
Kadhalika, inakadiriwa pia kuwa zaidi ya watu 35,000 hupata saratani hiyo kila mwaka na zaidi ya watu 27,000 hupoteza maisha huku ripoti ikionyesha mwaka 2010 peke yake, wanawake 6,000 waligundulika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi na 4,000 kati yao walikufa kutokana na maradhi hayo.
Rais Kikwete aliyasema hayo wakati akizungumza
na wakazi wa Mkoa wa Tabora katika uzinduzi wa huduma za uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti.
"Wataalam wanatuambia kuwa, saratani hii huwapata wanawake wa umri wa miaka 30 na 50 na inaongoza kwa asilimia kubwa hapa nchini kwetu ukilinganisha na nchi nyingine Afrika Mashariki ... wanawake wanaoishi na virusi vya Ukimwi wako katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo kwa asilimia 50, pamoja na tatizo hili, bado tuna changamoto ya saratani ya matiti ambayo ni ya pili kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi hapa nchini" alisema na kuongeza:
"Wanawake wako kwenye hatari kubwa ya kufa kwa saratani kuliko wanaume kwa sababu saratani nyinginezo, hazibagui ukiacha ile ya tezi dume inayowapata wanaume pekee, bahati nzuri, saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti zinaweza kutibika ikiwa zitagunduliwa mapema na njia pekee ni kupima mara kwa mara."
Hata hivyo, aliwapongeza na kuwashukuru Mewata kwa kuongeza mwamko na mwitikio mzuri kwa jamii kujitokeza kwa wanawake wengi kupima saratani ya matiti.
"Hatuna budi kuvunja ukimya na kuungana na Madaktari Wanawake kuzungumzia maradhi haya na kuelimishana ili wananchi, wadau na Serikali kwa umoja wetu au mmoja mmoja, tuchukue hatua stahiki za kukabiliana na maradhi haya," alisema.
Alisema lengo la serikali yake ni kutaka kupunguza mzigo mkubwa unaoielemea Hospitali Kuu ya Kansa ya Ocean Road.
Alitoa wito kwa wanawake wa Tabora kujitokeza kwa wingi kufanyiwa uchunguzi wa saratani.
Pia, aliwataka wanaume kujenga mazoea ya kupima afya zao hususan kuhusu saratani ya tezidume (prostate) kwa kuwa ni saratani inayoua wanaume wengi duniani na hapa nchini.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni