Tafakari masomo Dominika, ninafurahi tena kuwa
nawe katika safari yetu ya Majilio tukijiandaa kwa ajili ya ujio wa
Mwana wa Mungu. Ni wakati huu tunapoimba kwa furaha Masiha wetu njoo,
ukatuokoe.
Tuko
sasa Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio ambapo Neno la Mungu
linatualika kutambua kwa njia ya imani alama zinazomtambulisha Masiha.
Tunapata kutafakari katika Injili juu ya wasiwasi wa Yohane Mbatizaji
juu ya Masiha, kiasi kwamba anatuma wafuasi wake tokea gerezani
wakamwulize Bwana wakisema, eti wewe ndiye Masiha tuliyemtarajia au
tumngojee mwingine?
Yohane Mbatizaji anaingiwa na wasiwasi kwa
sababu aliweka matumaini yake katika alama zisizo za kweli! Kwetu sisi
yaweza tokea na inatokea mara kadhaa kutumaini katika bwana asiye
mwenyewe! Kumbe leo mwaliko ni huo, yaani kuwa makini ili tusianguke
katika mtego kama huo!
Mpendwa msikilizaji, alama ambazo zilisadikika
na Yohane Mbatizaji na wafuasi wake ni kuwa Masiha ajaye atakuwa hakimu
mkali atakayewapatiliza mbali wadhambi. Kinyume chake Masiha hafanyi
hilo isipokuwa upendo kwao akitafuta kuwaokoa katika taabu yao hiyo.
Mpendwa msikilizaji, kazi na wajibu wetu mkuu, ni kutambua wakati huo
tukijiuliza daima, ni alama zipi zinazomtambulisha Masiha ambaye
tunaimba kwa furaha tukisema uje kutuokoa!
Ndiyo kusema, alama za
kweli tunazipata katika Somo la kwanza toka kitabu cha Nabii Isaya
35:1-6,10 akisema ndipo vipofu na viziwi watakapoona na kusikia, mwenye
kupooza atarukaruka tena na bubu kuimba kwa furaha. Mara moja toka
katika alama hizi tunagundua kuwa Masiha anakuja kwa ajili ya kuwaondoa
walio katika taabu na kuwaweka huru. Taabu kwa kawaida ni tokeo la
dhambi, yawezekana dhambi ya mtu binafsi lakini hasa dhambi kwa ujumla.
Mpendwa
msikilizaji, katika hili tunaalikwa kuingia katika safari ya toba na
uaminifu kwa Injili kama tusomavyo katika Injili ya Marko. 1:15. Katika
toba na kuishi Injili tunafikia kwa namna ya pekee kabisa hatua ya
kutambua alama zinazomtambulisha Masiha.
Jukumu la kuishi alama hizi
linatuweka katika mazingira ya furaha na linatuonesha waziwazi kwamba
utawala wa Masiha unaanza kukolea katika maisha yetu.
Mpendwa mwana
wa Mungu, inawezekana ikajitokeza kukawa na kuchelewa katika
utekelezaji, yaani kuishi toba na hivi tukaweza kukata tamaa, basi Mtume
Yakobo anatutia moyo na tumaini akisema, kuweni na subira mpaka Bwana
atakapokuja. Katika subira tunataka polepole kutenganisha uovu na ubaya
ulio katika jumuiya na katika mtu awaye yote katika ubinafsi wake.
Katika
subira Mtume Yakobo anatuonya daima kuachana na tabia ya kuhukumiana
maana hakimu mwaminifu ni mmoja yaani Mfalme Masiha. Mtume Yakobo
anatuonya katika subira kutambua kuwa safari ya wokovu lazima itazamwe
kama mkulima anavyongojea mvua za masika na za vuli.
Mpendwa
msikilizaji, kipindi cha Majilio ni kipindi cha neema, ni kipindi cha
kupanda ili kujipatia mavuno hapo baadaye, na kwa hakika mavuno ni
furaha ya moyo inayokamilishwa katika Yesu Kristu mfufuka ambaye
atatufufua siku ya mwisho na kukaa naye katika kiti cha enzi pamoja na
Baba mbinguni.
Nikikutakia majilio njema napenda kusema fikiria
zaidi kuwalisha maskini na kuwahudumia wagonjwa katika jumuiya yako na
jitahidi kuwa adui wa dhambi kila siku ya maisha yako. Mpendwa, hiyo
ndiyo namna ya kuishi Majilio ya mwaka huu. Nakukumbusha tena hapo
jirani kwako kuna mtoto ambaye amekosa ada ya shule msaidie na mfundishe
namna ya kuitumia na zawadi yako kwa hakika ni mbinguni. Tumsifu Yesu
Kristo na Bikira Maria.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.