
Mechi kati ya Stars na Cranes ambao ndio mabingwa watetezi, inafananishwa na fainali kutokana na upinzani wa timu hizo. Itachezwa saa 8:00 mchana kisha kufuatiwa na mchezo mwingine wa hatua hiyo saa 10:00 jioni kati ya wenyeji Kenya ‘Harambee Stars’ na Rwanda.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen, alisema ana imani ya kufanya vema kutokana na ubora wa kikosi chake, hasa baada ya kuwasili kwa nyota wa kimataifa, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Poulsen alisema siku mbili tangu walipotoka kucheza na Burundi, amehakikisha anarekebisha matatizo aliyoyaona katika mchezo huo, hasa safu ya ulinzi ambayo ilionekana kulegalega.
Naye kipa wa Stars, Ivo Mapunda, alisema hakuna timu ambayo wanaihofia katika michuano hiyo, bali cha muhimu ni dakika 90 za uwanjani ndizo zitaamua nani anasonga mbele na nani anafungasha virago.
Alisema ana imani kubwa ya kufanya vema katika mchezo wa leo, huku akiwataka wachezaji wenzake kutulia na kucheza mpira, kwani kuwafunga Uganda kuko pale pale ila cha muhimu Watanzania ni dua zao.
“Unajua hakuna mtu aliyetegemea kama tutafika hapa tulipo sasa, hivyo basi kwanini mbele tushindwe? Uganda ni timu ya kawaida tu kama timu nyingine, nina imani tutashinda,” alisema Mapunda.
Naye Kocha wa Uganda, Milutin Micho aliyewahi kuifundisha Yanga, alisema anauhofia mchezo wa leo, baada ya kuwaona Samatta na Ulimwengu wakiwemo katika kikosi cha Kili Stars.
Micho alisema lolote linaweza kutokea katika mchezo huo, cha muhimu ni kusubiri dakika 90 za mwamuzi uwanjani ila Tanzania ni timu nzuri.
“Mechi hiyo itakuwa ngumu, kwa kuwa nimefuatilia mechi za Tanzania, ni wazuri, lakini vijana wangu pia watapambana ili kuhakikisha wanashinda,” alisema Micho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni