Mfuko
wa Msamaria mwema, unaosimamiwa na Baraza la Kipapa la huduma za
kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya kwa kushirikiana na
Idara ya afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Kampuni ya
Gilead Sciences kutoka Marekani, wamekubaliana kimsingi kusaidia juhudi
za kupambana na ugonjwa wa Ukimwi mkoani Shinyanga, kwa kusaidia juhudi
za kupima virusi vya Ukimwi kwa wananchi 120, 000 pamoja na kuwapatia
dawa za kurefusha maisha wale watakaokuwa wameathirika.
Makubaliano
hayo yamefikiwa Jijini Dar es Salaam, tarehe 11 Februari 2014 katika
Maadhimisho ya Siku ya 22 ya Wagonjwa Duniani. Huu ni mradi wa miaka
mitano kwa ajili ya kupima virusi vya Ukimwi na kutoa dawa za kurefusha
maisha. Ni mradi unaozingatia taaluma, maadili, usafi pamoja na mafunzo
kwa walengwa watakaofaidika na mradi huu, kwa kutoa kipaumbele cha
kwanza kwa watoto yatima.
Mradi huu utaendelea kuongeza nguvu
katika kuwahudumia wagonjwa wa Ukimwi, juhudi zinazofanywa na Jimbo
Katoliki la Shinyanga katika Vituo vya Afya vya: Ngokolo, Bugisi,
Buhangija na Mija. Mradi utatoa ufadhili kwa ajili ya mafunzo ya hali ya
juu kwa wahudumu wa sekta ya afya, ili kuweza kutekeleza wajibu wao
barabara pamoja na kuendelea kujikita katika mapambano dhidi ya Virusi
vya Ukimwi na maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto.
Wananchi
watakaogundulika kuwa na maambukizi ya Ukimwi watapewa dawa za
kurefusha maisha anasema Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la
Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya.
Mradi unapania pamoja na mambo mengine, kudhibiti maambukizi ya virusi
kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto, kama sehemu ya huduma makini
inayotolewa na Kanisa katika kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili,
kama sehemu ya mwendelezo wa agizo la Kristo katika kuwahudumia
wagonjwa.
Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, amemkumbuka kwa namna ya
pekee, Marehemu Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga,
aliyefariki dunia mwezi Novemba 2012. Aliamini kuhusu mafanikio ya mradi
huu katika kuwahudumia watanzania waliokuwa wameathirika kwa ugonjwa wa
Ukimwi. Ni mradi wa pekee, unaojumuisha Mfuko wa Msamaria Mwema, Baraza
la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya
pamoja na Kampuni ya Gilead.
Lengo li kuhakikisha kwamba, Kanisa
Katoliki linashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa
Ukimwi ambao umekuwa ni chanzo cha vifo na upotevu wa nguvu kazi nchini
Tanzania.
Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, yalianzishwa
kunako mwaka 1992 na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, ambaye hapo tarehe
27 Aprili 2014 anatarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu. Siku ya Wagonjwa
Duniani inalenga pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, wagonjwa
wanapata huduma bora pamoja na kuishirikisha Familia ya Mungu katika
huduma kwa wagonjwa, kwani wagonjwa bado wanayo nafasi ya pekee katika
maisha na utume wa Kanisa.
Kanisa linawahamasisha watu wa
kujitolea, ili waweze kuwashirikisha jirani zao upendo, kwa kuwaonjesha
upendo. Kanisa linapania pia kutoa majiundo makini ya kitaaluma na
kimaadili kwa wahudumu wa sekta ya afya.