Pamoja
na kupiga tubangi na kanywaji bado mzee mzima najua mipaka yangu. Najua
kuwa ninapotaka kuongea lazima kuhakikisha kuwa kichwa na mdomo
vinafanya mawasiliano. Huwa nahakikisha sijambi au kunonihino kwa mdomo
tena usawa huu wa umri huu hata kama kufanya hivyo kunawavutia na
kuwafurahisha inzi. Ninapoongea huwa nahakikisha sipayuki, situsi,
sikebehi, wala kusingizia bali kutoboa ukweli.
Mfano, hata ninapoandika kuhusu hawa wababu waropokaji na
watukanaji kama Beni Tunituni wa Kiwila bado siwezi kuwaita wakumbafu
hata kama ni malofa wa kimawazo na heshima bado siwezi kuwaita malofa
japo kweli ni malofa.
Nikiwaita malofa, wenye akili watashindwa kutofautisha kati ya lofa
na tajiri wa fikra. Kwa wanaojua sayansi ya tabia na mikakati ni kwamba
dalili ya kwanza ya ulofa wa kimawazo na ukumbafu ni kutumia mitusi
tena ya nguoni kama silaha au namna ya kupata ulaji.
Pamoja na kupayuka kwake, nakubaliana na Beni kuwa wapingaji ni
malofa kweli kweli. Kwani kwa ulofa wao wameweza kuvua papa wawili toka
chama Cha Maulaji (cCM). Si hilo tu, ukilinganisha utajiri utokanao na
ufisadi na ujambazi mwingine, uwezekano wa wapingaji kuwa malofa ni
mkubwa japo hakuna kipengele hata kimoja kinachowaonyesha kuwa
wakumbafu. Nadhani wangekuwa wapumbavu wasingeweza kuvuna vigogo na
mibuyu toka cCM.
Sometimes, nyani haoni kundule. Sijui kama tutaanza kutafutana
uchawi kati ya wapingaji na wale waliowabinafsisha wenzao nao
wakajibinafsisha nani atakuwa lofa kimawazo na mkumbafu wa kweli? Sijui
hawa wanaowaita wenzao wakumbafu wanamaanisha nini iwapo wao wamekaa
kwenye ulaji na kuruhusu kila aina ya kibaka kutoka nje na ndani
kuwaibia walevi?
Je? huu si ukumbafu wa kupindukia?
Kama siyo, inakuwaje wale walioko ndani wanakosa la kusema na
kuwaonyesha walevi badala yake wanakimbilia mitusi, kutumia ndata
kuwatisha na kuwazuia kufanya kampani zao? Inakuwaje kama si ukumbafu wa
kukaa kwenye mjengo na jumba lenyewe wakashindwa kutimiza walichoahidi
hadi sasa wanaanza kutegemea mitusi, vitisho na uchakachuaji?
Laiti hawa wanaowaita wakumbafu wenzao wangewauliza mafisadi kama
akina Rugemalayer na Singasinga na wengine waliowatumia huko nyuma
wangejua ni wapumbavu kiasi gani. Hivi majambazi kama wale wa India
waitwao ‘RITES’ waliopewa reli zetu wakajiibie watakao wanadhani
wanawaona washitiri wao kama wajanja au wakumbafu tu wa kawaida?
Kawaulize wahalifu wote waliokingiwa kifua kuanzia wale
walioghushi, waliofilisi mashirika ya walevi na wengine wanaouza pasi
zetu na kutumia mipaka yetu kama vitega uchumi wao wanawaonaje hawa
wanowaachia wakafanya uhalifu kama huu wa kuhujumu kaya.
Loo! Naona mibangi kanywaji na usongo vinapanda hadi naanza kuongea ‘kikameruni’ bure.
Tena kabla ya kusahau, lazima niseme wazi na kwa herufi na sauti kubwa: ‘walaaniwe mabingwa wa mitusi.’
Walaaniwe wakumbafu wote wanaoleta upumbavu wa kuita wenzao
wapumbavu wakati wao ndiyo. Tatizo na fyatu wengine ni kwamba
wakiharibikiwa wanadhani kila mlevi ameharibikiwa. Kama wewe ni mvuta
bangi au mlevi basi si wote waliokuzunguka ni walevi. Kama wewe ni
kibaka usidhani wote ni vibaka. Kama wewe ni lofa usidhani kila mlevi ni
lofa. Kama wewe ni mkumbafu, usidhani kila mlevi ni mkumbafu. Kwa vile
nina usongo na wakumbafu pamoja na ukumbafu, naona leo niishie hapa kwa
kuwataka wakumbafu wasituletee ukumbafu na mitusi yao. Wasitujazie mbu.
Watuache na amani yetu vinginevyo kuna mikumbafu itajikuta The Hague
wakila ugali na wmalofu wengine kama akina Laurent Gbagbo Ivory Coast na
Charles Taylor wa Liberia.
Ongeza msamiati maneno magumu, ukumbafu ni kufanya ndiyo siyo au bila kutumia bongo zote Mkumbafu ni yule anayefanya ukumbafu.
CHANZO:
NIPASHE