwenendo wa uchaguzi.
 
Mbali na asasi za ndani, lakini pia waangalizi wa nje, nao hufanya kazi hiyo.
 
Yapo mambo mbalimbali ambayo huangalia katika uchaguzi, ambayo kwa namna moja ama nyingine mwisho wa siku wanapaswa kuwaambia  wananchi nini ambacho wamegundua katika uchaguzi husika.
 
Yapo mambo mbalibali ya kuangalia katika uchaguzi, lakini mojawapo ni namna vyombo husika vinavyosimamia uchaguzi vinavyofanya kazi yake.
 
Mojawapo ni pamoja na kuangalia endapo vyombo hivyo vinatenda haki kwa kila mwanasiasa au chama chochote cha siasa ambacho kimepata sifa ya kushiriki katika uchaguzi.
 
Kadhalika, kama wananchi nao kwa upande wao wanapata haki yao ya kushiriki katika mchakato mzima wa upatikanaji viongozi wao kwa uhuru.
 
Kuangalia vyombo vya usalama navyo kwa upande  wake kama vinatimiza wajibu wake ipasavyo  upande wa usalama, kwa kuhakikisha wanapewa ulinzi, bila kujali ni mwanasiasa marufu ama siyo maarufu,  ni chama  kikubwa au siyo kikubwa.
 
Nyingine ni kuhakikisha watu katika makundi mbalimbali wanapewa nafasi na fursa nzuri ya kushirikishwa  katika mchakato wote wa uchaguzi kuanzia kujiandikisha, kushiriki katika kampeni kwa kupata fursa ya kusikiliza sera kwa wagombea na vyama mbalimbali na kupiga kura.
 
Hapa ni pamoja na makundi ya watu wenye ulemavu wa aina zote.
 
Kazi hii pamoja na wadau wengine, pia inapaswa kufanywa na vyombo vingine kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), vyombo vya usalama, na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa.
 
Miongozni mwa wadau ambao wamepewa mamlaka ya kuangalia mwenendo wa uchaguzi mwaka huu ni pamoja na Muungano wa waangalizi wa uchaguzi nchini (Cemot), ambao wameeleza kujipanua zaidi katika aina yao ya uangalizi.
 
Katika kufamikisha kazi yao hiyo, na kwa kuhakikisha wanaifanya kwa ufanisi, wameamua kuandaa ofisi maalum ambayo itakuwa kituo cha kutoa na kupokea taarifa mbalimbali za kile kinachoendelea katika uchaguzi.
 
Ofisi hiyo itajikita katika kukusanya taarifa mbalimbali  kutoka kwa waangalizi wake ambao wamewatawanya nchi nzima pamoja na kwa wananchi wenyewe ambao watapata fursa ya kutoa taarifa ya jambo lolote ambalo watabaini haliendi sawa au vinginevyo.
 
Mwenyekiti  Mwenza wa Muungano wa asasi hizo, Martina Kabisama, anasema  kituo hicho kitakuwa kinafanya kazi kwa kutoa taarifa kwa mtindo wa kisasa wa teknolojia ya habari (Teknohama)  na kwamba tayari wameandaa vifaa maalum vya kufanyia kazi hiyo.
 
Mbali na hilo, pia wameandaa wataalam wa kuchambua masuala yatakayokuwa yanajitokeza katika uchaguzi na pia kitawapa fursa wananchi kwenda kupata taarifa mbalimbali watakazohitaji.
 
Kabisama anasema waangalizi wa ndani zaidi ya 10,000 wamesambazwa  katika maeneo mbalimbali nchi nzima  kwa ajili ya kuhakikisha wanakusanya taarifa za kila kinachofanyika katika uchaguzi huo.
 
Pamoja na mambo mengine, anasema tathmini ya uchaguzi imeanza tangu mchakato wa kuandikisha wapiga kura kupitia mfumo wa kielektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR).
 
Anasema wanafanya hivyo kwa maslahi ya taifa na Watanzania ili kuhakikisha kila mtu anashiriki katika uchaguzi pasipo kubaguliwa.
 
“Nchi hii ni ya Watanzania wote, hakuna mtu mwenye hati miliki ya taifa hili na ndiyo maana tumeomba na tumepewa nafasi ya kufuatilia uchaguzi kama ambavyo tumekuwa tukifanya miaka mingine,” anasema na kuongeza:
 
“Lengo ni kuhakikisha haki inatendeka na kila mtu anashiriki katika kuchagua kiongozi ambaye anaamini atamletea maendeleo na pia kila chama na mwanasiasa apewe haki yake Kikatiba.”
 
Balozi wa Dernmark nchini, Einar Jensen, anasema hiki ni kipindi muhimu kwa Tanzania na inatakiwa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani ukiwa huru na haki.
 
“Ili uchaguzi ufanyika kwa amani, kitu kinachotakiwa kuzingatiwa ni kuhakikisha unakuwa huru na haki, hayo yote yanatakiwa kuanzia katika kundikishwa kwa kila mtu mwenye haki ya kuandikishwa kupiga kura ahakikishe amepata haki hiyo, haya yote yakizingatiwa ni lazima mvuke salama,” anasema.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni