Week Hot newz

‘Magufuli ni injini ya mabadiliko Tanzania’

INGAWA baadhi ya wanasiasa wanatumia neno mabadiliko kama kaulimbiu katika mikutano ya kampeni za uchaguzi, Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk John Magufuli anaonekana kuwa ndio injini ya mabadiliko ya kweli.

Katika mikutano yote ya Kampeni za kusaka kura za urais, Magufuli anahubiri mabadiliko na kusisitiza nia yake ya kuwa na Tanzania mpya.
Magufuli anataka Tanzania ya viwanda; itakayotokomeza umasikini kwa kutengeneza ajira kutoka asilimia tisa hadi asilimia 40. Hataki kuongoza serikali ambayo inakamua wazalishaji wadogo, kwa kuwatoza ushuru na kodi anazozitaja kuwa ni za hovyo. Anataka kuongoza mabadiliko ambayo yatawezesha mama lishe, wamachinga , wakulima, waendesha pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda, kufanya shughuli zao bila kubughudhiwa.

Ni mgombea ambaye amekuwa akijinadi kwa kutumia kaulimbiu ya ‘Magufuli kwa Mabadiliko’. Katika mikutano ya kampeni kwenye maeneo mbalimbali nchini, amekuwa akiweka bayana anavyochukia ufisadi na mafisadi. Amekuwa akitaja msimamo wake pia namna anavyochukia uzembe na watumishi wazembe , wakiwemo wala rushwa wanaonyonya watu wanyonge.

Magufuli anasema wazi kuwa hana hofu ya kunyimwa kura na kundi hilo la watu.
Isitoshe, anaamini mafisadi na wazembe wanamchukia kwa msimamo wake. Hata hivyo, anaamini, wapo watu wazuri ambao ndiyo wengi ; wanaopenda kupata serikali adilifu na yenye viongozi waadilifu waweze kutendewa haki na kunufaika na matunda ya nchi yao. “Baraza langu la mawaziri litakuwa dogo na lenye watu waadilifu…,” anasema Magufuli.
Ameahidi kuboresha kilimo na kwa kuhakikisha anaongeza thamani ya mazao mbalimbali hatimaye wakulima wanufaike kwa bei nzuri itakayowawezesha kumudu mahitaji yao. “Sizungumzi uongo wala kuwapamba kwa kutaka kura…kazi ya kwanza ya serikali yangu itakuwa kusimamia bei ya tumbaku… kuna makato mengi na wanunuzi wengi wanaringa,” ni kauli aliyoitoa wilayani Sikonge katika mkoa wa Tabora.
Akiwa mkoani Kagera, Magufuli alieleza azma yake ya kuboresha zao la kahawa na kueleza kuwa hakubaliani na hatua ya wananchi kuuza mazao nje ya nchi kwa kuwa kitendo hicho kinadidimiza uchumi wa ndani na kuimarisha wa nchi jirani. Anasema endapo ataingia madarakani atapunguza kodi zilizowekwa kwenye zao la kahawa ambazo zinatajwa idadi yake inafikia 26. Vile vile anaona ujenzi wa viwanda vya kusindika kahawa, ni suluhu nyingine ambayo itawezesha zao hilo kupanda bei.
Pamoja na masuala mengine, anaahidi serikali yake itatoa elimu bure kuanzia Darasa la Kwanza hadi Kidato cha Nne. Kwa ujumla, yako mambo mengi mapya ambayo Magufuli na CCM kwa ujumla, wanaamini yatapatikana katika uongozi wa serikali awamu ya tano. Pamoja na mikakati hiyo, Magufuli anakiri awamu zilizopita chini ya marais wanne, zimefanya kazi nzuri inayomwezesha kuendeleza juhudi za kuwaletea maendeleo makubwa Watanzania.
Miongoni mwa mafanikio ya awamu zilizopita , ni pamoja na kuweka msingi imara wa amani na usalama wa nchi.

Ujenzi wa barabara, usambazaji huduma ya umeme, ujenzi wa zahanati, ni maeneo mengine ambayo mgombea urais huyo wa CCM amekuwa akikiri kwamba umekwenda vizuri kiasi cha kumwekea msingi mzuri wa kuleta mabadiliko makubwa zaidi chini ya serikali yake.
Wakati Magufuli na chama chake wakiamini katika falsafa hiyo ya mabadiliko wapo wanasiasa wanaobeza mabadiliko hayo. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, anasema mabadiliko ndani ya CCM yaliendelea na hatua ya kupeleka chama kwa wananchi. Kupitia Sekretarieti ya CCM, ikiongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, aliyeteuliwa mwaka 2012 kuiongoza, alianza ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya chama.
Katika ziara hiyo iliyodumu miezi 28 kabla ya kuhitimishwa Julai mwaka huu , alibaini mambo yanayokera wananchi kwa ajili ya kuyafanyia kazi. Nape anaweka wazi kwamba, katika kuzungukia nchi nzima, walibaini miongoni mwa kero za wananchi ni rushwa, urasimu serikalini pamoja na dhuluma. Akiwa kwenye mkutano wa kampeni za mgombea urais, Mjini Iringa hivi karibuni, Nape anakiri kwamba, wapo watu wachache walitumia CCM vibaya kutokana na kuiba na kukimbilia kujificha kwenye chama.
“Chama chetu kikaanza kunyooshewa vidole…tukazunguka, tulipomaliza, tukaenda Dodoma tukasema tutafute mtu atakayeleta mabadiliko ya kweli kwenye utendaji wa serikali,” anasema Nape. Kwa mujibu wa Nape, katika orodha ya wagombea, hawakuona mwingine bali Magufuli. “Mabadiliko tunayoyataka ndani ya serikali, mabadiliko tunayoyataka ndani ya CCM, tutayapata kwa Magufuli. Magufuli ni chachu ya mabadiliko tunayoyataka,” Nape anasisitiza.
Baadhi ya wanasiasa wakongwe, wakiwamo Mawaziri wakuu wastaafu, John Malecela na Jaji Joseph Warioba, wanakiri Magufuli ndiye mtu sahihi wa kuleta mabadiliko nchini. Malecela ana imani kwamba CCM aliyoiacha Mwalimu Julius Nyerere bado iko imara na itaendelea kuimarika chini ya uongozi wa Magufuli. Kwa upande wake, Jaji Warioba anasema nchi ina kila sababu ya kumchagua Magufuli kwa kuwa ni mzalendo, anayehubiri amani muda mwingi.
“Wengine wanaona kama ni utani,” anasema Jaji Warioba mjini Dodoma hivi karibuni na kusisitiza kuwa anaamini Magufuli ataunganisha na kuimarisha umoja wa nchi. Jambo lingine linalomshawishi Jaji Warioba kuona Magufuli anafaa na ni chachu ya mabadiliko, ni kutokana na uadilifu na msimamo wake dhidi ya ufisadi. Jaji Warioba anasema, kipindi hiki panahitajika mtu mwadilifu kutokana na ufisadi kuwa tatizo kubwa nchini. “Magufuli ndiye mwenye uwezo huo,” Jaji Warioba anasisitiza.
Katika kudhihirisha nia na msimamo wake wa kuwezesha mabadiliko hayo, Magufuli katika mikutano yake, ameweka bayana kwamba hatakuwa na mchezo na wazembe, wala rushwa na mafisadi. Chini ya falsafa yake ya mabadiliko, Magufuli anachosisitiza ni kazi. Anaunga msimamo wa CCM kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Kinana ambaye baada ya kutembelea nchi nzima, alitoa karipio kwa viongozi wa chama na serikali, akiwataka waachane na kasumba ya kukaa maofisini, badala yake waende kwa wananchi wajue matatizo yao na wayafanyie kazi.
“Mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya tokeni ofisini, achanane na tai, viyoyozi nendeni mkakae na watu wa vijijini hao ndiyo wanaowalipa mishahara,” ni kauli aliyoitoa Kinana mjini Mwanza wakati akihitimisha ziara yake nchi nzima. Katika hotuba yake ya kuhitimisha ziara, Kinana aliweka bayana kwamba lengo ni kuhakikisha CCM inarudi kwenye misingi yake, aliyoiacha Mwalimu Nyerere.
Akionesha namna ambavyo Magufuli ni tunda la mabadiliko ndani ya chama, Nape anasisitiza katika kuhakikisha CCM inarudi kwenye misingi hiyo, tangu awali waliweka msimamo wa kuepuka wagombea wanaonunua uongozi. Hata kabla ya kura ya maoni, Nape akiwa kwenye mkutano wa mwisho mjini Mwanza, aliweka wazi kwamba chama hakikuwa tayari kukubali kupitisha mtu anayenunua uongozi.
Kwa ujumla, hoja iliyopo ni kwamba, pamoja na chama kupitisha mtu anayetarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika nchi, pia chenyewe kimejizatiti kuridhia mageuzi hayo kwa namna tofauti. Njia mojawapo ambayo imeshawekwa bayana, ni CCM kubadilisha mfumo kwa kutoruhusu Waziri Mkuu kuwa mwenyekiti wa wabunge wake katika Bunge ili kuepusha utamaduni uliokuwa umejengeka wa kupitisha kila kinacholetwa na serikali bungeni.