Mfumo mpya wa kutumia usajili wa leseni za biashara kwa kutunia mtandao, ambao ulizinduliwa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Rais Jakaya Kikwete, jijini Dar es Salaam juzi, utawawezesha wafanyabiashara kupata leseni za biashara kwa haraka zaidi katika maeneo yao na kukamilisha malipo ya ada kwa njia ya mtandao.
Huo ni mfumo mpya wa usajili wa wafanyabiashara kwa njia ya mtandao, ambao unalenga kuondoa urasimu na kuboresha mazingira ya kibiashara kwa Watanzania.
Kutokana na mfumo huo, inatarajiwa kuwa utapunguza pia msongamano wa wafanyabiashara wanaoenda kujiandikisha ili kupata leseni na kuzilipia katika taasisi husika.
Idadi kubwa ya wananchi hujipatia riziki zao kutokana na kufanya biashara, wakati huo huo Serikali nayo hutoza kodi kwa kila biashara inayofanywa, na sehemu kubwa ya mapato ya serikali hutokana na kodi mbalimbali zikiwemo za wafanyabiashara.
Ni dhahiri kwamba kutokana na uzinduzi huo, mfumo huu sasa umewarahizishia usajili wafanyabiashara, na wengi wao wataamua kujisajili kisheria ili kuepukana na kufanya biashara bila kusajiliwa suala ambalo ni kinyume na sheria za nchi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Frank Kanyusi, alisema mfumo huo pia utapunguza vitendo vya rushwa vinavyowahusisha wafanyabiashara na watendaji wa Brela.
Kwa mfumo huu, tunaamini kuwa urasimu utakaokuwa umepungua utawezesha TRA na TIC kutopata usumbufu wa kumfuata mfanyabiashara tena, badala yake mfanyabiashara atalipa stahiki zote kwa mara moja na wao wataweza kugawana.
Wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema TNBC ilifanya mkutano ili kujadili utekelezaji wa maazimio ya kuwashirikisha wananchi kwenye mambo ya kiuchumi, kuboresha mazingira ya biashara na kuangalia namna ya kukuza utalii.
Balozi Sefue alisema mkutano huo ulizingatia namna ya kuunganisha taasisi zote zinazohudumia wafanyabiashara ili kuwaondolea usumbufu wa aina yoyote.
Ni imani yetu kuwa hatua hizo, za kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara kupata leseni zao bila urasimu, itakuwa chachu kubwa kwa walengwa wengine kujisajili kwa wingi na kufanya biashara kwa uhuru bila kukwepa kwepa mamlaka husika kama ilivyokuwa huko nyuma.
Ni dhahiri kwamba ili serikali itekeleze kwa ufanisi malengo na mipango ya maendeleo, ni lazima ikusanye kodi kutoka vyanzo mbalimbali, wafanyabiashara ni wadau wakubwa wa kuiwezesha serikali kiuchumi kupitia kodi zao.
Tunaipongeza serikali kwa hatua hiyo muhimu ya maboresho ya uchumi na maendeleo ya wafanyabiashara nchini, tunaamini kuwa kutakuwepo na mwitikio mkubwa kwa wafanyabiashara kujisajili na kufanya malipo yao kwa njia ya dijitali badala ya usumbufu wa kufuatilia huko Brela.
Katibu Mkuu wa TNBC, Raymond Mbilinyi pia alisema yapo mafanikio makubwa ambayo yatarahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini, aliyataja kuwa ni pamoja na kitengo cha kushughulikia uwekezaji wa wazawa.
Mbilinyi alisema kitengo hicho kinatarajiwa kuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo eneo jingine alisema ni namna ya kuainisha sheria ili iwe rahisi kwa mfanyabiashara kujua ni ipi itamsaidia kufanya biashara kwa faida.
Mfumo huu wa usajili wa kampuni kwa kutumia mtandao umebuniwa na kutengenezwa na vijana wa Tanzania kwa kutumia mapato ya ndani.
Tunaamini taasisi nyingine nchini zitafuata mfano wa ubunifu uliofanywa na vijana hao waliotumia rasilimali za ndani badala ya kutegemea misaada ya wahisani wa kutoka nje.
CHANZO:
NIPASHE JANA JUMAPILI