
Mwanaharakati, Martina Kabisama.
Katika kipindi cha uchaguzi, vyombo mbalimbali zikiwamo asasi mbalimbali za kiraia hufanya kazi ya uangalizi wa mwenendo wa uchaguzi.
Mbali na asasi za ndani, lakini pia waangalizi wa nje, nao hufanya kazi hiyo.
Yapo mambo mbalimbali ambayo huangalia katika uchaguzi, ambayo kwa
namna moja ama nyingine mwisho wa siku wanapaswa kuwaambia wananchi
nini ambacho wamegundua katika uchaguzi husika.
Yapo mambo mbalibali ya kuangalia katika uchaguzi, lakini mojawapo
ni namna vyombo husika vinavyosimamia uchaguzi vinavyofanya kazi yake.
Mojawapo ni pamoja na kuangalia endapo vyombo hivyo vinatenda haki
kwa kila mwanasiasa au chama chochote cha siasa ambacho kimepata sifa ya
kushiriki katika uchaguzi.
Kadhalika, kama wananchi nao kwa upande wao wanapata haki yao ya
kushiriki katika mchakato mzima wa upatikanaji viongozi wao kwa uhuru.
Kuangalia vyombo vya usalama navyo kwa upande wake kama vinatimiza
wajibu wake ipasavyo upande wa usalama, kwa kuhakikisha wanapewa
ulinzi, bila kujali ni mwanasiasa marufu ama siyo maarufu, ni chama
kikubwa au siyo kikubwa.
Nyingine ni kuhakikisha watu katika makundi mbalimbali wanapewa
nafasi na fursa nzuri ya kushirikishwa katika mchakato wote wa uchaguzi
kuanzia kujiandikisha, kushiriki katika kampeni kwa kupata fursa ya
kusikiliza sera kwa wagombea na vyama mbalimbali na kupiga kura.
Hapa ni pamoja na makundi ya watu wenye ulemavu wa aina zote.
Kazi hii pamoja na wadau wengine, pia inapaswa kufanywa na vyombo
vingine kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), vyombo vya usalama, na
Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa.
Miongozni mwa wadau ambao wamepewa mamlaka ya kuangalia mwenendo wa
uchaguzi mwaka huu ni pamoja na Muungano wa waangalizi wa uchaguzi
nchini (Cemot), ambao wameeleza kujipanua zaidi katika aina yao ya
uangalizi.
Katika kufamikisha kazi yao hiyo, na kwa kuhakikisha wanaifanya kwa
ufanisi, wameamua kuandaa ofisi maalum ambayo itakuwa kituo cha kutoa
na kupokea taarifa mbalimbali za kile kinachoendelea katika uchaguzi.
Ofisi hiyo itajikita katika kukusanya taarifa mbalimbali kutoka
kwa waangalizi wake ambao wamewatawanya nchi nzima pamoja na kwa
wananchi wenyewe ambao watapata fursa ya kutoa taarifa ya jambo lolote
ambalo watabaini haliendi sawa au vinginevyo.
Mwenyekiti Mwenza wa Muungano wa asasi hizo, Martina Kabisama,
anasema kituo hicho kitakuwa kinafanya kazi kwa kutoa taarifa kwa
mtindo wa kisasa wa teknolojia ya habari (Teknohama) na kwamba tayari
wameandaa vifaa maalum vya kufanyia kazi hiyo.
Mbali na hilo, pia wameandaa wataalam wa kuchambua masuala
yatakayokuwa yanajitokeza katika uchaguzi na pia kitawapa fursa wananchi
kwenda kupata taarifa mbalimbali watakazohitaji.
Kabisama anasema waangalizi wa ndani zaidi ya 10,000 wamesambazwa
katika maeneo mbalimbali nchi nzima kwa ajili ya kuhakikisha
wanakusanya taarifa za kila kinachofanyika katika uchaguzi huo.
Pamoja na mambo mengine, anasema tathmini ya uchaguzi imeanza tangu
mchakato wa kuandikisha wapiga kura kupitia mfumo wa kielektroniki wa
Biometric Voters Registration (BVR).
Anasema wanafanya hivyo kwa maslahi ya taifa na Watanzania ili
kuhakikisha kila mtu anashiriki katika uchaguzi pasipo kubaguliwa.
“Nchi hii ni ya Watanzania wote, hakuna mtu mwenye hati miliki ya
taifa hili na ndiyo maana tumeomba na tumepewa nafasi ya kufuatilia
uchaguzi kama ambavyo tumekuwa tukifanya miaka mingine,” anasema na
kuongeza:
“Lengo ni kuhakikisha haki inatendeka na kila mtu anashiriki katika
kuchagua kiongozi ambaye anaamini atamletea maendeleo na pia kila chama
na mwanasiasa apewe haki yake Kikatiba.”
Balozi wa Dernmark nchini, Einar Jensen, anasema hiki ni kipindi
muhimu kwa Tanzania na inatakiwa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa
amani ukiwa huru na haki.
“Ili uchaguzi ufanyika kwa amani, kitu kinachotakiwa kuzingatiwa ni
kuhakikisha unakuwa huru na haki, hayo yote yanatakiwa kuanzia katika
kundikishwa kwa kila mtu mwenye haki ya kuandikishwa kupiga kura
ahakikishe amepata haki hiyo, haya yote yakizingatiwa ni lazima mvuke
salama,” anasema.
CHANZO:
NIPASHE