IMAMU wa Msikiti wa Sawiyatu Qadiria, Hassan Bashir (33) amejeruhiwa vibaya usoni na sehemu ya bega la kushoto baada ya kumwagiwa kimiminika kinachodhaniwa kuwa ni tindikali.
Akizungumza na akiwa kwenye wodi ya wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru anakopatiwa matibabu, imamu huyo alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya kati ya saa 3:30 na saa 4:00 usiku karibu na Msikiti wa Tindiga, uliopo eneo la Unga Ltd.
Alisema ana maumivu makali sehemu ya uso pamoja na bega la upande wa kushoto.
Sheikh huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa shida kutokana na maumivu makali, alisema alikumbwa na mkasa huo muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo na babu yake ambaye pia ni Mwenyekiti wa Msikiti, Ismail Olomi na Mwenyekiti wa Ujenzi, Abdalah Kaduma, juu ya maandalizi ya Maulid yanayotazamiwa kufanyika msikitini hapo.
“Tulipomaliza kuzungumza mimi nikawa
naelekea nyumbani kwangu, jirani na hapo msikitini. Wakati ninatembea nikapita kwenye duka la dawa nikaona kuna mtu kavaa koti jeusi nikamsalimu lakini sijui kama aliitikia.
“Wakati nakaribia kuingia kwenye shule ya Madrasa ambayo iko jirani na nyumbani kwangu, nikahisi kama kuna mtu ananifuata nyuma, ile nageuka tu, nikaona mtu ananiziba uso na kunimwagia kitu usoni na kikopo alichokuwa amekibeba kikadondoka chini na yeye akakimbia.
“Kiasi kidogo cha kimiminika hicho kiliingia mdomoni nikasikia uchachu ndipo nikaanza kusikia maumivu makali usoni na kwenye bega la kushoto nikapiga kelele kuomba msaada kwani nilikuwa nasikia kizunguzungu,” alisema Imamu Bashir huku akitokwa machozi.
Alisema kuwa alisaidiwa na mkewe, Zulfa Said, pamoja na majirani na kuwaonyesha lile kopo ambalo baadaye walilikabidhi polisi.
Imamu huyo anahusisha tukio hilo na ugomvi kati yake na mtu mmoja ambaye jina lake kwa sasa linahifadhiwa, ambaye ni Mwislamu mwenye msimamo mkali.
Alisema mtu huyo mwaka jana aliongoza kundi la vijana kuvamia msikiti mdogo wa babu yake ulioko Sombetini, yeye alikwenda kuwaondoa na tangu wakati huo, mtu huyo akaahidi kulipa kisasi.
Imamu Bashir alisema mbaya wake huyo aliwahi kumjeruhi kijana wake wa madrasa, Saban Yunus na kumshitaki Polisi na shauri lao lilimalizika Desemba mwaka jana kwa mtu huyo kuhukumiwa kifungo cha nje.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa wanamshikilia mtu mmoja ambaye hakumtaja jina.
Alisema kopo lililotumika kubebea kimiminika hicho litapelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa uchunguzi ili kubaini kitu kilichotumika kumdhuru imamu huyo.
Hili ni tukio la pili kutokea jijini hapa. Julai 14, mwaka jana, Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Said Juma Makamba, alijeruhiwa kwa kumwagiwa maji yanayohisiwa kuwa tindikali na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake eneo la Kwa Mromboo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni