
RAIS John Magufuli, aliyeanza kazi juzi kwa kumteua Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, baada ya kumuapisha jana amefanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Wizara ya Fedha, Hazina.
Tofauti na ziara za viongozi wengine wakiwemo mawaziri waliowahi kuongoza ofisi hiyo, ambao huingia katika vyumba vya mikutano au ofisi za viongozi, Dk Magufuli yeye alianza kuingia katika ofisi za watumishi wa kawaida.
Dk Magufuli aligeuka kivutio kwa wananchi, pale alipotoka katika lango kuu la Ikulu Dar es Salaam kwa miguu kwenda wizarani hapo kupitia njia ambayo imekuwa ikitumiwa zaidi na wananchi.
Wizara hiyo mbali na kuwa karibu na Ikulu, lakini imezungukwa na ofisi nyingi, ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Ofisi Ndogo ya Bunge na mara kwa mara nje kuna kawaida ya kuwa na wananchi na magari mengi yenye madereva wa maofisa wanaofika wizarani hapo na wengine katika ofisi nyingine kwa shughuli mbalimbali.
Baada ya kuingia katika ofisi hizo, Dk Magufuli alianza kufungua milango ya ofisi za watumishi hao na kuwasalimia aliowakuta na kuhoji pale alipokuta meza haina mtendaji.
Katika hatua hiyo, Dk Magufuli alishangazwa kukuta meza sita kati ya nane katika moja ya ofisi hizo, hazina watumishi akalazimika kuuliza majina ya watumishi husika na alipoambiwa walikuwepo, akahoji walikokwenda akajibiwa walikwenda kunywa chai. Huku akionekana kutoridhishwa na majibu hayo, Dk Magufuli alitikisa kichwa huku akisema “wameenda kunywa chai eee!” na kuondoka ofisini hapo kwenda kwenye ofisi za viongozi wa wizara hiyo.
Alipoingia ndani, alifanya kikao cha muda mfupi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile pamoja na makamishna wa fedha na alipotoka taarifa za wizara hiyo zilieleza kuwa Dk Magufuli ameagiza watumishi wa Wizara hiyo inayosimamia Mamlaka ya Mapato (TRA), kuhakikisha wanaongeza kasi ya ukusanyaji mapato, na akaelekeza hasa kwa wafanyabiashara wakubwa.
Mbinu aliyotumia Dk Magufuli, ni ya kitawala ambapo viongozi husimamia wizara kwa kufanya ziara za ghafla, au kutembelea maeneo ya watumishi bila kutoa taarifa, tena bila kufuata utaratibu wowote. Lengo lake mara nyingi ni kujulia hali ya watumishi na matunda yake ni kuongeza ari ya kufanya kazi, kuhimiza na kusisitiza malengo ya taasisi.
*Kuapishwa kwa Masaju
Awali kabla ya kufanya ziara hiyo, Dk Magufuli alimuapisha Masaju kuendelea kushikilia nafasi hiyo, ambapo Mwanasheria Mkuu huyo aliahidi kuendelea kusimamia kesi mbalimbali dhidi ya Serikali ili kuokoa fedha za umma.
Uapisho huo ulifanyika Ikulu na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu Othman Chande, Spika wa Bunge, Anna Makinda na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu.
Masaju alisema ni tumaini lake kuwa wananchi wataendelea kutii sheria za nchi, ili kudumisha amani na mshikamano kama ilivyokuwa wakati wote huku Serikali ikiendelea kuimarisha utii wa sheria.
“Serikali shughuli yake ya msingi ni kusimamia utekelezaji wa sheria na yenyewe ina jukumu la kusimamia amani. Nashauri ushirikiano uliotolewa wakati wa Uchaguzi Mkuu uendelee kudumishwa,” alisema Masaju.
Masaju alisema Serikali inaokoa fedha nyingi za umma kwa kushinda kesi dhidi yake na kwamba inajitahidi kuendesha kesi zake kwa weledi, huku akitoa mfano wa mashauri 34 ya kesi za uchaguzi ya kupinga matokeo zilizofunguliwa mwaka 2010, ambazo Serikali ilizishinda zote.
Alishukuru kupatikana kwa Serikali mpya kwa amani na kwa kuzingatia maelekezo ya sheria na kuomba hali hiyo iendelee ili shughuli mbalimbali ziendelee hasa zile za kujenga uchumi na za kijamii. Alitaka amani ya nchi ipewe kipaumbele na kuonya kuwa ikivurugika hakuna kazi itakayofanyika na kusisitiza amani ndiyo itakayodumisha uchumi wa nchi.