Week Hot newz

'Viongozi wateule shughulikieni vifo vya wazazi, watoto'


Wazazi waliotoka kujifungua wakiwa na watoto wao.

Tatizo la vifo vya wajawazito na watoto wachanga linasababisha majonzi makubwa kwa jamii lakini pia linaleta  ongezeko la watoto waliodumaa, wagonjwa, watoto wa mitaani kupunguza  nguvu kazi ya taifa.
 
Ili taifa lisonge mbele kimaendeleo halina budi kuimarisha huduma za afya kwa wananchi , ili kupunguza vifo vya wajawazito, wazazi na watoto wachanga kwa lengo   la  kuepusha matatizo hayo.
 
Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii za mwaka 2014 zinaonyesha kwamba Tanzania ni nchi ya saba duniani kwa idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi, ikikadiriwa kuwa  wajawazito karibu 7,900  hufa kila mwaka, huku wastani wa watoto wachanga 40,000 wakipoteza maisha kila mwaka kabla ya kutimiza mwezi mmoja baada ya kuzaliwa.
 
Kama vile haitoshi inakadiriwa kwamba watoto 100,000 hufa kila mwaka kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano.Kadhalika wengine 50,000 huzaliwa wakiwa wafu kutokana na sababu mbalimbali ambazo iwapo jitihada za makusudi zingechukuliwa mapema, zaidi ya asilimia 45 ya vifo hivyo visingezuiliwa.
 
Pia asilimia 44 ya wasichana wanaofikisha umri wa miaka 19 nchini wanapata ujauzito, haijalishi wapo shuleni au nje ya masomo.
 
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 asilimia 54 ya Watanzania ni watu walio chini ya miaka 20 na hii inatafsirika kuwa takribani miaka 15 hadi 20 ijayo idadi kubwa ya vijana wataingia katika umri wa uzalishaji mali na kuwa nguzo ya kiuchumi.
 
Kutokana na hali hiyo makala hii inawapa changamoto wateule wa nafasi za urais na ubunge kuweka wazi namna watakavyo lishughulikie tatizo kubwa la vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
 
Ukweli ni kwamba viongozi hawa wanakwenda kufunga mkataba kati yao na raia kwa miaka mitano ijayo hivyo kazi yao ni kutafuta ufumbuzi wa kumaliza tatizo hili.
 
Waliochaguliwa wafahamu kuwa afya ya mama ni muhimu kama ilivyo ya mtoto wajue kuwa tangu mwanzo suala hili halijapewa kipaumbele cha kutosha kutokana na kutokuwapo mfumo bora wa kutoa huduma kikamilifu.
 
Ni vyema sasa wabunge na mawaziri watakaounda serikali ya awamu ya tano wakatueleza kwa kina namna gani watakavyosimamia na kuhakikisha uzazi salama wa mpango unavyosimamiwa ili kuhakisha kuwa adha ya kufa wakati wa kujifungua inamalizika ama kuondoka.
 
Aidha viongozi waieleze jamii vipaumbele vyao kwenye afya ya mama na mtoto ikiwa ni pamoja na kuishauri serikali kuona suala hilo kuwa na umuhimu wa kipekee na kulipa kipaumbele zaidi ikilinganishwa na masuala mengine.
 
Tafiti mbalimbali zilizofanywa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ya DSW, Marie Stopes Tanzania, Pathfinder International, Chama cha Maelezi Bora (Umati) na HDT zinabainisha kuwa tatizo la uzazi wa mpango ni kubwa.
 
Tafiti za mashirika hayo zinaonyesha kuwa mimba zisizotarajiwa husababisha uwezekano mkubwa wa vifo vya mama na mtoto kwa asilimia tisa ya vifo vinavyotokea nchini.
 
Angalizo linatolewa kuwa kiwango hicho kinaweza kuongezeka zaidi iwapo hatua za makusudi hazitatolewa katika jamii kwa hiyo ni suala ambalo wabunge wanatakiwa kulitizama na kulipa umuhimu wa kipekee.
 
Uzazi wa mpango ni mkakati muhimu wa kuwasaidia wanawake kupanga muda wa kutosha kati ya kizazi kimoja na kingine, kuzuia mimba katika umri mdogo na kuepuka mimba zisizotarajiwa.
 
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, (WHO) gharama za kuzuia ujauzito ni za chini zaidi kuliko za matibabu yanapotokea wakati wa kujifungua.
 
Kwa hiyo uzazi wa mpango unazipa familia au mtu binafsi uwezo wa kuchagua ukubwa wa familia ambayo anaimudu, kuwekeza katika elimu na makuzi ya kila mtoto na kubaki na fedha za ziada hatua inayoweza kuchangia kukuza uchumi wa taifa. 
 
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake Moke Magoma, anasema kuna uwezekano mkubwa wa Tanzania kupiga hatua za haraka kimaendeleo iwapo jamii itapata uelewa wa kutosha kuhusu uzazi wa mpango.
 
“Ni muhimu sana kuwepo kwa huduma za afya ya mjamzito na mtoto mchanga, ambayo katika uhalisia wake inajidhihirisha kwa kila aliye hai sasa amepatikana kupitia mama yake kuwa mjamzito” anasema Dk. Magoma.
 
“Uzazi wa mpango ni muhumu kwa kuwa wanaweza kudhibiti na kupanga idadi ya watoto, kuendeleza na kutunza familia kitaaluma, lishe na wakati huo wakafanya kazi wanazozitaka na kushiriki katika maamuzi ya kiuchumi na kisiasa”
Daktari Magoma anasema uzazi wa mpango ni njia bora zaidi katika afya ya mama na mtoto na kwamba mbinu za kitaalamu za uzazi wa mpango hazina madhara kama baadhi ya watu wanazovumisha na kuwatia hofu wananchi.
 
Naye Dk. Msiima Mushumba,kutoka shirika la Marie Stopes Tanzania,anasema jamii inapaswa kutambua kuwa kuzaa watoto wengi bila mpangilio ni kuhatarisha maisha ya mama, watoto na kudumaza uchumi wa taifa.
 
Anasema kwa wastani familia inapaswa kuzaa watoto wasiozidi watano na kwamba kuanzia mimba ya sita na kuendelea huitwa mimba hatarishi ambapo anaitaka jamii kufuata njia za uzazi wa mpango.
 
Kadhalika anabainisha kuwa wananchi ambao hawakusoma wanazaa zaidi kuliko waliosoma kwa kuwa wengi wao hutambua umuhimu wa kuzaa kwa mpango kuliko ambao hawakusoma.
 
Dk. Mushumba, anasema jitihada za makusudi zinahitajika kupitia serikali, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na jamii kwa ujumla kuhakikisha huduma za uzazi wa mpango zinawafikia wanawake wote nchini.