Week Hot newz

Rushwa imeshindikana nchini?



Mkurugenzi wa Takukuru, Edward Hoseah.
Ninapenda  sana Takukuru ifanikiwe katika kutokomeza rushwa nchini. Lakini nina uhakika kuwa, haitafanikiwa na nina sababu za kwa nini nasema hivyo.
 
Rushwa sio suala la kupeana fedha chini ya meza, kwa msingi usio wa halali, na kwa mtu asiyestahili; kupeana huduma kwa upendeleo au kwa kutaka kulipwa kitu fulani kwanza; au hutoa huduma kwa misingi ya udugu, familia, mapenzi, ukabila, dini. Lakini rushwa ni matokeo, sio chanzo cha matatizo. 
 
Kama rushwa ni mtoto wa chanzo fulani, basi madhara yanayotokana na rushwa ni mjukuu wa chanzo ambazo TAKUKURU wanatakiwa kukimaizi na kukishughulikia. Lakini kama mnaweza!
 
Niliwahi kuandika kuwa, Rushwa ni mtazamo- a frame! Mtazamo huu umejenga fikra za kiitikadi na kujikita katika fikra za wananchi kiasi kwamba, hatuoni namna ingine ya kuishi ila hiyo ya kutoa rushwa. 
 
Na TAKUKURU wanapokuja na mtazamo kinzani- challenger frame,  kuwa rushwa ni jinai, ni makosa, wanakuta sisi tuko tayari tumeshajikita katika utamaduni wa kutoa rushwa. 
 
Ni sehemu ya maisha, ni mazoea- practice. Na kwa kweli hatuoni kuwa binadamu anaweza kuishi bila kutoa au kupewa rushwa. Na mazoea haya yana msingi wa kihistoria katika uchumi na siasa.
 
Kuna wakati nchi hii, ilikuwa na uchumi mzuri sana. Wakati ule tulisema dola moja ilikuwa sawa na shilingi tano; dala! Noti ya shilingi ishirini ilikuwa ikiitwa pauni; pauni moja ilikuwa sawa na shilingi ishirini. 
 
Nchi hii ilikuwa bora katika uzalishaji wa bidhaa za walaji kutoka viwandani na mashambani. Nchi ilikuwa na viwanda na ajira kwa sisi tuliokuwa tunamaliza masomo haikuwa shida. Nchi ilikuwa na wanasiasa ambao kazi yao ilikuwa ni kufikiria namna gani viwanda, kilimo na huduma vitoe ajira kwa wananchi. 
 
Nakumbuka wakati ambao nikiwa likizo ya masomo niliweza kupata kazi ya muda viwandani. Nakumbuka tulipokuwa tunamaliza masomo yetu tulikuwa tukijaza fomu za kuomba kupelekwa kwenye ajira mbalimbali- CEL Form. Ikaja kufa. Viwanda vilikufa, kilimo kilikufa na sekta ya huduma ikafifia. Nchi ikaharibu uchumi wa viwanda vyake kwa kuruhusu soko lifanye kazi yake. Wanasiasa waliona kuwa kazi ya kufikiri juu ya uchumi sio yao tena bali ya IMF, WB na nchi wahisani. 
 
Sisi sio wa kufikiri tena bali kufikiriwa. Wanasiasa hawakukaa na hawakai kutafuta majibu ya matatizo yetu, bali kuandika bajeti ambayo wafadhili watajiridhisha kuwa tunafaa kukopeshwa au kupewa msaada; kufanya maandiko ya miradi kwa ajili ya ufadhili. 
 
Fedha ikawa inaingia serikalini. Wanasiasa badala ya kufikiria kuziongeza kwa kufanya uwekezaji wa kiserikali- public sector investment, wakaona sasa aliye mjanja na mwenye meno awahi hizo fedha. 
 
Wakakimbilia kununua hisa kwenye viwanda, mashirika, na kununua mapande ya ardhi na kuyalimbikiza. Fedha zilizoingia serikali hazikuwa tena kwa ajili ya kuzizungusha kama mtaji bali kugawana kwa wale wanaojua zilipo na namna ya kuzichota. 
 
Na ajira ikawa sasa kwa undugu, urafiki, mapenzi, ukabila. Ndio tunasikia hayo ya watoto wa vigogo BOT. 
 
Wanasiasa wakaona siasa ndio sekta pekee ya kuiwekea fedha za kutosha- lakini sekta za afya, elimu uzalishaji wa kilimo na viwanda na huduma, hakuna. Nchi ikaanza kushindwa kusafirisha bidhaa nje; tukaanza kuwa waagizaji; ajira na uzalishaji vikapungua, tukaambiwa tuwe wajasirimali kwa ajili ya soko ambalo limejaa bidhaa za nje tayari. 
 
Aidha viongozi wamekuwa sasa ndio wanaolindana sasa. Wote ni wale wale. Kama hakuna utashi wa kisiasa wa kupigana na rushwa kwa maana ya (i) kutooneana aibu, (2) kutafuta majibu ya kuuokoa uchumi unaodorara, (3) kusaidia taasisi za kupambana na rushwa- polisi, Usalama wa Taifa na TAKUKURU, kufanya kazi kwa meno halisi badala ya kutumia ya bandia, mnawezaje kuiondoa rushwa. 
 
Sitaki kuwa mtu mwenye kejeli- cynical, kuhusiana na hili. Huu ndio ukweli niuonao, na niuonavyo. Hatuwezi kupambana na rushwa, nasubiri siku rais aseme sasa imetosha na rushwa ni adui wa haki. 
 
Na atakayesema, uchumi na ukue, atakayesema sasa imetosha. Hayupo na hatapatikana kama wale wanaotoa rushwa ndio wanaoweza kupitishwa kuwa rais Oktoba 2015.