Week Hot newz

Pambano Taifa Stars, Algeria kesho gumzo

PAMBANO la kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka 2018 kati ya timu ya soka ya Tanzania `Taifa Stars’ dhidi ya Algeria, linalotarajiwa kupigwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, limekuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa soka ndani na nje ya nchi. Aidha, idadi kubwa ya mashabiki katika `vijiwe’ vya soka, wameonesha dhamira ya dhati ya kutaka kuiunga mkono Stars. Ujio wa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa Stars wanaochezea klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na pia taarifa za Rais, Dk John Magufuli kuwa atajitokeza kuishangilia timu ya taifa ya Tanzania `Mwanzo Mwisho’, kwa pamoja vimechangia kuongeza hamasa ya mchezo huo.
Samatta na Ulimwengu wametoka kuweka historia ya kuwa wa wanasoka wa kwanza wa Tanzania kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya klabu yao kufanya hivyo mwishoni mwa wiki, huku Samatta akiongeza taji jingine la ufungaji bora.
Aidha, kwa Magufuli, hilo litakuwa pambano lake la kwanza kushuhudia akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu alipoapishwa kuchukua nafasi ya Rais Jakaya Kikwete, mwanamichezo aliyeondoka madarakani baada ya kumaliza muda wake wa uongozi kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Tayari waamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Mali, Keita Mahamadou, Diarra Bala, Niare Drissa Kamory na mwamuzi wa akiba Coulibaly Harouna wameshawasili nchini tangu jana asubuhi, huku mtathimini wa waamuzi Attama Ibrahim Boureima kutoka nchini Niger naye akiwa tayari nchini tangu juzi usiku.