
Rais Dk. John Magufuli, akiwa na Waziri Mkuu mstaafu wa
Kenya, Raila Odinga, katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria Parokia ya
Chato mkoani Geita jana. PICHA: IKULU
Rais Magufuli ambaye jana alishiriki ibada ya asubuhi katika kanisa
hilo akiwa na Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga, aliahidi
kuchangia Sh. milioni 10 kwa ajili ya upanuzi wa Kanisa.
Baada ya ibada hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson
Msingwa, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema fedha alizoahidi
Rais aliposali misa ya kwanza, zimekabidhiwa kanisani hapo wakati wa
misa ya pili na Naibu Mnikulu, Ngusa Samike.
MAGUFULI KANISANI
Wakati wa misa ya asubuhi, Paroko wa kanisa hilo, Padri Mlinganisha
Mwilinde, alimtaka Rais Magufuli kuwasalimia waumini wenzake kwani
tangu alipochaguliwa mwaka jana kuwa Rais, hakuwa amekutana nao.
Alipokuwa akisalimia, Rais Magufuli alisema: "Nimesikia kwenye
matangazo kuwa mnahitaji kukamilisha ujenzi wa kanisa hili…na mimi
niwaahidi kuwa nitatoa Shilingi milioni 10…hizi nina uhakika nazo
nikirudi Dar es Salaam, nitazituma…tena nitaziwahisha ili ikiwezekana
ndani ya wiki moja ziwe zimefika," alisema Rais Magufuli na kuongeza:
"Ila niwape tahadhari. Fedha hizo zitumike vizuri na nitafuatilia
ili kujua zimefanya nini, vinginevyo nitawatumbua humu ndani ya
Kanisa."
"Lazima na mimi nichangie maana hapa ni kwetu na hata nikifa
nitaletwa kuzikwa Chato…hata wakati nikiwa mdogo, nilikuwa mtumikiaji
hapa hapa kanisani," alisema.
Awali, aliwataka waumini wote kushikamana na kuacha kutengana na
kubaguana kutokana na itikadi za kisiasa, ukabila na dini kwani wote ni
Watanzania na wajikite kudumisha amani, upendo na mshikamano.
Hata hivyo, alimwelezea Odinga pamoja na familia yake kuwa ni
marafiki wake wa karibu na kwamba amewahi kuja Chato kumsalimia awamu
mbili ikiwamo wakati wa mazishi ya baba yake, marehemu Joseph Magufuli.
"Baba Paroko, kama utaniruhusu niombe pia kumtambulisha rafiki
yangu kwelikweli aliyelazimika kutoka Kenya kuja Tanzania baada ya
kusikia nipo nyumbani kwetu Chato.
Ni rafiki yangu wa ukweli kwani urafiki haujali nchi, kabila, chama
wala rangi ya mtu…amekuja jana kunisalimia na yeye amelala kijijini
kwetu Rubambangwe," alisema na kuongeza:
"Huyu rafiki yangu amekuwa mtu wangu wa karibu sana…amenisaidia
mambo mengi…kwa kuwa leo tupo hapa Chato, naomba na yeye mumuone kwani
ni mtoto wenu."
ODINGA
Akizungumza na waumini waliokuwa kanisani hapo, Odinga aliweka
wazi siri ya ukaribu wake na Tanzania, akisema alikwenda kusoma nje ya
nchi yake baada ya kutumia hati ya kusafiria ya Tanganyika.
Odinga aliyekuwa ameongozana na mkewe pamoja na binti yao, Winny
Odinga, alisema hatua hiyo ilitokana na uhusiano mwema kati ya Baba wa
Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na baba yake (Odinga), Jaramogi
Odinga.
"Wakati nikiwa mdogo na Kenya ikiwa bado inatawaliwa na wakoloni,
Baba yangu alitaka niende ng'ambo, lakini wakoloni hao waligoma kabisa
kunipa passport (hati ya kusafiria)… kilichofuata baba yangu Jaramogi,
alinituma Tanzania nikaja kuonana na Mwalimu Nyerere ambaye ndiye
aliyenipa passport ya Tanganyika nikafanikiwa kwenda ng'ambo," alisema
na kuongeza:
"Kwa mantiki hiyo, unaweza kuona mimi nilivyo ndugu yenu…kikubwa
ninachoweza kusema hapa ambacho pia padri alikikazia, ni kukuomba Rais
Magufuli umwombe Mungu akupe hekima kama mtumishi wa Mungu Selemani
alivyochagua."
"Kungoza taifa ni kazi ngumu na kwamba katika nafasi yako utakutana
na majaribu mengi kama aliyokutana nayo Yesu kule mlima wa
Yeliko…lakini inapotokea; sema toka shetani," alisema Odinga.
Ondinga ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu na mpinzani wa karibu wa Rais
Uhuru Kenyatta, anatajwa kuwa atawania nafasi ya urais wa nchi hiyo
mwakani.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni