Beki wa Kati wa Yanga na timu ya taifa (Taifa
Stars), Kelvin Yondani, ameongeza mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo
ya Jangwani kabla ya kukwea pipa na kuelekea Nairobi, Kenya kushiriki
michuano ya Kombe la Chalenji ya kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza muda mfupi baada ya hafla ya kuiaga Taifa Stars jijini Dar es Salaam jana, Yondani alisema kwa kifupi: "Nilisaini mkataba mpya juzi (Jumamosi)".
Juni mwakani, Yondani alikuwa anamaliza mkataba wake wa awali wa miaka miwili na Yanga uliozua 'balaa' akitokea kwa watani wao wa jadi, Simba.
Kwa mkataba huo mpya unaoanza Juni mwakani, Yondani, Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, ataitumikia Yanga hadi Juni 2016.
Hata hivyo, alipotafutwa na mwandishi kuthibitisha taarifa za mkataba mpya wa nyota huyo, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema bado hajapewa taarifa na uongozi kuhusu suala hilo.
Simu ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mashindano ya klabu hiyo, Abdallah Bin Kleb iliita bila kupokelewa jana alipotafutwa kuzungumzia usajili huo.
Nahodha mpya Stars
Katika hatua nyingine, Kocha wa Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen jana alimteua Yondani kuwa nahodha wa timu hiyo baada ya kutemwa kwa aliyekuwa nahodha, kipa Juma Kaseja.
Pouslen alimtambulisha Yondan kuwa nahodha mpya wa timu hiyo, anayechukua nafasi ya Kaseja aliyeachwa kwenye kikosi hicho kilichoondoka nchini jana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni