
MKUU
wa msafara wa timu ya taifa ya wanawake ya Afrika Kusini chini ya miaka
20, Peter Manchonyane, ameelezea wasiwasi wa kikosi chake kuathiriwa na
msiba wa Rais wa zamani wa nchi yake, Nelson Mandela, katika mechi ya
leo dhidi ya Tanzania ‘Tanzanite’.
Bara la Afrika na dunia kwa jumla, inaomboleza msiba wa Mandela,
aliyefariki juzi usiku, saa chache baada ya kikosi cha vijana cha nchi
hiyo kutua nchini kwa mechi ya mchujo kuwania kufuzu fainali za dunia
kwa wanawake chini ya umri huo, zitakazochezwa nchini Canada mwakani.
Manchonyane alisema kuwa kikosi chake kinachojulikana kwa jina la
‘Basetsana’, kimekumbwa na simanzi miongoni mwa wachezaji na viongozi,
baada ya kifo cha Mandela na kwamba anahisi kitaathiri harakati zao leo.
Pamoja na hofu hiyo, kiongozi huyo alisisitiza kuwa lengo
lililowaleta ni kupigana kusaka ushindi, ili kujiwekea mazingira mazuri
kuelekea mechi ijayo kuwania tiketi ya kufuzu raundi ya tatu na ya
mwisho ya mchujo huo wa fainali za mwakani huko Canada.
“Tumeshtushwa na kifo cha Mzee Mandela, kambi imejaa simanzi. Licha
ya kutarajia ugumu kucheza tukiwa katika hali hiyo, lakini tunaamini
tutashinda changamoto hiyo na kuibuka na ushindi ili kuondoa presha
katika mechi ya marudiano nyumbani,” alisema Manchonyane.
Kwa upande wake kocha wa Tanzanite, Rogasian Kaijage, alisema, kauli
ya kiongozi huyo ni ‘danganya toto’ iliyobeba mantiki ya kuwahadaa na
kuvimbisha kichwa na kwamba ameligundua hilo na kikosi chake kitacheza
kwa tahadhari dhidi ya Basetsana.
Alisema, anakitambua kikosi cha Basetsana ni kizuri, imara na bora,
hivyo kazi ya nyota wake itakuwa kupigania matokeo mazuri nyumbani kama
ilivyokuwa dhidi ya Msumbiji na wala hawatobweteka kwa alichokiongea
kiongozi huyo.
“Basetsana kama jina lao lilivyo ni wasichana wadogo, ambao ni vigumu
kushikwa na simanzi kubwa juu ya msiba wa kiongozi ambaye wakati
anatawala wengine walikuwa wadogo, wengine hawajazaliwa. Watoto mara
nyingi hawaguswi sana na vifo,” alifafanua Kaijage.
Aliongeza kuwa, nia yao kama timu ni kupigania matokeo mazuri na
kuwataka Watanzania kumiminika kwa wingi kuwasapoti mabinti hao, ili
kuwapa nguvu ya kushinda na kujiweka pazuri kuelekea raundi ya tatu ya
michuano hiyo.
Kwa upande wake nahodha wa Tanzanite, Fatuma Issa, alisema, morali
katika kikosi chake iko juu na kwamba, Watanzania wanapaswa kujitokeza
kwa wingi Uwanja wa Taifa ili kuwashangilia kuwaongezea nguvu na Mungu
akipenda wataibuka na ushindi.
Viingilio katika mechi ya leo itakayopigwa kuanzia saa 10:00 alasiri,
vitakuwa ni sh 1,000, sh 2000, sh 5,000 na sh 10,000, ambako tiketi
zitauzwa uwanjani hapo leo.