INGAWA baadhi ya wanasiasa wanatumia neno mabadiliko kama kaulimbiu
katika mikutano ya kampeni za uchaguzi, Mgombea Urais kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk John Magufuli anaonekana kuwa ndio injini
ya mabadiliko ya kweli.
Katika mikutano yote ya Kampeni za kusaka kura
za urais, Magufuli anahubiri mabadiliko na kusisitiza nia yake ya kuwa
na Tanzania mpya.
Magufuli anataka Tanzania ya viwanda; itakayotokomeza umasikini kwa
kutengeneza ajira kutoka asilimia tisa hadi asilimia 40. Hataki kuongoza
serikali ambayo inakamua wazalishaji wadogo, kwa kuwatoza ushuru na
kodi anazozitaja kuwa ni za hovyo. Anataka kuongoza mabadiliko ambayo
yatawezesha mama lishe, wamachinga , wakulima, waendesha pikipiki za
abiria maarufu kama bodaboda, kufanya shughuli zao bila kubughudhiwa.
Ni mgombea ambaye amekuwa akijinadi kwa kutumia kaulimbiu ya
‘Magufuli kwa Mabadiliko’. Katika mikutano ya kampeni kwenye maeneo
mbalimbali nchini, amekuwa akiweka bayana anavyochukia ufisadi na
mafisadi. Amekuwa akitaja msimamo wake pia namna anavyochukia uzembe na
watumishi wazembe , wakiwemo wala rushwa wanaonyonya watu wanyonge.
Magufuli anasema wazi kuwa hana hofu ya kunyimwa kura na kundi hilo la
watu.
Isitoshe, anaamini mafisadi na wazembe wanamchukia kwa msimamo wake.
Hata hivyo, anaamini, wapo watu wazuri ambao ndiyo wengi ; wanaopenda
kupata serikali adilifu na yenye viongozi waadilifu waweze kutendewa
haki na kunufaika na matunda ya nchi yao. “Baraza langu la mawaziri
litakuwa dogo na lenye watu waadilifu…,” anasema Magufuli.
Ameahidi kuboresha kilimo na kwa kuhakikisha anaongeza thamani ya
mazao mbalimbali hatimaye wakulima wanufaike kwa bei nzuri
itakayowawezesha kumudu mahitaji yao. “Sizungumzi uongo wala kuwapamba
kwa kutaka kura…kazi ya kwanza ya serikali yangu itakuwa kusimamia bei
ya tumbaku… kuna makato mengi na wanunuzi wengi wanaringa,” ni kauli
aliyoitoa wilayani Sikonge katika mkoa wa Tabora.
Akiwa mkoani Kagera, Magufuli alieleza azma yake ya kuboresha zao la
kahawa na kueleza kuwa hakubaliani na hatua ya wananchi kuuza mazao nje
ya nchi kwa kuwa kitendo hicho kinadidimiza uchumi wa ndani na
kuimarisha wa nchi jirani. Anasema endapo ataingia madarakani atapunguza
kodi zilizowekwa kwenye zao la kahawa ambazo zinatajwa idadi yake
inafikia 26. Vile vile anaona ujenzi wa viwanda vya kusindika kahawa, ni
suluhu nyingine ambayo itawezesha zao hilo kupanda bei.
Pamoja na masuala mengine, anaahidi serikali yake itatoa elimu bure
kuanzia Darasa la Kwanza hadi Kidato cha Nne. Kwa ujumla, yako mambo
mengi mapya ambayo Magufuli na CCM kwa ujumla, wanaamini yatapatikana
katika uongozi wa serikali awamu ya tano. Pamoja na mikakati hiyo,
Magufuli anakiri awamu zilizopita chini ya marais wanne, zimefanya kazi
nzuri inayomwezesha kuendeleza juhudi za kuwaletea maendeleo makubwa
Watanzania.
Miongoni mwa mafanikio ya awamu zilizopita , ni pamoja na kuweka
msingi imara wa amani na usalama wa nchi.
Ujenzi wa barabara, usambazaji
huduma ya umeme, ujenzi wa zahanati, ni maeneo mengine ambayo mgombea
urais huyo wa CCM amekuwa akikiri kwamba umekwenda vizuri kiasi cha
kumwekea msingi mzuri wa kuleta mabadiliko makubwa zaidi chini ya
serikali yake.
Wakati Magufuli na chama chake wakiamini katika falsafa hiyo ya
mabadiliko wapo wanasiasa wanaobeza mabadiliko hayo. Katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, anasema mabadiliko ndani ya CCM
yaliendelea na hatua ya kupeleka chama kwa wananchi. Kupitia
Sekretarieti ya CCM, ikiongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana,
aliyeteuliwa mwaka 2012 kuiongoza, alianza ziara ya kukagua utekelezaji
wa ilani ya chama.
Katika ziara hiyo iliyodumu miezi 28 kabla ya kuhitimishwa Julai
mwaka huu , alibaini mambo yanayokera wananchi kwa ajili ya kuyafanyia
kazi. Nape anaweka wazi kwamba, katika kuzungukia nchi nzima, walibaini
miongoni mwa kero za wananchi ni rushwa, urasimu serikalini pamoja na
dhuluma. Akiwa kwenye mkutano wa kampeni za mgombea urais, Mjini Iringa
hivi karibuni, Nape anakiri kwamba, wapo watu wachache walitumia CCM
vibaya kutokana na kuiba na kukimbilia kujificha kwenye chama.
“Chama chetu kikaanza kunyooshewa vidole…tukazunguka, tulipomaliza,
tukaenda Dodoma tukasema tutafute mtu atakayeleta mabadiliko ya kweli
kwenye utendaji wa serikali,” anasema Nape. Kwa mujibu wa Nape, katika
orodha ya wagombea, hawakuona mwingine bali Magufuli. “Mabadiliko
tunayoyataka ndani ya serikali, mabadiliko tunayoyataka ndani ya CCM,
tutayapata kwa Magufuli. Magufuli ni chachu ya mabadiliko tunayoyataka,”
Nape anasisitiza.
Baadhi ya wanasiasa wakongwe, wakiwamo Mawaziri wakuu wastaafu, John
Malecela na Jaji Joseph Warioba, wanakiri Magufuli ndiye mtu sahihi wa
kuleta mabadiliko nchini. Malecela ana imani kwamba CCM aliyoiacha
Mwalimu Julius Nyerere bado iko imara na itaendelea kuimarika chini ya
uongozi wa Magufuli. Kwa upande wake, Jaji Warioba anasema nchi ina kila
sababu ya kumchagua Magufuli kwa kuwa ni mzalendo, anayehubiri amani
muda mwingi.
“Wengine wanaona kama ni utani,” anasema Jaji Warioba mjini Dodoma
hivi karibuni na kusisitiza kuwa anaamini Magufuli ataunganisha na
kuimarisha umoja wa nchi. Jambo lingine linalomshawishi Jaji Warioba
kuona Magufuli anafaa na ni chachu ya mabadiliko, ni kutokana na
uadilifu na msimamo wake dhidi ya ufisadi. Jaji Warioba anasema, kipindi
hiki panahitajika mtu mwadilifu kutokana na ufisadi kuwa tatizo kubwa
nchini. “Magufuli ndiye mwenye uwezo huo,” Jaji Warioba anasisitiza.
Katika kudhihirisha nia na msimamo wake wa kuwezesha mabadiliko hayo,
Magufuli katika mikutano yake, ameweka bayana kwamba hatakuwa na mchezo
na wazembe, wala rushwa na mafisadi. Chini ya falsafa yake ya
mabadiliko, Magufuli anachosisitiza ni kazi. Anaunga msimamo wa CCM
kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Kinana ambaye baada ya kutembelea nchi
nzima, alitoa karipio kwa viongozi wa chama na serikali, akiwataka
waachane na kasumba ya kukaa maofisini, badala yake waende kwa wananchi
wajue matatizo yao na wayafanyie kazi.
“Mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya tokeni ofisini, achanane na tai,
viyoyozi nendeni mkakae na watu wa vijijini hao ndiyo wanaowalipa
mishahara,” ni kauli aliyoitoa Kinana mjini Mwanza wakati akihitimisha
ziara yake nchi nzima. Katika hotuba yake ya kuhitimisha ziara, Kinana
aliweka bayana kwamba lengo ni kuhakikisha CCM inarudi kwenye misingi
yake, aliyoiacha Mwalimu Nyerere.
Akionesha namna ambavyo Magufuli ni tunda la mabadiliko ndani ya
chama, Nape anasisitiza katika kuhakikisha CCM inarudi kwenye misingi
hiyo, tangu awali waliweka msimamo wa kuepuka wagombea wanaonunua
uongozi. Hata kabla ya kura ya maoni, Nape akiwa kwenye mkutano wa
mwisho mjini Mwanza, aliweka wazi kwamba chama hakikuwa tayari kukubali
kupitisha mtu anayenunua uongozi.
Kwa ujumla, hoja iliyopo ni kwamba, pamoja na chama kupitisha mtu
anayetarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika nchi, pia chenyewe
kimejizatiti kuridhia mageuzi hayo kwa namna tofauti. Njia mojawapo
ambayo imeshawekwa bayana, ni CCM kubadilisha mfumo kwa kutoruhusu
Waziri Mkuu kuwa mwenyekiti wa wabunge wake katika Bunge ili kuepusha
utamaduni uliokuwa umejengeka wa kupitisha kila kinacholetwa na serikali
bungeni.