
Papa akipokewa na Rais Obama mara baada ya kutua katika uwanja wa Kijeshi wa Marekani akitokea Cuba - EPA
Akipita katika anga za nchi, kwa njia ya telegramu alipeleka salaam zake za matashi mema kwa wakuu wa nchi akianzia Rais Raul Castro Ruz, akisema “wakati naondoka katika taifa pendwa la Cuba, napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwako wewe na watu wote wa Cuba kwa mapokezi mazuri mliyonipatia. Nami nawaombea Baraka za Mwenyezi Mungu, kwenu nyote na ninawahakikishia maombi yangu kwa ajili ya amani na ustawi wenu nyote”.
Aidha Papa akipita katika anga la nchi ya Bahamas, alipeleka salaam zake kwa Mheshimiwa Rais Marguerite Pindling, Gavana na Mkuu wa Jumuiya ya Visiwa vya Bahamas , akisema, “Kwa mara ingine ninapopita katika taifa lako, napenda kurudia kutoa matashi mema kwako wewe na kwa wananchi wa nchi hii , nikiwaombea Baraka za Mwenyezi Mungu kwa Bahama yote”.
Baba Mtakatifu alitua katika uwanja wa ndege wa Kijeshi wa Andrews wa Mjini Washington D.C majira ya saa kumi kwa saa za Marekani , ambako alipokelewa na Rais Obama akiwa ameandamana na familia yake, mkewe na watoto, wakiwepo pia viongozi wengine wa Kiserikali na Kanisa. Wachambuzi wanasema, hi ilikuwa ni mara ya kwanza katika urais wake, Obama kumpokea uwanjani Rais wa Nchi anayetembelea Marekani. Kwa kawaida hukutana na wageni muhimu wanaomtembelea katika jengo la Ikulu. Na pia hii ilikuwa ni mara ya kwanza nje ya , itifaki iliyozoeleka, kwa Makamu wa Rais kuwa familia yake uwanjani kukaribisha mgeni.
Na pia ni tukio la kukumbukwa kwamba, Rais George W. Bush na Laura Bush pia walisafiri hadi uwanjani hapo kwa ajili ya kusalimiana na Papa Francisko, wakikumbuka pia tukio la Mstaafu Papa Benedict XVI alipotembelea nchini Marekani mwaka 2008.
Hii ni mara ya pili kwa Papa Francisko, kukutana na Rais Obama ambaye kwa mara ya kwanza, walikutana Vatican Machi 2014.
Katika muda wa siku sita za kuwa Marekani, Papa Francisko kati ya matukio makuu, itakuwa ni pamoja na kutembelea Ikulu ya Marekani- kuongoza Ibada ya Misa na ikiwemo ile kumtaja katika daraja la Watakatifu Mwenye Heri Padre Junipero Serra na Ibada za masifu ya jioni , kukutana na Kutembelea Congress ya Marekani mjini Washington D.C , Kutembelea Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na Ground Zero New York na kushiriki katika Mkutano wa Dunia wa Familia huko Philadelphia. Papa atakamilisha ziara hii Marekani siku ya Jumapili 27 Septemba 2015