NA MWANDISHI WETU, MWANZA
AZAM FC wameshindwa kuibuka na ushindi katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na wenyeji Toto Africans katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Toto Africans wanaodaiwa kuwa na udugu na Yanga, wametibua mbio za Azam FC za kuwania ubingwa wa ligi hiyo baada ya kuwazuia kuondoka na pointi tatu muhimu katika mchezo huo wa kiporo.
Kwa matokeo hayo, Azam FC imefikisha pointi 51 wakiwa nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 53 huku vinara wa ligi hiyo, Simba wakiendelea kuwa kileleni kwa pointi 57.
Katika mchezo huo wa jana, Azam FC walipata bao kupitia kwa John Bocco dakika ya 23 baada ya kuunganisha pasi safi ya Khamis Mcha.
Toto Africans walisawazisha bao hilo dakika ya 40 kupitia kwa Waziri Juma, matokeo ambayo yalidumu hadi dakika tisini.
Michezo mingine ya ligi hiyo, Stand United iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, mabao yao yakifungwa na Elius Maguli na Vitalis Mayanga. Katika Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, JKT Ruvu wamefanikiwa kuididimiza African Sports ya jijini Tanga bao 1-0, likifungwa na Musa Kiumbu ambaye baadaye alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mchezaji wa Sports.
Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, wenyeji Ndanda FC wamegawana pointi na Tanzania Prisons kutoka Mbeya, baada ya kutoka suluhu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni