Na: Paskal LindaKardinali
Mauro Piacenza, mhudumu mkuu wa Toba katika barua yake kwa mapadre
waungamishaji anasema kwamba, kila mara Mkristo anapoungama dhambi zake
na kupokea msamaha, huruma na upendo wa Mungu kutoka kwenye kiti cha
maungamo, kwa Mkristo hii ni Pentekoste Mpya! Siku kuu ya Pentekoste,
ili ni fursa kwa waamini kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao,
ili kuweza kumpokea vyema Roho Mtakatifu anayemiminwa mioyoni mwao,
tayari kumtolea Mwenyezi Mungu ushuhuda wa maisha adili na matakatifu!
Neema
ya Sakramenti ya Upatanisho anasema Kardinali Piacenza ni mang'amuzi
mapya ya Pentekoste kwani hapa Roho Mtakatifu anaendelea kulitakasa
Kanisa la Kristo kwa njia ya huduma ya maungamo inayotolewa na Padre
akiwa ameungana na Yesu Kristo, ili kusikiliza na kupima, kuamua na
kutoa ushauri na hatimaye, kuponya dhambi kwa kumwondolea mwamini dhambi
zake. Hii ni kazi ya Roho Mtakatifu anayetenda kwa njia ya wachungaji
wake wanaojisadaka katika viti vya maungamano.
Mapadre
wanakumbushwa kwamba, wamechaguliwa na kuwekwa wakfu kwa ajili ya
kuwahudumia watu wa Mungu si kwa mastahili yao wenyewe bali kwa njia ya
neema ya Roho Mtakatifu inayowaunganisha kwa dhati kabisa na Kristo
mwenyewe, ili kushiriki upendo na kazi yake ya ukombozi. Kwa sababu hii,
Padre ni mhudumu wa huruma ya Mungu na daraja kati ya waungamaji na
Kristo mwenyewe.
Mapadre wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa
wasikivu kwa Roho Mtakatifu na karama zake zinazoliwezesha Kanisa
kujitakasa na kuwatakatifuza watoto wake kwa njia ya Sakramenti ya
Upatanisho!